ILIPOISHIA
“MUNGU wangu, hivi wewe mtoto
una akili timamu kweli?” alisema baba huku akionyesha kushtuka mno, akageuka na
kumuonyesha ishara baba yake Rahma kwamba aje, harakaharaka akaja mpaka pale
tulipokuwa tumesimama.
SASA ENDELEA...
“UNASIKIA majanga ya huyu
mtoto aliyoyazua tena?”
“Kuna nini?”
“Eti alikuwa kujitolea damu.”
“Mungu wangu, kwani hujawahi
kumwambia ukweli?”
“Ukweli? Ukweli gani?”
niliuliza kwa mshtuko.
“Wewe ni mpuuzi sana, yaani
hili halijaisha unaanzisha jingine, kwa hiyo tutakuwa na kazi ya kurekebisha
makosa yako tu muda wote,” baba alisema kwa kufoka, baba yake Rahma akawa
anamtuliza na kumkumbusha kwamba kuna kazi hawajaimaliza.
“Huyu ndiyo ilitakiwa
akaifanye hiyo kazi lakini ameshaharibu tena, unafikiri itakuwaje?”
“Twende tu tutajua hukohuko,”
alisema baba Rahma huku akinishika mkono, akanipeleka mpaka kwenye gari aina ya
Toyota Noah lililokuwa limepaki jirani na geti la kutokea. Kumbe tayari Rahma
alishatolewa wodini na alikuwa ameshaingizwa ndani ya gari, mama na mama Rahma
wakawa wamempakata.
Tulipoingia tu, gari
liliwashwa na kuondoka, mama akageuka na kunitazama kwa uso wa huzuni kama
anayeniuliza ‘ulikuwa wapi?’
Nilikaa na kutulia kimya,
safari ikaendelea. Watu wote walikuwa kimya kabisa ndani ya gari, sauti pekee
iliyokuwa inasikika, ilikuwa ni ya Rahma aliyekuwa anakoroma. Dereva aliendesha
gari kwa kasi na baada ya takribani dakika thelathini, tayari tulikuwa tumefika
nyumbani.
Siku hiyo hata sikuwa na hamu
ya kulishangaa jiji, maghorofa yote ambayo awali nilikuwa na hamu ya kuyatazama
jinsi yalivyo marefu na yenye kuvutia, hayakuwa na maana tena kwangu.
Baba na baba yake Rahma
walisaidiana kumshusha mgonjwa na moja kwa moja wakampeleka chumbani kwake.
“Nenda bafuni kaoge, usitumie
sabuni, utatumia hii badala ya sabuni,” alisema baba huku akinipa kitu kama
jiwe laini lenye rangi nyekundu.
Nikageuka na kuanza kuelekea
chumbani kwangu kwa lengo la kubadilisha nguo kwanza.
“Unaenda wapi tena?
Nimekwambia kaoge, moja kwa moja bafuni nakuja hukohuko,” alisema baba kwa
sauti iliyoonyesha kutokuwa na masihara hata chembe. Nilitii alichoniambia,
kauli yake kwamba ‘dawa’ ya kumtibu Rahma nilikuwa nayo mimi, ikaanza kujirudia
kichwani.
Nilipofika mlangoni, nilivua mabuti
yangu, maana siwezi kuita viatu bali mabuti kutokana na jinsi muundo wake
ulivyokuwa. Kule kwetu kijijini mabuti hayo yalikuwa yakivaliwa siku za sikukuu
au kunapotokea safari kama hiyo tu lakini siku nyingine zote, mimi na wenzangu
tulikuwa tukitembea pekupeku, si unajua maisha ya kijijini tena.
Basi niliyavua pale mlangoni
na kuvaa ndala, nikaingia bafuni na kuvua nguo, nazo nikazitundika kwenye
misumari maalum na kusogea kwenye bomba. Safari hii sikutaka kutumia bomba la
mvua kwani tangu niliposhtukia nikioga damu badala ya maji, nilikuwa na hofu
kubwa ndani ya moyo wangu.
Nilichoamua ni kuoga kwa
kutumia maji yaliyokuwa kwenye ndoo ya kuogea, nikajimwagia mwilini kwa kutumia
kopo kisha nikaanza kujipaka ile dawa aliyonipa baba. Cha ajabu, nilipokuwa
nikijipaka, ilikuwa ikitoa povu kama sabuni na ilikuwa na harufu fulani isiyo
ya kawaida.
Yote tisa, kumi ni kwamba
nilipojimwagia maji tena juu ya ile dawa, nilishangaa maji yaliyokuwa yakitoka
mwilini mwangu yakiwa meusi kama maji yaliyochanganywa na mkaa au masizi. Mara
ya kwanza nilihisi kama nipo ndotoni, nikakodoa macho lakini ndiyo ulikuwa
ukweli.
Ilibidi niendelee kujimwagia
maji kwa wingi na kadiri nilivyokuwa nazidi kujimwagia, ndiyo ule weusi
ulivyokuwa ukizidi kupungua. Nilijipaka kwa mara ya pili na kujimwagia maji,
bado uchafu mweusi ukawa unanitoka kwa wingi, nikawa najimwagia maji kwa wingi
mpaka ulipoisha kabisa.
“Ina maana mimi ndiyo
nilikuwa mchafu kiasi hiki? Halafu huu ni uchafu gani unakuwa mweusi kiasi
hiki?” nilijiuliza maswali mengi yasiyo na majibu. Wakati naendelea kuoga,
nilisikia mlango ukigongwa, ukafuatiwa na sauti ya baba.
Iweje baba anifuate bafuni?
Alikuwa anataka kufanya nini? Nikiwa bado najiuliza maswali, nilisikia tena
sauti ya baba akinilazimisha nifungue mlango. Ikabidi nifungue kidogo na
kumchungulia.
“Umetumia hiyo dawa?”
“Ndiyo.”
“Umeona nini?”
“Maji meusi kama ya mkaa
yalikuwa yananitoka.”
“Safi, sasa vaa hii,” alisema
baba huku akinyoosha mkono na kupenyeza kitambaa cheupe kupitia ule upenyo
mdogo niliouacha. Akanisisitiza kwamba nisiziguse kabisa nguo zangu, nijifunge
na yeye ananisubiri nje.
Nilirudisha mlango na
kuufunga vizuri, nikawa nakitazama kile kitambaa alichonipa. Japokuwa sikuwa
mzoefu wa shughuli za mazishi kiasi hicho, niliweza kukitambua vizuri kitambaa
hicho kwamba kilikuwa ni sanda. Ninavyofahamu mimi, sanda huvalishwa maiti,
sasa baba alikuwa na maana gani kuniambia nivae sanda?
Sikupata majibu. Nikawa
naendelea kuishangaa sanda hiyo huku mapigo ya moyo yakinienda mbio kuliko
kawaida. Nikiwa bado katika hali ile, nilisikia baba akigonga tena mlango kwa
nguvu, akaniambia ananisubiri.
Ilibidi niivae harakaharaka,
kisha nikafungua mlango. Baba alinitazama kuanzia juu hadi chini,
akanirekebisha sehemu ambazo sikuwa nimejifunga vizuri, akatoa kipande kingine
na kunifunga kichwani, akanisogelea sikioni na kuniambia:
“Upumbavu uliofanya ndiyo
uliotufikisha hapa tulipo. Lazima ufanye kila kinachowezekana kuokoa maisha ya
Rahma. Kwa hiyo, utalazimika kufanya kile nitakachokwambia bila kuhoji
chochote, ukikosea masharti Rahma atakufa na wewe ndiyo utakuwa umemuua,
hutakiwi kuzungumza chochote mpaka tutakapomaliza hii kazi,” alisema baba kwa
sauti isiyokuwa na masihara hata kidogo.
Nilizidi kutetemeka, yaani
mimi ndiyo niwe nimemuua Rahma? Kwa lipi? Hata hivyo, kwa kuwa ndani ya moyo
wangu, licha ya yote yaliyotokea nilishatokea kumpenda mno Rahma,
nilichojiapiza ni kwamba nitafanya kila kinachowezekana kuhakikisha naokoa
maisha yake.
“Nifuate,” alisema baba huku
akigeuka, akawa anatembea kwa hatua ndefundefu, alipofika kwenye mlango wa
chumba cha Rahma, aliniambia nigeuke na kuupa mlango mgongo.
“Utaingia kinyumenyume mpaka
ndani,” alisema baba, bado kidogo nimuitikie ‘sawa’ lakini nikakumbuka
alichoniambia kwamba sitakiwi kuzungumza chochote. Alitangulia, akafungua
mlango, nikamfuata kinyumenyume kama alivyonielekeza.
“Chumba kizima kilikuwa
kimefukizwa ubani wenye harufu kali, alinipa ishara kwamba niendelee kutembea
kinyumenyume mpaka aliponipa ishara kwamba nisimame, nikageuka na kutazama pale
kitandani. Rahma alikuwa amelala, damu nyingi zikiendelea kumtoka na
kulowanisha kitanda kizima.
Hakuwa na nguo yoyote mwilini
zaidi ya kipande cha sanda alichokuwa amefunikwa kuanzia juu kidogo ya mapaja
mpaka kifuani ambacho nacho kilikuwa na damudamu.
Baba akanitazama usoni, na
mimi nikamtazama nikiwa na shauku kubwa ya kusikia kile atakachoniambia.
Nilikuwa tayari kwa chochote ilimradi Rahma apone.
Je, nini kitafuatia? Usikose
next issue.
No comments:
Post a Comment