ILIPOISHIA:
“UNASEMA?” Mama yake Rahma aliuliza kwa
mshtuko, huku akiacha kila kitu
alichokuwa akifanya. Haraka akakimbilia chumbani kwa mwanaye huku akionyesha
wasawasi mkubwa moyoni mwake, mama naye akamfuata, na mimi uzalendo
ukanishinda, nikainuka na kuwafuata.
SONGA
MBELE...
TULIPOINGIA chumbani, mama yake Rahma akaanza
kumuamsha kwa kumwita lakini hakuitika wala kutikisika, akasema; “mwanangu
umepatwa na nini?” Hata hivyo, Rahma hakuitika wala kufumbua macho, jambo hilo
lilitushtua sana, mama naye alipojaribu kumwita hali ikawa vilevile, Rahma
alitulia kimya.
Sikukubaliana na hali hiyo, nilijongea
kitandani alipolala Rahma, nikamshika begani na kuanza kumtikisa huku nikimwita,
kama ilivyokuwa kwa mama yake na mama, kipenzi changu Rahma hakuitika.
Kilichofuatia ni kila mmoja wetu kuanza kulia kwani tulijua alikuwa ametutoka,
kufuatia vilio vyetu baba yake Rahma alisikia akaja mbio kujua kilitokea nini,
akina mama wakiwa wanalia walishindwa kumweleza chochote zaidi ya kulia.
“Eti Togo, kimetokea nini?” akaniuliza.
Nilimfahamisha kilichotokea, akiwa amepata mshtuko, mzee huyo alimshika Rahma
kifuani akagundua mapigo yake ya moyo yalikuwa yakidunda kwa mbali, akawauliza
akina mama alipatwa na nini. Mama ya Rahma akamweleza kila kitu, mzee huyo
aliwaambia wanyamaze kwani Rahma alikuwa hajafa, mzee huyo aliniambia niende
haraka kwa jirani aliyekuwa na usafiri ili amkimbize Rahma hospitali.
Nikiwa nimechanganyikiwa na tukio hilo, nilikwenda
kwa jirani huyo ambaye alikuja na gari lake tukampakiza Rahma na kumkimbiza
hospitali, alipofikishwa huko alifanyiwa uchunguzi na kuibainika alikunywa dawa
mchanganyiko ili ajiue. Madaktari walimuwekea dripu ya maji kisha antpoison
kuondoa sumu hiyo, wakati akipewa matibabu hayo alikuwa hajitambui, madaktari
walituambia tusiwe na wasiwasi kwani baada ya muda mfupi hali yake
ingetengemaa.
“Kati yenu ni nani wazazi wa huyu binti?”
Daktari aitwaye Jason aliwauliza akina mama na akina baba! “Mimi mama yake na
huyu hapa ndiye baba yake,” mama ya Rahma alimjibu daktari huyo huku
akimuonyeshea mumewe. “Oke, naomba twendeni ofisini kwangu tukazungumze
kuhusiana na tatizo la binti yenu,” daktari huyo aliwaambia.
“Hakuna shida daktari,” baba ya Rahma alimwambia.
“Kwanza nawapeni pole kwa jambo lilitokea kwani najua ni kwa kiasi gani mmepata
mshtuko,” daktari aliwaambia. “Tunashukuru dokta, pia tunashukuru kwa jinsi
ulivyompokea na kumhudumia kwa wakati,” mama yake Rahma alimwambia daktari.
Alipoambiwa, daktari aliwaambia wasijali kwani huo ndiyo wajibu wao kwa
wagonjwa kisha akawauliza kilitokea nini nyumbani kilichosababisha Rahma kutaka
kujiua!
“Kwa kweli hata sisi tumeshangazwa sana na
uamuzi wake, ameamka akiwa mukheri wa afya, tumeshinda naye vizuri hadi mchana
mama yake alipomtuma ndugu yake akamuamshe kwa ajili ya kula ndipo akarudi mbio
na kumweleza alimwita hakuitika na alipojaribu kumtikisa alitulia tu!” baba ya
Rahma alimweleza daktari.
“Oh poleni sana, lakini lazima kutakuwa na
sababu kwani katika hali ya kawaida siyo rahisi kwa mtu kuchukua uamuzi wa
kutaka kujiua bila ya kukwazwa na jambo f’lani, je, yupo katika uhusiano wa
kimapenzi na mtu yeyote?” Daktari aliwauliza. “Hatuelewi maana hatujawahi
kumuona na mwanaume yeyote,” mama Rahma alimwambia.
Alipotoa kauli hiyo, daktari Jason aliwauliza
tena kama binti yao alikuwa na ugomvi na mtu yeyote hasa marafiki zake, wazazi
wake wakamwambia hakuwa na ugomvi. “Labda aliomba mnunulie kitu f’lani
mkamkatalia kwa ukali?”
Daktari huyo alizidi kuwabana kwa maswali ili
tu kujua sababu ya Rahma kutaka kujiua. “Kwa upande wangu hajaniomba chochote
labda mwenzangu,” mama yake alimjibu daktari. “Eh! Baba au alikuomba fedha
ukamnyima,” daktari akamwuliza. “Hapana daktari, tena juzi tu nimempatia fedha
za kutosha kwa ajili ya matumizi yake,” mzee huyo alimwambia.
Baada ya maswali hayo na majibu, daktari
aliwaambia lazima kuna jambo ambalo wazazi hawalifahamu lililosababisha Rahma
kutaka kujiua, akawashauri wawe wanachunguza nyendo za watoto wao hasa mabinti
kwa sababu wana mambo mengi sana.
***
Wakati kule ofisini kwa daktari Jason
akiendelea kuzungumza na wazazi wa Rahma, nje baba yake Togo na mama yake ambao
hawakuwa na furaha walikuwa wakizungumza kuhusu tukio hilo. “Hivi mama Togo,
kitendo cha kuwauliza hawa watoto kama wanafahamiana tangu zamani na kwamba
ukaribu wao unatutia shaka inaweza kuwa sababu ya Rahma kutaka kujiua?” baba
Togo alimwuliza mkewe.
“Sidhani, nahisi kutakuwa na jambo lingine tu
mume wangu,” mama huyo alimwambia mumewe. Alipoambiwa hivyo, mumewe alimweleza
mkewe kwamba huenda tayari walishaanza kufanya utundu na sababu ya kutaka
kujiua ni baada ya kuwaambia walikuwa ndugu!
“Ila unachosema naona umenifungua kichwani,
huenda ikawa hivyo ili kuficha aibu ya kutembea na kaka yake, lakini tusiwaze
sana kuhusu hilo tutajua tu ukweli!” mama Togo alimwambia mumewe.
Hata hivyo, baba Togo alimwambia mkewe kwamba
ngoja wamsubiri Togo aliyekuwa amekwenda kununua maji ya kunywa arejee ili
wambane kwani walihisi alikuwa anajua sababu za mwenzake kutaka kujiua.
“Nakuunga mkono, atakuwa anajua japo anajifanya hajui chochote,” mama Togo
alimwambia mumewe. “Mh! Huyu mtoto ana hatari sana, hata kama wameshafanya
utundu na kaka yake uamuzi aliochukua siyo mzuri hata kidogo,” baba Togo
alimwambia mkewe kwa huzuni.
“Ila
mke wangu kama kweli hawa watoto watakuwa wamefanya utundu itakuwa dhambi kubwa
ambayo italeta balaa na tutakuwa tumesababisha sisi kushindwa kuwaambia mapema
kwamba walikuwa ndugu,” baba Togo alimwambia mkewe.
“Sijui itakuwaje sasa mume wangu, lazima balaa
litokee tuombe tu Mungu Togo atuhakikishie kwamba hawafanyi mapenzi na ndugu
yake,” mama Togo alimwambia mumewe. Wakati wakizungumza hayo, mara wakawaona
baba na mama Rahma wanakwenda walipokuwa wakitokea ofisini kwa daktari,
wakaacha mazungumzo yao. Je, kilifuatia nini? Usikose mwendelezo wa hadithi
hii katika Gazeti la Championi Ijumaa.
No comments:
Post a Comment