ILIPOISHIA:
“SIJUI itakuwaje sasa mume wangu, lazima
balaa litokee tuombe tu Mungu Togo atuhakikishie kwamba hawajafanya mapenzi na
ndugu yake,” mama Togo alimwambia mumewe.
Wakati wakizungumza hayo, mara wakawaona
baba na mama Rahma wanakwenda walipokuwa wakitokea ofisini kwa daktari,
wakaacha mazungumzo yao.
SASA ENDELEA...
“VIPI anaendeleaje?”
“Anaendelea
vizuri, mtoto mjinga sana huyu.”
“Mh! Usimuite
mjinga, huu siyo muda wake, uchungu wake naujua mimi, nimembeba kwenye tumbo
langu kwa miezi tisa,” alisema mama yake Rahma akionyesha kutofurahishwa na
kauli ya mumewe. Walitoka pamoja na kwenda kukaa kwenye benchi lililokuwa nje
ya jengo hilo la hospitali, mimi nikaenda kukaa upande wa pili.
“Hivi, mnajua
mimi bado sina majibu juu ya haya maswali niliyonayo.”
“Maswali gani
yanayokusumbua?”
“Ni kwa sababu
gani Rahma amechukua uamuzi wa kuyakatisha maisha yake?”
“Mh! Hawa watoto
wetu wa siku hizi, mimi nahisi alikuwa anampenda Togo sasa kitendo cha
kuwaambia kwamba ni ndugu ndiyo maana ameamua kufanya aliyoyafanya, tumshukuru
Mungu bado yupo hai.”
“Unachokisema ni
sawa lakini nahisi kuna kitu zaidi ya hicho, nahisi hawa watoto walikuwa
wameshaanza kufanya mapenzi.”
“Mh! Ninavyomjua
Togo huwa hana kawaida ya kuwa karibu na wasichana kabisa, ni muoga sana wa
wasichana, sidhani kama hilo linawezekana.”
“Hata Rahma naye
si mcharuko kiasi hicho, sijawahi hata kumuona akiwa na mwanaume kichochoroni,
kama mambo hayo anayafanya basi anafanya kwa siri sana, kwa ufupi
anajiheshimu.”
“Sasa kama
tatizo siyo hilo, mnafikiri nini kinaweza kuwa chanzo?”
“Mh! Mimi
nakuunga mkono rafiki yangu, kuna kitu nimekihisi na kwa kuunganisha matukio,
inawezekana ni kweli wakawa wameshaanza kukutana kimwili,” alisema baba na
kusimama, akageuka huku na kule, nilishajua ananitafuta mimi na hakuwa akijua
kwamba kumbe nilikuwa palepale jirani yao, nikisilikiza kila kilichokuwa
kinaendelea.
“Hebu njoo
hapa,” alisema huku uso wake ukiwa na jazba, nikasogea huku uso wangu nikiwa
nimeuinamisha chini.
Pale kulikuwa na
makundi mawili, baba yake Rahma na baba, wao walikuwa waking’ang’ania kwamba
lazima mimi na Rahma tayari tumeshavunja amri ya sita wakati mama na mama yake
Rahma, wao walikuwa wakitutetea, kila mmoja na mwanaye.
“Ule mzigo
niliokupa safarini uko wapi?” nilishangaa baba akiniuliza swali tofauti kabisa
na nililolitegemea. Nikaanza kuvuta kumbukumbu anazungumzia mzigo gani, kwa
kutumia tafsida akanifafanulia mpaka nikaelewa kwamba kumbe alikuwa akimaanisha
ile dawa aliyonipa pale Mlima Nyoka, Mbeya baada ya kunusurika kwenye ajali
mbaya ya gari.
“Ipo nyumbani,”
nilimdanganya lakini ukweli ni kwamba licha ya kunisisitiza sana niitunze dawa
hiyo, ilikuwa imeniponyoka na kutumbukia kwenye shimo la choo, nyumbani kwa
akina Rahma wakati nikioga.
“Una uhakika?”
“Ndi...
ndi...yo,” nilibabaika. Baba alikuwa akinijua vizuri, nadhani kwa kubabaika
huko, alielewa kwamba dawa hiyo haipo salama, akasimama na kunishika mkono,
akanivuta kwa nguvu pembeni.
“Nakuuliza kwa
mara ya mwisho, dawa yangu iko wapi?”
“Baba nisamehe,
ilitumbukia chooni.”
“Unasemajee?”
baba alishtuka kuliko kawaida. Mshtuko aliouonyesha ulinifanya nielewe kwamba
kumbe dawa ile kutumbukia chooni halikuwa jambo la kawaida.
“Kwa nini
umeniangusha mwanangu? Kwa nini umewapa ushindi?” alisema baba huku akiwa
anatingisha kichwa chake kwa masikitiko, nikawa sielewi anamaanisha nini.
“Halafu kwa nini
usiniambie mapema ili tujue nini cha kufanya?”
“Nisamehe baba.”
“Nataka uniambie
ukweli, wewe umeshafanya mapenzi na Rahma, kweli si kweli?” baba alinihoji,
safari hii akiwa amenikazia macho usoni, nikawa nashindwa kama nikubali au
nikatae.
“Unaona upumbavu
wako? Yaani hili halijaisha umeanzisha jingine, hivi una nini wewe?” alisema
baba, akiwa tayari ameshajipa majibu kuhusu swali alilouliza. Nilishindwa cha
kusema, nikajiinamia chini kwa aibu, masikitiko na huzuni vyote kwa wakati
mmoja.
“Upumbavu
ulioufanya utasababisha matatizo makubwa sana kwa watu wasio na hatia, hata
sijui itakuwaje,” alisema baba huku akionyesha kuchanganyikiwa kabisa,
akaondoka na kuniacha palepale nikiwa nimesimama, na mimi nikiwa
nimechanganyikiwa.
Alienda pale
alipokuwa amemuacha mama na wazazi wa Rahma, wakawa wanazungumza kitu kisha
nikaona wote wamegeuka na kunitazama, hata sijui walikuwa wakizungumza nini.
“Wakiwa bado
wananitazama, nesi mmoja alifungua mlango wa wodi aliyokuwemo Rahma na kutoka
mbiombio mpaka kwenye ofisi ya madaktari iliyokuwa hapohapo jirani, muda mfupi
baadaye akatoka tena mbiombio lakini safari hii alikuwa ameongozana na
madaktari wawili ambao nao walikuwa wakikimbia.
Niliwaona akina baba
wakikatisha mazungumzo yao na kusimama, huku macho yao yakiwa kwenye ule mlango
wa wodi. Mle wodini kulikuwa na wagonjwa kadhaa ila sijui kwa nini akili yangu
ilinituma kuamini kwamba walikuwa wakimkimbilia Rahma. Hata akina baba nao
nadhani walishajua kwamba mwenye tatizo ni Rahma.
Sikutaka
kuandikia mate wakati wino upo, nilitimua mbio kutoka pale nilipokuwa na
kukimbilia kwenye mlango wa ile wodi, nikaupiga kikumbo mlango na kuingia mpaka
ndani, macho yakiwa pale kwenye kitanda alichokuwa amelazwa Rahma.
Madaktari na
manesi walikuwa wamemzunguka, nikasogea kutaka kujionea amepatwa na nini?
Nilichokiona sikukiamini. Rahma alikuwa akitapatapa kama anayetaka kukata roho,
kibaya zaidi damu nyingi zilikuwa zikimtoka mdomoni na puani, kiasi cha
kusababisha mashuka meupe aliyokuwa amelalia yalowe damu.
“Aisee,
huruhusiwi kuingia humu, muda wa kuona wagonjwa haujafika,” mlinzi ambaye
mkononi alikuwa na rungu kubwa, aliniambia huku akilitingisha lile rungu,
akanionyesha ishara kwamba nitoke nje vinginevyo ataniadhibu.
Ilibidi nitoke
tu kwani sikutaka matatizo zaidi, ukizingatia na hali niliyomuona nayo Rahma
ndiyo nilizidi kuchanganyikiwa.
“Vipi kuna
nini?” baba aliniuliza nilipotoka tu, ikabidi nimueleze hali halisi, nikamuona
na yeye akishusha pumzi ndefu na kushika kiuno.
“Haya yote ni
kwa sababu yako na hawezi kupona kwa kutibiwa hospitali, dawa yake unayo wewe,”
alisema baba huku akinitazama kwa macho ya ukali.
“Mimi? Dawa
gani?”
“Inabidi ufute
makosa ya upumbavu wako wote ulioufanya, hiyo ndiyo itakuwa ponapona yake,
mtoto mshenzi sana wewe, wala sikukutegemea,” alisema baba huku akinisogelea
mwilini, nikahisi lazima atanizabua makofi kwa sababu anapokasirika sana huwa
hawezi kudhibiti hasira zake.
“Itabidi
tuwaombe tuondoke naye mpaka nyumbani, nitaenda kukuelekeza nini cha kufanya
kumsaidia,” alisema kwa sauti ya kunong’ona, nikahisi kama amechanganyikiwa
akili. Yaani kwa hali aliyokuwa nayo, halafu eti akawaombe madaktari tuondoke
naye kurudi nyumbani? Niliona ni kitu kisichowezekana.
Baba aligeuka na
kuondoka, akasogea pembeni na kuanza kuzungumza na baba yake Rahma. Akina mama
wao niliwaona wameshaanza kuchanganyikiwa, mama yake Rahma akawa analia.
Nilijisikia vibaya sana ndani ya moyo wangu, hasa kwa jinsi baba alivyokuwa
ananishutumu kwamba mimi ndiyo chanzo cha yote yale.
Mara mlango wa
wodi ulifunguliwa, daktari mmoja akachungulia nje na kuwaonyesha ishara ya
kuwaita baba na baba yake Rahma, mapigo ya moyo wangu yakalipuka mno, sikujua
anaenda kuwaambia nini, akilini nikawa nahisi kabisa kwamba mambo
yameshaharibika.
Je, nini
kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment