ILIPOISHIA:
Alipofikisha tatu, nilifumba macho,
nikashtukia ghafla tumehama pale tulipokuwa na kwenda upande wa pili, kule
barabarani ambako watu wengi walikuwa wamesimama wakishangaa, tukajichanganya
na wale watu.
“Hebu angalia wanachokishangaa,” alisema
huku akinitaka nitazame pale tulipokuwa tumekaa awali. Macho yalinitoka nikiwa
ni kama siamini.
SASA ENDELEA...
Watu wawili, mmoja akionesha kuwa
mwanamke na mwingine mwanaume, wakiwa watupu kabisa huku miili yao iking’aa
sana, walikuwa wamekaa kwenye msingi wa nyumba, wakiwa wanazungumza. Macho ya
kila mmoja yalikuwa yaking’aa sana na nyuso zao zilikuwa na gizagiza fulani
ambalo lilifanya iwe vigumu kwa watu kuwatambua sura zao.
“Hivi ndivyo tulivyokuwa tukionekana
ndiyo maana unaona hawa watu wote wamekusanyika hapa,” alisema Isri huku
akiniegamia.
Nilibaki nimepigwa na butwaa huku
nikiwatazama wale watu ambao wala hawakuwa na taarifa kwamba tulikuwa
tumeshajichanganya nao. Nilitamani kumuuliza Isri kwamba sasa iweje wale watu
wawe wanaendelea kutuona wakati tulishahama na kujichanganya nao? Kabla hata
sijamjibu, ni kama alizisoma hisia zangu, akaniambia kile walichokuwa
wakiendelea kukiona, ilikuwa ni kiini macho.
Akaniambia kwamba watu wengi hawajui
lakini hakuna jambo la hatari kama kusimama usiku na kuanza kutazama vitu
usivyovijua au visivyo vya kawaida kwa sababu kama ni watu wenye nia ovu,
unapowatazama tu wanajua kwamba unawatazama na wanao uwezo wa kubadilisha kile
unachokiona wewe na kukuonesha kitu cha tofauti kabisa.
Akaniambia ndiyo maana baadhi ya watu
hupata matatizo makubwa sana baada ya kuona majini usiku, wengine huona watu
warefu wenye kwato, wengine huona miti ikibadilika au huona viumbe vya ajabu
wakati kiukweli ni kwamba wanakuwa wamewaona wachawi wakiwa kwenye maumbo yao
ya kawaida lakini kwa kuwa wachawi nao wanakuwa wameshagundua kwamba
wanatazamwa, wanawafanyia kusudi.
“Sijaelewa, kwa hiyo unamaanisha hata
mimi na wewe ni wachawi?”
“Sijamaanisha hivyo.”
“Kwani wewe ulijua kwamba wanatutazama?”
“Ndiyo nilijua,” alinijibu Isri na
kunifanya nipigwe na mshangao mkubwa. Watu walikuwa wakizidi kuongezeka na
wengi walikuwa ni walinzi wa maeneo ya jirani na pale, wengine wakiwa ni
Wamasai na wengine wakiwa ni wafanyabiashara wanaodamka alfajiri na mapema kuwahi
kuchukua bidhaa zao.
“Sasa mbona wanazidi kuongezeka,
itakuwaje? Ina maana hapa hawatusikii wala hawatuoni?” nilimuuliza, akatingisha
kichwa kuonesha kukubali, akaniambia ipo namna ya kuwatawanya. Aliposema hivyo
tu, mara nilishangaa wale watu ambao watu wote walikuwa wakiwatazama,
wakibadilika na kuwa mbwa wawili wakubwa, dume na jike.
Wakaanza kubweka kwa hasira na kuanza
kutimua mbio kulifuata lile kundi la watu. Kiukweli kwa jinsi mbwa hao
walivyokuwa wakubwa, wenye hasira huku meno yao makali yakiwa yametoka nje,
hata mimi mwenyewe nilijikuta nikiogopa mno. Kufumba na kufumbua, kundi lote
lilianza kutimua mbio, kila mmoja kivyake.
Na mimi nilitaka kukimbia lakini Isri
alinikamata mkono kwa nguvu, wale mbwa wakawa wanazidi kuja kwa kasi, ikabidi
nisimame nyuma yake. Watu walizidi kutimua mbio huku wakipiga kelele na ghafla
tukasikia breki kali za gari zikifuatiwa na kishindo kikubwa.
“Tayari!” alisema Isri lakini sikumtilia
maanani, akili zangu zote zikawa kwa wale mbwa. Cha ajabu, japokuwa sisi tulikuwa
tumesimama, walitupita kwa kasi kubwa na kuendelea kuwatimua wale watu.
“Tayari huko,” alisema Isri kwa mara
nyingine, ikabidi nimuulize tayari nini? Akaniambia twende tukajionee wenyewe.
Yeye alitangulia, mimi nikawa namfuata, tukanyoosha na ile barabara ya lami
mpaka mahali palipokuwa na njia panda, akanionesha kwa kidole nitazame
mwenyewe.
Gari dogo aina ya Toyota Carina lilikuwa
limeacha njia na kugonga kingo za daraja na kuingia mtaroni, huku barabarani
kukiwa na mtu amelala huku damu nyingi zikimtoka akionekana amegongwa na gari
lile.
“Mungu wangu,” nilisema kwa mshtuko,
akaniambia mtu huyo alikuwa miongoni mwa wale waliokuwa pale wakitushangaa na
wakati akiwakimbia wale mbwa ndipo akaingia barabarani bila kutazama, hali
iliyosababisha agongwe na gari hilo kisha na lenyewe likapoteza mwelekeo na
kugonga kingo za barabara.
Yaani kwa jinsi Isri alivyokuwa
akizungumza kirahisirahisi, ungeweza kudhani anasimulia stori au anazungumza
masihara, alikuwa anarahisisha sana mambo hali ambayo ilinifanya nigeuke na
kumtazama usoni.
Nilishtuka sana nilipomtazama usoni,
macho yake yalikuwa yamebadilika rangi na kuwa mekundu sana na kung’aa huku
kwenye kingo za mdomo wake kukiwa kama na michuruziko ya damu, meno makali kama
ya wale mbwa yakiwa yametokea kila upande.
Mshtuko nilioupata ulikuwa hauelezeki,
nikahisi na mimi nipo kwenye mtego mbaya wa kifo, sikusubiri chochote,
nilikurupuka na kuanza kutimua mbio kwa kasi kubwa nikiwa hata sielewi naelekea
wapi.
“Togo! Togo rudi nakwambia, ohooo!”
alisema kwa sauti kali ya kutisha lakini wala sikuvijali vitisho vyake. Jambo
ambalo najisifia, ni uwezo mkubwa wa kutimua mbio. Unajua maisha ya kule
kijijini tuliyokulia, ilikuwa ni lazima tu ujifunze kukimbia kwa kasi kubwa,
kwani kinyume na hapo usingeweza kuambulia chochote mnapoenda kuwinda wanyama
wa porini.
Nilikimbia kisawasawa, dakika chache
baadaye nikawa nimeshafika mbali kabisa, nikatokezea kwenye barabara kubwa ya
lami ambayo japokuwa ilikuwa ni usiku, yenyewe ilikuwa na magari mengi
yakiendelea kupita, hasa makubwa ya mizigo.
Kiukweli nilikuwa mgeni kabisa na jiji
lakini niliona ni bora nipotee kuliko kuendelea kukaa karibu na Isri. Japokuwa
alikuwa amenieleza mambo mengi kuhusu yeye, yale mambo aliyoyafanya dakika za
mwisho, ikiwemo kuwabadilisha wale watu kuwa mbwa, jinsi alivyokuwa akichekelea
ile ajali iliyosababisha maafa makubwa na jinsi alivyobadilika na kuwa kama
mnyama mkali wa porini, yalinifanya nimuogope mno.
Nikawa naendelea kukimbia pembezoni mwa
barabara nikiwa hata sijui naelekea wapi. Kwa mbali kulianza kupambazuka,
nikaanza kuona watu wachache wakifanya mazoezi ya kukimbia pembeni ya barabara.
Niliamini hao ndiyo wanaoweza kunisaidia
uelekeo wa kufika nyumbani kabla hakujapambazuka kabisa.
Cha ajabu, kila nilipokuwa nikimkaribia
mtu yeyote anayefanya mazoezi, alikuwa akitimua mbio za ajabu kunikwepa,
mwingine almanusra agongwe na gari kwani alikuwa akija kwa mbele, na mimi
nikawa nakimbia taratibu huku nikionesha dalili za kutaka kusimama ili nimuulize
lakini ghafla aliponiona, alipiga kelele na kuvuka barabara kwa kasi kubwa
mpaka upande wa pili bila hata kutazama, lori kubwa likapiga honi kali na
dereva akakata kona kali kumkwepa.
Ilibidi nisimame na kujitazama mwilini
kwa nini watu wananikimbia. Jambo la kwanza ambalo lilinishtua, kumbe kwa muda
wote huo nilikuwa nikikimbia kwa kutumia mikono na miguu, hata sijui kwa nini
muda wote huo sikujishtukia, harakaharaka nikainuka na kusimama kwa kutumia
miguu.
Nilipojitazama mwilini, nilishtuka mno
kugundua kwamba kumbe nilikuwa na manyoya mengi kama mnyama wa porini,
nilipojitazama mikono, nilizidi kupagawa baada ya kugundua kuwa kumbe mikono
yangu ilikuwa imebadilika na kuwa kama ya mbwa.
Mara nilishtukia jiwe kubwa likirushwa
na kunikosakosa, kabla sijatulia nikashtukia jiwe lingine likinikosakosa,
nikaona naweza kuuawa bure, nikaanza kutimua mbio lakini nilipojaribu kukimbia
kwa miguu nilijikuta nikishindwa, ikabidi nijaribu kutumia na mikono, nikaweza
na kasi ilikuwa kubwa zaidi. Nilikimbia sana huku nikilia nikiwa sielewi nini
itakuwa hatma yangu.
Ni hapo nilipogundua kwamba kumbe Isri
alikuwa amenigeuza umbo langu na kuwa kama mbwa mkubwa, nilimlaani sana moyoni
mwangu na kujikuta nikiyakumbuka maneno ya baba ambaye mara kwa mara alikuwa
akinionya kuhusu msichana huyo.
Nikiwa naendelea kukimbia, nilishtukia
mtu mmoja akija kwa kasi kubwa nyuma yangu, nikazidi kuongeza kasi lakini kabla
sijafika mbali nilishtukia kamba nene ilipita shingoni mwangu na kunifunga
kitanzi, nikadondoka chini kama mzigo.
Nikiwa bado hata sijui nini cha kufanya,
nilishtukia nikifungwa mikono na miguu, nikajaribu kukurupuka lakini sikuweza
kufanya chochote, ikabidi nitulie na kuanza kumtazama ni nani aliyenifanyia
kitendo hicho na alikuwa na lengo gani kwangu maana niliona kifo changu kikiwa
kimewadia. Na hata kama ningeuawa, kila mtu angeamini aliyekufa ni mbwa mkubwa.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment