ILIPOISHIA:
Nilianza kuwatazama mmoja baada ya
mwingine, kuanzia mama ambaye uso wake ulikuwa na huzuni kubwa, baba ambaye
alionesha kuwa katika tafakuri nzito na ndugu zangu wote ambao walikuwa
wamenikodolea macho, kila mmoja akiwa na maswali mengi yasiyo na majibu. Mara
mlango wa wodi ulifunguliwa, watu wote wakageuka kutazama ni nani aliyekuwa
akiingia kwa kasi kiasi kile.
SASA ENDELEA...
“Shikamooni! Samahani naomba kuuliza eti
hii ndiyo wodi aliyolazwa Togo?” alisema mtu huyo lakini kabla hajajibiwa,
tayari alikuwa ameshasimama sehemu ambayo ilinifanya mimi na yeye tutazamane.
Moyo wangu ulinilipuka mno kugundua kuwa
kumbe alikuwa ni yule msichana tuliyekutana naye kwenye basi na kujenga naye
urafiki utafikiri tumejuana miaka kumi iliyopita.
Sikuelewa amejuaje kwamba nilikuwa
hospitalini hapo kwa sababu mara ya mwisho alipokuja nyumbani na kunikuta
nikiwa na Rahma, tukiondoka kuelekea ufukweni, nilimueleza kwamba tunaenda Coco
lakini baadaye tukabadili uelekeo na kuelekea Msasani Beach kwa lengo la
kumkwepa.
Kwa harakaharaka, isingewezekana mtu
ambaye ametufuata Coco ajue kwamba kumbe tulienda Msasani na kama hiyo
haitoshi, ajue kwamba kuna tatizo limetokea na kujua mpaka wodi niliyokuwa
nimelazwa. Kengele ya hatari ililia ndani ya kichwa changu.
“Ooh! Ahsante Mungu, Togo... umepatwa na
nini baba?” alisema huku akinisogelea pale kitandani lakini baba alimzuia.
“Binti, sidhani kama nakujua. Wewe ni
nani?”
“Togo alisema hawafahamiani ila walikaa
siti moja kwenye basi tu, hata sijui amefuata nini,” alidakia Rahma na
kuzungumza kwa chuki, moyoni nikajisikia vibaya sana kwa sababu kama mtu
alikuwa amekuja kwa ajili ya kuniona, achilia mbali utata mkubwa uliokuwa nyuma
ya tukio la yeye kujua mahali nilipo, hakupaswa kufanyiwa vile.
“Mruhusuni. Ni rafiki yangu!” nilitamka
kwa sauti dhaifu ya kukwamakwama, yakiwa ndiyo maneno yangu ya kwanza kuyatamka
tangu niliporejewa na fahamu. Baba akageuka na kunitazama kwa sekunde kadhaa,
akageuka na kumtazama yule dada usoni, akageuka na kumtazama Rahma ambaye
utulivu ulimuisha.
Akamruhusu anisogelee pale kitandani,
huku uso wake ukilengwalengwa na machozi, aliniinamia pale chini kwa heshima.
“Pole baba, nimeona picha ya tukio la
wewe kuokolewa ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii, nikajaribu kuulizia ndiyo
nikaambiwa umelazwa hapa. Pole sana,” alisema huku safari hii machozi yakiwa
yanamtoka. Nadhani kwa jinsi alivyoonesha kuguswa na hali yangu, hata baba
alianza kumkubali kwani nilimsikia akishusha pumzi ndefu.
“Najua hakuna anayeweza kukuelewa
ukieleza kilichotokea, nakuombea upone haraka,” alisema msichana huyo na
kunifanya nikodoe macho kama fundi saa aliyepoteza nati. Alijuaje kwamba hakuna
atakayenielewa nikieleza kilichotokea? Alijuaje kwamba maelezo ya Rahma
yalikuwa tofauti kabisa na kile nilichoamini kwamba ndiyo ukweli? Nilijikuta
nikichanganyikiwa.
Nikiwa bado nimepigwa na butwaa,
alinibusu kwenye mkono wangu uliokuwa na sindano ya dripu, akageuka na
kuwashukuru watu wote kisha kwa heshima kubwa akaondoka zake. Japokuwa mavazi
aliyokuwa amevaa yalimtafsiri katika picha nyingine tofauti kabisa, alionesha
nidhamu ya hali ya juu mno.
“Huyu ni nani?” swali la baba
lilinizindua kutoka kwenye dimbwi la mawazo, akanikazia macho akionesha kuwa na
shauku ya kutaka kusikia nitamjibu nini.
“Ni rafiki yangu.”
“Huyu ndiyo mliyekuwa naye kwenye basi?”
“Ndiyo.”
“Na ndiyo aliyekupa simu si ndiyo?”
“Ndiyo.”
“Amejuaje kama umelazwa hapa?”
“Anasema kuwa ameniona kwenye mitandao.”
“Mitandao? Wewe umefikaje kwenye
mitandao?” baba alinihoji, huku na yeye akionesha kutokuwa na uelewa wa mambo
ya teknolojia kama mimi. Nilimuona baba yake Rahma naye akisogea na kuja
kuungana na baba pale pembeni ya kitanda changu.
“Eti anasema amemuona kwenye mitandao,”
alisema baba huku akimgeukia baba yake Rahma.
“Inawezekana, unajua hawa vijana wa siku
hizi ni wepesi sana wa kutumia mitandao ya kijamii kama Facebook, WhatsApp na
Instagram kwa hiyo tukio lisilo la kawaida likitokea tu, haraka wanapiga picha
kwa kutumia simu zao na kuliweka mtandaoni kwa hiyo habari zinasambaa kwa
kasi,” alisema baba yake Rahma.
Na mimi nikawa nimepata elimu kidogo
maana kiukweli sikuwa najua chochote kuhusu hayo mambo maana kule ‘bush’ kwetu
tulichokuwa tunakijua ni redio tu. Muda mfupi baadaye, madaktari waliingia na
kuwataka watu wote wawapishe ili waweze kuendelea kunipa huduma.
Madaktari walifurahi kuniona nikiwa na
hali ile, wakaanza kuniuliza jinsi nilivyokuwa najisikia. Niliwaambia kwamba
nahisi mwili wote umekuwa mzito, kila kiungo hakina nguvu. Waliniambia ni kwa
sababu ya kiwango kikubwa cha chumvi nilichokuwa nimekula na mwili kukosa hewa
safi kwa muda.
Hata hivyo, waliniambia kwamba hali hiyo
ni ya muda tu, mwili utapata nguvu hasa baada ya kumaliza kiwango cha dripu
walichonipangia, ambazo zilikuwa zikiendelea kutiririka kwa kasi kuingia
mishipani mwangu.
“Kwa hiyo leo naweza kuruhusiwa kutoka?”
“Leoleo utatoka wala usiwe na wasiwasi.”
“Kwani saizi ni saa ngapi?”
“Ni saa moja za jioni,” alisema daktari
huku akinipima mapigo ya moyo kwa kutumia kifaa maalum, akarekebisha kasi ya dripu
kuingia mwilini mwangu kisha akawa anaandika jambo kwenye faili huku
akijadilianana wenzake.
“Kwani wewe hujui kuogelea.”
“Najua vizuri tu.”
“Sasa mbona maji yalikuzidi nguvu? Si
vizuri kucheza na maji kama hujui kuogelea vizuri, sawa kijana?” alisema
daktari huku akinitazama. Niliamua kukaa kimya maana hata ningeeleza
kilichotokea, hakuna ambaye angenielewa. Kwa kifupi ni kwamba ilionesha eti
mimi nilikuwa nachezea maji ya baharini ndiyo maana nikazama na kutaka kupoteza
maisha.
Hicho ndicho walichokuwa wakikiamini
watu wote lakini ukweli nilikuwa nao moyoni mwangu, nikaona njia nzuri ni
kunyamaza tu kwa sababu sikuwa napenda kukaa hospitalini, isitoshe hiyo ndiyo
ilikuwa mara yangu ya kwanza kulazwa. Kule kijijini kwetu, mtu ukiumwa ilikuwa
hakuna kwenda hospitali, baba anamaliza kila kitu yeye mwenyewe.
Kwenye majira ya kama saa tatu za usiku,
nilimuona baba na baba yake Rahma wakiingia wodini wakiwa wameongozana na wale
madaktari waliokuwa wakinitibu, wakapewa baadhi ya maelekezo kisha wakaja pale
kitandani kwangu, daktari mmoja akanichomoa dripu na kuniambia nijaribu
kusimama.
Nilifanya hivyo, japokuwa kwa mbali
nilikuwa nasikia kizunguzungu, niliweza kusimama vizuri. Wakaniambia nijaribu
kutembea hatua chache, nilifanya hivyo na wote waliridhishwa na maendeleo
yangu. Yule daktari akawaelekeza akina baba sehemu ya kwenda kulipia, baba yake
Rahma akanishika mkono na kuanza kuniongoza kuelekea nje.
Nguo nilizokuwa nimevaa hazikuwa zile
nilizovaa wakati nilipotokewa na tukio lile, hata sikukumbuka nani alinibadilisha
na alinibadilisha saa ngapi. Nilipotoka nje, niliwakuta ndugu zangu wote wakiwa
wamekusanyika, wote wakainuka baada ya kuniona nikitembea kwa kujivuta, wakaja
na kunizunguka.
“Unaendeleaje mwanangu,” alisema mama
huku akija na kunikumbatia, nikamwambia naendelea vizuri, akaja mama yake Rahma
ambaye naye alinikumbatia, akaja dada Sabina, Rahma na wengine wote, kila mtu
akawa ananikumbatia na kunipa pole kwa kilichotokea.
Wote wakageuka na kuanza kuniongoza
kwenye gari aina ya Toyota Noah lililokuwa eneo la mapokezi, mimi nikasaidiwa
kukaa siti ya mbele, pembeni ya dereva, ndugu zangu wengine wote wakakaa nyuma.
Kwa sababu ya wingi wao, hawakutosha, ikabidi mama na mama Rahma pamoja na baba
zetu wao wapande kwenye teksi iliyokuwa imepaki mbele ya ile Noah tuliyopanda.
Muda mfupi baadaye, dereva aliingia,
akanisabahi na kunisaidia kufunga mkanda, kabla hajaondoka nilimuona yule
msichana akitokea upande wa pili, akamuonesha dereva ishara kwamba asiondoe
kwanza gari, akaja pale kwenye dirisha la siti niliyokuwa nimekaa.
“Togo, vipi unaendeleaje?”
“Naendelea vizuri, namshukuru Mungu.”
“Pole sana mpenzi wangu,” alisema,
nikiwa bado nashangaa kwa nini ameniita hivyo, alinivuta na kugusanisha mdomo
wake na wangu, nikabaki nimeganda kama nimepigwa na shoti ya umeme.
Aliponiachia, harakaharaka niligeuka kuangalia kama Rahma hakuwa ameona kitendo
hicho, kwa bahati nzuri alikuwa akipiga stori na dada Sabina, kiufupi hakuna
aliyeona zaidi ya dereva ambaye naye alizuga kama hajaona kitu.
“Hii ni zawadi maalum kutoka kwako,”
alisema huku anikipa bahasha kubwa ya rangi ya pinki, akanibusu kwenye paji la
uso kisha akaniachia na kunipungia mkono, akampa ishara dereva kwamba aondoke.
Wakati hayo yakiendelea, kumbe baba aliyekuwa amekaa siti ya mbele ya ile teksi
iliyokuwa imeshaanza kutoka pale eneo la maegesho, alikuwa akishuhudia kila
kilichokuwa kinaendelea.
Nilipomtazama, macho yangu na yake
yaligongana, akanikazia macho, ikabidi nikwepeshe macho yangu, safari ya kurudi
nyumbani ikaanza huku mara kwa mara baba akichomoza kichwa na kunitazama, jambo
ambalo sikulifurahia.
Bado nilikuwa na maswali mengi kuhusu
huyu msichana, sikuwa najua ndani ya ile bahasha kuna nini na kwa sababu gani
anaonekana kunijali kiasi hicho. Baada ya dakika kadhaa, tukawa tumeshawasili
nyumbani.
Magari yaliposimama tu, baba alishuka
haraka na kunifuata, kabla hata dereva hajanisaidia kufungua mkanda, baba
alifika na kunitazama kwa macho ya ukali, safari hii nikaona kama ananionea, na
mimi nikamkazia macho, tukawa tunatazamana kama majogoo yanayotaka kupigana,
huku nikiificha ile bahasha asiione maana angeweza kunipokonya kama alivyofanya
kwenye simu.
“Kwa nini unakuwa huelewi unapoonywa
jambo? Unataka mpaka nini kitokee ndiyo ujue kwamba yule msichana ni mtu hatari
kwako na kwetu sisi sote?”
Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa
kwenye Championi Ijumaa.
Magari yaliposimama tu, baba alishuka
haraka na kunifuata, kabla hata dereva hajanisaidia kufungua mkanda, baba
alifika na kunitazama kwa macho ya ukali, safari hii nikaona kama ananionea, na
mimi nikamkazia macho, tukawa tunatazamana kama majogoo yanayotaka kupigana,
huku nikiificha ile bahasha asiione maana angeweza kunipokonya kama alivyofanya
kwenye simu.
“Kwa nini unakuwa huelewi unapoonywa
jambo? Unataka mpaka nini kitokee ndiyo ujue kwamba yule msichana ni mtu hatari
kwako na kwetu sisi sote?”
Itaendelea next issue.
No comments:
Post a Comment