ILIPOISHIA:
Nilikuja
kugundua kuwa huenda tunaelekea Mwananyamala Hospitali baada ya kuumaliza Mtaa
wa Makumbusho na kushika Barabara ya Mwananyamala, moyoni nilianza kugubikwa na
maswali mengi, nilijiuliza kama ni kweli nilipelekwa katika Hospitali hiyo ilikuwa
ni kufanya nini?
SASA
ENDELEA…
“Tumekuleta huku hospitalini kwa sababu kwanza
maelezo uliyoyatoa kituoni, kwa kiasi fulani yanapishana na maelezo aliyoyatoa
huyu mgonjwa kwa sababu wewe ulisema humfahamu kwa undani zaidi ya kuanza
kuwasiliana naye kwenye simu siku chache zilizopita.
“Lakini yeye amesema wewe ni mpenzi wake wa siku
nyingi, mna mipango ya kufunga ndoa na tayari ana ujauzito wako,” alisema
askari mmoja wa kike, miongoni mwa wale waliokuja kunichukua mahabusu, wakati
huo tukiwa tayari tumeshawasili Hospitali ya Mwananyamala.
Akaendelea: “Lakini kingine ni kwamba amekataa kutoa
ushirikiano wa kueleza nini kilichotokea mpaka wewe uwepo ndiyo maana
tumekufuata, hutakiwi kuzungumza chochote, umenielewa?”
Nilitingisha kichwa kuonesha kukubali kile
alichokisema. Mfululizo wa matukio ya kushangaza ulikuwa unaendelea,
nilijiuliza iweje tena Shenaiza awaeleze polisi kwamba mimi nilikuwa mpenzi
wake na kwamba tulikuwa na mipango ya kufunga ndoa?
Yote tisa, kumi nilijiuliza iweje awaambie kwamba
alikuwa na ujauzito wangu wakati hatukuwahi kukutana kimwili hata mara moja?
Kama kweli alikuwa mjamzito, mimi nilikuwa nahusikaje? Nilikosa majibu.
“Jamal! Ooh my God! Thanks for coming my dear,”
(Jamal! Ooh Mungu wangu, ahsante kwa kuja mpendwa wangu) alisema Shenaiza kwa
sauti ya chini akionesha kwamba yupo kwenye maumivu makali, alizungumza kwa
Kiingereza kizuri huku akitanua mikono yake kama ishara ya kunitaka
nimkumbatie.
Sikuwahi kumsikia akizungumza Kiingereza, nikabaki
na swali jingine lakini sikutaka kumuonesha chochote, nikalilazimisha tabasamu
usoni kwangu, nikamuinamia pale kitandani alipokuwa amelala, dripu ikiendelea
kutiririka kwa kasi kuingia mishipani mwake, nikamkumbatia, akanibusu shavuni
na kuning’ang’ania kifuani kwake, tukiwa kwenye hali hiyo alinibusu mdomoni na
kunifanya nijisikie aibu ndani ya moyo wangu.
Kwa jinsi alivyokuwa akinidekea, mtu yeyote angeweza
kuamini kwamba kweli sisi ni wapenzi wa muda mrefu, nikageuka na kumtazama yule
askari ambaye moyoni ni kama alikuwa anasema ‘unabisha nini sasa? Kama siyo
mpenzi wako angekubusu mdomoni?’.
“Please help me Jamal, they want to kill me! You are
my only savior,” (Tafadhali nisaidie Jamal, wanataka kuniua! Wewe ndiyo
mkombozi wangu wa pekee) alisema Shenaiza kwa sauti ya chini akiwa bado
amenikumbatia. Japokuwa yule askari alikuwa mita chache tu kutoka pale
kitandani, hakuweza kusikia chochote.
Kwa kuwa nilishaambiwa sitakiwi kuzungumza chochote,
sikumjibu chochote zaidi ya kumtazama usoni huku nikiwa na shauku kubwa ya
kutaka kujua hao anaosema wanataka kumuua ni akina nani na ilikuwaje mpaka watake
kumuua?
“Inatosha sasa, hebu kaa pembeni. Binti, naamini
sasa utatoa ushirikiano maana uliyekuwa unamtaka tumeshamleta,” alisema yule
askari huku akinielekeza kukaa pembeni ya kitanda cha mgonjwa, akarudi
kinyumenyume na kufungua mlango, askari wengine watatu, akiwemo yule
aliyenihoji mimi wakaingia na kusimama kwa kutuzunguka.
Yule askari wa kike akawaeleza jambo kwa sauti ya
chini ambayo mimi na Shenaiza hatukusikia kisha tukawaona wote wakitoka,
akabaki yule mmoja aliyenihoji mimi siku iliyopita, mkononi akiwa na ‘diary’,
akavuta kiti na kukisogeza karibu na pale Shenaiza alipokuwa amelala.
“Si umeshaambiwa maelezo yote kwamba hutakiwi
kuzungumza chochote?” yule askari ambaye nilishamtambua kwamba ni mpelelezi,
aliniambia.
“Ndiyo.”
“Oke vizuri, binti unaendeleaje?”
“Naendelea vizuri,” alijibu Shenaiza, akamwambia
anataka kuanza upya kumhoji na anaamini atatoa ushirikiano kwa sababu mimi
nilikuwepo.
“Jina lako kamili unaitwa nani?”
Shenaiza alinitazama kabla ya kuanza kujibu,
akanionesha ishara ambayo sikuielewa, nikabaki kumtazama tu huku na mimi nikiwa
na shauku kubwa ya kutaka kusikia maelezo yake maana kiukweli hata mimi sikuwa
namfahamu kwa undani.
“Shenaiza Petras Loris,” alijibu Shenaiza.
Nilishangazwa na jina lake, sikuwahi kusikia Mtanzania yeyote akiwa na jina
hilo, akilini nikaanza kupata majibu kwamba kile nilichokuwa nakihisi awali
kwamba msichana huyo hakuwa Mtanzania kutokana na mwonekano wake kilikuwa
kweli.
Yule askari aliendelea kumhoji maswali kama polisi
wote wanavyofanya, akafikia swali la kabila na utaifa wake, Shenaiza
akanitazama tena na kushusha pumzi ndefu kisha akamjibu:
“Kabila langu ni Aethikes,” alijibu, yule askari
akapigwa na butwaa na kuacha kuandika, akamtazama Shenaiza kwa muda kisha
akanigeukia na mimi, mshangao aliokuwa nao ulikuwa sawa na niliokuwa nao mimi.
‘Bini, hebu kuwa ‘serious’, hilo ndiyo kabila gani?
Tangu nianze kufanya kazi huu mwaka wa kumi sasa sijawahi kusikia kabila kama
hilo hapa Tanzania, hebu taja kabila lako,” alisema yule askari kwa sauti
iliyoonesha kutokuwa na hata chembe ya masihara.
“Mimi siyo Mtanzania, natokea Greece (Ugiriki),
asili yetu ni Attica, baba yangu amezaliwa na kukulia kwenye Jiji la Athens
lakini mama yangu ni mpare wa Mtae, Lushoto mkoani Tanga ndiyo maana unaona
naweza kuzungumza Kiswahili vizuri,” alisema msichana huyo huku akionesha
kujiamini mno.
Nilimuona yule askari akiandika maelezo hayo kwenye
‘diary’ yake, akaendelea kumhoji maswali mengine ambapo niligundua kwamba
msichana huyo, alikuwepo nchini kisheria na kubwa zaidi, kumbe alikuwa ni
mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mahojiano yaliendelea, kikafikia kipengele cha
muhimu ambacho ndiyo hasa nilichokuwa nakisubiri kwa shauku kubwa, cha kutaka
kujua nini kilitokea mpaka msichana huyo mrembo akajeruhiwa vibaya na kwenda
kulazwa Hospitali ya Amana kabla ya mimi kumsaidia kutoroka mpaka nyumbani
kwangu, na kile kilichokuwa kimetokea nyumbani kwangu usiku.
Shenaiza alivuta pumzi ndefu baada ya kuulizwa swali
hilo, akazishusha kisha akatulia, ukimya mkubwa ukapita kati yetu mle wodini.
Ilibidi yule askari avunje ukimya na kurudia tena kumuuliza swali lile lakini
badala ya kutoa majibu kama alivyokuwa akifanya kwa maswali yote, alikaa kimya
huku machozi mengi yakimtoka na kulowanisha uso wake.
‘Kijana hebu naomba utupishe mara moja, toka nje
nitakuita,” alisema yule askari, ikabidi nitii, nikawaacha wenyewe wawili mle
wodini.
Je,
nini kitafuatia? Usikose Jumatatu kwenye Gazeti la Championi Jumatatu.
No comments:
Post a Comment