ILIPOISHIA:
Harakaharaka, huku akilia, aliwaita
walinzi ambao nao walimuita daktari wa familia hiyo, muda mfupi baadaye wote
wakawa wamejaa ndani ya chumba hicho wakijaribu kuokoa maisha ya msichana huyo
lakini ilionesha kwamba tayari walikuwa wamechelewa.
SASA
ENDELEA...
Shenaiza
alikuwa akitapatapa, akirusharusha mikono na miguu, mapovu mengi
yaliyochanganyikana na damu yakimtoka mdomoni na puani, harakaharaka Shenaiza
alitolewa kwenye chumba alichokuwa amefungiwa na kulazwa juu ya kitanda cha
magurudumu, akakimbizwa kwa kasi mpaka nje na kupakizwa kwenye gari.
Muda
mfupi baadaye, gari lililombeba lilikuwa tayari lipo barabarani, likikimbia kwa
kasi kubwa, taa zote za mbele zikiwa zimewashwa huku yule daktari akiwa bize
kuhakikisha anaokoa maisha ya Shenaiza.
Japokuwa
baba wa msichana huyo mrembo hakuwepo nchini kwa muda huo, tayari taarifa
zilimfikia huko alikokuwa juu ya kilichomtokea binti yake.
Naye
akajikuta akichanganyikiwa mno kwani Shenaiza alikuwa mtu muhimu sana kwake.
Bila yeye, mambo yake mengi yangekwama, jambo ambalo hakuwa tayari kuona
linatokea. Muda hohuo aliwapigia simu wasaidizi wake na kuwaambia ni lazima
wafanye kila kinachowezekana kuhakikisha anapona.
Baada
ya kufikishwa hospitalini, harakaharaka Shenaiza alilazwa juu ya kitanda chenye
magurudumu, akakimbizwa kupelekwa kwenye wodi ya wagonjwa mahututi, madaktari
kadhaa, wakisaidiana na yule daktari wa familia, walianza kuhaha kuhakikisha
wanaokoa maisha ya msichana huyo.
***
“Lakini mimi sijafa Shenaiza, mimi niko
hai.”
“Ungekuwa hai ndiyo ungekuwa huku? Acha
kujidanganya Jamal!”
“Hapana sijafa! Mimi sijafa! Niko
haiii,” nilisema kwa sauti kubwa iliyofuatiwa na kilio.
“Sasa unalia nini Jamal? Kwani kufa ni
jambo la ajabu? Mbona mimi mwenyewe nimeamua kuyakatisha maisha yangu?”
“Hapana, mimi bado nina ndoto zangu
nyingi sana sijazitimiza maishani. Isitoshe umri wangu bado mdogo, familia
yangu haijafaidi matunda yangu hata kidogo, bado sijaoa wala sina mtoto hata
mmoja, itakuwaje nife?”
“Kwani wote wanaokufa wanapenda wenyewe kufa?
Usikufuru Jamal, inabidi umshukuru Mungu kwa kila kitu, naamini hakuna
kilichoharibika, si utakuwa hapa na mimi?”
“Hapana Shenaiza, hapanaaa!” nilizidi
kupingana naye, akazidi kuning’ang’aniza kwamba eti nilikuwa tayari nimekufa na
hilo halikuwa tatizo kubwa kwa sababu hata yeye aliamua mwenyewe kufa.
Bado akili yangu ilikuwa na maswali
mengi yaliyokosa majibu. Unajua mtihani ambao Mungu ametupa sisi wanadamu, ni
kushindwa kuelewa kinachotokea baada ya mtu kufa. Kama angekuwepo mtu hata
mmoja, ambaye angekuwa na uwezo wa kuelezea kwa ufasaha kinachotokea baada ya
mtu kufa, pengine angewasaidia sana binadamu kupunguza hofu ya kifo
inayowatesa.
Kwangu mimi hali ni tofauti, hata
sielewi nitumie maneno gani kuelezea kilichotokea lakini naamini kwamba ukiendelea
kunifuatilia msomaji wangu, utaelewa ni nini hasa kilichotokea na pengine
kitakusaidia na wewe kuweza kuyaelewa maisha na kifo katika upeo mpana zaidi,
pengine kuliko ulivyokuwa unafikiria mwanzo.
Bado mjadala mkubwa kati yangu na
Shenaiza, ulikuwa ni juu ya suala la kifo. Msichana huyo alikuwa akisisitiza
kwamba mimi na yeye tumekufa na ndiyo maana tulikuwa kule lakini mimi nikawa
naendelea kumbishia kwamba sijafa kwa sababu bado nilikuwa na akili zangu
timamu.
Nilikuwa naelewa vizuri kila kilichokuwa
kinaendelea, jambo ambalo bado hakuna ushahidi wa kutosha kwamba wafu huwa
wanaelewa kinachoendelea. Nitakuja kulifafanua hili zaidi hapo baadaye.
Basi ile safari ambayo hata sijui mwisho
wake ulikuwa ni wapi, iliendelea, treni lilizidi kuchanja mbuga, moshi ukazidi
kuongezeka mle ndani sambamba na kelele za vyuma kugongana. Hata hivyo, bado
niliweza kumsikia vizuri Shenaiza kwa kila alichokuwa anakizungumza.
Bado nilikuwa na hamu ya kutaka kujua ni
nini kilichotokea mpaka na yeye aseme amekufa kwa sababu mpaka muda huo, bado
nilikuwa gizani. Nilifumba macho na kujaribu kuvuta picha kwa nguvu, nikashtuka
kuliko kawaida kujikuta nimetokezea kwenye wodi nyingine tofauti na ile ambayo
mwili wangu ulikuwepo.
Nilipotazama vizuri ndani ya wodi hiyo,
kama ilivyokuwa mwanzo kule kwenye ile wodi niliyokuwa nimelazwa, madaktari
wengi walikuwa wakihangaika kuokoa maisha ya mtu aliyekuwa amelala juu ya
kitanda, akionesha kabisa kwamba alikuwa kwenye hatua za mwisho za uhai wake.
Nilipomtazama vizuri mtu huyo, hakuwa mwingine
bali Shenaiza ambaye sekunde chache zilizopita nilikuwa nimekaa naye kwenye
siti moja ya treni la ajabu. Ni hapo ndipo nilipoelewa kile alichokuwa
anakisema Shenaiza kwamba ameamua kuyakatisha maisha yake.
Madaktari walikuwa wakihangaika mno,
Shenaiza akaunganishwa kwenye mashine ya kumsaidia kupumua huku dripu nyingi
zikitiririka kwa kasi kuingia kwenye mishipa yake ya damu.
Kibaya zaidi, kadiri muda ulivyokuwa
unazidi kusonga mbele ndivyo mashine maalum ya kusoma mapigo ya moyo aliyokuwa
ameunganishiwa msichana huyo na kuunganishwa kwenye kompyuta, ilivyokuwa
ikionesha kwamba mapigo yake ya moyo yalikuwa yakishuka kwa kasi kubwa, jambo
ambalo lilimaanisha kwamba muda mfupi baadaye, mapigo ya moyo yatasimama kabisa
na kukata roho.
“Hapana! Hapana... Shenaiza noooo!”
nilipiga kelele kwa sauti kubwa, nikajikuta muda huohuo nimehama kutoka kule
hospitalini mpaka ndani ya treni, nikageuka kumtazama Shenaiza, nikamuona akiwa
amejikunyata na kujiinamia, kama anayesubiri jambo fulani litokee.
Sijui nilipata wapi nguvu lakini
nilijikuta nikimshika Shenaiza na kuanza kumtingisha kwa nguvu, akashtuka kwa
nguvu na kunitolea macho akionesha kukasirishwa na kitendo changu cha kumshtua.
Wakati ananitazama, alianza kupiga
chafya mfululizo, akili yangu ilihama tena na kurudi wodini, nikapigwa na
butwaa baada ya kumuona mgonjwa akipiga chafya mfululizo huku damu ikimtoka
puani na mdomoni kwa mabongemabonge!
“She is back into her consciousness! Ooh
thanks God! She was almost dead!” (Amerejewa na fahamu zake! Ooh ahsante Mungu,
alishafikia hatua ya kufa) nilimsikia daktari mmoja akipaza sauti mle wodini,
nikaona nyuso za wote waliokuwemo ndani ya wodi hiyo ya wagonjwa mahututi
zikianza kuonesha matumaini makubwa, tofauti kabisa na mwanzo.
Harakaharaka Shenaiza alizungukwa pale
kitandani, kazi ya kunusuru maisha yake ikazidi kupamba moto. Nikiwa naendelea
kushangaashangaa, nilishtuka nikiguswa begani, akili zangu zikarudi tena kule
kwenye treni.
“Kwa nini umeniokoa? Ungeniacha nife,”
alisema Shenaiza huku akilia, nikatanua mikono yangu kama ishara ya
kumkumbatia, akajilaza kifuani kwangu na kunikumbatia kwa nguvu huku akiendelea
kulia.
Nikiwa katika hali ileile, nilishtuka
muda mfupi baadaye na kujikuta nikiwa nimejikumbatia mwenyewe. Shenaiza
hakuwepo tena, nikageuka huku na kule, hakukuwa na mtu mwingine yeyote kwenye
lile treni, nilibaki peke yangu huku mwanga wa ile taa iliyokuwa ndani ya
behewa nililokaa ukizidi kufifia, muda mfupi baadaye giza nene likatanda kila
mahali.
“Jamal! Jamal! Jamal!” nilishtuka baada
ya kuisikia tena ile sauti nzito ya kutetemeka, iliyoniita kwa mara ya kwanza
kabisa, ikiniita tena, ikafuatiwa na vicheko vya kutisha vya watu wengi, nikawa
nageuka huku na kule lakini sikuona chochote zaidi ya giza nene, hofu kubwa
ikatanda moyoni mwangu.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment