ILIPOISHIA:
Wote
waliacha kila walichokuwa wanakifanya, wakawa wananitazama kwa macho makali.
Sikuelewa nini hasa kimetokea, wakati nikiendelea kuwatazama vizuri kwa mara ya
pili, kuna jambo moja lilinishtua mno mpaka nikajikuta nimetoa mkono mfukoni,
giza likarudi kama lilivyokuwa mwanzo.
SASA
ENDELEA...
Japokuwa kulikuwa na giza, niliweza
kuonamacho ya wale watu yaking’ara kama wanyama wakali wa porini, nikawa
najilaumu kwa kile nilichokifanya. Hata sijui nini kilitokea kwani kuanzia
mwanzo nilikuwa nimejiapiza kwamba siku hiyo sitaleta ujuaji wowote mbele ya
watu hao lakini cha ajabu, ndani ya muda mfupi tu, tayari nilishakuwa nimewekwa
mtu kati.
Sikujua safari hii wataniadhibu vipi
lakini niliamua kupiga moyo konde, liwalo na liwe. Bado nilikuwa najiuliza
maswali mengi kuhusu kile kilichokuwa kwenye mfuko wangu, sikujua ni nini na
kilikuwa na uhusiano gani na ule mwanga uliotokeza ghafla mle ndani ya
mahabusu.
Sijui nilipata wapi ujasiri lakini
nilijikuta nikiingiza tena mkono taratibu mfukoni, nilipokigusa tu kile kitu
mle mfukoni, ule mwanga ulirudi tena vilevile, wale watu ambao safari hii
walikuwa wamejikusanya na kutengeneza kama nusu duara hivi, waliinua wote
shingo zao na kunigeukia tena, nikakishika kile kitu kwa nguvu huku na mimi
nikiwa nawatazama.
Katika hali ambayo sikuitegemea, nilishangaa
wa kwanza akisimama na kukimbilia kwenye ile kona alipokuwa amekaa yule
mahabusu ambaye awali alikuwa akipiga kelele. Safari hii alikuwa amelala, tena
kwa kuinamisha kichwa mbele, katikati ya miguu yake.
Nikamuona yule mtu wa kwanza, mikono
yake akiwa amejiziba sehemu nyeti, akisogea mpaka kwenye kona, alipoikaribia,
aligeuka na kuanza kutembea kinyumenyume, akamkanyaga yule mahabusu kisha
nikashangaa akipotelea kwenye ukuta.
Ni hapo ndipo nilipoamini yale maneno
niliyowahi kuyasikia kwamba wachawi wanao uwezo wa kuingia na kutoka ndani ya
nyumba hata kama milango imefungwa.
Nilishindwa kuelewa ni nini hasa kilichofanya iwezekane kwa yule mtu kupotelea
kwenye ukuta.
Nikiwa bado nimepigwa na butwaa,
nilimuona mwingine naye akiinuka, akaanza kutembea kuelekea kwenye ile kona,
wengine nao wakasimama, wakawa wanatembea huku wote wakiwa wananitazama kwa
macho mabaya. Ni kama nilikuwa nimewavurugia mipango yao, nikazidi kukishikilia
kile kitu mfukoni.
“Hiyo ndiyo nafasi yako ya kutoka
mahabusu, hakikisha unamshika mmoja kati yao na kumvua usinga aliovaa shingoni
kisha na wewe utatoka kama hao wengine walivyotoka,” nilisikia sauti masikioni
mwangu ambayo niliitambua vizuri kwamba ni ya baba.
Bado sikuwa nimeelewa ni mbinu gani
anayoitumia baba kuwasiliana na mimi kwa sauti ambayo hakuna mtu mwingine
yeyote anayeisikia. Hata hivyo, sikutaka sana kuhoji, nilichokifanyailikuwa ni
kufuata maelekezo.
Cha ajabu, wale watu walipoona
nawafuata, walianza kukimbia lakini kwa sababu ya nafasi ndogo iliyokuwepo,
walishindwa kutoka wote kwa mkupuo, nikafanikiwa kumkamata mmoja ambapo moja
kwa moja nilipeleka mkono shingoni ambapo alikuwa amevaa kitu kama kamba
nyembamba lakini iliyosokotwa kwa nywele, ikakatika na kubaki mkononi mwangu.
Kitendo hicho kilisababisha alie kwa
sauti kubwa lakini cha ajabu sasa, sauti yake ilitoka kama zile sauti
zinazotolewa na mapaka yanayolia usiku, akadondoka chini na kuendelea kulia kwa
sauti kubwa kama paka.
Cha ajabu, wakati nikiwa nimeshageuka na
kuupa mgongo ukuta, tayari kwa kufanya kile baba alichoniambia nikifanye, yule
mtu aliinua uso wake huku akionesha ishara kwamba nimsamehe. Kilichonishtua ni
kwamba sura yake ilikuwa ikifanana na mimi kwa kila kitu wakati awali hakuwa
vile.
Nikiwa bado naendelea kumshangaa,
nilisikia sauti ya baba ikinisisitiza kutoka haraka. Sikuwa nimewahi kushiriki
uchawi mkubwa kiasi hicho, nikawa natetemeka nikiwa siamini kama kweli naweza
kupita ukutani. Nilipiga hatua kurudi nyuma mpaka nilipoufikia ukuta.
Cha ajabu, nilipouegamia ulilainika kama
pazia, nikapiga hatua nyingine na kujikuta nusu ya mwili wangu tayari ipo nje,
nikapiga hatua nyingine, nikawa nimetoka nje kabisa. Nilibaki nimesimama kwenye
maua yaliyopandwa pembezoni mwa ile mahabusu nikiwa bado siamini.
Niligeuka na kutazama huku na kule,
hakukuwa na mtu yeyote eneo hilo, harakaharaka nikatembea na kupotelea kwenye
kota za askari wa kituo kile, nikawa nazidi kutembea nikiwa sielewi naelekea
wapi. Nilizimaliza kota hizo, kwa mbali nikawa nawasikia mbwa wakibweka,
nikaongeza mwendo na muda mfupi baadaye, nilitokeza kwenye barabara ya lami.
Siwezi kuficha jinsi nilivyofurahi
kutoka mle mahabusu. Hapohapo nikajikuta eti na mimi nikitamani kuwa mchawi ili
nipate nafasi ya kufaidi mambo mengi kwenye hii dunia ambayo binadamu wa
kawaida hawawezi.
Hebu vuta picha, hata kama ni wewe,
yaani ndugu yako yupo gerezani anateseka halafu leo ukiambiwa kuna ujuzi
ukifundishwa ndugu yako anaweza kutoka kiulaini, tena bila kutumia nguvu wala
fedha, huwezi kutamani kweli?
Labda kamauna imani kali ya dini ndiyo
unaweza kuukwepa mtego huo lakini kwangu mimi, siwezi kuficha kwamba nilifurahi
sana na kutamani kuwa mchawi, tena niliyebobea. Nilijiapiza kwamba nitakapopata
nafasi ya kuzungumza na baba, nitamueleza nia yangu bila kujali
atanichukuliaje.
Niliendelea kutembea kufuata ile
barabara ya lami huku muda mwingi tabasamu likiwa limechanua kwenye uso wangu.
Tafsiri ya kile kilichotokea n kwamba asubuhi polisi wangeingia na kufanya
ukaguzi mle mahabusu wangekuwa na imani kwamba bado nipo, labda watashtuka kwa
nini sijavaa nguo kwa sababu yule mchawi hakuwa amevaa nguo.
Nilielewa kwa nini baba aliniambia
nisitoe maelezo yoyote kwa sababu kama yule mtu niliyebadilishana naye na
kumuacha mle ndani mahabusu atahojiwa, maelezo atakayoyatoa yatakuwa hayaungi
chochote na tukio lililotokea kwa hiyo uwezekano wa baadaye kuja kuachiwa kwa
sababu ya kukosekana ushahidi ulikuwa mkubwa.
Sikujua atasota kwa muda gani mle
mahabusu, tena kesi yenyewe ikiwa ni ya mauaji lakini niliona kama anastahili
maana ni uchawi wa aina gani watu wanaenda kuufanyia sehemu hatari kama
mahabusu? Niliendelea kutembea huku mara kwa mara nikicheka mwenyewe maana
nilijiona bonge la mjanja kuukwepa msala ule.
Nikiwa naendelea kutembea nikiwa sijui
naelekea wapi kwa sababu kama nilivyoeleza, sikuwa naijua mitaa ya Jiji la Dar
es Salaam, nilisikia vishindo vya mtu akija huku akikimbia akitokea nyuma
yangu. Baba amewahi kuniambia kwamba ukiwa unatembea usiku, ni mwiko kugeuka
nyuma.
Alizidi kunikaribia, nikawa najiuliza
kama atakuwa ni mtu mbaya itakuwaje? Niliendelea kujikaza kisabuni, vishindo
vikazidi kunikaribia na alipofika usawa wangu, nikasikia akipunguza mwendo.
Kilichonifanya niamini kwamba hawezi kuwa mtu mbaya, ni jinsi manukato
aliyokuwa amejipulizia mwilini yalivyokuwa yakinukia vizuri.
“Mambo,” sauti ya kike ilisikika, safari
hii ikiwa usawa wangu kabisa, ikabidi nisimame, nikageuza shingo yangu upande
wa kulia alipokuwepo mtu huyo aliyenisalimu. Muda huo kwa makadirio ilikuwa ni
kama saa nane za usiku maana kuna sehemu nilipita nikasikia redio kwa mbali
ikitangaza kwamba ni saa nane kasoro za usiku.
“Mbona umeshtuka Togo!” alisema huku
akinisogelea. Siwezi kuficha, mshtuko nilioupata nusura nidondoke na kuzimia.
Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa kwenye
Gazeti la Championi Ijumaa.
No comments:
Post a Comment