ILIPOISHIA:
Ilibidi
yule askari avunje ukimya na kurudia tena kumuuliza swali lile lakini badala ya
kutoa majibu kama alivyokuwa akifanya kwa maswali yote, alikaa kimya huku
machozi mengi yakimtoka na kulowanisha uso wake.
“Kijana
hebu naomba utupishe mara moja, toka nje nitakuita,” alisema yule askari,
ikabidi nitii, nikawaacha wenyewe wawili mle wodini.
SASA
ENDELEA…
Nilihisi kichwa changu kikipata moto, nilikuwa na
shauku kubwa mno ya kutaka kuufahamu ukweli wa kilichokuwa kimemtokea Shenaiza.
Lile swali la awali kwamba yeye ni nani, tayari nilishapata majibu kwa kiasi
fulani lakini bado nilitaka kujua nini hasa kilichomtokea.
Mazungumzo kati ya Shenaiza na yule mpelelezi kule
ndani yaliendelea kwa muda na baada ya kama dakika kumi na tano kupita, mlango
ulifunguliwa na yule mpelelezi akatoka, akanionesha ishara kwamba niingie
ndani.
Nikaenda ambapo nilimkuta Shenaiza akiwa anajifuta
machozi, macho yake yakiwa yamebadilika rangi na kuwa mekundu sana.
“Come to me Jamal, you are my comfort,” (Njoo Jamal,
wewe ndiyo faraja yangu) alisema Shenaiza kwa sauti ya chini, nikamsogelea pale
kitandani na kumkumbatia, akanibusu shavuni na kuniomba radhi kwa kilichotokea.
“Unaniomba radhi kwa nini Shenaiza?”
“Najua hujajisikia vizuri kwa mimi kuzungumza
kilichonitokea wakati wewe ukiwa nje, nilitamani na wewe usikie lakini naona
kwa sasa siyo muda muafaka lakini nakuahidi kwamba muda mfupi ujao nitakueleza
wala usijali,” alisema Shenaiza huku akiendelea kunibusu sehemu mbalimbali za
mwili wangu.
Nilimtoa wasiwasi na kumtaka awe huru na mimi,
akaniachia kisha nikakaa pembeni ya kitanda chake.
“Walitaka kuniua jana, yaani ni Mungu tu na naamini
hata wao wanajua kwamba nimekufa, wamenipiga sana,” alisema Shenaiza na
kuniambia anajisikia vibaya sana kuniingiza kwenye matatizo ambayo wala
hayakuwa yakinihusu.
“Nakuomba sana nikishapata nafuu kidogo tu tuondoke,
hata ikibidi kwenda kuishi hotelini mimi nitagharamia kila kitu maana wanaweza
kurudi tena kule nyumbani kwako kwa sababu wanaamini kwamba nimeshakwambia kila
kitu kinachoendelea.”
“Kwa hiyo unataka kusema wanaweza tena kurudi
nyumbani kwangu?”
“Ndiyo! Wanaweza kurudi na kukudhuru bure wakati
hauna hatia yoyote,” alisema Shenaiza, kauli ambayo ilinishangaza na kunijaza
hofu kubwa moyoni. Kuna wakati nilikuwa najuta sana kwa kujiingiza kwenye mdomo
wa mamba bila kujua.
Shenaiza aliendelea kuniongelesha mambo mbalimbali
lakini wala akili yangu haikuwa pale, nilikuwa nikiwaza mambo tofauti kabisa.
Baadaye nesi aliingia na kunieleza kwamba mgonjwa alikuwa anahitaji kupumzika
kwa hiyo nitoke na kumuacha peke yake.
Shenaiza alikuwa mbishi kidogo lakini baadaye
alikubali, akaomba kabla sijatoka nimbusu, nikamuinamia pale kitandani kwa
lengo la kumbusu kwenye shavu lake lakini alinishika shingoni na kunivutia
kwake, ndimi zetu zikagusana na kunifanya nipigwe na ganzi kwa sekunde kadhaa,
aliponiachia, nilibaki nimeganda vilevile mpaka nesi aliponishtua.
“Inabidi uende nje kaka ili tumhudumie mkeo kisha
apate muda wa kupumzika,” alisema yule nesi, nikashtuka kama mtu aliyekuwa usingizini,
nikageuka na kumtazama Shenaiza pale kitandani, akanifinyia jicho lake moja na
kunibusu kwa mbali, nikatoka mpaka nje huku tabasamu pana likiwa limechanua
kwenye uso wangu.
“Jamal! Uko salama mpenzi wangu? Nakupigia simu
lakini sikupati mpaka imebidi nije huku,” alisema Raya ambaye aliponiona tu
nikitoka wodini, alikuja na kunikumbatia kwa nguvu, akionesha kuwa na hofu
kubwa na ukimya wangu.
Hata hivyo sikumtilia sana maanani, japokuwa
nilitoka nikiwa natabasamu, nilipomuona nilikunja sura, nikaingiza mkono
mfukoni na kutoa simu, nikagundua kuwa kumbe kweli ilikuwa imejizima bila mimi
kufahamu, nikaiwasha na kusogea mpaka pembeni kulikokuwa na mabenchi, nikakaa.
Raya naye akaja na kukaa pembeni yangu, akawa na shauku kubwa ya kutaka kusikia
chochote kutoka kwangu.
“Niache kidogo Raya, akili yangu haijatulia kabisa,
tutazungumza baadaye,” nilimjibu msichana huyo kwa kifupi, nikamuona akishusha
pumzi ndefu na kutulia kimya. Maskini Raya! Alionesha kuwa na hisia nzito juu
yangu lakini kwa bahati mbaya mwenzake nilikuwa namchukulia kawaida sana.
Sote tukiwa kimya kabisa, nilikumbuka kilichotokea
kati yangu na Raya usiku na kujikuta nikishindwa kumeza chakula
nilichotafuniwa, nikageuka na kumtazama usoni, naye akanitazama, nikagundua
kwamba alikuwa akilengwalengwa na machozi.
“Najua hunipendi Jamal lakini hiyo isiwe sababu ya
kuninyanyasa, nakupenda sana mwenzio kuliko mtu yeyote chini ya jua, naamini
ipo siku utaujua ukweli,” alisema msichana huyo, nikarudia kumsisitiza kwamba
aniache kidogo hayo mambo tutayajadili baadaye, safari hii nilizungumza kwa
sauti ya chini nikiwa kama nambembeleza f’lani, nikamuona ametulia.
Nikiwa nimekaa pale, nilimuona yule askari mpelelezi
akiwa na wenzake, nikamuomba Raya anisubiri hapohapo, nikainuka na kumfuata
huku bado nikiwa na shauku kubwa ya kutaka kujua alizungumza nini na Shenaiza.
Hata hivyo, licha ya kumfuata askari huyo na
kumuomba anidokeze alichoelezwa na Samantha, alikataa katakata kwa maelezo
kwamba atavuruga upelelezi, nikakosa cha kufanya. Nilirudi hadi pale nilipokuwa
nimemuacha Raya, nikakaa pembeni yake huku nikiwa kimya kabisa.
“Nakushuru kwa jinsi ulivyojitoa kunisaidia katika
haya matatizo yanayonikabili,” nilivunja ukimya na kumsemesha Raya, nikamuona
akiinua uso wake ambao muda wote alikuwa ameuinamisha chini, akanitazama huku
tabasamu hafifu likichanua kwenye uso wake.
“Usijali Jamal, nipo kwa ajili yako na kamwe
sitakuacha peke yako hata iweje.”
“Yaani japokuwa ulikuwa unalia lakini macho yako
yamezidi kuwa mazuri,” nilimtania Raya, akashindwa kujizua na kucheka kwa
nguvu. Hakuna kitu alichokuwa anakipenda Raya kama kusikia kauli yoyote ya
kumsifia kutoka kwangu. Ile huzuni aliyokuwa nayo, iliyeyuka kama theluji
juani, akachangamka kabisa.
“Na leo si tutaenda kulala pamoja nyumbani kwetu?”
“Kwani wazazi wako bado hawajarudi?”
“Bado!”
“Ok, tutaangalia itakavyokuwa,” niliamua kumjibu
hivyo Raya ili kumridhisha ingawa ukweli ni kwamba kauli hiyo haikuwa imetoka
ndani ya moyo wangu. Wakati tukiendelea kuzungumza, niligundua jambo lisilo la
kawaida.
Mita chache kutoka pale tulipokuwa tumekaa, kulikuwa
na maegesho ya magari. Magari mengi yalikuwa yameegeshwa lakini miongoni mwa
magari hayo, ndani ya gari moja kulionekana kuwa na watu zaidi ya mmoja ambao
baadaye nilikuja kushtukia kwamba walikuwa wakitutazama sana mimi na Raya pale
tulipokuwa tumekaa na zaidi walikuwa wakiniangalia mimi.
Nilipogeuka haraka na kuwatazama, macho yangu na yao
yaligongana lakini wakazuga kwamba hawakuwa wakinitazama, wakawa wanaendelea na
mazungumzo yao.
“Kwani nini wananitazama mimi?” nilijikuta
nikizungumza kwa sauti, Raya akashtuka na kuniuliza nilikuwa namaanisha nini?
Nikataka kumzuga lakini haikuwa rahisi, akafanikiwa kugundua kuwa nilikuwa
nawatazama watu gani.
“Hata mimi nimewaona muda mrefu tu, tangu unatoka wodini
walikuwa wakikutazama lakini sikuwatilia maanani.”
“Tuondoke!” nilisema huku nikiinuka pale nilipokuwa
nimekaa kwani tayari kengele ya hatari ililia ndani ya kichwa changu, Raya naye
akainuka, tukaanza kuelekea kwenye lango la kutokea nje ya hospitali hiyo
lakini cha ajabu zaidi, tukiwa getini tunataka kutoka, nililiona lile gari nalo
likija kule tulipokuwepo.
Je,
nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment