ILIPOISHIA:
Nikiwa bado naendelea kumtazama kwa
jicho baya, mara nilishtuka kusikia vishindo viwili vikubwa juu ya bati, kama
vile nilivyokuwa navisikia usiku uliopita, moyo wangu ukapatwa na mshtuko
mkubwa mno. Mara nilisikia vishindo vingine vitatu mfululizo, nikawa nimepigwa
na butwaa huku macho yangu yote yakiwa juu.
SASA ENDELEA...
Kwa jinsi vishindo hivyo vilivyokuwa
vikisikika, ilikuwa ni kama kuna watu wanaruka kutoka angani na kudondokea juu
ya bati kwani vilikuwa vizito mno. Safari hii nilitaka kuwa makini kushuhudia
je, kile ninachokisikia mimi, kila mtu anasikia hivyohivyo maana nilishahisi
kuna kitu hakipo sawa kwangu lakini baba hataki kuniambia ukweli.
Baada ya vishindo vile vya kama watu au
vitu kutua juu ya bati, mara vilianza kusikika vishindo vya mtu akitembea juu
ya bati.
Unajua haya matukio kama hujawahi
kutokewa nayo, huwezi kuelewa ile hofu unayokuwa nayo lakini kiukweli, ni bora
tu uwe unasikia lakini yasikutokee. Hakuna hofu inayotesa kama hofu ya matukio
kama haya yanapokutokea, hasa usiku kama huo.
Nilijikuta nywele zikisisimka vibaya
mno, mapigo ya moyo yakawa yananienda kwa kasi maana sikujua safari hii
wanakuja kwa mtindo gani. Vishindo viliendelea kusikika kisha kikasikika
kishindo kingine ambacho kwa makadirio yangu ya haraka, kilikuwa ni kwenye
sakafu ya mle mahabusu.
Nilishindwa kuelewa, inawezekanaje
usikie mtu anatembea juu ya bati, tena kwa nje halafu muda mfupi baadaye umsikie
akirukia na kudondokea kwa ndani, tena jirani kabisa na pale ulipo! Inatisha
sana.
“Humu ndani kuna wanga eeh! Mbona nywele
zinanisisimka? Sasa ole wake mtu aniguse,” mmoja kati ya wale mahabusu
tuliokuwa nao mle ndani, aliyekuwa amekaa kwenye kona nyingine, alisikika
akiongea kilevilevi, akawa anaporomosha matusi mazitomazito.
Kitendo kile kilinifanya niamini kwamba
hatimaye sasa sikuwa peke yangu ambaye nilikuwa nikishuhudia mchezo uliokuwa
ukiendelea. Niliamini hivyo kwa sababu kwenye kona aliyokuwa amekaa yule
mahabusu ambaye alikuwa akiendelea kutukana, ndiko ambapo makadirio yangu
yalinionesha kwamba yule mtu aliyekuwa akitembea juu ya bati alidondokea
palepale.
Matusi aliyokuwa akitukana,
yalisababisha mahabusu wengine ambao bado hawakuwa wamelala, waanze kucheka kwa
nguvu na kumtania kwamba amelewa lakini kelele zote zilizimika ghafla bila mtu
yeyote kutoa amri, ikatokea tu kwamba watu wote wapo kimya.
Katika ukimya huo, ulisikika msonyo
mkali ambao japokuwa wale mahabusu wengine waliamini kwamba umetolewa na yule
mahabusu aliyekuwa akitoa matusi mazito kwa wale aliowaita wanga, mimi
nililitazama tukio hilo katika sura nyingine tofauti.
Haikuwa mara ya kwanza kusikia msonyo wa
namna hiyo ingawa safari hii ulionekana kutoka kwa mtu tofauti ambaye sijawahi
kuisikia sauti yake. Unajua kuna watu wamezaliwa wakiwa na uwezo fulani wa
kipekee, sijui niuiteje lakini kwa kifupi mtu anakuwa na uwezo wa kufikiri na
kuyaona mambo kwa utofauti na wengine.
Yaani kuna baadhi ya watu, nyie wengine
wote mnaweza kuamini kwa mfano ajali iliyotokea barabarani imesababishwa na
uzembe wa dereva kukimbia kwa mwendo kasi akiwa hajafunga mkanda, lakini mtu
mwingine hapohapo akalitazama tukio na kutoa jibu tofauti kabisa ambalo pengine
halikutegemewa.
Baba amewahi kunifundisha kwamba
japokuwa watu wa namna hii huwa wanachekwa au kuzomewa na kuonekana wanaishi
kwenye ulimwengu wa ndoto, lakini wao ndiyo huwa sahihi kwa sababu wanautazama
ulimwengu kwa jicho tofauti na watu wengine wote.
Ndicho kilichotokea mle mahabusu, wakati
watu wote wakilichukulia tukio la yule mahabusu kudai kule ndani kuna wachawi
kisha akaanza kuporomosha matusi, wengi walimuona kama mlevi tu lakini mimi
nilimtazama kwa jicho tofauti.
Hata uliposikika ule msonyo na watu
kuanza kumtuhumu kwamba anawavurugia usingizi wao, mimi nilikuwa nikiamini
kwamba hakuutoa yeye na alichokuwa akikisema kwamba mle ndani kulikuwa na
wanga, ulikuwa ni ukweli mtupu.
“Sikilizeni, sikilizeni,” alisema yule
mahabusu, kwa msaada wa mwanga hafifu uliokuwa ukipenya kutokea nje, nilimuona
akiinua kichwa chake juu kutazama darini, lakini kelele za mahabusu wengine
zikamfanya ashindwe kusikia alichokuwa akitaka kukisikia.
“Au naye ana nguvu kama mimi?”
nilijiuliza kwa sababu wakati akiwataka watu wote watulie ili wasikie, ni kweli
juu ya bati kuna mtu alikuwa akitembea kwa vishindo kabisa kisha naye akasikika
akidondokea ndani ya ile mahabusu.
Baada ya hapo, vilianza kusikika
vishindo vya watu wakirukia mle mahabusu mfululizo, nikawa natetemeka nikiwa
sijui nini kitatokea maana kama unavyojua, milango ya mahabusu huwa muda wote
imefungwa na haiwezekani ikafunguliwa kwa muda ule. Nilichokuwa nakiomba, ni
wachawi hao wasije wakawa wamekuja kwa shari kama ilivyotokea kwangu na safari
hii, nilijifunza kuufyata mkia, sikutaka kuzungumza chochote zaidi ya kuzidi
kukodoa macho yangu gizani kama nitaona kitu chochote.
Nilishangaa mfuko wa suruali yangu
ukianza kutetemeka kama ndani kulikuwa na kitu ‘kinacho-vaibreti’, sikukumbuka
kama niliweka kitu chochote mfukoni na hata kama ni simu, wala sikuwa
nikimiliki baada ya baba kunipokonya ile niliyopewa na yule dada ambaye ndiye
aliyesababisha muda huo nikawa nyuma ya nondo.
Kwa hofu kubwa niliingiza mkono mfukoni
huku nikiwa bado nimekodoa macho, nikagundua kwamba kulikuwa na kitu kwenye
mfuko wangu ambacho sikuwa najua ni kitu gani.
Mbaya zaidi, sikujua ni nani aliyekiweka
kwenye mfuko wa nguo yangu kwa sababu wakati naingizwa na wale askari,
waliniambia pale kaunta nitoe kitu chochote nilichokuwa nacho mfukoni na wala
sikuhitaji kujisachi kwa sababu nilikuwa najua sina chochote.
Cha ajabu, nilipokigusa kitu hicho tu, kiliacha
kutetemeka lakini yote tisa, kumi ni kwamba nilianza kuona vitu vya ajabu mno.
Japokuwa mle ndani kulikuwa na giza, niliweza kuwaona watu wote vizuri, mpaka
sura zao utafikiri ilikuwa mchana, ila tofauti yake ni kwamba hakukuwa na
mwanga wenye uangavu kama wa mchana bali ulifanana kwa mbali na nuru ya
mbalamwezi.
Kwa wale tuliokulia vijijini nadhani
wanaelewa vizuri usiku wa mbalamwezi unavyokuwa, yaani unaweza kusema ni mchana
kabisa kwani vitu vyote vinaonekana japo siyo vizuri kama vile nilivyokuwa
naona mimi.
Nilianza kuwatazama mahabusu wenzangu
mmoja baada ya mwingine maana kama unavyojua, niliingizwa giza likiwa
limeshaingia na kwa sababu mle ndani hakukuwa na taa, watu pekee niliowaona
vizuri ni wale waliokuwa jirani na mimi.
Cha ajabu, wakati nikiendelea kuwatazama
mahabusu hao ambao wengi walishaanza kusinzia kutokana na uchovu, niligundua
kwamba kulikuwa na watu wengine wasio wa kawaida mle ndani, nao wakiwa
wamejichanganya na mahabusu lakini tofauti yao ilikuwa moja.
Karibu wote walikuwa na macho mekundu
sana na walikuwa wakinitazama kama wanaosubiri kuona nitafanya nini lakini
kubwa, wote walikuwa watupu kabisa. Nilipopiga jicho harakaharaka na kujaribu
kuwahesabu, walikuwa kama saba hivi, tena wengine wawili walikuwa ni wanawake
na kama unavyojua mahabusu huwa hawachanganywi wanawake na wanaume.
Wote waliacha kila walichokuwa
wanakifanya, wakawa wananitazama kwa macho makali. Sikuelewa nini hasa
kimetokea, wakati nikiendelea kuwatazama vizuri kwa mara ya pili, kuna jambo
moja lilinishtua mno mpaka nikajikuta nimetoa mkono mfukoni, giza likarudi kama
lilivyokuwa mwanzo.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment