ILIPOISHIA:
MARA mlango wa wodi ulifunguliwa, daktari
mmoja akachungulia nje na kuwaonesha ishara ya kuwaita baba na baba yake Rahma,
mapigo ya moyo wangu yakalipuka mno, sikujua anaenda kuwaambia nini, akilini
nikawa nahisi kabisa kwamba mambo yameshaharibika.
SASA ENDELEA... “Kuna tatizo.” “Nini tena
daktari?” “Mgonjwa wenu anaishiwa damu kwa kasi kubwa mno, isitoshe anatapika
damu, hatujui tatizo ni nini kwani vipimo havioneshi tatizo lingine lolote
zaidi ya kwamba alikunywa sumu kwa lengo la kujiua.”
“Sasa tutafanyaje dokta?” “Inabidi kwanza
tushughulikie hili suala la kupungukiwa damu, inabidi wanandugu muitane kwa
ajili ya kuchangia damu, mkiwa tayari mniambie ngoja nizungumze na watu wa
kitengo cha damu waandae vifaa,” alisema yule daktari na kuingia wodini, nikawaona
baba na baba yake Rahma wakitazamana.
“Nahisi kuna nguvu za giza nyuma ya hili suala
na kama tusipotumia nguvu za ziada, tunaweza kumpoteza binti yetu,” alisema
baba, mwenzake akawa anatingisha kichwa kuonesha kuunga mkono alichokuwa
anakisema. “Mimi nina wazo, unaonaje tukiondoka na mgonjwa wetu tukamtibu
nyumbani. Kuna kitu tukikifanya mara moja anapona huyu.”
Nilishangazwa sana na uamuzi walioufikia,
yaani mgonjwa ana hali mbaya kiasi kile halafu wamuondoe hospitali na kwenda
naye nyumbani? Akifa je? Nilijiuliza bila kupata majibu. Muda mfupi baadaye,
baba aligonga tena mlango wa wodi, yule daktari akafungua mlango kwa lengo la
kusikiliza walichokiamua. “Mmeshakubaliana kuhusu kuchangia damu?”
“Hapana, imani yetu hairuhusu kuchangia damu,
tunamuomba mgonjwa wetu tuondoke naye tukajaribu sehemu nyingine,” alisema baba
kwa kujiamini, nikamuona yule daktari akiwatazama wote wawili usoni kwa
mshtuko. “Ndivyo mlivyokubaliana?”
“Ndiyo,” alisema baba, nikamuona akishusha
pumzi ndefu na kuonesha ishara kwamba wasubiri, akaingia ndani nadhani kwa
lengo la kwenda kujadiliana na wenzake, muda mfupi baadaye alipotoka,
aliwaambia madaktari wenzake wamekataa wazo hilo, wakawaambia afadhali kama
wangekuwa wanaomba rufaa kwenda hospitali kubwa lakini kama ni kumrudisha
nyumbani, hilo suala haliwezekani.
“Hawa washenzi sana, kwa hiyo wanaamini
hatuwezi kumchukua mgonjwa wetu bila ridhaa yao?” alisema baba huku akimshika
mkono baba yake Rahma na kuondoka naye, walitoka mpaka nje kabisa ya eneo la
hospitali. Nilikuwa na shauku kubwa ya kumsaidia Rahma, nilipohakikisha akina
baba wametoka nje, na nilipowatazama mama na mama Rahma kwa mbali ambao
walikuwa wakibembelezana pale kwenye
benchi, harakaharaka nilitembea kuelekea kule
wodini. “Unasemaje kijana?” “Huyu ni dada yangu, nataka kumtolea damu.” “Ooh!
Umefanya jambo la maana sana, twende huku,” alisema yule daktari huku
akinishika mkono, tukatoka wodini na kuanza kutembea harakaharaka kwenye
korido, tukaelekea mpaka kwenye chumba maalum cha kutolea damu ambapo niliwakuta
watu wengine watatu wakiwa wamekaa kwenye vitanda maalum, wakiwa wanajitolea
damu.
“Kaa hapo,” alisema yule daktari huku
akinionesha sehemu ya kukaa, akapitiliza na kwenda kuzungumza na mwenzake
ambaye alikuwa bize akishughulika na mmoja kati ya wale watu waliokuwa wakitoa
damu. Akazungumza naye kisha nikaona wote wawili wamegeuka na kunitazama. Muda
mfupi baadaye, yule daktari alitoka na kuniaga, akaniambia nikishamaliza niende
nikamuone. Alipotoka, yule daktari mwingine ambaye yeye alikuwa amevalia sare
za rangi tofauti, alikuja pale nilipokuwa nimekaa, tukasalimiana kisha
akaniuliza kama nilikuwa nataka kujitolea damu, nikamjibu kwamba ni kweli.
Alinisogelea na kuanza kunitazama kwenye mkono
wangu wa kushoto, akachukua pamba iliyokuwa na spirit, akanipaka sehemu ya
ndani ya mkono wangu kisha akanifunga kwa mpira maalum upande wa juu wa mkono,
mishipa ikatokeza kwa wingi mkononi. “Huwa unafanya mazoezi?” aliniuliza.
Nilielewa kwa nini ameniuliza swali lile, kazi
ngumu za kijijini, ikiwemo kulima na kupasua kuni zilinifanya mimi na ndugu
zangu tuwe na nguvu sana mithili ya watu wanaonyanyua vyuma. “Hapana, ni kazi
za kawaida tu,” nilimjibu, akatabasamu na kusema wanaume wengi huwa na miili
legelege kwa hiyo linapokuja suala la kuchangia damu, inakuwa vigumu kuuona
mshipa mkuu wa damu lakini kwangu mimi ulikuwa ukionekana vizuri na ulikuwa
mkubwa kama mtu anayefanya mazoezi.
Nikamuona akichukua sindano moja nene
iliyounganishwa na mrija kwa nyuma ulioenda hadi kwenye kibegi kidogo cha
plastiki cha kuhifadhia damu. Kiukweli sikuwahi kuchomwa sindano hata mara moja
kwenye maisha yangu, kule kijijini kwetu mtu ukiumwa zipo dawa za mitishamba
kibao. Ukizingatia baba alikuwa mtaalamu wa mambo hayo, alikuwa akizijua dawa
za magonjwa karibu yote. Hata hivyo, sikutaka kuonekana mshamba, ikabidi
nijikaze kiume, akanichoma taratibu na kuiingiza ile sindano kwenye mshipa,
akanifunga na
bandeji kwa juu kisha akafungua ule mpira,
damu ikaanza kutiririka kwa kasi kufuata ule mrija mpaka kwenye kile kimfuko.
“Mh! Hii damu yako ikoje?” alisema huku akikiinua kile kimfuko cha damu na
kuanza kukitazama kwa karibu. Tofauti na damu za watu wengine mle ndani, yangu
ilionesha kuwa nyeusi sana mpaka nikawa najishtukia.
“Ina nini kwani?”
“Ni nyeusi sana na inaganda humu kwenye huu
mfuko, sijawahi kukutana na hali kama hii,” alisema huku akinitaka nitulie,
akaenda kuwaita wenzake na muda mfupi baadaye, walinizunguka, kila mmoja akiwa
ananishangaa. “Unaitwa nani?” “Togo.” “Umewahi kuchangia damu kabla ya leo?”
“Hapana, leo ndiyo mara ya kwanza.” “Mbona damu yako iko hivi?” aliniuliza
daktari mmoja, ikabidi amuelekeze yule aliyenichomeka ile sindano, harakaharaka
wakanitoa ile sindano, wakawa wanaendelea kujadiliana kuhusu damu yangu.
“Tunaomba utusubiri pale nje tutakuita,” alisema
yule daktari ambaye ndiye aliyenipeleka kwenye chumba kile, nikainuka huku na
mimi nikiwa na maswali mengi kuliko kawaida, nikatoka huku nikiwa nimebana
pamba pale kwenye jeraha la sindano ili damu isiendelee kutoka. “Ulikuwa wapi
tunakutafuta huku?” baba alinidaka juujuu, macho yake yakatua kwenye pamba
niliyokuwa nimeikandamiza pale kwenye jeraha la sindano.
“Na hiki ni nini?” alisema huku akinishika
mkono kwa nguvu. “Nilikuwa natoa damu.” “Mungu wangu, hivi wewe mtoto una akili
timamu kweli?” alisema baba huku akionesha kushtuka mno, akageuka na kumuonesha
ishara baba yake Rahma kwamba aje, harakaharaka akaja mpaka pale tulipokuwa
tumesimama.Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Championi
Ijumaa.
No comments:
Post a Comment