ILIPOISHIA:
Nilipokuja kushtuka, nilijikuta nikiwa
nimelala kitandani, mapigo yangu ya moyo yakinienda mbio kuliko kawaida, nikiwa
nimeunganishwa mashine ya kunisaidia kupumua huku mwili wangu ukiwa
umeunganishwa na vifaa vingi vya kitabibu, milio ya mashine mbalimbali
ikisikika ndani ya chumba kile ambacho hata bila kuuliza, niligundua kwamba ni
wodini.
“Amefumbua macho! Dokta... amefumbua
macho! Njooni haraka!”
SASA ENDELEA...
Harakaharaka
madaktari wengi waliingia ndani ya kile chumba na kuzunguka kitanda changu, kwa
mbali nikawa nawatazama mmoja baada ya mwingine, wote wakionekana kukiinamia
kitanda changu. Macho yangu yalikuwa na ukungu, hali iliyonifanya nisiwe na
uangavu wa kutosha machoni kuwaona ingawa bado nilikuwa na uwezo wa kutambua
sura zao.
“Unaendeleaje
Jamal?” nilisikia daktari mmoja akiniuliza. Kwa jinsi sauti yake ilivyokuwa
ikisikika, ilikuwa mithili ya inayotoka kwenye redio mbovu. Nilijaribu kufumbua
mdomo lakini nilishindwa kwani nilikuwa nimeunganishwa na mabomba mengi,
mdomoni na puani, nikawa natingisha tu kichwa kuashiria kwamba najisikia
vizuri.
Jopo
la madaktari waliendelea kunizunguka pale, nikamuona mwingine akinipima kwa
kutumia kifaa maalum kusikiliza mapigo ya moyo wangu, mwingine akaniweka ‘thermometer’
kwapani kwa lengo la kunipima joto huku mwingine akiwa bize kufuatilia
maandishi yaliyokuwa yanaonekana kwenye mashine inayofanana na kompyuta,
iliyokuwa ikipiga kelele kwa kutoa milio ya ‘kubipu’ kila mara.
“He
is recovering! His heartbeats are stabilizing, blood sugar is coming to normal
and the wound is healing!” alisema daktari mmoja wakati akiwaambia wenzake, kwa
kuwa Kiingereza hakikuwa kikinipiga chenga, niliweza kuelewa vizuri kwamba
alikuwa akiwaambia wenzake kwamba nimeanza kupata nafuu, mapigo yangu ya moyo
yanaimarika, kiwango cha sukari kinarudi kwenye hali ya kawaida na jeraha langu
linapona.
Niliwaona
wote wakitabasamu na kunitazama usoni, kila mmoja akawa ananipongeza kwamba eti
nimepigania vizuri maisha yangu kwa sababu nilikuwa na hali mbaya sana. Daktari
mwingine ambaye kiumri alikuwa kijana mdogo, alinitania kwamba eti mimi ndiye
binadamu wa kwanza niliyeweza kwenda kuzimu na kurudi, wenzake wote wakacheka.
Japokuwa
mwenyewe alizungumza kama utani na wenzake nao wakacheka wakichukulia utani,
kile alichokisema hakikuwa utani ingawa siwezi kusema kwamba kule nilikofika
ndiyo kuzimu kwenyewe au la lakini ukweli ni kwamba nilikuwa nimefika mahali ambako
sidhani kama kuna binadamu aliye hai amewahi kufika.
Kuna
muda nilihisi huenda bado nipo kwenye ile hali ya kuuona mwili wangu wakati
mwenyewe nikiwa pembeni lakini haikuwa hivyo, ni kweli nilikuwa nimerejewa na
fahamu na kila kilichokuwa kinaendelea kilikuwa kikitokea kwenye ulimwengu
halisi.
Unajua
namna nyepesi ya kujigundua kwamba unaishi kwenye ulimwengu wa kawaida unapoona
upo kwenye mazingira ambayo huelewielewi kama upo ndotoni au la, ni kujaribu
kupepesa macho, kukunja vidole vya mikono au kuigusa ngozi ya mwili wako kwa
kutumia kitu chenye ncha kali.
