ILIPOISHIA:
Ghafla tulishtushwa na kishindo kikubwa
ambacho hata sikuelewa kimetokea wapi. Watu walianza kupiga kelele kwa nguvu
huku wale waliokuwa baharini wakianza kukimbia kuokoa maisha yangu. Ilibidi
tugeuke kutazama kule kishindo kile kilichotokea ambako bado zile kelele
zilikuwa zikitokea.
SASA ENDELEA...
Lahaula! Samaki mkubwa ambaye sikuwahi
kumuona ingawa baadaye nilisikia kwamba anaitwa papa, akiwa na meno makali
yaliyochongoka, aliipiga kikumbo boti ndogo ya uvuvi iliyokuwa eneo hilo na
kusababisha kishindo kikubwa, wavuvi waliokuwa ndani ya boti hiyo wote
wakarukia majini na kuanza kuhaha kuokoa maisha yao.
Nikiwa bado namshangaa samaki yule
ambaye alijirusha kwa nguvu kutoka majini na sasa akawa anaonekana mzimamzima,
wote tulishtukia akimfuata mmoja kati ya wale wavuvi, akafunua mdomo wake
uliokuwa na meno makali kama msumeno, akamkamata kiunoni, kufumba na kufumbua
akaubana mdomo wake kwa nguvu, yule mvuvi akagawanyika vipande viwili.
Sijui nilipata wapi ujasiri, nilijikuta
nikiinuka kwa kasi kubwa pale tulipokuwa tumekaa na Rahma, akabaki anapiga
kelele za kuniita huku akiniuliza nakwenda wapi na kufanya nini? Sikuelewa
swali lake lilimaanisha nini kwa sababu kila kitu kilikuwa wazi, nilikuwa
nakwenda kutoa msaada kwa wale wavuvi.
Nilikimbia mpaka eneo ambalo maji
yalianza kunifika kiunoni, kwa kuwa nilikuwa na uzoefu wa kutosha wa kupiga
mbizi, nilianza kuelekea eneo la tukio. Kadiri nilivyokuwa nazidi kusonge mbele
ndivyo kelele zilivyokuwa zikizidi kuongezeka. Sikuwahi kudhani kwamba samaki
ana sauti ya kutisha kiasi kile maana alikuwa akitoa milio ya ajabu.
Nikiwa naendelea kupiga mbizi,
nilimshuhudia akikifuata kile kipande cha kichwa cha yule mvuvi, akaanza
kukichanachana kwa meno yake makali, akararua minofu yote na kubakiza mifupa
michache tu, akahamia kile kipande kingine cha kichwa, akakitafuna na kuacha
kichwa tu. Nilijikuta nikipatwa na hofu ya ajabu, hakika sikuamini nilichokuwa
nakiona.
Maji yote ya eneo lile yalibadilika
rtangi na kuwa mekundu, mimi nikawa nazidi kupiga mbizi nikiwa hata sijui
naenda kufanya nini maana uwezo wa kupambana na samaki yule kwenye maji, hakika
sikuwa nao, nikasikia kelele za watu wakinizuia na kunitaka nirudi maana tayari
wale wavuvi wengine walishapotea kwenye upeo wa macho yangu.
Ghafla nilihisi kama kuna kitu
kimenishika kwenye mguu wangu wa kushoto na kuanza kunivutia chini, tayari
nilishafika kwenye kina kirefu, nikatumia nguvu kubwa kujaribu kupambana na
kile kitu kilichokuwa kimeninasa ambacho bado sikuwa najua ni nini, ghafla
nikajikuta nikizama.
Nilipoibuka, nilikuwa nimemeza kiasi
kikubwa cha maji ya chumvi na nikiri kwamba unaweza kuwa unajua sana kuogelea
kwenye maji baridi lakini maji chumvi ni hatari sana maana yakikuingia puani au
ukiyanywa, ile chumvi inakufanya uzidi kuwa kwenye hali mbaya.
Nilijaribu kupiga mbizi kwa nguvu lakini
bado kile kitu kilikuwa kimenibana mguu na kuzidi kunivuta, nilitamani nigeuke
niangalie ni nini lakini sikuweza kutokana na jinsi nilivyokuwa napambana na
mawimbi makali. Nikajikuta nikizama tena na kunywa maji mengi zaidi ya mwanzo,
nikaibuka na kuendelea kutapatapa, safari hii mwili ukiwa umeishiwa kabisa
nguvu kiasi cha kuanza kuhisi giza nene machoni.
Sikuelewa tena kilichoendelea kwani giza
nene lilinizingira usoni huku nikianza kuona picha za majinamizi ya kutisha.
***
“Nisaidieni jamani mchumba wangu
anakufaaaa, msaada?” Rahma alipiga kelele kwa nguvu na kuwafanya watu wote
waliokuwa ufukweni hapo, wakiwemo wavuvi waliokuwa wakivuta nyavu zao, kuacha
kila walichokuwa wakikifanya na kukimbilia kule baharini kwenye kina kirefu.”
“Imekuwaje tena jamani?”
“Mh hata sijui nini kimetokea, hawa
walikuwa wamekaa pale ufukweni na mwenzake, mara mwanaume akaanza kukimbilia
baharini, tena akiwa na nguzo zake zote.”
“Mimi mwenyewe nimemuona, nikasema huyu
jamaa kachanganyikiwa nini? Unaambiwa kakimbia mpaka kule, akaanza kupiga mbizi
kwa kasi kubwa kama samaki, mara tunashangaa anaanza kutapatapa, mwisho maji
yanamzidi anazama,” alisema mwanaume mmoja, shuhuda wa tukio lile.
“Binti kwani amepatwa na nini?”
“Nisaidie kwanza kumsaidia, mengine
tutajua baadaye,” alijibu Rahma huku akilia na kurusharusha miguu kama
amekanyaga siafu. Muda mfupi baadaye, wavuvi watatu tayari walikuwa
wameshamfikia pale alipokuwa ambapo kwa sababu alishazama na kuibuka kwa mara
ya tatu, ilibidi wazame chini kumtafuta.
Kwa bahati nzuri, walifanikiwa kumpata,
wakaibuka naye na kupiga mbizi mpaka ufukweni kwenye mchanga ambapo watu wengi
walikuwa tayari wameshakusanyika, zoezi la kumsaidia kurejesha pumzi zake
likaanza ambapo wale wavuvi walianza kumkandamiza tumboni kwa nguvu.
***
“Kwani ilikuwaje Rahma?”
“Hata sijui baba, siwezi kuelezea maana
naona ni zaidi ya maajabu,” nilisikia sauti za watu wakizungumza kwa mbali
ambapo nilizitambau vyema sauti hizo kuwa ni Rahma na baba. Bado macho yangu
nilikuwa nimeyafumba, nikihisi kila kiungo kwenye mwili wangu kikiwa kizito na
kilichokosa nguvu kabisa.
Nilijaribu kufumbua macho mara kadhaa
lakini nilikuwa nashindwa, nikawa nimelala tu lakini nikiwa na uwezo wa kusikia
kila kilichokuwa kinaendelea.
“Tueleze ili angalau tupate mwanga maana
mpaka sasa sote tupo gizani na wewe ndiye uliyekuwa naye kabla hajafikwa na
haya matatizo.”
“Tulikuwa salama tu lakini baada ya ile
simu mliyopiga ndiyo mambo yalipoharibika, kwa sababu mwanzo tulikuwa tumekaa
kwenye mchanga baada ya kuwa Togo ameshacheza sana na maji ya bahari, tena
akawa ananichekesha kwa kuniambia eti ukipia chakula hakuna haja ya kuweka
chumvi.
“Muda mfupi baada ya kumaliza kuzungumza
na simu, nilishangaa kusikia akiniambia kama nimesikia hicho kishindo kikubwa,
nikawa nashangaa maana hakukuwa na kishindo chochote, mara akasimama huku
akitazama baharini, akawa ni kama ameona kitu ambacho mimi hata sijui ni nini.
“Nikiwa bado nimepigwa na butwaa,
nilishangaa akianza kukimbilia baharini, alipofika kwenye maji mengi alipiga
mbizi kwa kasi kubwa mpaka alipofika kwenye kina kirefu, mara akaanza
kutapatapa mpaka akazama, wavuvi wakaenda kumuokoa akiwa hajitambui, tumbo
likiwa limejaa maji,” nilimsikia Rahma akitoa ufafanuzi ambao ulinishangaza
sana.
Nilijikuta nikipata nguvu za ghafla,
nikafumbua macho na mimi nikitaka kutoa ufafanuzi wa kilichotokea. Kitendo cha
mimi kufumbua tu macho, kiliwafanya wote waache kila walichokuwa wanakifanya,
wakanisogelea na kuzunguka pale kitandani huku nikimsikia Rahma akimuita nesi.
Wakati wao wananishangaa na kuniuliza
nilikuwa najisikiaje, mimi bado nilikuwa nikitafakari maelezo aliyoyatoa Rahma
ambayo niliyasikia vyema kabisa. Nilishangaa kwa nini akwepeshe ukweli wa
kilichotokea? Yaani alibadilisha maelezo kwa faida ya nani?
Kwani yeye hakumuona yule papa mkubwa
aliyekuwa akimla mvuvi huku wenzake wakiponea kwenye tundu la sindano? Ina
maana hakusikia kile kishindo cha samaki yule mkubwa anayetisha alipoipiga
kikumbo kikubwa boti ile ya wavuvi? Kwa nini hawaambii kwamba nilikuwa naenda
kuwaokoa wavuvi? Nilijiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu.
Nilianza kuwatazama mmoja baada ya
mwingine, kuanzia mama ambaye uso wake ulikuwa na huzuni kubwa, baba ambaye
alionesha kuwa katika tafakuri nzito na ndugu zangu wote ambao walikuwa
wamekodolea macho, kila mmoja akiwa na maswali mengi yasiyo na majibu.
Mara mlango wa wodi ulifunguliwa, watu
wote wakageuka kutazama ni nani aliyekuwa akiingia kwa kasi kiasi kile.
Je,
nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment