ILIPOISHIA:
“TOGO,” nilisikia sauti
nzito ya baba ikiniita, harakaharaka nikamtoa Rahma, kila mmoja akawa anahaha
kujiweza vizuri.
“Togooo,” alirudia
kuniita, mapigo ya moyo yakawa yananienda mbio mno huku mdomo ukiwa mzito
kufunguka.
SASA ENDELEA…
“NAAM!”
“Hebu sogea hapa
dirishani,” alisema baba, harakaharaka nikavaa nguo zangu, Rahma naye akawa
ameshavaa nguo zake na bila kujali atakutana na nani nje, alitoka kwa kasi.
“Wewe Togo, si nimekwambia
sogea hapa?” alisema baba, safari hii akigonga kioo cha dirisha. Kwa kuwa
tayari nilishavaa, nilisogea pale dirishani na kufunua pazia pamoja na dirisha
moja, nikamuona baba amenikazia macho.
“Unafanya nini?”
“Nilikuwa nafanya mazoezi
ya kupiga pushapu.”
“Kweli?”
“Kweli baba.”
“Hebu funua pazia lote,”
alisema baba, kwa kuwa nilikuwa na uhakika Rahma ameshatoka, nilifunua pazia
lote, akatazama huku na kule kisha akarudi kunitazama usoni.
“Mwanangu Togo, mbona
tangu tumeanza safari umekuwa ni mtu wa kututia aibu kila sehemu? Una
nini kwani wewe?”
“Mama sasa kwani mi
nimefanya nini? Ina maana hata kufanya mazoezi ndani nako ni makosa?” nilimjibu
mama ambaye kumbe alikuwa na baba kule nje, nikavaa uso wa huruma ili kuwafanya
waniamini kile nilichokuwa nakisema.
“Hivi unatufanya sisi wote
ni watoto wadogo kama wewe?” alisema baba huku akiwa amekazia macho suruali
niliyokuwa nimevaa, ikabidi na mimi nijiangalie. Cha ajabu, suruali niliyokuwa
nimevaa nilikuwa nimeigeuza nje ndani, aibu niliyoihisi ilikuwa kubwa mno,
ikabidi niliachie pazia na kurudi kitandani huku nikikosa cha kujibu.
“Nitasema wakati wa kuvaa
nimevaa harakaharaka, bado nitaendelea kukataa kwamba sijafanya chochote,”
nilijisemea huku nikiivua ile suruali na kuivaa vizuri. Kwa kuwa mwanzo Rahma
alipokuja aliniambia kwamba chai ipo tayari, ili kuzidi kupoteza ushahidi,
niliamua kupitia kwanza bafuni kabla sijaenda sebuleni.
Nikanawa uso harakaharaka
na kutoka kuelekea sebuleni, bado wale mafundi walikuwa wakiendelea kutengeneza
mlango na nahisi walikuwa wanajua kilichokuwa kinaendelea kati yangu na Rahma
kwa sababu wakati natoka bafuni, wote waliacha kila walichokuwa wanakifanya na
kunitazama usoni, wakionyesha dhahiri kwamba walikuwa na shauku ya kunijua.
Sikuwasemesha kitu, hata
salamu sikuwapa, nikapitiliza moja kwa moja mpaka sebuleni ambako niliwakuta
karibu watu wote wakiwa wanakunywa chai isipokuwa wazazi wa pande zote mbili,
kwa maana ya baba na mama yetu na baba na mama yao akina Rahma, kila mmoja
akiwa na kikombe chake na vitafunwa vyake.
Kabla hata sijakaa, Rahma
aliinuka na kunichukulia kikombe, akanimiminia chai na kunisogezea pale
nilipokuwa nimekaa pamoja na vitafunwa. Watu wote walikuwa kimya kabisa, macho
yakiwa kwenye runinga kubwa ya kisasa.
Wakati akinisogezea chai,
Rahma alinitazama kwa macho ya kuibia, na mimi nikamtazama, macho yetu
yakagongana ambapo nilimuona akiachia tabasamu pana huku aibu za kikekike
zikiwa zimetawala kwenye uso wake.
Hakutaka kurudi kukaa pale
alipokuwa amekaa awali, alichukua kikombe chake cha chai na kuja kukaa pembeni
yangu, nikawaona ndugu zangu, akiwemo dada Sabina wakinitazama kwa macho ya
chinichini.
Ukimya uliendelea
kutawala, tukaendelea kunywa chai na baada ya kumaliza, Rahma na dada Sabina
waliinuka na kuanza kutoa vyombo, tayari kwa ajili ya kwenda kuviosha lakini
ghafla mama aliingia akiwa ameongozana na mama yake Rahma. Kwa kuwatazama tu
sura zao, ilionyesha kuna jambo halikuwa sawa.
“Togo, njoo huku,” alisema
mama, mama yake Rahma naye akamuita Rahma, ikabidi aache kutoa vyombo, wote
tukaelekea kule nje ambako tulikuta wazazi wetu wakiwa wamekaa kwenye viti
vilivyokuwa pale nje, wote wakionyesha kutokuwa na furaha kwenye nyuso zao.
“Hebu tumbieni, hivi Togo
na Rahma mlikuwa mnafahamiana kabla?” aliuliza baba yake Rahma, muda mfupi tu
baada ya sisi kufika.
“Hapana,” nilisema huku
nikitingisha kichwa.
“Mbona ndani ya muda mfupi
tu tangu mkutane mmekuwa na nyendo zinazotutia mashaka? Hivi mnajua kama nyie
ni ndugu?” alisema baba yake Rahma na kunifanya nishtuke.
Alichokuwa ametuambia
baba, ni kwamba baba yake Rahma alikuwa ni rafiki yake wa siku nyingi ambaye
walishirikiana vitu vingi pamoja na ndiyo maana hata alipoona mambo hayaendi
vizuri kule Chunya, majirani na wanakijiji wakiituhumu familia yetu kuwa
inajihusisha na Imani za kishirikina aliamua kuondoka na sisi mpaka jijini Dar
es Salaam.
“Sikuwa nimewafafanulia
mwanzo lakini ukweli ni kwamba ukiacha urafiki wetu, sisi ni ndugu, mama yangu
kwa maana ya bibi yenu na mama mzazi wa baba Rahma ni mtu na mdogo wake, kwa
hiyo sisi ni ndugu na nyie ni ndugu, tena wa damu kabisa,” alisema baba, kauli
ambayo ilinishtua mno.
“Msije mkatuletea aibu ya
mwaka hapa maana naona mmeshaanza kuonyesha kupendana, nyie ni ndugu na kwa
ukoo wetu sisi ndugu wakifanya dhambi kama hiyo, husababisha mabalaa makubwa
sana kwenye ukoo mzima,” baba yake Rahma alizidi kupigilia msumari.
Japokuwa ilikuwa ni
asubuhi, nilijikuta kijasho chembamba kikinitoka, lilikuwa ni jambo ambalo
sikulitegemea kabisa, nikageuka na kumtazama Rahma, nikamuona akiwa amejiinamia
kwa aibu.
Sikuwahi kuwa na skendo
yoyote ya mapenzi na hata wazazi wangu hawakuwahi kusikia jambo lolote baya
kuhusu mimi lakini cha ajabu, ndani ya muda mfupi tu niliokutana na Rahma na
kunionjesha ulimwengu wa kikubwa, tayari kila mtu alikuwa na wasiwasi na mimi. Nilijisikia
aibu sana.
“Mmeelewa?” alihoji baba,
nikajibu kwa kutingisha kichwa, wakatuambia tukaendelee na tulichokuwa
tukikifanya, wakati tukiondoka tukawasikia wakipiga stori na kucheka, nadhani
baba alizungumza kitu kuhusu mimi kilichowavunja mbavu wote.
Tulipoingia sebuleni,
tulikuwa kama tumemwagiwa maji ya baridi, afadhali mimi kidogo niliweza
kujikaza, Rahma alionyesha kuchoka mno, macho yakawa mekundu kama anayetaka
kulia.
Hakuweza kuendelea kukaa
pale sebuleni, nilimuona akiinuka kwa unyonge, akaelekea chumbani kwake ambapo
tayari mafundi walikuwa wamemaliza kutengeneza mlango wa chumba chake, akaingia
ndani na kujifungia.
Sikumuona tena akitoka
mpaka muda wa chakula cha mchana, mimi na ndugu zangu tukawa tunaendelea
kushangaa runinga na vitu vingine vya kisasa vilivyokuwa mle ndani.
Baada ya chakula cha
mchana kuiva, mama yake Rahma alimtuma mdogo wake kwenda kumuita chumbani kwake
wakati chakula kikipakuliwa. Muda mfupi baadaye, alikuja na majibu kwamba dada
yake alikuwa amelala chumbani lakini alipojaribu kumuamsha, hakuamka.
“Unasema?” mama yake Rahma
aliuliza kwa mshtuko, huku akiacha kila alichokuwa anakifanya. Haraka
akakimbilia chumbani kwa mwanaye, huku akionyesha kuwa na wasiwasi mkubwa
moyoni mwake, mama naye akamfuata, na mimi uzalendo ukanishinda, nikainuka na
kuwafuata.
Je, nini kitafuatia?
Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Championi Jumatatu.
No comments:
Post a Comment