Ukiona
umeweza kupepesa macho, kukunja vidole au umesikia maumivu baada ya kujifinya
au kujichoma na kitu chenye ncha kali, basi ujue kwamba haupo ndotoni au kwenye
ulimwengu wa tofauti bali upo kwenye ulimwengu halisi. Hicho ndicho
nilichokifanya mimi na kweli majibu yalionesha kwamba nilikuwa nimerejea kwenye
ulimwengu wa kawaida.
Madaktari
waliendelea kujadiliana na mwisho walifikia muafaka wa kuamua kunipunguza
baadhi ya vifaa mwilini mwangu, ikiwemo mirija ya kunisaidia kula pamoja na ile
ya kutolea haja ndogo kwani kwa kipindi chote nilichokuwa sina fahamu, kila
kitu kilikuwa kikifanyika kwa msaada wa mirija.
Hilo
lilifanyika, kitu pekee kilichoachwa mwilini mwangu ilikuwa ni mashine ya
kunisaidia kupumua ambayo nayo walikubaliana kwamba niendelee kuitumia kwa muda
lakini nitakapofikia hatua ya kuweza kupumua mwenyewe vizuri, wataitoa.
Niliwaona
madaktari wote wakiwa na nyuso za furaha sana mle ndani ya wodi yangu, tofauti
kabisa na kipindi nilipokuwa nikiwatazama kutokea pembeni kabla sijarejewa na
fahamu ambapo kila mmoja alikuwa akionesha sura ya kukata tamaa.
“Vipi
Jamal, unajisikiaje?” nesi mmoja wa kike aliniuliza kwa sauti ya upole wakati
akinisafisha mwili wangu kwa kutumia kitambaa laini kilichokuwa kimewekwa
kwenye kopo lenye maji ya uvuguvugu.
Nikamjibu
kwa sauti ya chini kwamba nilikuwa najisikia vizuri, akaendelea kunifutafuta
uso wangu, hasa kwenye yale maeneo niliyokuwa nimebandikwa bandeji za
kushikilia ile mirija iliyotolewa. Yule nesi aliendelea kunipigisha stori za
hapa na pale, huku mara kwa mara akiingizia utani ambao nilielewa kwamba
ulikuwa ni kwa lengo la kunichangamsha.
Unajua
jambo ambalo watu wengi hawalijui, madaktari, manesi na wauguzi, huwa
wanafundishwa saikolojia ya namna ya kucheza na akili za mgonjwa na kumfanya
ajisikie amani ndani ya moyo wake na kuamsha upya matumaini ya kupona, hata
kama alikuwa mahututi.
Ndiyo
maana ni nadra sana kumuona daktari aliyesomea vizuri kazi yake na kuhitimu,
akimfokea mgonjwa au kuzungumza naye kwa lugha isiyo rafiki. Fuatilia kwa
makini, madaktari karibu wote, wa hospitali za binafsi na za serikali, huwa
wanakuwa wapole sana wanapozungumza na wagonjwa wao, hata kama una tatizo
kubwa, atakupa maneno laini ya kishujaa yatakayokufanya uamini kwamba lazima
utapona.
Hata
manesi wale waliofundishwa vizuri na kuelewa, huwa wapole sana kwa wagonjwa kwa
sababu wamefundishwa hivyo. Ukiona nesi anawabwatukia wagonjwa wake, anawatolea
lugha chafu na za matusi, wengi wanakuwa ni wale ambao wameingia kwenye fani
hiyo kwa njia za kiujanjaujanja, pengine wamefoji vyeti au vyuoni walifeli
lakini wameingizwa kwa migongo ya ndugu zao au kwa kutoa rushwa.
Basi
yule nesi aliendelea kunipa maneno matamu, eti akawa ananisifia kwamba japokuwa
nilikuwa nimepoteza fahamu kwa muda mrefu, eti bado nilikuwa naonekana
‘handsome’, nikashindwa kujizuia na kuachia tabasamu hafifu.
Akaniambia
eti kama angekuwa hana aibu za kikekike, angenitongoza ili nimuoe, nikazidi
kuachia tabasamu pana kwani sijawahi kusikia eti mwanamke anamtongoza mwanaume
amuoe, japokuwa anaweza tu kumrahisishia mazingira ya kumpata, nikajikuta nikivutiwa
naye kwani ukiachilia mbali masihara yake, pia alikuwa na sura nzuri ya kuvutia
na umbile lililokaa kikekike haswaa!
“Yaani
sikomi tu, tamaa za wasichana warembo na huruma zangu ndiyo iliyonifanya
niingie kwenye mtego wa Shenaiza, hata kupona vizuri bado nimeanza kumzimikia
nesi,” nilijisemea mwenyewe moyoni na kuzidi kutabasamu.
Alizidi
kunipigisha stori mpaka nikaona ile mashine ya kunisaidia kupumua kama
inaninyima uhuru, nikamuomba aitoe ili nijaribu kupumua mwenyewe, akafanya
hivyo na kwa bahati nzuri, tayari nilikuwa na uwezo wa kupumua mwenyewe vizuri,
madaktari wakazidi kufurahi na kushauri kwamba kwa kuwa nilikuwa na hali nzuri,
nihamishiwe kwenye wodi za kawaida kwa sababu kwa muda wote huo, bado nilikuwa
kwenye wodi ya wagonjwa mahututi (ICU).
Mipango
ilianza kuandaliwa na hatimaye nilihamishiwa kwenye wodi ya wanaume ambapo
nilipoingizwa tu, ndugu, jamaa na marafiki walianza kufurika kwa wingi kuja
kuniona kwani fursa hiyo waliikosa nilipokuwa ICU kwa sababu kule huwa ndugu
hawaruhusiwi kumuona mgonjwa ambaye yupo kwenye hali mbaya kama niliyokuwa nayo
mimi, labda kama kuna sababu maalum.
Miongoni
mwa watu wa mwanzomwanzo kabisa kuja kuniona, alikuwa ni Raya ambaye hakuamini
kabisa aliponiona nikiwa nimefumbua macho, akanikumbatia kwa nguvu pale
kitandani bila kujali dripu niliyokuwa nimeunganishwa, akawa ananibusu sehemu
mbalimbali za mwili wangu huku akiangua kilio kwa nguvu.
“Nilijua
nimekupoteza mpenzi wangu, ooh ahsante Mungu! Ahsante Mungu,” alisema Raya,
ikabidi niinue ule mkono ambao haukuwa na dripu nikaupitisha mgongoni kwake na
kumkumbatia, nikambusu shavuni, kitendo ambacho kwa kiasi kikubwa kilimfariji
sana.
Japokuwa
mwili wangu haukuwa na nguvu, ilikuwa ni lazima nifanye hivyo kwa sababu kusema
ukweli, tangu nipatwe na matatizo, Raya alionekana kuguswa pengine kuliko mtu
mwingine yeyote.
Niliamini
uchungu ambao alikuwa nao msichana huyo, ungekuwa sawa na wa mama yangu endapo
angefahamu kilichokuwa kimenitokea mwanaye lakini kwa kuwa wazazi wangu
hawakuwa wakijua chochote kutokana na mazingira ambayo mimi mwenyewe ndiye
niliyeyatengeneza (nitafafanua kuhusu hili baadaye), Raya ndiye aliyesimama
kwenye nafasi ya mama yangu.
Kingine
nilichojifunza, ni kuacha kuhukumu watu wote kwambe eti siku hizi duniani
hakuna tena mapenzi ya kweli! Siyo sahihi kabisa, kuna watu wana mapenzi mpaka
shetani mwenyewe anayaogopa, mmoja wapo akiwa ni Raya.
Niliendelea
kumkumbatia msichana huyo huku marafiki na jamaa zangu wengine wakiwa pembeni
wakitutazama, tukiwa kwenye hali hiyo, nilisikia mlango wa wodi ukifunguliwa na
mtu akaingia mbiombio mpaka pale kitandani kwangu, nikashtuka na kumuachia
Raya, Raya naye akainua uso wake, watu wote tukawa tunamtazama kwa mshangao mtu
yule aliyeingia, tukiwa ni kama hatuamini.
Je,
nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment