ILIPOISHIA:
Safari iliendelea mpaka tulipofika Magomeni ambako
kulikuwa na foleni kubwa sana asubuhi hiyo, jambo ambalo halikuwa la kawaida.
“Nimekwambia kwamba sijui kama tutafika salama,
umewahi kuona asubuhi namna hii kunakuwa na foleni kama hii?” alisema Shenaiza
huku akizidi kuonesha hofu kubwa ndani ya moyo wake, nikawa nazidi kumtuliza.
SASA ENDELEA…
Tulikaa kwenye foleni kwa zaidi ya dakika ishirini,
magari yakiwa hayaendi mbele wala hayarudi nyuma. Nilitegemea kwamba muda mfupi
baadaye askari wa usalama barabarani (trafiki) watafika na kusaidia kuondoa
foleni hiyo lakini haikuwa hivyo.
Madereva wengine walipochoka, walianza kupiga honi
kwa nguvu, huku wengine wakiteremka kwenye magari yao na kusogea upande wa
mbele kujaribu kuangalia kilichokuwa kinasababisha foleni hiyo.
“Nasikia kuna ajali huko mbele, hapa hatuwezi
kuondoka sasa hivi mpaka trafiki waje, wapime ajali yenyewe, wayatoe magari
yaliyopata ajali unafikiri itakuwa sasa hivi?” kondakta wa daladala
tuliyopanda, alisema na kutufanya abiria wote tuishiwe nguvu.
“Sasa tutafanyaje?”
“Inabidi tushuke tutembee kwa miguu, kule hospitali
wakishtukia kwamba nimetoroka wanaweza kuanza kutufuatilia na huenda wakatukamata
hapahapa, tuondoke,” alisema Shenaiza huku akisimama kwenye siti aliyokuwa
amekaa, na mimi nikasimama, tukamlipa kondakta nauli yake kisha tukashuka.
“Inabidi tutembee mpaka upande wa pili tukachukue
Bajaj au bodaboda,” alisema Shenaiza huku akizidi kujitanda ushungi wake ili
isiwe rahisi kwa mtu yeyote kumtambua, na mimi nilishusha kofia yangu ya pama,
tukawa tunatembea kuelekea kule kwenye Bajaj.
Tukiwa tunatembea katikati ya tuta la barabara
lililokuwa linatenganisha barabara mbili za lami, ghafla tulishtushwa na
muungurumo mkali wa pikipiki kubwa mbili zilizokuwa zinakuja upande wetu,
tukiwa hata hatujui zimetokea wapi.
“Tulijua lazima tutakupata tu, wewe ndiyo unajifanya
kimbelembele kuingilia ishu za watu si ndiyo?” alisema mwanaume mmoja kwa sauti
ya kukwaruza, wote wakiwa wamesimamisha pikipiki zao kubwa huku na kule na
kutufanya mimi na Shenaiza tubaki katikati, hofu kubwa ikanitanda ndani ya moyo
wangu.
Cha ajabu zaidi, wakati wakiwa wametuzunguka pale
barabarani, foleni ilianza kutembea, magari yakaanza kuondoka huku abiria
waliokuwa wameshuka, nao wakiingia kwenye magari na kuendelea na safari.
“Leave him alone, what wrong has he done? (Mwacheni,
kwani kuna jambo gani baya amefanya?) Kama mnanitaka mimi nichukueni lakini
siyo huyu kijana wa watu,” alisema Shenaiza lakini hakuna aliyemsikiliza,
ukichanganya na kelele za magari na vyombo vingine vya usafiri vilivyokuwa
vikiondoka baada ya foleni kuanza kutembea, hakuna mtu aliyejua kilichokuwa
kinaendelea.
“Siku nyingine hutakiwi kuingilia mambo yasiyokuhusu,”
alisema mwanaume mmoja huku akinisogelea, nikawa nazidi kutetemeka kwani kwa
jinsi hali ilivyokuwa, wangeweza kunifanya chochote wanachokitaka bila mtu
yeyote kujua kilichokuwa kinaendelea.
“Nimesema muacheni?” alisema Shenaiza lakini kabla
hata hajamalizia, mmoja kati ya wale wanaume wanne, alimtwanga ngumi nzito ya
usoni, akapepesuka na kutaka kudondoka lakini mwingine alimdaka na
kumsimamisha.
Hofu niliyoipata ilikuwa haielezeki, kama Shenaiza,
mwanamke mrembo kiasi kile alipigwa ngumi nzito kiasi kile, mimi je?
Nilijiuliza huku nikizidi kutetemeka, tayari nilishaanza kusikia harufu ya
mauti.
Ghafla iliibuka pikipiki nyingine ambayo tofauti na
zile nyingine, yenyewe ilikuwa na mtu mmoja tu, tena mwanaume aliyeonesha kuwa
na umri mkubwa kuliko wale wengine, akafunua kioo cha kofia ngumu (helmet)
aliyokuwa ameivaa, akanitazama kwa ukali, macho yangu yakagongana na yake.
Nilichokigundua, hakuwa Mtanzania na kwa kiasi
kikubwa, alikuwa na sura inayofanana na Shenaiza kwa mbali, jambo lililonifanya
niamini kwamba lazima atakuwa na uhusiano wa kindugu na msichana huyo, aliendelea
kunitazama bila kuzungumza kitu chochote.
Nikiwa bado naendelea kutetemeka, magari yaliyokuwa
kwenye foleni yakiwa yamepungua kabisa na eneo lote kurejewa na hali yake ya
utulivu, nilimuona yule mwanaume akiwapa ishara fulani wale watu waliooonesha
kuwa ni wafuasi wake, Shenaiza ambaye sasa alikuwa akivuja damu nyingi puani,
akabebwa juujuu na kupakizwa kwenye pikipki ya yule mwanaume kisha akaondoka
kwa kasi kubwa na kutokomea.
“Hili litakuwa funzo kwako na kwa watu wengine wenye
tabia kama yako, usipende kuwasogelea wanawake usiowajua,” alisema mmoja kati
ya wale wanaume, nikashtukia nikipigwa na kitu kizito kichwani, nikadondoka
mzimamzima kama gunia. Sikuweza hata kupiga kelele za kuomba msaada.
Nikiwa pale chini, kwa taabu nilimuona mwanaume
mmoja akichomoa kisu kikubwa na kunikalia, akakinyanyua na kukishindilia upande
wa kushoto wa kifua changu bila huruma. Siwezi kuyaelezea maumivu ambayo
niliyasikia, nikafumbua mdomo ili kupiga kelele za kuomba msaada lakini sauti
haikutoka, nikasikia wale watu wakipongezana kisha wakapanda kwenye pikipiki
zao na kuondoka kwa kasi.
Damu nyingi zilikuwa zinanitoka upande wa kushoto wa
kifua changu kiasi cha kunifanya nilowe chapachapa. Nilijitahidi kuinuka pale
nilipokuwa nimelala huku damu nyingi zikiendelea kunitoka lakini maumivu makali
yalinirudisha chini.
Kwa kutumia mikono yangu miwili, nilijaribu kuminya
pale kwenye jeraha kubwa ili kuzuia damu isiendelee kunimwagika lakini
nilijikuta mikono ikikosa nguvu, kadiri muda ulivyokuwa unasonga mbele ndivyo
nilivyokuwa nazidi kuishiwa nguvu.
Watu wengi walianza kukimbilia pale nilipokuwa
nimeanguka na kunizunguka, niliwasikia wengine wakishindwa kuficha hisia zao na
kuanza kuangua vilio. Nadhani hali waliyoniona nayo iliwafanya waamini kwamba
siwezi kabisa kupona kutokana na damu zilivyokuwa zinaendelea kunimwagika
mithili ya bomba lililopasuka.
Nikiwa kwenye maumivu makali, nilijigeuza na kuanza
kutazama angani, upeo wa macho yangu ukagota kwenye mawingu meupe na ya bluu
yaliyokuwa yakilipendezesha anga, nikabaki nimetulia nikiwa kwenye hali hiyo.
Kelele za watu wengi waliokuwa wanazidi kuongezeka
eneo la tukio kunishangaa, zilianza kupungua taratibu masikioni mwangu,
zikazidi kupungua na baadaye nikawa nasikia kama watu wananong’ona. Kwa mbali
nilisikia mlio wa ving’ora ambavyo hata hivyo sikujua ni vya nini.
Nikiwa naendelea kutazama angani, taswira ndani ya
mboni za macho yangu ilianza kufifia taratibu na kadiri muda ulivyokuwa unazidi
kusonga mbele ndivyo nayo ilivyozidi kufifia, japokuwa ilikuwa ni asubuhi,
kigiza kikaanza kutanda kwenye macho yangu.
Nakumbuka neno la mwisho nililofanikiwa kulisema,
ingawa ilikuwa ni kwa taabu kubwa kutokana na midomo yangu kuwa mizito, ilikuwa
ni: Mungu nisaidie! Nikafumba macho na giza totoro likatawala kila sehemu,
sikuelewa tena kilichoendelea baada ya hapo!
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment