ILIPOISHIA:
Nilimtazama
Raya aliyekuwa bado amelala juu ya kifua changu, nikajiuliza mara mbilimbili
kama nipokee au la. Mpaka simu inakata, sikuwa nimeamua nini cha kufanya,
ikaanza tena kuita mfululizo ambapo nililazimika kuipokea, sauti ya Samantha ikasikika
upande wa pili, ikinipa taarifa ambazo zilinishtua mno.
“Unasemaaa?”
nilijikuta nikiuliza kwa sauti ya juu, iliyomzindua Raya usingizini.
SASA
ENDELEA…
Wamekuja tena hapa hospitalini wanataka kuniua na
wametishia kwamba wanahisi na wewe unahusika kwenye hiki kinachoendelea kwa
hiyo wameapa kufanya kila kinachowezekana kuhakikisha wanatupoteza wote wawili.
“Lakini Shenaiza, hivi ingekuwa wewe ndiyo upo
kwenye nafasi yangu ungejisikiaje? Yaani unajikuta tu upo katikati ya mambo ya
hatari, maisha yako yanawindwa usiku kucha lakini hata huelewi chanzo ni nini,
ungejisikiaje?”
“Ningejisikia vibaya Jamal lakini si nilishakwambia
nitakueleza kila kitu? Wala huna haja ya kuwa na haraka wala kukasirika.”
“Utaniambia lini? Unajua kilichonitokea nilipoondoka
hapo hospitalini? Bado kidogo ningekufa leo, kibaya ni kwamba sijui hasa
kinachoendelea, sijui chochote kuhusu wewe wala matatizo yako ambayo sasa
yameshakuwa yangu pia.”
“Huu sio muda wa kulaumiana Jamal, nakuomba kama
ulivyofanya mara ya kwanza, njoo unitoroshe tena hospitali na nakuahidi safari
hii tukitoka tu, nitakueleza ukweli wa kila kitu.”
“Hapana! Siwezi Shenaiza, tafuta mtu mwingine wa
kuifanya kazi hiyo, sipo tayari.”
“Jamani Jamal, kwa hiyo upo tayari kuona nakufa
wakati uwezo wa kunisaidia unao? Tena asubuhi hii ndiyo muda mzuri, watu wakija
kuwaletea wagonjwa chai na sisi tunatumia muda huohuo kutoroka, nipo chini ya
miguu yako,” alisema Shenaiza kwa sauti iliyoonesha alikuwa akilengwalengwa na
machozi.
Nilishindwa cha kumjibu, nikamuona Raya naye ambaye
bado alionesha kuwa na usingizi, akijigeuza pale kitandani na kunikumbatia tena
ikiwa ni ishara kwamba hakufurahishwa na kitendo cha mimi kuzungumza na
Shenaiza alfajiri ile.
“Ok, basi sawa nitajua cha kufanya,” nilijibu
harakaharaka kisha nikakata simu. Nililazimika kumkatisha kwa sababu sikutaka
kuendelea kumkasirisha Raya.
“Good morning baby!” (Habari za asubuhi mpenzi)
alisema Raya huku akijinyoosha mwili kwa uchovu, akanibusu mdomoni na
kunikumbatia tena.
“Ulikuwa unaongea na nani kwenye simu?” aliniuliza
swali ambalo nilijua kwamba majibu yake anayo ila anataka kunitega.
“Si huyu Shenaiza, asubuhi yote hii anaanza kuleta
matatizo mengine!”
“Mh! Anasemaje tena?”
“Ananiambia kuwa wale watu wanaotaka kumuua,
wameanza kunitafuta na mimi na wamemuapia kuwa ni lazima watufanye kitu kibaya,
mimi na yeye.”
“Ooh! Mungu wangu, nakuomba Jamal uachane na huyo
msichana, achana kabisa na mambo yake, kama ni matatizo ni yake wala wewe
hayakuhusu, isitoshe mtu mwenyewe ndiyo kwanza mmejuana, achana naye nakuomba,”
alisema Raya kwa hisia za hali ya juu.
Japokuwa alikuwa na hoja kwa alichokuwa
anakizungumza, akili zangu zilikuwa ni kama zimezingirwa na ukungu, nikawa
sielewi nataka nini maishani mwangu. Niliona kama matatizo yaliyokuwa
yanamkabili Shenaiza, yalikuwa yananihusu sana na ni mimi pekee ndiye
niliyekuwa na uwezo wa kumsaidia.
Japokuwa kuna wakati mwingine nilikuwa nikiona kama
nabebeshwa mzigo nisioustahili, bado niliona ninayo nafasi ya kumsaidia.
Ilibidi niamke na kuelekea bafuni, Raya naye akaamka na kunifuata, tukaoga
pamoja huku Raya akionesha kufurahishwa mno na ukaribu wangu.
Tulirudi chumbani ambapo wakati mimi nikijiandaa,
Raya alienda jikoni kuandaa kifungua kinywa. Nilipomaliza kujiandaa, tayari
kifungua kinywa kilikuwa tayari, Raya akiwa ndani ya khanga moja tu,
akanikaribisha mezani.
Mwenyewe alitamani asubuhi hiyo tuendelee kukaa
kimahaba kama ilivyokuwa usiku lakini akili zangu zilikuwa zikienda mbio sana,
nikapata kifungua kinywa harakaharaka kisha nikamuaga.
Haikuwa rahisi kwake kuniruhusu, ikabidi nimdanganye
kwamba nitarudi muda mfupi baadaye na sitatoka tena siku hiyo mpaka usiku.
Ilibidi aniruhusu kwa shingo upande lakini akanitaka kuwa makini sana kwa kila
kitu nitakachokuwa nakifanya.
Tulikumbatiana, nikambusu kwenye paji la uso wake
kisha nikatoka, hatua kadhaa mbele niligeuka na kumtazama, nikamuona machozi
yakimlengalenga, sikuwa na cha kufanya zaidi ya kuendelea na safari yangu.
Nilitoka na kwenda moja kwa moja mpaka hospitalini
alikokuwa amelazwa Shenaiza, bado ilikuwa ni mapema sana na ndugu, jamaa na
marafiki wa wagonjwa wengi walikuwa wakiwapelekea vifungua kinywa.
Ilibidi na mimi niingie kwenye mgahawa mmoja ulikuwa
nje ya hospitali na kuchukua kifungua kinywa kwa ajili ya Shenaiza. Nilifanya
hivyo ili isiwe rahisi kwa walinzi na madaktari kunihisi vibaya. Saa kumi na
mbili kamili nilikuwa nikiingia kwenye mlango wa wodi aliyokuwa amelazwa
Shenaiza.
Niliingia kimyakimya bila kuonekana na mtu yeyote
mpaka pembeni ya kitanda cha Shenaiza, nikamuinamia na kumsemesha kwa sauti ya
chini.
“Shenaiza! Shenaiza!”
“Ooh! Jamal, ahsante kwa kuja mpenzi wangu,” alisema
Shenaiza ambaye kwa ilivyoonesha, hakuwa amelala bali aligeukia ukutani tu,
akanikumbatia na kunibusu kwa hisia nzito huku akionesha mwili wake kuwa kwenye
maumivu makali.
“Ni wewe pekee ndiye unayeweza kunisaidia kwa sababu
hata polisi nao naona wanasuasua tu, najua nakubebesha mzigo mzito lakini
nakuhakikishia wema wako hautapita bure, usichoke kunisaidia,” alisema Shenaiza
kwa sauti ya chini akijaribu kujikakamua na kuinuka pale kitandani.
Nilimsaidia kufanya hivyo, akakaa juu ya kitanda na
kuanza kuangaza macho huku na kule.
“Huu ndiyo muda mzuri, inabidi tuondoke kabla hawa
mashetani hawajafika,” alisema Shenaiza, nikawa naitika kila kitu alichokuwa
ananiambia. Japokuwa nilikuwa najua kwamba ninachokifanya ni kosa jingine
kubwa, nilijikuta nikiwa sina cha kufanya zaidi ya kutii kile Shenaiza
alichokuwa anakitaka.
Tukatoka mpaka nje ya hospitali hiyo bila
kugunduliwa na mtu yeyote, sikutaka kufanya makosa kama yale niliyoyafanya siku
ile nilipomtorosha Shenaiza kule Amana, tukaenda mpaka kwenye kituo cha
daladala na kupanda iliyokuwa inaelekea Makumbusho.
Ili kuzidi kupoteza ushahidi, nilimwambia Shenaiza
ajifunike khanga yake, na mimi nikavaa kofia kubwa ya pama, tukatulia kwenye
siti ya watu wawili. Abiria wengine waliendelea kuingia na baada ya gari kujaa,
safari ilianza huku moyoni nikisali kusitokee jambo lolote baya.
“Sidhani kama tutafika salama huko tunakokwenda,
moyo wangu unasita sana,” alisema Shenaiza kwa sauti ya kutetemeka. Sijui
alikumbwa na nini mpaka aanze kuzungumza maneno yake, nikawa nampa moyo kwamba
asiogope chochote.
Safari iliendelea mpaka tuklipofika Magomeni ambako
kulikuwa na foleni kubwa sana asubuhi hiyo, jambo ambalo halikuwa la kawaida.
“Nimekwambia kwamba sijui kama tutafika salama,
umewahi kuona asubuhi namna hii kunakuwa na foleni kama hii?” alisema Shenaiza
huku akizidi kuonesha hofu kubwa ndani ya moyo wake, nikawa nazidi kumtuliza.
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatatu kwenye Gazeti
la Championi Jumatatu.
No comments:
Post a Comment