“Jamal! Jamal! Jamal!” nilishtuka baada
ya kuisikia tena ile sauti nzito ya kutetemeka, iliyoniita kwa mara ya kwanza
kabisa, ikiniita tena, ikafuatiwa na vicheko vya kutisha vya watu wengi, nikawa
nageuka huku na kule lakini sikuona chochote zaidi ya giza nene, hofu kubwa
ikatanda moyoni mwangu.
SASA ENDELEA...
“Hujafika hapa kwa bahati mbaya Jamal,
ilikuwa ni lazima uje huku ili ufunuliwe haya mambo ambayo kwa akili ya kawaida
usingeweza kuyajua, hebu nifuate,” ilisikika ile sauti nzito ya kutetemeka na
kutisha, nikiwa sielewi ni nani aliyekuwa akizungumza nami na alikuwa anataka
nimfuate wapi, nilishtukia nikishikwa mkono.
Kufumba na kufumbua, tulitokezea sehemu
ambayo kulikuwa na watu wengi wa kila aina wamekusanyika. Wengine walikuwa
wamekaa, wengine wamesimama, wengine wamejiinamia na wengine wamelala.
Walikuwa wengi mno, wakubwa kwa wadogo,
vijana kwa wazee, wanaume kwa wanawake. Cha ajabu, licha ya wingi wao, wote
walikuwa kimya kabisa, hakuna aliyekuwa anazungumza chochote, sauti pekee zilizokuwa
zinasikika zilikuwa ni za watu wachache waliokuwa wakigugumia kuonesha wapo
kwenye maumivu makali.
“Hapa ni wapi na hawa ni akina nani?”
niliuliza lakini hakukuwa na mtu wa kunijibu, yule mtu aliyenileta sikumuona
tena, nilijikuta nikiwa peke yangu lakini kukawa na nguvu fulani iliyokuwa
inaniongoza sehemu ya kwenda.
Niliendelea kujipenyeza ndani ya lile
kundi la watu, nikawa makini kuwatazama wale watu usoni nikiamini naweza
kukutana na ninaowafahamu lakini sura nyingi zilikuwa ngeni kwangu. Nikiwa
naendelea kushangaashangaa, nilimuona mtu ambaye nilikuwa namfahamu vizuri
lakini nilishangaa iweje nikutane naye?
Hakuwa mwingine bali Mzee Muyombe, huyu
alikuwa dereva wa halmashauri na nilimkumbuka vizuri kwa sababu mwanaye,
Mathayo, tulisoma naye darasa moja tukiwa shule ya msingi na alikuwa rafiki
yangu kipenzi. Kilichonishangaza, ni kwamba ilikuwa imepita karibu miaka tisa
tangu mzee huyu afariki!
Alipoteza maisha kwenye ajali mbaya ya
gari baada ya gari alilokuwa anaendesha kugonganga uso kwa uso na gari dogo
lililokuwa linaendeshwa na kijana mmoja wa palepale mtaani. Nakumbuka hata siku
ya mazishi yake nilikuwepo na nilikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wanamfariji
Mathayo kwa kuondokewa na baba yake.
Kumbe wakati nikiendelea kutafakari
hivyo, na yeye alinikumbuka ingawa alionekana ni kama ananifananisha, akawa
ananitazama kwa kunikazia macho. Kiukweli niliogopa sana maana kwa tafsiri
nyepesi, yule hakuwa binadamu wa kawaida bali mzimu kwa sababu mwenyewe
alishakufa siku nyingi zilizopita.
Tuliendelea kutazamana kwa muda, akaanza
kunionesha ishara kama ya kunikataza jambo ambalo sikulielewa, akawa anatumia
mikono yake kunizuia, nikiwa naendelea kujaribu kutuliza kichwa ili nielewe
alikuwa akimaanisha nini, nilishangaa ameyeyuka na kupotea kwenye upeo wa macho
yangu.
Nilifikicha macho na kutazama tena pale
alipokuwepo, hakuwepo. Nikabaki na maswali mengi yaliyokosa majibu. Nilijikuta
nikiendelea na safari, nikazidi kupenya kwenye ule umati huku nikimtazama kila
mmoja usoni, kwa mara nyingine nikajikuta nikishtuka mno baada ya kumuona mtu
ambaye nilikuwa namfahamu.
Huyu hakuwa mwingine bali Hezron,
tuliyekuwa tukicheza naye enzi za utoto ambaye naye kama ilivyokuwa kwa mzee
Muyombe, alikuwa amefariki dunia miaka mingi iliyopita. Nakikumbuka vizuri kifo
chake, alipoteza maisha baada ya kuzama baharini wakati akiogelea na ndugu
zake, akazidiwa na mawimbi yaliyomvutia baharini na baadaye mwili wake kuokotwa
ukiwa ufukweni, akiwa tayari amefariki dunia.
Nilishangaa imekuwaje nikutane na mtu
mwingine ambaye naye alikuwa amepoteza maisha? Kingine kilichonishangaza,
wakati anapoteza maisha, Hezron bado alikuwa kijana mdogo lakini siku hiyo,
naye alionekana kuwa mkubwa, akiwa analinganalingana na mimi.
Sikuwahi kusikia wala kusoma mahali
popote kwamba mtu akifa akiwa mtoto, anaendelea kukua huko kwenye maisha yake
mengine mpaka hatua ya kufikia utu uzima, nilibaki nimepigwa na bumbuwazi. Cha
ajabu, naye alikuwa akinioneshea ishara kama ya kunikataza jambo, sikuelewa pia
ni jambo gani alilokuwa akinikataza.
Nilipoendelea kumtazama, naye aliyeyuka,
nikaendelea kusonga mbele ambapo sasa nilianza kukutana na watu wengi niliokuwa
nawafahamu. Miongoni mwao, wote walishatangulia mbele za haki kwa maana kwamba
walishakufa. Kadiri nilivyokuwa nazidi kukutana nao ndivyo hofu ilivyokuwa
inazidi kupungua ndani ya moyo wangu.
Kati ya yote, ilionesha watu wote
niliokuwa nafahamiana nao walikuwa wakinikataza jambo ambalo bado sikuwa
nimelielewa ni nini. Nikiwa naendelea kushangaashangaa, nilisikia mlio wa
kengele ya ajabu, ikalia mfululizo kisha nikawaona watu wote wakiinamisha
vichwa vyao chini, giza nene likaanza kutanda.
“Tuondoke, muda huu haufai kabisa wewe
kuwepo huku, unaweza kupitiliza moja kwa moja,” niliisikia ile sauti kisha
nikahisi nikishikwa kwa nguvu, kufumba na kufumbua nilikuwa nimerejea tena kule
kwenye giza nilikokuwepo awali lakini bado niliendelea kuisikia ile sauti ya
kengele ikilia.
Sikukumbuka nimeshuka saa ngapi kwenye
treni na limeelekea wapi ila nilijikuta tu nikiwa nimesimama. Mlio wa ile
kengele ulipokoma, nilianza kusikia sauti za watu wengi wakilia kwa sauti za
ajabuajabu, wakionesha kwamba wapo kwenye maumivu makali.
“Mbona unaonesha kuwa na hofu kubwa
moyoni mwako?” niliisikia ile sauti ikiniuliza, nikashindwa cha kujibu zaidi ya
kujiinamia. Wale watu niliowaona kule, walinifanya nijawe na huzuni kubwa
kwenye moyo wangu. Kumbukumbu ya misiba mingi niliyohudhuria tangu nikiwa mdogo
ilianza kujirudia kichwani mwangu.
Kwa mbali nikaanza kuamini maneno ya
Shenaiza kwamba huenda ni kweli nilikuwa nimekufa. Nilijisikia uchungu mkali
sana ndani ya moyo wangu, nilitamani nirudi kwenye maisha yangu ya kawaida kwa
sababu bado sikuwa nimekamilisha mambo mengi sana kwenye ulimwengu wa kawaida.
Kama kweli huo ndiyo ungekuwa mwisho wa
maisha yangu, tafsiri yake ni kwamba ingekuwa sawa na kusema kwamba sijafanya
chochote maishani mwangu, yaani nimezaliwa, nikaishi kisha nikafa bila kufanya
jambo lolote la maana maishani mwangu, jambo ambalo liliniumiza sana.
“Najua unavyojisikia ndani ya moyo wako,
nalijua hitaji la moyo wako na ndiyo maana nataka nikuoneshe kilichofanya
uletwe huku. Kama nilivyosema, hukuletwa huku kwa bahati mbaya bali kuna kazi
ambayo unatakiwa kwenda kuifanya.
“Kuna mamia ya watu wanaendelea kuwa
wahanga kwa sababu ya tamaa za watu wachache. Maisha yako yalikuwa yamefikia
mwisho lakini umshukuru Mungu wako kwa kupata nafasi hii, huwa siyo kila mtu
anaipata.
“Tabia yako njema uliyoionesha katika
maisha yako tangu ulipopata akili, ikiwemo kushika ibada, kufuata maandiko kwa
kuacha kufanya yale yaliyokatazwa na kuishi katika misingi ambayo ndiyo hasa
binadamu anayotakiwa kuishi, ni miongoni mwa sababu zilizofanya upate hii
nafasi ya kurudi tena duniani.
“Ukirudi duniani, ukawe balozi mzuri wa
kuwahamasisha binadamu wenzako ambao bado wapo hai juu ya kumuabudu Mungu,
kuwapenda binadamu wenzao na kuwatendea mambo mema, kuacha kufanya maovu na
maasi na kubwa zaidi, kwenda kuikomesha kazi inayofanywa na baba yake Shenaiza
na watu wake, maelezo mengine utakuwa unaletewa hukohuko,” ilisikika ile sauti
nzito ya kutisha.
Sikuelewa aliyekuwa anayasema hayo ni
nani na pale nilikuwa wapi maana nilimsikia akizungumzia kuhusu kurejea
duniani, akimaanisha kwamba pale hapakuwa duniani. “Umenielewaa?” ilihoji ile
sauti na kusababisha ngurumo nyingi zianze kusikika kutoka kila upande,
zikiambatana na upepo mkali uliokuwa ukivuma kwa kasi kubwa.
“Ndiyooo!” nilijibu kwa sauti iliyojaa
hofu kubwa, iliyokuwa ikitetemeka ambayo kama nilivyoeleza kuanzia mwanzo,
ilikuwa ikitokea moyoni na siyo mdomoni, nikasikia radi kubwa ikipiga jirani
kabisa na pale nilipokuwepo, sikuelewa tena kilichoendelea.
Nilipokuja kushtuka, nilijikuta nikiwa
nimelala kitandani, mapigo yangu ya moyo yakinienda mbio kuliko kawaida, nikiwa
nimeunganishwa mashine ya kunisaidia kupumua huku mwili wangu ukiwa
umeunganishwa na vifaa vingi vya kitabibu, milio ya mashine mbalimbali
ikisikika ndani ya chumba kile ambacho hata bila kuuliza, niligundua kwamba ni
wodini.
“Amefumbua macho! Dokta... amefumbua
macho! Njooni haraka!”
Je,
nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment