ILIPOISHIA:
Nikiwa naendelea kulia, nilipaliwa na
mate, hali iliyofanya nikohoe mfululizo, ajabu zaidi, na ule mwili wangu pale
kitandani ukakohoa, madaktari wakazidi kupigwa na butwaa, wakawa wanatazamana
wakiwa ni kama hawaamini kilichokuwa kinatokea.
SASA ENDELEA...
“Amerejewa na fahamu zake, amezinduka,”
alisema daktari mmoja kwa sauti, nikaona pilikapilika zimeanza tena kupamba
moto mle wodini. Daktari mmoja akaja kunipima mapigo ya moyo huku akiwatazama
wenzake, nikamuona akitingisha kichwa.
Niliendelea kupewa matibabu ya uhakika,
kila mmoja akawa anachakarika kwa nafasi yake. Nilimuona daktari mmoja
akifungua mlango na kutoka nje, akasogea mpaka pale akina Raya walipokuwa
wamekusanyika.
Nikamuona akizungumza nao mambo fulani,
ghafla nikamuona Raya akimrukia mwilini kwa furaha, akamkumbatia kwa nguvu
kisha akainua mikono juu kama ishara ya kumshukuru Mungu.
Japokuwa sikuwa nimesikia walichokuwa
wanakizungumza, niliamini kwamba lazima yule daktari atakuwa ameenda kuwaambia
kwamba sikuwa nimekufa kama wanavyofikiria. Nilijikuta nikisisimka sana, yale
machozi yaliyokuwa yananitoka yakaacha, nikawa namtazama Raya alivyofurahi kama
mwendawazimu.
Nilijikuta nikitabasamu kwa jinsi
maichana huyo alivyokuwa amefurahi, nikamuona akimkumbatia kila mtu kwa furaha,
huku tabasamu likichanua kwenye uso wake uliokuwa umeloweshwa na machozi. Kumbe
vile nilivyokuwa nikitabasamu mwenyewe, hata ule mwili wangu pale kitandani
ulikuwa ukitabasamu, nikawaona madaktari wote wakipeana mikono kama ishara ya
kupongezana.
Ama kweli hii dunia ina maajabu,
nilisema mwanzo na sitaacha kusisitiza, hii dunia ina mambo mengi sana ambayo
kwa akili za kawaida ni vigumu sana kuyaelewa. Najua bado kuna watu wengi
hawaelewi au hawaamini ninachokisema lakini napenda tu kuwaambia watu kwamba maisha
yana siri kubwa sana.
Ni wale tu ambao wako tayari kujifunza
vitu vipya kila siku wanaoweza kuendana na kasi halisi ya maisha. Ukitazama kwa
juujuu, unaweza kuona kama maisha au uhai wa mtu ni jambo jepesi sana lakini
haipo hivyo. Ukiijua thamani halisi ya maisha na uhai, kamwe huwezi kumtendea
ubaya binadamu mwenzako, huwezi kuyakatisha maisha ya mtu wala huwezi
kuwadharau wengine.
Basi wakati watu wote wakionesha
kufurahishwa na maendeleo yangu pale kitandani, mimi mwenyewe nilikuwa
nikijihisi hali tofauti kabisa. Japokuwa nilikuwa nimefungwa bandeji kubwa
kwenye lile jeraha langu kubwa kifuani na mara kwa mara lilikuwa likisafishwa
na kuwekwa dawa nyingine, huku katika ulimwengu wa peke yangu sikuwa nikihisi
maumivu hata kidogo.
Hata watu walivyokuwa wakihangaika,
nilibaki kuwashangaa tu kwa sababu sikuwa najihisi kama naumwa sehemu yoyote na
hata pale walipokuwa wanasema kwamba nimekufa, mwenyewe bado nilikuwa na akili
zangu timamu na nilikuwa naelewa kila kitu kilichokuwa kinaendelea.
Katika ukuaji wangu, nimewahi kusikia
kwamba mtu anapokufa, anakuwa anaendelea kuishi kwa siku kadhaa, na hata siku
ya mazishi yake, huwa mwenyewe anashuhudia anavyozikwa, anaangalia nani analia
sana, nani halii, nani anafurahia kifo chake na watu wangapi wamehudhuria kwenye
mazishi yake.
Kabla sijatokewa na mkasa huu, na mimi
nilikuwa mgumu sana kuamini lakini leo naamini kwamba kumbe hata wafu huwa
wanaishi, kwa hiyo usimtendee mtu ubaya ukiamini kwamba akishakufa huo ndiyo
mwisho wake, unajidanganya!
Hata katika vitabu mbalimbali vya dini,
vinaeleza kwamba kuna maisha baada ya kifo, natamani sana kila mtu awe anaishi
maisha yake akielewa kwamba kuna maisha baada ya kifo!
Nikiwa bado nimesimama palepale
nikijitazama mwili wangu pale kitandani na watu wote waliokuwa ndani ya wodi
hiyo, kwa mara nyingine nilijikuta nikishikwa tena mkono na kuvutwa kwa nguvu
na mtu ambaye sikumuona.
Safari hii alikuwa na nguvu pengine
kuliko hata mara ile ya kwanza, kufumba na kufumbua nikajikuta nimerudishwa
tena kule nilikokuwa mwanzo lakini tofauti yake, safari hii giza halikuwa nene
sana wala hakukuwa na milio ya wanyama wa kutisha.
Jambo ambalo bado lilikuwa likifanana,
ni kwamba kila nilichokuwa nikikiwaza moyoni, kilikuwa kikisikika kwa sauti ya
mwangwi utafikiri nimekitamka mdomoni. Yule mtu hakunisemesha chochote,
akaniacha mahali ambapo sipajui kisha akayeyuka kama upepo.
“Jamal! Nisamehe Jamal,” niliisikia
sauti ambayo niliitambua kwamba ni ya Shenaiza ikinizungumzisha kwa mbali,
ikawa inasikika kwa mwangwi kama sauti nyingine. Nilishtuka sana,
kilichonishtua ni kugundua kwamba Shenaiza naye alikuwepo kwenye mazingira yale
ya ajabu na kutisha kuliko kawaida.
“Nimekusamehe Shenaiza ila nataka
kuufahamu ukweli wako,” nilitamka lakini kama ilivyokuwa mwanzo, sauti
haikutoka kabisa, nikashusha pumzi ndefu na kuanza kuzungumzia moyoni, nikarudia
maneno yaleyale, kweli sauti ikatoka.
“Mimi sina ubaya wowote na wewe Jamal,
haya yote ameyasababisha baba yangu.”
“Baba yako amesababisha kivipi? Na hapa
nilipo ni wapi? Nimefikaje?”
“Sijui chochote Jamal, mi nahisi kama
nipo ndotoni ila nasikia wewe ulishakufa,” alisema Shenaiza na muda huohuo,
nikajikuta nimehama pale nilipokuwepo na kutokezea sehemu nyingine tofauti
kabisa. Nilijikuta nimetokezea kwenye chumba cha kifahari, kilichokuwa na kitanda
kikubwa na vitu vingine vya thamani.
Juu ya kitanda hicho, alikuwa amelala
msichana mrembo ambaye bila hata kuuliza, niligundua kuwa ni Shenaiza.
Nilishindwa kuelewa pale ni wapi na imekuwaje nifike pale, pia nikawa najiuliza
kuhusu kauli ya Shenaiza kwamba eti mimi nimekufa. Kama Shenaiza amelala,
niliyekuwa nazungumza naye ni nani? Au ndiyo maana alisema anahisi kama yupo
ndotoni?
“Shenaiza!” nilimuita lakini sauti
haikutoka, nikamuita moyoni! Cha ajabu aliitika, nikamuona japokuwa alikuwa
amelala, midomo yake ilikuwa ikichezacheza kuonesha kwamba ni yeye ndiye
aliyekuwa akizungumza.
“Unasema baba yako ndiyo anahusika na
haya yote, hebu niambie kivipi.”
“Siwezi kukwambia chochote Jamal kwa
sababu wewe umeshakufa, ila kaa ukielewa kwamba baba yangu siyo mtu mzuri hata
kidogo.”
“Nataka uniambia ukweli, ilikuwa
ukaipata namba yangu na kuanza kuwasiliana na mimi wakati ukijua kabisa
unanisababishia matatizo na kwa sababu gani unang’ang’ania kusema nimekufa?”
”Hayo hayana maana tena Jamal, nakuomba unisamehe
kwa kukusababishia kifo.”
“Kifo? Mimi sijafa Shenaiza.”
“Najua naongea na mzimu wako Jamal,
nakuomba sana msamaha, siku ya mazishi yako nitajitahidi kufika nikuage,
nilikupenda sana lakini ndiyo hivyo tena, Mungu amekuchukua kipindi ambacho
hata sijakufaidi, najisikia vibaya sana Jamal.”
“Unazungumza nini? Mimi sijafa Shenaiza!
Sijafaaa,” nilisema kwa sauti kubwa huku nikimtingisha pale kitandani azinduke
usingizini, ghafla nikashangaa msichana huyo akikurupuka usingizini na kupiga
kelele kwa nguvu!
“Mzimuuu! Mzimu wa Jamal umenifuata,
nisaidieni nakufaaa!” alisema Shenaiza na kuendelea kupiga kelele, muda mfupi
baadaye, mlango wa chumba chake ukafunguliwa, wakaingia wanawake wawili ambao
walikuwa wamefanana naye, wakamshika huku na kule na kuanza kumuuliza
kilichotokea.
“Umepatwa na nini?”
“Nimetokewa na mzimu.”
“Mzimu? Mzimu gani wakati sasa hivi ni
mchana?”
“Nilikuwa nimelala nikatokewa na mzimu
wa marehemu Jamal!”
“Mh! Au unaanza kuchanganyikiwa
mwenzetu? Jamal gani unayemzungumzia?”
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment