ILIPOISHIA:
“Kuna tukio baya linataka kutokea, kuwa
makini,” nilisikia sauti ya baba ikiniongelesha sikioni mwangu, nikageuka huku
na kule, baba hakuwepo, nikajua kwa vyovyote lazima alikuwa ameona jambo ndiyo
maana akanipa tahadhari, nikajiweka vizuri kitini, nikawa natazama huku na
kule.
SASA ENDELEA...
Niliingiza mkono mfukoni na kutoa ile
dawa aliyonipa baba, nikaishika ili chochote kikitokea iwe rahisi kufanya kama
nilivyoelekezwa. Tukaanza kuteremka kwenye mteremko mrefu, wenye konakona
nyingi na makorongo ya kutisha wa Kitonga.
Nilielewa kwa sababu gani eneo hilo
lilikuwa maarufu sana, barabara ilikuwa imechomngwa pembezoni mwa milima na
mawe makubwa, hali iliyofanya kama upande mmoja kukiwa na ukuta wa mlima basi
upande wa pili kuna bonde refu sana.
Yaani kwa kutazama tu urefu wa yale
makorongo, nilijikuta nikihisi kizunguzungu, nikawa najiuliza ikitokea dereva
akakosea na kupeleka gari kwenye yale makorongo nini kitatokea? Sikupata majibu.
Safari iliendelea, dereva akawa
amepunguza sana mwendo, abiria wote ndani ya gari wakiwa kimya kabisa. Nadhani
kila mmoja alikuwa na kumbukumbu ya kilichotokea Mlima Nyoka. Ghafla tulishtuka
baada ya kuona kuna lori la mafuta, tena likiwa na trela kwa nyuma, likija kwa
kasi kubwa nyuma yetu.
Tulishtushwa na kishindo kikubwa
kilichosikika nyuma, wote tukageuka na kusimama kwenye siti, tukawa tunatazama
nini kinachoendelea? Inavyoonesha, lile lori lilikuwa limepasuka tairi la mbele
na kumshinda dereva, sasa likawa linayumba barabara nzima.
Abiria wote walianza kupiga kelele
kwenye lile basi, hakuna ambaye alijua nini kitatokea kwa sababu kama lile gari
lori lingeendelea kuja kwa mwendo ule, lingeligonga basi letu kwa nyuma na kwa
ile kasi yake, maana yake lingeturushia kwenye korongo refu na kutuangukia kwa
juu.
Sijui kama kuna mtu angepona,
ukizingatia kwamba lilikuwa ni lori la mafuta na lilionesha kuwa na mzigo.
Nilichokifanya, kwa haraka nilimnyunyizia ule unga dereva ambaye bado hakuwa
akijua afanye nini. Nilipomnyunyizia tu, nilimuona akibadili gia haraka,
akaongeza mwendo na kulifanya basi lianze kushuka mteremko ule kwa kasi kubwa.
Kuongeza kasi kwa ghafla kuliwafanya
abiria wengine wazidi kuchanganyikiwa, kelele zikazidi ndani ya basi, lile lori
nalo likawa linazidi kuja kwa kasi kubwa nyuma yetu.
Wakati dereva akizidi kukanyaga mafuta
na kulifanya basi lishuke kwa kasi ya ajabu mteremko ule hatari, ghafla
tulishtukia lori jingine likiwa limepaki mbele yetu, dereva na utingo wake
wakiwa wamekata matawi ya miti na kusambaza barabarani, ishara kwamba lilikuwa
limeharibika.
Kwa kasi ambayo gari tulilopanda
lilikuwa likishuka nayo, hata mimi mwenyewe sikuamini kama dereva ataweza
kulimudu na kulikweopa lile lori mbele yetu.
Hata hivyo, dereva alitumia kile ambacho
wengi huita uwezo binafsi, bila kupunguza mwendo hata kidogo, alizungusha
usukani kwa kasi, gari likageuka kama linaenda kugonga jiwe kubwa lililokuwa
pemebini ya barabara, kisha akazungusha tena usukani kwa kasi, gari likageuka
tena upande wa pili.
Kitendo kile kililifanya basi letu
lipenye kwenye uwazi mwembamba uliokuwepo kati ya lile gari lililoharibika na
ukuta wa upande wa pili, kufumba na kufumbua likapita pale katikati kwa kasi
kubwa na kulipita lile gari bovu, dereva akaanza kupunguza mwendo huku
akibadilisha gia.
Sekunde chache baadaye, kilisikika
kishindo kikubwa nyuma yetu, lile lori la mafuta lilikuwa limeligonga lile lori
jingine bovu kwa nyuma na kulisukuma mita kadhaa kabla ya yote mawili kuangukia
kwenye korongo refu, watu wote wakawa hawaamini kilichotokea.
Cha ajabu sasa, wakati watu wote
wakitazama kilichotokea kule nyuma, nilishtuka kugundua kwamba kumbe aliyekuwa
akiendesha gari hakuwa yule dereva wetu bali baba, macho yakanitoka pima nikiwa
siamini ninachokiona. Alipogundua kwamba namtazama, naye alinigeukia na
kunitazama kwa sekunde chache, akawa aanendelea kubadili gia huku akifunga
breki.
Mbele kidogo kulikuwana uwazi pembeni ya
barabara ambao uliwekwa maalum kwa ajili ya magari yanayoharibika njiani, akaendelea
kufunga breki na hatimaye, akalisimamisha kabisa basi letu. Wakati watu bado
wakiwa bize kushangaa kule nyuma, alifungua mlango wa dereva, akashuka huku
akiendelea kunitazama na kunionesha ishara kwamba nisiseme chochote.
Akapotea kwenye upeo wa macho yangu na
kuniacha na maswali mengi yasiyo na majibu. Cha ajabu kingine, aliposhuka, pale
kwenye siti ya dereva alikuwa amekaa dereva yuleyule, tena akiwa amefunga na
mkanda kabisa lakini kama ilivyokuwa mara ya kwanza, naye alionesha kushtuka
kama mtu aliyekuwa amelala usingizi mzito. Akageuka huku na kule, macho yangu
na yake yakagongana.
‘Kwani kumetokea nini?” aliniuliza kwa
sauti ya chini huku akitaka mtu mwingine yeyote asielewe. Nadhani hata yeye
alishagundua kwamba kuna mambo yasiyo ya kawaida yalikuwa yakiendelea.
“Ajali, ajali mbaya sana,” nilimjibu
huku nikimuonesha kule nyuma tulikotoka ambako moshi mzito mweusi ulikuwa
ukifuka kutoka bondeni. Tayari abiria wengi walikuwa wameshashuka kwenye basi
na kuanza kurudi kule eneo la tukio. Harakaharaka dereva alifungua mlango na
kushuka, na mimi ikabidi nishuke tena safari hii nilipitia pale kwenye mlango
wa dereva.
Tukawa tunakimbilia pale eneo la tukio.
Trela moja la lile lori la mafuta, lilikuwa limekatika na kuanguka katikati ya
barabara kimshazari, jambo lililofanya mawasiliano kati ya pande hizo mbili za
barabara yakatike. Hakukuwa na gari ambalo lingeweza kuvuka tena mpaka trela
lile liondolewe.
Ajali ilikuwa mbaya kiasi cha kumfanya
kila mmoja aliyeshuhudia, ainue mikono yake juu na kumshukuru Mungu kwa sababu
kama isingekuwa miujiza iliyotokea, ilibidi basi letu ndiyo ligongwe na
kuangukia kule bondeni kisha kuanza kuungua kama ilivyokuwa imetokea.
Tukiwa bado tunaendelea kushangaa
kilichotokea, tulishangaa kuona mtu akitoka ndani ya lile lori la mafuta lakini
mwili wake wote ukiteketea kwa moto, akawa anajaribu kukimbia lakini hakufika
mbali, moto ukamzidi na kumfanya aanguke chini.
Kwa jinsi magari hayo yalivyodondokea
chini bondeni, hakuna mtu yeyote ambaye angewahi kwenda kumsaidia yule mtu kwa
sababu kwanza eneo lenyewe lilikuwa haliwezi kupitika kirahisi, watu wakawa
wanapiga kelele huku tukimshuhudia yule mtu ambaye sijui ndiyo alikuwa dereva
au utingo wa gari lililopata ajali akiteketea bila msaada wowote.
Muda mfupi baadaye, magari mengine mengi
yalishawasili eneo hilo na kwa sababu barabara ilikuwa imefungwa, yalisimama na
kupanga foleni ndefu, abiria na madereva wakawa wanashuka kuja kujionea
kilichotokea.
Kila aliyekuwa anaona kilichotokea,
alikuwa haamini kabisa. Ilikuwa ajali mbaya mno ambayo kama ingehusisha gari la
abiria, sidhani kama kuna mtu yeyote angetoka salama.
Kwa kuwa tulikuwa nyuma ya muda na bado
tulikuw ana safari ndefu, ilibidi turudi kwenye basi letu, dereva naye akawa
anaonekana kuwa na maswali mengi kuliko majibu.
Japokuwa kwa mara nyingine abiria wote
walikuwa wakimsifia kwa jinsi alivyoweza kuepusha ajali ile, mwenyewe alikuwa
akijua kutoka ndani ya moyo wake kwamba siyo yeye aliyefanya kazi hiyo na
hakuwa akijua chochote kilichotokea.
Tulirudi kwenye basi na baada ya
kuhakikisha abiria wote wameingia, dereva aliondoa gari kwa mwendo wa taratibu,
gumzo kubwa ndani ya basi likawa ni juu ya ajali hiyo. Wakati watu wakiendelea kujadiliana
kuhusu ajali hiyo, mimi bado nilikuwa na maswali mengi mno kuhusu baba.
Bado sikuwa na majibu na hakukuwa na mtu
yeyote wa kunijibu zaidi ya baba mwenyewe. Jambo kubwa ambalo lilikuwa
likijirudia ndani ya kichwa changu, lilikuwa ni je, kweli baba ni mchawi?
“Unasemaje?” nilisikia sauti ya baba
akiniuliza kwa ukali, nikageuka huku na kule lakini baba hakuwepo.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment