MAKABURI YA NUNGWI- NUNGWI GRAVES
MWANGWI
wa vilio na simanzi kutoka kwa watu waliopoteza maisha baada ya meli kuzama
kwenye mkondo wa bahari wa Nungwi, Zanzibar, uliambaa kwenye maji na kwenda kugota kwenye
ukuta wa chini ya bahari, mahali palipokuwa na maelfu ya makaburi yaliyochongwa
kwenye mwamba mgumu kuhitimisha safari ya wote waliopoteza maisha yao kwenye
ajali hiyo ya kihistoria.
Kwa binadamu wa kawaida, wenye macho yanayoweza
kutofautisha giza na mwanga pekee, hiyo ilikuwa ni ajali ya bahati mbaya kama
zilivyo ajali nyingine lakini kwa wale wenye uwezo wa kuona zaidi ya upeo wa kawaida wa binadamu (beyond normal vision),
haikuwa ajali ya bahati mbaya bali kitu kikubwa zaidi kilichopangwa na
kuratibiwa kwa umakini wa hali ya juu.
“Babu!
Mbona nasikia vilio vya watu wengi sana !
Kwani kuna nini?” kijana mdogo anayefundishwa imani za kishirikina, Kahungo, alikuwa akimuuliza babu yake.
“Hivyo
ni vilio vya roho zilizopokonywa miili yao bila kujiandaa.“
“Unamaanisha
nini babu?”
“Ili
binadamu akamilike anapaswa kuwa na mwili na roho, vitu hivi vinapotengana, binadamu
hufa. Sasa hawa wametenganishwa miili na
roho ghafla kwenye ajali bila hata kujiandaa na ndiyo maana wanalia sana.”
“Sasa mbona
wanazikwa wakiwa hai? Kwa nini wengine wanalia sana wakati wengine hawalii? Na hawa
waliokuwa wanachimba makaburi huku chini ya bahari walikuwa wanatumia vifaa
gani?”
”Hawazikwi
wakiwa hai. Zile unazoziona ndiyo roho, zinapambana kurudi kwenye miili yao inayoelea juu ya maji
lakini zinashindwa. Wanaolia sana ni wale ambao
kwenye maisha yao
walimsahau Mungu na wakazama dhambini! Wale unaowaona hawalii ni wale ambao
walikuwa wanafuata maagizo ya Mungu. Waliochimba makaburi haya ya Nungwi
walitumia kitu chepesi sana , walitumia maarifa
ya giza !”
“Maarifa
ya giza ? Lakini
mbona hata misalaba inayowekwa kwenye makaburi haya siyo kama
ile tuliyozoea kuiona kule duniani? Naona kama ni mifupa ya binadamu imefungwa
na kutengenezwa misalaba,“ Kahungo alizidi kumhoji babu yake kwani kila
alichokuwa anakiona kilikuwa kinamshangaza.
“Hizi
ni kanuni za nguvu za giza !
Mbona hushangai mimi na wewe kufika huku chini ya bahari bila ya kuwa na
mitungi ya gesi wala nini na bado
tunapumua kama kawaida?”
“Mh!
Kweli dunia ina mambo. Halafu nilisikia kuna wazamiaji kutoka Kusini mwa Afrika
walishindwa kufika huku, mbona sisi tumefika kirahisi na bado naona watu wengi
tu wakiendelea na shughuli za mazishi?”
“Hii
dunia mjukuu wangu tunafaidi sisi wenye nguvu za giza ! Hakuna kinachotushinda na ndiyo maana
nataka nikuandae na wewe ufuate nyayo zangu, si unaona mimi nimeshakuwa mzee! Kuna
kazi sana mpaka kufikia huku tulipo, inakubidi uvuke ngazi nyingi sana. Wengi
hata ngazi ya kwanza hushindwa kuivuka.”
“Kwani
hapa tulipo panaitwaje babu?”
“Nungwi!
Kuna mkondo bahari wenye nguvu sana
hapa na kuna wakati maji huwa yanachemka. Kutokana na maajabu ya hapa ndiyo
maana wachawi waliamua kuweka kituo chao kikuu. Maji yanapishana kwa ngazi
kuanzia juu hadi chini.
“Unataka
kusema hiki ni kituo cha wachawi?”
“Eee! Wengi
watashangaa kwa sababu ya ajali iliyotokea, lakini ukweli ni kwamba Nungwi ipo
kwa miaka mingi iliyopita. Hii siyo ajali ya kwanza kutokea hapa. Mimi tangu
nikiwa mdogo nilikuwa nakuja hapa kuongeza nguvu za kichawi na nilikuwa
nikishuhudia ajali kubwa kuliko hata hii.”
Maelezo ya babu yake yalimshangaza mno Kahungo.
Alizoea kusikia au kusoma hadithi za kutisha kwenye vitabu lakini sasa alikuwa
eneo la tukio akishuhudia mwenyewe kila kitu. Babu yake akazidi kumfafanulia
mambo.
“Siyo
binadamu wote unaowaona duniani wanaishi kihalali, wengi hawafuati maagizo na
mafundisho ya Mungu! Wanavunja amri zake kwa makusudi. Wanaabudu sanamu na kutukuza
dhambi! Hawaogopi kufa wala adhabu za kaburi! Watu kama hawa wakiingia kwenye
mitego ya nguvu za giza
hawaponi!
“Sisi
(wachawi) huwa tunasaidia kuwafikisha kwa urahisi kuzimu kwa kuwapitisha kwanza
kwenye malago ya wachawi ambapo hutumikishwa kwa kipindi fulani kisha kuachwa
waendelee na safari zao. Miongoni mwa njia za kuwasaidia wafike upesi kwenye
safari zao ni kuwazika chini ya bahari.
“Babu!
Unataka kusema makaburi chini ya bahari yapo hapa Nungwi pekee?”
“Yapo
sehemu nyingine nyingi, lakini kwa miaka mingi hapa ndiyo kwenye makaburi
maarufu na mengi zaidi, ndiyo maana hata mkondo bahari wa hapa una nguvu kubwa
na husababisha ajali nyingi na kubwa kuliko sehemu nyingine.”
“Aaah!
Mbona unanichanganya! Kwani kilichoanza
kuwepo hapa Nungwi ni makaburi ya chini ya bahari au mkondo wenye nguvu
unaosababisha ajali?”
Swali
lile lilimfanya yule mzee amkazie macho mjukuu wake huku akiwa ni kama ambaye hakutegemea kulisikia kutoka kwake. Aliachia
tabasamu hafifu kisha akasema:
“Naona
umekua siku hizi mjukuu wangu kwani unauliza maswali ambayo hata mimi nilipokuwa
na umri kama wako sikuweza kuyafikiria. Kwa kuwa
una hamu ya maarifa juu ya ulimwengu usioonekana kwa macho ya kawaida, nitakufafanulia
kila kitu.”
“Cha
kwanza kuwepo kilikuwa ni kituo kikuu cha wachawi miaka mingi sana iliyopita. Kutokana
na nguvu za giza zinazozalishwa chini ya bahari
kila wachawi kutoka sehemu mbalimbali wanapokutana, maji yalikuwa yakivurugika sana na kuchemka, ndiyo
mkondo wa bahari ukaanza kutokea taratibu kisha ukawa unazidi kuongezeka nguvu.
“Mkondo
huo ulianza kusababisha ajali nyingi kwa wasafiri wa majini na kupoteza maelfu
ya roho za watu, waliokuwa wanakufa wakawa wanaletwa kuzikwa huku chini, ndiyo
yakatokea makaburi haya ambayo yalizidi kuongezeka wingi kwa kadiri ajali zilivyokuwa
zinazidi kutokea.”
Baada
ya kukaa kule chini ya bahari kwa saa nyingi akishuhudia mauzamauza mengi ya
kichawi, Kahungo alimuomba babu yake waondoke kwani moyo wake ulishindwa
kuvumilia yale aliyokuwa anayaona na kuyasikia. Wakashikana mikono na babu yake
kisha wakafanya ishara za kichawi, Kahungo akaambiwa afumbe macho kama alivyofanya awali wakati wa kuja. Kufumba na
kufumbua wakajikuta wako mchangani, ufukweni mwa bahari.
Baada
ya kutoka kule chini ya bahari na kujikuta wakiwa ufukweni mwa bahari, Kahungo
na babu yake waliwalikuta watu wengi wakiendelea na kazi ya kuopoa kile wakichoamini
ni miili ya ndugu zao waliozama kwenye ajali ya meli iliyotokea katika mkondo
bahari wa Nungwi.
“Babu
hawa wanafanya nini?”
“Wawaokoa
ndugu zao waliokufa kwenye ajali.”
“Sasa
mbona wanabeba vipande vya migomba?”
“Shhhh!
Usiongee chochote, watakusikia. Nyamaza!“ babu yake Kahungo alimnyamazisha
mjukuu wake. Alipoona hataki kutulia, alifungua kimkoba chake cha ngozi na
kutoa unga fulani mweusi, akajimiminia kidogo kiganjani kisha akaupulizia usoni
mwa Kahungo.
“Hebu fikicha macho yako,“ alisema babu yake
Kahungo. Alipofanya vile alivyoambiwa,
alishangaa kuona mambo aliyokuwa anayaona awali yakipotea ghafla, akaanza kuona
kawaida kama wengine walivyokuwa
wanaona.
“Babu roho inaniuma sana ,
hivi kama kweli Mungu yupo kwa nini anaruhusu
haya yatokee kwa waja wake?”
“Kahungo
mjukuu wangu! Jifunze kuwa na roho ngumu, angalia mpaka unamkufuru Mungu wako!
Kila jambo linatokea kwa sababu. Badala ya kumlaumu Allah tunapaswa kumshukuru
kwa kila kitu.”
“Lakini
babu, hivi kwa nini wachawi wanakuwa na uwezo wa kuwadhuru wengine kuliko kuwasaidia?
Tazama kila jambo baya siku hizi
linahusishwa na uchawi au dini ya shetani. Kwa nini?”
“Aah, hayo
maswali yako utaenda kuniuliza nyumbani, hapa tujadili haya yanayoonekana mbele
yetu tu.”
“Sawa,
lakini hoja yangu nilikuwa nataka kukuuliza kuwa kama
wachawi wote wakikutana kwa kikao cha dharura, hawawezi kutafuta mbinu za kusaidia
uokoaji maana kule chini ya bahari bado watu wengi wapo hai.”
“Hilo haliwezekani mjukuu
wangu! Ingekuwa watu wote wanaamini uchawi tungekuwa na nguvu za kufanya hivyo
lakini serikali na dini za kisasa
haziutambui kabisa uchawi, hivyo kuukosesha nguvu ya pamoja.”
“Kwani
babu wewe unaabudu dini gani?
“Mi namuabudu
Mungu, dini au madhehebu ni kama njia tu ambazo zote zinaelekea sehemu moja.”
“Siyo
kweli, ungekuwa unamuabudu Mungu usingekuwa unashiriki kwenye michezo ya nguvu
za giza .”
“Kuwa
mwelewa mjukuu wangu. Mungu ndiye aliyeumba vitu vyote, vyenye uhai na visivyo
na uhai, binadamu na majini. Hizi nguvu zenyewe zinazotumika na wachawi au
wafuasi wa jamii za siri kama Masoni na
Illuminati zinatoka kwa Mungu, sema watu wengi huwa hawaelewi, tatizo kubwa la
binadamu wanaoishi duniani leo ni ukosefu wa maarifa.”
Wakati
Kahungo na babu yake wakiendelea kuzungumza ufukweni mwa bahari wakiwa wamekaa
juu ya mchanga, lilikuja kundi la vijana kadhaa na kuwazunguka.
“We
mzee wewe! Yaani sisi tunahangaika kuwaokoa ndugu zetu waliokufa kwenye ajali
ya meli wewe umekaa na kijukuu chako mnapiga soga? Una akili kweli wewe? Badala
ya kuja kutusaidia unaleta ujinga wako hapa,” kijana mmoja alisema kwa jazba,
wale wenzake wakadakia na kuanza kuzomea.
Kahungo
na babu yake walitazamana, wakiwa bado hawajakubaliana nini cha kufanya, wale
vijana waliwainua juujuu na kuanza kuwasukuma kuelekea kule shughuli za uokoaji
zilikokuwa zinafanyika.
“Kahungo!“
“Naam
babu,” aliitikia na alipomtazama babu yake, alimkonyeza na kumpa ishara ya nini
cha kufanya. Kwa kasi kubwa Kahungo alitekeleza, kufumba na kufumbua wale
vijana wakajikuta wamebeba magogo mawili, moja kubwa na jingine dogo.
“Hee!
Kumetokea nini?“
“Wamejigeuza
kuwa magogo, he kumbe wachawi? Mungu
wangu… tumekwisha!”
“Acheni kuogopa
nyie, tufanyeni dua haraka kisha haya magogo tukayachome moto,“ alisema
mmoja wao lakini kabla hawajatekeleza, kulitokea upepo mkali uliokuwa unavuma kutokea baharini, ukazoa
mchanga mwingi na kuzunguka kama
kimbunga. Kufumba na kufumbua yale magogo nayo yakatoweka kimiujiza.
Kutokana
na woga, wale vijana walitimua mbio, kila mmoja akashika njia yake huku
wakipiga mayowe ya kuomba msaada.
“Babu
kwani pale kumetokea nini mpaka tukaondoka kirahisi namna ile?”
“Wale
watoto wanataka kucheza na moto. Unajua tulikuwa na uwezo wa kuwadhuru lakini
kwa sababu tupo kwenye msiba mzito nimeamua kuwasamehe.
Tulichokifanya
pale ni kuhama kwa kutumia nguvu za giza kutoka dunia ya kawaida hadi dunia ya
giza inayoongozwa na nguvu za kichawi, ndiyo maana tulipoondoka walijikuta
wamebeba magogo kisha nayo yakachukuliwa na kimbunga.
“Kwa
hiyo hapa hawatuoni?”
“Hawatuoni,
si ndiyo maana wametupita hapahapa wakati wakikimbia?”
“Sasa babu kwa nini huu uwezo mkubwa ulionao
usiutumie kuisaidia serikali kwenye mambo ya maendeleo au kuokoa waathirika wa
majanga kama hili badala ya kuishia kuwatesa na kuwatishia maisha watu?”
“Unajua
maswali yako yanachosha sana. Nimeshakwambia ni kwa sababu serikali na watu
wake hawaamini katika uchawi. Lakini siku inakuja ambapo dunia yote itakuwa na
imani moja, hapo ndipo haya unayoyauliza mara kwa mara yatakapotimia.”
“Babu
mbona nimewahi kusikia kuwa hicho unachokisema ndiyo sera kuu ya dini ya
shetani ya Masoni? Hiyo si ndiyo New World Order?”
“Kwa
nza nikurekebishe… Masoni siyo dini ya shetani, mimi nimekuwa mwanachama wake
tangu nikiwa mdogo lakini mafundisho yote yanasisitiza kumpenda Mungu na kutii
amri zake, nawashangaa wanaosema ni dini ya shetani.”
“Pamoja na hayo bado hujajibu swali langu.”
“Vyovyote
unavyofikiria lakini wakati unakuja ambapo dunia nzima itakuwa na dini moja, na
hapo ndipo haya unayoyataka yatakapotimia.”
”Lakini
babu unajua mi bado roho inaniuma sana juu ya wale watu wanaoteseka chini ya
bahari, naomba unipeleke tena labda naweza kupata wazo la nini cha kufanya ili
kuwasaidia.”
Bila
hiyana, babu yake Kahungo alimuelekeza mjukuu wake kitu cha kufanya, akamwambia
afumbe macho mpaka atakapomwambia afumbue. Baada ya sekunde chache, tayari
walikuwa chini ya bahari, kwenye mkondo bahari wa Nungwi, eneo ambalo
walikuwepo muda mfupi uliopita.
Shughuli za mazishi zilikuwa bado zikiendelea
huku vilio vikizidi kuongezeka kwa kadiri muda ulivyokuwa unaenda.
“Babu
nakuomba kwa huruma yako tuwaokoe hawa watoto wadogo wanaotaka kuzikwa hai,
angalau nao wakayafaidi maisha ya duniani kabla ya kuletwa tena huku
makaburini.”
“Kwa
kuwa umeng’ang’ania sana, ngoja nikaongee na Barthaayin, akikubali ndiyo
tutaifanya hiyo kazi.”
“Kwani
huyo Barthaayin ndiyo nani?”
“Ni
mfalme wa roho ya mauti anayefanya kazi na Zirail. Binadamu wanapokufa yeye
ndiyo hufanya kazi ya kuwahamisha kutoka kwenye ulimwengu wa roho kisha
kuwaweka tayari kwa ajili ya safari ya kuzimu au peponi. Waliokuwa wanatenda
amali njema wakati wa uhai wao huelekea peponi wakati watenda maovu huelekea
kuzimu,” alisema babu na kuondoka kwa kasi.
Akamuacha
Kahungo akiwa anayafikiria maelezo aliyompa juu ya huyo Barthaayin. Baada ya
muda, babu alirejea huku sura yake ikiwa na tabasamu hafifu. Akamwambia kuwa
mkuu wa roho ya mauti ameridhia ombi lake la kuwatoa baadhi ya watoto kutoka
kwenye janga la umauti. Kauli ile ilimfurahisha sana, bila kupoteza muda akamsogelea
babu na kumuuliza wanaanzia wapi.
“Lakini
amesema idadi yao lazima iwe witiri na zaidi amependekeza watoto wa kiume saba
ndiyo waachiwe huru, warejee kwenye familia zao,” alisema babu yake huku akitoa
vitu kama dawa za kienyeji kutoka kwenye mkoba wake mdogo. Baada ya hapo akamwacha
palepale alipokuwa, akamwambia kuwa bado hakuwa na nguvu za kutosha kuingia
kwenye hali ya umauti na kurejea.
“Ili
kumuokoa mtu ambaye ameshaionja roho ya mauti lazima na wewe umfuate hukohuko,
kisha utoke naye. Usipokuwa na nguvu za kutosha unaweza kubakia hukohuko,”
alisema babu yake huku akisisitizia kuwa makini na kuondoa hofu ndani ya moyo
wake.
Alimwambia
kuwa ili muujiza wowote utokee, sharti binadamu aishinde hofu na kuitawala
akili yake. Alibaki ameshika tama akitaka kuona kama kweli kile alichokuwa
anakisema kinawezekana. Baada ya kuagana naye, alipotea kimiujiza. Baada ya kama dakika mbili
tangu alipopotea, alianza kusikia vilio vya watoto wa kiume kutokea ndani ya
ukuta wa bahari.
Japokuwa babu yake alimsisitiza kupambana na
hofu, alijikuta akitetemeka mwenyewe.
Hii nayo ndugu yangu ndio imeisha au inaendelea....kitambo sana
ReplyDeleteMaya
Kazi nzuri
ReplyDeleteSwadakta
ReplyDeletehongera kwa kazi nzuri
ReplyDelete