ILIPOSHIA:
Mpaka muda huo nilikuwa
nimeshindwa kabisa kujizuia nisiendelee kuporomokea kule chini, kwa mbali
nikaanza kuliona shimo kubwa ambalo ukubwa wake hata sijui nifananishe na nini
lakini kwa kifupi lilikuwa kubwa mno, lisilo na mwisho, moto mkali ukiwa
unawaka ndani yake. Kibaya zaidi, na mimi nilikuwa nikiendelea kuporomoka
kuelekea ndani ya shimo hilo, nikajua huo ndiyo mwisho wangu.
SASA ENDELEA...
“Jamal!
Jamal! Don’t go my love, come back to me! Come back Jamal,” (Jamal! Jamal!
Usiende mpenzi wangu, rudi kwangu! Rudi kwangu Jamal) wakati nikiendelea
kuporomokea kule kwenye lile shimo kubwa lililokuwa na moto mkali ambao siwezi
kuuelezea, nilisikia sauti ikiniita.
Tofauti
na sauti za kutishatisha nilizokuwa nikizisikia, hii ilionesha dhahiri kwamba
siyo ngeni masikioni mwangu. Ilikuwa ni sauti ambayo niliitambua kuwa ni ya
Raya, msichana aliyetokea kunipenda kwa moyo wake wote.
Raya
alikuwa akipaza sauti huku akilia, maneno aliyokuwa akiniambia yalinichoma sana
moyoni mwangu.
Katika
hali ambayo sijui niielezeeje, nilijikuta nikipata nguvu kubwa kutoka ndani,
nikajipindua kwa nguvu na kujikuta ile kasi ya kuporomokea kule chini
inapungua, nikazidi kufurukuta kupambana na ile nguvu kubwa iliyokuwa inanivuta
na hatimaye nikajikuta nikiangukia sehemu nyingine tofauti kabisa na kule
nilikokuwa nikielekea.
Pale
nilipoangukia, palikuwa na unyevunyevu mkubwa chini utafikiri nimekanyaga
matope lakini giza lilikuwa nene pengine hata kule nilikotoka, nikawa naangaza
macho huku na kule lakini sikuweza kuona chochote. Ukimya wa ajabu ukatanda
kiasi cha kunifanya nianze kuyasikia mapigo ya moyo wangu yalivyokuwa
yakinidunda.
Kufumba
na kufumbua, nilijikuta nimerudi pale nilipokuwepo mwanzoni kabisa, kwenye kona
ya ile wodi niliyolazwa. Kama ilivyokuwa mwanzo, nilikuwa nauona mwili wangu
ukiwa umelazwa pale kitandani lakini tofauti na awali, safari hii nilikuta
ubize mle ndani ya wodi ukiwa umeongezeka sana.
Madaktari
walikuwa wakipigana vikumbo, kila nesi alikuwa bize kuhakikisha anaokoa maisha
yangu. Sikuelewa nini kimetokea mpaka ubize uongezeke kiasi kile lakini
niliwasikia baadhi ya madaktari wakijadiliana kwamba kilichonitokea kilikuwa
kitu adimu sana.
“His
heartbeats almost stopped but now they are stabilizing, ooh my God he was
dead!” (Mapigo ya moyo wake yalisimama kabisa lakini sasa naona yameanza kurudi
kwenye hali yake ya kawaida, ooh Mungu wangu, alikuwa tayari amekufa).
“It’s
my eleventh year in this career and I have never witnessed something like this,”
(Huu ni mwaka wangu wa kumi na moja nafanya kazi hii, sijawahi kushuhudia tukio
kama hili) alisema daktari mmoja, kila mtu akawa anaendelea kuzungumza lake.
Bado
niliendelea kujiuliza maswali mengi bila majibu lakini kwa jinsi mazungumzo
hayo yalivyokuwa yakiendelea, inaonesha nilikuwa nimetokewa na jambo baya sana.
Nikiwa bado palepale kwenye kona ya ile wodi, nikiangalia kila kilichokuwa
kinaendelea mle ndani, niliisikia tena ile sauti niliyoisikia muda mfupi
uliopita, tena ikizungumza maneno yaleyale.
“Jamal! Jamal! Don’t go my love, come
back to me! Come back Jamal,” (Jamal! Jamal! Usiende mpenzi wangu, rudi kwangu!
Rudi kwangu Jamal).
Ilikuwa ni sauti ya Raya na ilionesha
ikitokea nje ya ile wodi. Nilijikuta nikiwa na shauku ya kutaka kumuona Raya,
ile kuwaza tu kwamba nataka kumuona, nilijikuta tayari namtazama lakini katika
mazingira ambayo yalionesha kwamba yeye pamoja na watu wengine wote waliokuwa
wamemzunguka, hawakuwa na taarifa juu ya uwepo wangu mahali pale.
“Jamal is dead! (Jamal amekufa) Nitakuwa
mgeni wa nani mimii? Eeeh Mungu, kwa nini mimi? Why?”
“Raya ukilia sana unakufuru. Wewe unajua
jinsi Jamal alivyo rafiki yangu kipenzi lakini mwenzio bado sitaki kuamini kama
ni kweli ametangulia mbele za haki. Hebu jikaze, tunaweza kuwa tunamchulia akafa
kweli.”
“Usinipe moyo Justice, wote tumeshuhudia
mashine ya kusoma mapigo yake ya moyo ikishuka mpaka mwisho kuonesha kwamba
mapigo yake ya moyo yamesimama, madaktari wamefanya kila kitu na kujiridhisha
kwamba amekufa, ina maana huamini tu?”
“Angekuwa ameshakufa angezungushiwa
shuka la kijani pale kitandani kwake na madaktari wote ungeona wameshatoka
chumba cha wagonjwa mahututi, mimi naamini bado yupo hai,” Justice na Raya
walikuwa wakizungumza pale nje, Raya akilia kwa uchungu huku wafanyakazi wenzao
kadhaa pamoja na watu wengine, wakisaidiana kumtuliza msichana huyo.
Pembeni kulikuwa na kundi lingine la watu
ambao siwafahamu vizuri, lakini nao walionesha kufika pale kwa sababu yangu,
muda mwingi wakawa wanajadiliana huku wakiwatazama akina Raya.
Niliwaona pia waandishi wawili wa
habari, mmoja nadhani alikuwa anatoka kwenye kituo cha runinga na mwingine wa
magazeti. Niliwatambua hivyo kutokana na jinsi walivyokuwa wamevaa na zana za
kazi ambazo kila mmoja alikuwa amebeba. Nilijaribu kuangaza huku na kule
kuangalia kama nitamuona Shenaiza lakini hakuwepo eneo hilo.
Nilitamani sana kujua ukweli wa mambo
yote ambayo Shenaiza alikuwa akinificha lakini sikujua nitaanzia wapi. Yeye
ndiye aliyekuwa chanzo cha matatizo yote yaliyonitokea lakini cha ajabu ni
kwamba hata mimi, muathirika namba moja wa mambo yote yale yaliyokuwa
yakiendelea kutokea, nilikuwa sielewi hasa nini kilichojificha nyuma ya pazia.
Kwa tafsiri nyepesi nyepesi, kama Mungu
angeamua kunichukua moja kwa moja, ningeacha maswali mengi sana ambayo hakuna
mtu yeyote ambaye angeweza kuyajibu, zaidi ya Shenaiza mwenyewe. Hali ilikuwa
ya simanzi kubwa pale nje ya hospitali, niliwaona watu wengine wakizungumza na
simu, kila mmoja akilitaja jina langu.
Maneno mengi yalikuwa yakiendelea
kumtoka Raya, akiendelea kulia kwa uchungu kiasi cha kufikia hatua ya kukufuru.
Kwa juujuu tu, kupitia maelezo yake pamoja na yale niliyoyasikia kule ndani kwa
madaktari, nilielewa kilichokuwa kimetokea.
Ilionesha kwamba, kuna muda mapigo ya
moyo wangu yalisimama, kwa tafsiri nyepesi, kuna muda nilikufa! Lilikuwa ni jambo
la ajabu ambalo lilinitisha sana. Sikuelewa ni muda gani nilikuwa nimekufa kwa
sababu muda wote nilikuwa timamu na nilikuwa naelewa kila kilichokuwa
kinaendelea.
Sikukumbuka muda ambao pengine
nilipoteza fahamu au sikuwa naelewa kinachoendelea! Nasisitiza tena, muda wote
nilikuwa na akili zangu timamu. Nilijisikia uchungu sana kwa jinsi Raya
alivyokuwa akilia, ukichanganya na hofu kubwa niliyokuwa nayo, nilijikuta
nikianza kutokwa na machozi. Ajabu ni kwamba, wakati mimi nikiendelea kulia,
wale madaktari pale kitandani walishtuka baada ya kuona mwili wangu nao
ukitokwa na machozi, wakawa wanatazamana. Nikiwa naendelea kulia, nilipaliwa na
mate, hali iliyofanya nikohoe mfululizo, ajabu zaidi, na ule mwili wangu pale
kitandani ukakohoa, madaktari wakazidi kupigwa na butwaa, wakawa wanatazamana
wakiwa ni kama hawaamini kilichokuwa kinatokea.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment