ILIPOISHIA:
“YULE uliyekuwa umekaa
naye kwenye basi ni nani?”
“Ni rafiki yangu.”
“Unamjua wewe? Na hicho
alichokupa una uhakika gani kama ni simu? Ujinga wako utaiponza familia nzima,”
alisema maneno ambayo yalinishangaza sana.
SASA ENDELEA…
“NI simu baba!”
“Sitaki kukuona naye
tena na hiyo simu lete,” alisema huku akinipokonya ile simu. Nilizidi
kumshangaa baba, nikaona kama anataka kunikosesha bahati ya bure. Kwa mara ya
kwanza nilijikuta nikipandwa sana na hasira juu yake. Hata hivyo sikuwa na cha
kufanya, tuliondoka Ubungo huku kila mmoja ndani ya gari tulilokuwa tumepanda,
akiwa anashangaa mandhari ya Jiji la Dar es Salaam.
Japokuwa tulikuwa
tumebanana sana kwenye ile teksi kwa sababu ya wingi wetu, kila mmoja alikuwa
akitamani yeye ndiyo akae dirishani. Tulikatiza mitaa mingi na hatimaye
tukaiacha barabara ya lami na kuingia kwenye barabara ya vumbi. Baada ya muda,
tulitokeza kwenye nyumba moja nzurinzuri, baba akawa wa kwanza kuteremka kwenye
gari, na sisi wengine tukafuatia na kuanza kushusha mizigo.
Wakati tukiendelea
kushusha mizigo, geti kubwa lilifunguliwa, mwanaume wa makamo aliyeonekana
wanafahamiana vizuri na baba, alimuita kwa jina lake, baba akaacha kila
alichokuwa anakifanya na kwenda kumkumbatia, wote wawili wakionyesha kuwa na
furaha kubwa kwa kukutana.
“Hii ndiyo familia
yangu, shemeji yako na watoto,” alisema baba huku akituonyeshea sisi,
akatusogelea na kusalimiana na mama, kisha akaanza kutupa mikono, mmoja baada
ya mwingine huku akituuliza majina.
“Naitwa Togolai,”
nilimwambia aliponifikia, akanitazama usoni.
“Wewe ndiyo Togo?”
“Ndiyo,” nilisema huku
na mimi nikiachia tabasamu hafifu kwa sababu na yeye alikuwa akitabasamu. Baada
ya hapo, alitukaribisha ndani, wakati tunabeba mizigo kuingiza, walikuja watu
wengine watatu, wasichana wawili na mwanaume mmoja ambao kwa kuwatazama tu,
walionyesha dhahiri kwamba ni wanaye kwa jinsi walivyokuwa wamefanana na
kupishana umri.
Mkubwa alikuwa wa kike,
aliyemfuatia alikuwa wa kiume na mdogo kabisa naye alikuwa wa kike.
Hawakupishana sana umri, yule mkubwa alikuwa akilinganalingana na dada yetu
Sabina.
Tofauti yao na sisi,
ilikuwa kubwa sana, kuanzia jinsi walivyokuwa wamevaa na mpaka muonekano wa
miili yao. Walikuwa na mwonekano wa kimjini haswaa wakati sisi tulikuwa na mwonekano
wa ‘bushi’, kuanzia sura zetu, mavazi yetu mpaka jinsi tulivyokuwa
tukizungumza.
Walitukaribisha mpaka
ndani, tukaenda kukaa kwenye sebule kubwa na ya kisasa. Japokuwa tulikuwa
wengi, lakini wote tulitosha kwenye masofa ya kisasa. Ushamba wetu uliendelea
kujidhihirisha mle ndani kwani tulikuwa tukishangaa kila kitu, kuanzia taa za
umeme, feni, mapazia, kuta zilizokuwa zimenakshiwa kwa rangi nzuri na marumaru,
kila kitu kilikuwa kigeni kwetu.
Tuliandaliwa chakula na
mama wa familia ile ambaye alikuwa mchangamfu na anayependeza kimwonekano
kuliko mama yetu. Kilikuwa ni chakula kizuri mno, ambacho ama kwa hakika
tulikifurahia. Tukala mpaka kumaliza, mwenzetu mmoja akawa anataka kulamba
bakuli la mboga, mama akamkata jicho la ukali na kumfanya aogope.
Baada ya chakula,
tulianza kushangaa runinga maana kule hakukuwa kuangalia, ilikuwa ni mara yetu
ya kwanza kuona runinga lakini achilia mbali runinga ya kawaida, ile iliyokuwa
mle ndani ilikuwa kubwa sana, tena ya kisasa kabisa iliyounganishwa na spika
ndogo za kisasa zilizokuwa zinatoa mdundo mzito.
Mpaka muda wa kulala
unafika, hakuna aliyekuwa tayari kubanduka pale sebuleni, kila mmoja alikuwa
anatamani kama akeshe palepale akitazama vipindi vizuri vilivyokuwa vinaonyeshwa.
Ilibidi mama atumie ukali, kwani kwa muda huo baba ambaye ndiyo tunayemwogopa
sana, alikuwa nje kwa mazungumzo na yule rafiki yake.
Kabla ya kwenda kulala,
ilibidi kwanza tuende kuoga mmojammoja kuondoa vumbi na uchafu tuliotoka nao
kijijini. Mimi ndiye niliyekuwa wa mwisho kwenda kuoga ambapo nilipoingia
kwenye bafu hilo la kisasa, nilishangazwa kwa jinsi lilivyokuwa safi. Yaani
hata kama ningeambiwa nikae mle ndani kwa siku nzima na kuletewa chakula nilie
humohumo ningekubali kwa sababu ya usafi wake.
Kule kijijini tulizoea
kwenda kuoga mtoni, wakati mwingine kuogelea lakini mjini mambo yalikuwa
tofauti. Nilivua nguo zangu na kuzikung’uta kwanza kwa sababu zilikuwa na vumbi
jingi. Kwa bahati mbaya, wakati nikiikung’uta suruali niliyokuwa nimevaa,
nilisahau kwamba ile dawa niliyopewa na baba nilikuwa nimeiweka kwenye mfuko,
nilipokung’uta ikadondoka chini na kwa kuwa choo na bafu vilikuwa vimeungana,
yaani upande mmoja kuna bafu na upande wa pili kuna choo, iliteleza mpaka
kwenye sinki la choo.
Kutokana na umuhimu wa
dawa hiyo, ilibidi niende kuiokota haraka lakini kabla sijafanya hivyo,
niliitundika ile suruali kwenye bomba lililokuwa pembeni. Nikashtuka kuona maji
yakianza kumwagika, yakaisomba ile dawa na kuipeleka kwenye shimo la choo,
ikapotelea kwenye bomba la kutolea maji machafu.
Nilishangaa sana yale
maji nani ameyafugulia lakini nilipotazama vizuri, niligundua kuwa kumbe pale
nilipokuwa nimetundika suruali ile ilikuwa ni koki ya bomba ambayo kwa jinsi
ilivyokuwa ya kisasa nilishindwa kuitambua.
“Ayaaa!” nilisema kwa
sauti kubwa kwa sababu sikutegemea kabisa kile kilichotokea na hata sikujua
nitamwambia nini baba kwa sababu wakati ananipa, alinisisitiza kuitunza sana
dawa hiyo. Ilibidi nifunge maji kwanza, nikaegamia kwenye marumaru za bafuni,
nikiwa na mawazo mengi juu ya nini cha kufanya.
Mwisho nilipiga moyo
konde na kujiambia kwamba nitaenda kumweleza baba hali halisi na kwa sababu
ananipenda na ananiamini. Nilimalizia kuvua nguo, nikawa nataka nioge maji kwa
kutumia bomba linalomwaga maji kama mvua, kama nilivyokuwa nimeona kwenye
runinga muda mfupi uliopita.
Kwa umakini mkubwa
nilichunguza mahali ilipo koki yake, nilipoiona niliifungua, maji yakaanza
kumwagika, harakaharaka nikaingia katikati yake na kuanza kujimwagia.
Ilibidi nifumbe macho
wakati najipaka sabuni lakini taratibu nilianza kuona maji yanaanza kuwa ya
uvuguvugu kidogo halafu yanakuwa kama mazito kidogo na yana chumvichumvi.
Nikawa nikipaka sabuni haiishi mwilini, ikabidi nisogeze kichwa pembeni kidogo
na kufumbua macho.
“Mungu wangu,” nilipiga
kelele kwa nguvu baada ya kugundua kwamba kumbe kile nilichokuwa nikiamini
kwamba ni maji, zilikuwa ni damu zikimwagika kama maji. Uda mfupi baadaye
tayari nilikuwa kwenye mlango wa bafuni lakini cha ajabu, licha ya kutoa loki
niliyoiweka wakati nikiingia, mlango uligoma kufunguka, nikawa nagongagonga kwa
nguvu huku nikiendelea kupiga kelele.
Wa kwanza kufika
alikuwa ni yule msichana ambaye alionyesha kuwa ndiyo mtoto mkubwa wa yule
mzee, akasukuma mlango kwa nguvu kutokea nje. Nguvu alizotumia, ukichanganya na
kwamba miguu yangu ilikuwa na majimaji, nilijikuta nikiteleza na kuanguka chini
kama mzigo akaingia na kupigwa na butwaa kutokana na hali aliyonikuta nayo
kwani sikuwa na nguo hata moja na bado nilikuwa nikipiga mayowe ya kuomba
msaada.
Alichokifanya, haraka
alivua khanga aliyokuwa amejifunga juu ya gauni lake na kunirushia ili
nijisitiri kisha haraka akageuka na kutoka, nikamsikia akijifungia mlango wa
chumbani kwake, nadhani alijisikia aibu sana kwa hali aliyonikuta nayo.
Cha ajabu sasa, wakati
nageuka kutazama kule zile damu zilikokuwa zikimwagika, nilishangaa kuona
kinachotoka si damu bali maji na wala hakuna dalili yoyote ya damu. Tayari kaka
zangu walishafika na kunikuta nikihangaika kujifunga ile khanga niliyopewa,
wakataka kujua nini kimetokea
Kelele hizo kumbe hata
baba na yule mwenzake walizisikia, nao wakaja haraka kutaka kujua nini
kimetokea.
Je, nini kitafuatia?
Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment