ILIPOISHIA:
Bado sikuwa na majibu na hakukuwa na mtu
yeyote wa kunijibu zaidi ya baba mwenyewe. Jambo kubwa ambalo lilikuwa
likijirudia ndani ya kichwa changu, lilikuwa ni je, kweli baba ni mchawi?
“Unasemaje?” nilisikia sauti ya baba
akiniuliza kwa ukali, nikageuka huku na kule lakini baba hakuwepo.
SASA ENDELEA...
“Sijaongea kitu,” nilijibu, nikasikia
baba akiachia msonyo mrefu kisha ukimya ukatawala. Kumbe nilipotamka lile neno
‘sijaongea kitu’, niliongea kwa sauti kubwa kiasi cha kuwafanya abiria wengi
ndani ya basi, wanisikie.
“Kaka, unaongea na nani?” sauti ya
msichana aliyekuwa akicheka kwa sauti ilisikika, ikifuatiwa na abiria wengine,
ndiyo iliyonizindua kutoka kwenye lindi la mawazo. Nikashtuka na kukaa vizuri
kwenye siti yangu.
“Anaogopa ajali huyo,” alipaza sauti
abiria mwingine, watu karibu wote kwenye basi wakacheka. Nilimgeukia mama,
nikamuona yeye yupo siriasi tofauti na abiria wengine, nikageuka na kukaa
vizuri kwenye siti yangu.
Yule msichana aliyekuwa amekaa siti ya
upande wa pili na pale nilipokuwa nimekaa, alivua ‘headphones’ zake, akawa
anaendelea kunitazama huku tabasamu pana likiwa limechanua kwenye uso wake.
Tangu tunaanza safari wala sikuwa najua
kwamba kuna mtu kama yeye ndani ya gari, ni mpaka pale alianza kunicheka ndipo
nilipoanza kumtilia maanani. Alikuwa ni msichana mdogo lakini wa kisasa, akiwa
na simu ya kisasa mkononi, halafu akiwa amevalia mavazi kama wasichana wa mjini
ambao nilizoea kuwaona kwenye TV.
Nilipoendelea kumtazama kwa macho ya
kuibia, niligundua kwamba alikuwa na sura nzuri sana halafu akitabasamu kuna
vishimo kwenye mashavu yake vinajitokeza, nikajikuta navutiwa kumtazama.
Safari iliendelea lakini mara kwa mara
yule msichana alikuwa akinigeukia na kunitazama, tofauti na mara ya kwanza
ambapo alikuwa kama anacheka kwa kunidharau, safari hii alikuwa akinitazama kwa
makini.
Katika ujanja wangu wote niliokuwa
nikiuonesha kijijini kwetu, makongorosi, Chunya, hakuna kitu nilichokuwa
nakiogopa kama kuzungumza au kujichanganya kwa namna yoyote na wasichana, hasa
wa rika langu.
Tangu naanza kupevuka, mpaka namaliza
shule ya msingi na hata baada ya kuanza maisha ya mtaani, sikuwahi kuwa na
mazoea na msichana yeyote, zaidi ya dada zangu kwa hiyo kitendo cha msichana
huyo kuwa ananitazama mara kwa mara, tena msichana mwenyewe mrembo kwelikweli,
kilinikosesha mno utulivu.
Kuna wakati nilikuwa natamani hata
nirudi kule kwenye siti yangu ya mwanzo, nilikokuwa nimekaa namama na ndugu
zangu lakini nilipofikiria kuhusu kazi nzito niliyopewa na baba, ilibidi
nijikaze kiume.
Nilipoona anazidi kunitazama, kuna
wakati nilifumba macho na kujifanya nimelala lakini nikasikia ile sauti ya
ajabu ya baba ikinijia, akaniambia sitakiwi kulala kwa sababu nina jukumu la
kuhakikisha safari inakuwa salama.
Nikawa sina cha kufanya zaidi ya
kujikaza kiume, safari hii na mimi niliamua kuwa namtazama. Kama kawaida yake,
alinigeukia, akawa ananitazama kwa makini, ikabidi na mimi nimgeukie, tukawa
tunatazamana. Cha ajabu, alipoona na mimi namtazama japo kwa uso uliojawa na
aibu, aliachia tabasamu pana.
Nikajikuta na mimi nikitabasamu, haraka
nikakwepesha macho yangu na kugeukia upande wa dirishani, nikawa natazama nje.
Safari iliendelea huku nikiendelea kujishtukia, baadaye nilipomgeukia tena yule
msichana, niligundua kwamba tayari alishalala huku headphones zake zikiwa
masikioni.
Nikashusha pumzi ndefu kama mtu aliyetua
mzigo mzito kichwani, nikakaa vizuri kwenye siti yangu na kuendelea nakazi
niliyopewa na baba. Kwa bahati nzuri, safari hii hakukuwa na kipingamizi
chochote, safari ikaendelea mpaka tulipofika sehemu maarufu iitwayo Chalinze
Choma Nyama.
Dereva alipunguza mwendo na kusimamisha
basi, akatutangazia abiria kwamba anatoa dakika kumi tukachimbe tena dawa na
kujinyoosha. Bila kupoteza muda, abiria walianza kuteremka, mimi nikageuka na
kutazama pale mama na wale ndugu zangu walipokuwa wamekaa, nikawaona nao
wakiinuka.
Ilibidi nisubiri abiria wengine wapite,
ndugu zangu walipokaribia, niliinuka na kuungana nao, tukawa tunataniana na kaka
na dada zangu kama kawaida yetu tunapokutana. Cha ajabu, eti nao walikuwa
wakinicheka kwamba woga wa kupata ajali ulisbabisha niwatie aibu kwa kupayuka
kwenye basi.
Wakawa wananicheka na kunisukumasukuma,
jambo ambalo sikupendezewa nalo. Tuliposhuka chini, waliendelea kunitania
lakini kwa kuwa sikuwa naupenda utani wao, niliamua kujitenga nao, nikazunguka
mpaka nyuma ya gari, nikasimama nikiegamia basi huku nikitazama kule
tulikotokea, uso wangu ukiwa umekosa amani.
“Hawa washenzi wangejua mimi na baba ndiyo
tuliowalinda wasipate ajali wasingekuwa wananicheka hivi,” nilisema huku
nikikumbuka pia vicheko vya abiria wengine ndani ya basi, muda ule nilipopayuka
kwa nguvu ndani ya basi.
Mawazo yangu yalizama kwenye hisia
chungu, nikawa naendelea kuwaza mambo mengi ndani ya kichwa changu. Ghafla
nilishtushwa na sauti ya kike pembeni yangu.
“Mambo!”
“Safi tu,” nilijibu huku nikianza
kujichekesha, aibu zikiwa zimenijaa baada ya kugundua kuwa ni yule msichana wa
kwenye basi aliyekuwa akinitazama sana.
“Mbona umekaa peke yako huku halafu
unaonekana kama una mawazo sana?”
“Ahh! Kawaida tu, nahisi uchovu wa
safari,” nilimjibu, huku lafudhi ya kijijini ikishindwa kujificha kwenye
mazungumzo yangu. Aliendelea kunipigisha stori za hapa na pale, akionesha
kuchangamka mno utafikiri tunafahamiana.
“Nisindikize kule upande wa pili
nikanunue soda za kopo, naona huku hakuna,” alisema msichana huyo ambaye
manukato yake mazuri aliyojipulizia, yalizifurahisha mno pua zangu.
Tulisimama pembeni ya barabara, akageuka
huku na kule kuangalia kama hakuna gari linalokuja, na mimi nikawa namfuatisha
kwa sababu sikuwa mzoefu sana wa barabara ya lami na sikuwa najua vizuri namna
ya kuvuka barabara. Alipohakikisha kwamba hakuna gari, alinishika mkono,
nadhani aliniona jinsi nilivyokuwa na hofu moyoni, tukaanza kuvuka.
Mikono yake ilikuwa laini mno kiasi
kwamba nilifurahia jinsialivyonishika. Kwa mara ya kwanza maishani mwangu,
nikaanza kuhisi hali isiyo ya kawaida. Tulivuka mpaka ng’ambo ya pili,
akafungua pochi yake ndogo na kutoa noti ya shilingi elfu kumi, akampa muuzaji
wa vinywaji aliyekuwa na kibanda chake pembeni ya barabara.
“Unakunywa soda gani?” aliniuliza huku
yeye akichukua soda yake, nikakosa cha kujibu zaidi ya kuanza kuchekacheka tu.
“Nakuchagulia, nataka unywe ninayokunywa
mimi,” alisema huku akinigeukia, akanipa soda ya Sprite ya kopo, akafungua ya
kwake na kuingiza mrija, mimi nikawa nashangaashangaa kwa sababu sikuwahi
kunywa soda ya kopo hata mara moja wala sikuwahi kutumia mrija.
Akiwa ameshapiga funda moja, alichukua
lile kopo la soda mikononimwangu, anaipa ile ambayo alishaifungua na kunywa
kidogo, nikawa namshangaa kwani hayo yalikuwa mambo mageni kabisa kwangu,
nilizoea kuyaona kwenye video.
Alifungua na ile nyingine, nayo akapiga
funda moja, nikawa sina cha kufanya zaidi ya kuendelea kunywa, akawa
ananitazama kwa macho yaliyobeba ujumbe mzito.
“Unaitwa nani?”
“Togo,” nilimjibu kwa kifupi, akageuka
kama anayetazama upande wa pili wa barabara, nikapata fursa ya kulisanifu
vizuri umbo lake. Alikuwa ni msichana mzuri sana, upande wa nyuma alikuwa
amejazia huku kiuno chake kikiwa kimegawanyika, kama nyigu ambao kule kijijini
tulikuwa tukiwaogopa kutokana na sumu yao wanapokung’ata.
Suruali ya jeans aliyovaa, ililifanya
umbo lake lijichonge vizuri, ghafla akageuka, akanibamba nikiwa namtazama kwa
nyuma, nikazidi kujisikia aibu.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment