ILIPOISHIA:
Baada ya kumjibu jambo lililonishitua zaidi ni pale
aliponiambia kuwa ilibainika Shenazia alikuwa ni mgonjwa aliyelazwa katika Hospitali
ya Amana siku iliyopita na kutoroshwa, hoja ya msingi ilikuwa mimi nilimtoa
wapi na utetezi wangu ni upi juu ya kuhusika kwenye tukio lililompata!
SONGA NAYO…
MACHO yalinitoka pima nikimtazama yule askari
aliyekuwa amekaa mbele yangu akinihoji maswali mfululizo huku akiwa amenikazia
macho. Nilijiuliza niseme nini hata askari huyo anielewe bila kupata majibu, ukweli
ni kwamba japo moyoni nilifahamu sikuwa kabisa na hatia katika kila kilichokuwa
kinaendelea juu ya Shenaiza lakini ilikuwa ni vigumu kuuelezea ulimwengu hata
ukaniamini kuwa nilichosema ndicho kilikuwa kweli.
Moyoni nilizidi kugubikwa na majuto, nilifahamu fika
hayo yote yaliyonitokea nilijitakia maana kama si ujinga wangu wa kumuamini
msichana ambaye sikuwa ninafahamiana naye zaidi ya kuwa na mawasiliano naye
kwenye simu nisingefika hapo nilipokuwa.
Huku hayo yote yakiendelea ndani ya akili yangu yule
askari alizidi kunisisitiza kujibu maswali aliyokuwa ananiuliza, machozi
yakinitiririka niliamua kufunguka kwa mara nyingine ukweli wote kuhusu mimi na
Sheneiza. Kuanzia tulivyoanza kuwasiliana na hata nilivyopata taarifa kuwa
amelazwa katika Hospitali ya Amana na yote yaliyoendelea baada ya hapo.
Askari yule alikuwa ananisikiliza kwa makini huku
akiandika kwenye kitabu chake kidogo (diary), nafkiri mambo muhimu kutoka
katika maelezo yangu niliyompa. Hakuacha kunihoji maswali kwa ajili ya kupata
uhakika kwa yale niliyokuwa ninamuelezea baada ya saa zima la mahojiana
alimuita askari polisi aliyekuwa zamu akamtaka kunirudisha nyuma ya nondo.
Siyo siri kila kitu ndani ya maisha yangu niliona
kuwa kilikuwa kimebadilika na kuwa kigeni mana hata siku moja sikuwahi kufikiri
ningeingia mahabusu hasa kwa sababu kama hiyo iliyonipeleka wakati huo.
Nikiwa katika
chumba hicho cha mahabusu machozi yalikuwa yanazidi kunibubujika mfururizo. Tofauti na mawazo niliyokuwa nayo hali halisi ilikuwa inatisha, hakukuwa na hewa
ya kutosha maana kidirisha pekee kilichokuwepo katika chumba hicho kilikuwa
kidogo na kilikuwa juu, kila mmoja alikuwa anagombania aweze kupata hewa kwa
kuwa karibu na dirisha.
“Eee Mungu, naomba uniokoe katika mtihani huu, ni mkubwa
sana kwangu, nashindwa kuhimili, onyesha miujiza yako ili maisha yangu
yasiishie pabaya,” niliwaza huku machozi yakiendelea kunibubujika.
“Wewe vipi mbona unalialia, humu kiumeni unatakiwa
kujikaza,” nilisikia sauti ikiniambia kutoka pembeni yangu.
“Mtoto wa mama huyu, humu ndiyo ubayani, hakuna baba
wala mama, suipojikaza utaolewa,” alisema mtu mwingine.
Niligeuza uso wangu na kuwatazama kwa zamu hao waliokuwa
wanazungumza, wote walionekana kuwa watu wa miraba minne tena wenye makovu
mengi usoni, macho yangu yaliganda kwao kwa sekunde kadhaa kisha nikayatoa bila
kujibu neno lolote lile.
Saa zikazidi kusonga mbele kwa tabu sana upande
wangu nikiwa ndani ya chumba hicho cha mahabusu, majira ya mchana rafiki yangu
Justice na Raya walifika katika kituo hicho cha polisi kufanya mipango ili
niweze kuachiwa kwa dhamana.
Lakini suala hilo lilionekana kuwa bado gumu sana,
polisi hawakuhitaji kabisa kuwasikiliza maana hata pale walipojaribu kuuzunguka
mbuyu kwa kuhonga pesa kwa baadhi ya askari wenye nguvu ili angalau nitoke nje
kwa dhamana huku upelelezi ukiendelea waliambiwa wasiwe na haraka kwanza maana
ishu yenyewe haikuwa ndogo.
Waliambiwa wapelelezi walikuwa wameivalia njuga kesi
hiyo na suala la muhimu kama kweli nilikuwa sihusiki katika mipango ya kumuua
Sheneiza ilikuwa ni kusali kwa nguvu zote ili msichana huyo aweze kupata nafuu
hata azungumze ukweli mzima wa nini kilimtokea mpaka akawa anaandamwa na watu
waliokuwa wanataka kupoteza maisha yake.
Rafiki zangu hawakuwa na namna ya kulazimisha kama
walivyokuwa wanataka wao, walichofanya ilikuwa ni kuomba ruhusa ya kuzungumza
na mimi japo kwa dakika chache tu. Kwa kuwa kuna chochote walikuwa
wamekwishapenyeza kwa askari hao hilo halikuwa suala gumu sana, waliruhusiwa,
nikatolewa mahabusu na kwenda kuzungumza nao.
“Haya yote yatakwisha, hutakiwi kujali kabisa baba, jipe
moyo kila kitu kitakuwa sawa,” Raya aliniambia huku machozi yanambubujika kwa
wingi.
“Asante Raya, ninaamini hivyo pia, Mungu
atanisimamia na kila kitu kitakwenda sawa.” Nilimjibu.
“Hapa kaka ni muhimu kuomba kwa nguvu zote huyo
mgonjwa maendeleo yake yawe mazuri ili aeleze ukweli mzima wa nini kimetokea,
hicho pekee ndicho kinachoweza kukutoa kwenye hii hatia,” Justice aliniambia.
“Ndivyo askari walivyosema?”
“Ndiyo, mimi pia ninaunga mkono suala hilo maana
hakuna njia nyingine ya kukunusuru.”
“Dah! Kwani
Sheneiza amelazwa wapi?” Nilimuuliza Justice swali lingine.
“Yuko Mwananyamala hospitali lakini sijafahamu
amelazwa katika wodi namba ngapi.”
“Fuatilia kaka ufahamu pia na maendeleo yake maana
huyo ndiyo kila kitu kwenye hili suala kama unavyosema. Lakini kuna kitu pia
nilikuwa ninakifikiria ambacho tunaweza kuzungumza na askari polisi wazidishe
ulinzi katika hospitali hiyo kutokana na hali halisi, hao watu wanaotaka kumuua
wakigundua kuwa bado ni mzima lazima wataendelea kumuandama.”
“Hilo ni kweli kaka, niachie mimi, nitazungumza na
mkuu wa kituo maana ni mtu mzuri, ametupokea vyema mimi na Raya.”
Baada ya kuzungumza mawili matatu na rafiki zangu
hao ambao walionekana kuniunga mkono kwa kiasi kikubwa ikiwa ni pamoja na kunifariji
katika matatizo yangu hayo yaliyokuwa yananisonga, nilirudishwa mahabusu na wao
walikwenda kama tulivyozungumza kwa mkuu wa kituo na kumwambia juu ya kuongeza
ulinzi kwenye Hospitali ya Mwananyamala.
Hatimaye siku hiyo ilimalizika nikiwa ndani ya kituo
hicho cha polisi, siku iliyofuata majira ya asubuhi Raya alikuwa kituoni hapo
kwa ajili ya kuniletea kifungua kinywa. Ukweli ni kwamba hakuna wakati
niliyomuona Raya kuwa ni mtu wa muhimu kwangu kama wakati huo nilipopata
matatizo.
Huko nyuma nilikuwa mtu wa kumchukulia poa sana kwa
vitendo vyake vya kuonyesha kuwa ananipenda lakini wakati huo thamani yake
niliiona na niliamini kweli mwanamke huyo alikuwa ananipenda kwa dhati.
Baadaye Raya aliondoka na mimi niliendelea kukaa kwenye
chumba kile cha mahabusu ambapo mchana nikiwa sina hili wala lile nilishituka
baada ya kumuona askari polisi akija kwenye nondo na kuita jina langu,
nilipoitika alinichukua mpaka mapokezi nikapewa nguo zangu na kuambiwa nivae,
baada ya kuvaa akanitaka nimfuate kuelekea nje, nilifanya hivyo na tulipoanza
tu kutoka nje askari wengine watatu walioshika mtutu wa bunduki mkononi
walitufuata nyuma tukaenda kuingia pamoja kwenye difenda.
Difenda hilo liliwashwa na kuanza kuelekea mahali
ambapo sikuweza kupafahamu kwa mara moja, nilikaa kimya katikati ya askari hao
bila kuzungumza neno lolote lile na safari ikazidi kupamba moto. Nilikuja
kugundua kuwa huenda tunaelekea Mwananyamala Hospitali baada ya kuumaliza Mtaa
wa Makumbusho na kushika barabara ya Mwananyamala, moyoni nilianza kugubikwa na
maswali mengi, nilijiuliza kama ni kweli ninapelekwa katika hospitali hiyo
ilikuwa ni kufanya nini?
Je, nini kitaendelea kwenye simulizi hii? Usikose next
issue!
No comments:
Post a Comment