Wednesday, August 23, 2017

The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 28


ILIPOISHIA:
Baba alitoa kichupa kilichokuwa na unga mweusi lakini kabla hajafanya chochote, aliniambia nikajitazame kwenye kioo kilichokuwa humo chumbani.
“Mungu wangu,” nilisema kwa mshtuko usio wa kawaida.
SASA ENDELEA...
Uso wangu ulikuwa umebadilika na kuwa mweusi tii kama mkaa. Kilichoonekana ilikuwa ni macho na meno tu. Nilishindwa kuelewa kwa nini mimebadilika na kuwa vile, sikujua kama ni yale makofi ya nguvu niliyopigwa au ni nini.
“Usishtuke, na huo mchezo wako ukiendelea nao yatakufika makubwa zaidi, yaani unaonekana umeonja asali na sasa unataka kuchonga mzinga kabisa. Hukuwa na mambo ya kupenda wanawake, nini kimekusibu?” alisema baba lakini maneno yake yaliingilia sikio moja na kutokea jingine.
Akili yangu ilikuwa ikiwaza kuhusu mabadiliko yaliyotokea kwenye uso wangu. Nilishindwa kuelewa itakuwaje kama nitaendelea kuwa hivyo, nilijikuta nikiishiwa nguvu kabisa, nikakaa chini huku hofu kubwa ikiwa imetanda moyoni mwangu.
“Si naongea na wewe?” alinihoji baba huku akiwa amekishika kile kichupa, sikumjibu chochote kwa sababu akili yangu ilikuwa ikiwaza mambo mengine tofauti kabisa. Suala la kuacha kufaidi penzi la Rahma halikuwepo kabisa kichwani mwangu, kwa sababu hata wao wenyewe walijaribu kulizuia lakini kilichotokea kila mmoja akawa shahidi.

“Hebu inuka,” alisema baba kwa jazba, nadhani ni baada ya kuona simpi ushirikiano. Nilisimama, akatoa wembe kwenye mfuko wa mbele wa shati yake, akanichanja kwenye paji la uso, juu kidogo ya sehemu nywele zinapoanzia.
Akanipaka ile dawa, yaani kwa jinsi ilivyokuwa inauma, nilishindwa kujizuia, nikawa napiga kelele, baba akanikamata na kuniziba mdomo huku akinionesha ishara ya kunyamaza.
“Inatakiwa ujikaze, halafu hakikisha asubuhi hakuna mtu yeyote anayejua kilichotokea, ni mambo ya aibu sana na yatatusababishia matatizo makubwa, si unajua ndiyo kwanza tumefika na hapa ni kwa watu?”
“Nataka kujua wale ni akina nani na wametoka wapi? Kwa nini wameingia chumbani kwa Rahma?”
“Nitakujibu lakini siyo leo,” alisema baba huku akinisisitiza kwamba nilale na nisiende tena chumbani kwa Rahma. Hakuna jambo ambalo lilikuwa likinikera kwa baba kama kila ninapomuuliza kuhusu mauzauza yanayonitokea yeye anakimbilia tu kusema kwamba atanijibu. Alitoka na kurudia kunisisitiza kwamba nisitoke na asubuhi nisimwambie yeyote kuhusu kilichotokea.
“Na huu uso itakuwaje?”
“Hiyo dawa niliyokupaka itakusaidia, mtu yeyote akikuuliza mwambie umeamka tu asubuhi na kujikuta ukiwa hivyo,” alisema. Nikasogea tena kwenye kioo na kujitazama. Yaani hata sikujua kama asubuhi kukipambazuka halafu nikawa bado kwenye hali hiyo itakuwaje maana kiukweli nilikuwa natisha.
Kwenye upande wa shavu la kushoto na kulia, kulikuwa na alama za vidole za yule bibi kizee sehemu aliponipiga makofi, nikaapa siku nitakayomjua halafu nikakutana naye barabarani, lazima na mimi nimlipizie.
Nilijaribu kujilaza kitandani lakini usingizi haukuja kabisa, mara kwa mara nilikuwa nikisikia vishindo vikubwa juu ya bati kama kuna watu wanapigana, huku wakati mwingine sauti za ajabu zikisikika. Nilikuja kupata usingizi wakati kumeshaanza kupambazuka kabisa.
Kwa kuhofia kwamba ndugu yangu akiamka anaweza kuniona nilivyokuwa natisha usoni, nilijifunika ‘gubigubi’. Nilimsikia akijiongelesha kama aliyeshtuka kuniona nimelala pembeni yake wakati hakumbuki usiku niliingia saa ngapi.
“Unaendeleaje Togo,” aliniuliza lakini nilijikausha na kujifanya nimepitiwa na usingizi.
“Togoo!” aliniita huku akivuta shuka kwa nguvu. Kwa kuwa sikutegemea tukio hilo, alifanikiwa kunifunua na mimi bila hata kufikiri mara mbili, nikaamka kwa hasira, tukawa tunatazamana.
“Mbonaunapenda kunisumbua wakati unajua mwenzio naumwa?”
“Hee... huko usoni umefanya nini?” aliniuliza huku akirudi nyuma kwa hofu, akafungua mlango na kutoka mbio. Nilijikuta nikikosa amani mno, ikabidi nisogee na kujitazama tena kwenye kioo. Bado uso wangu haukuwa umerudi kwenye hali yake.
Japokuwa ule weusi kidogo ulikuwa umepungua lakini bado mtu yeyote asingeweza kunitazama usono bila kushtuka. Pia mashavu yote mawili yalikuwa yamevimba huku damu ikiwa imevilia kwenye zile alama za vidole na kwenye jicho langu la kushoto.
“Eti kuna nini,” baba alisema huku akifungua mlango. Kumbe kutokana na mshtuko alioupata alikuwa amekimbia na kwenda kumuita baba.
“Huyu mjinga eti mimi nimelala yeye ananivuta shuka,” nilisema huku nikikwepa kutazamana usoni na baba. Aliligundua hilo, akanilazimisha nimuangalie.
“hebu ngoja nakuja, na wewe acha ujinga wa kupigapiga kelele, inamaana hujui kama mwenzenu anaumwa,” alisema baba kwa kumkaripia yule ndugu yangu, nikamuona ‘limemshuka’ maana alitegemea baba atashtuka kama yeye.
“Kwanza ondoka muache apumzike,” alisema baba, ikabidi atoke naye, nikajilaza tena kitandani nakujifunika vizuri. Nikawa naendelea kutafakari mambo mengi yasiyo na majibu. Muda mfupi baadaye, baba alirejea akiwa na kimkoba chake kidogo, akaniamcha na kunitaka nifanye kama anavyoniambia.
Kuna kimzizi fulani alikitoa kwenye mkoba wake, akipa na kuniambia nikitafune lakini nisimeze mate. Nilipokitia mdomoni, niligundua kwamba kilikuwa kichungu sana, nikakitafuna huku nikiwa nimekunja sura.
‘Temea mate kwenye mkono wako wa kushoto na ujipake kwenye shavu la kulia,” alisema huku akinisisitiza kuwa makini. Nilifanya hivyo, nikajipaka kwenye shavu na kuhisi kama moto unawaka. Tema mengine kwenye mkono wa kulia na ujipake kwenye shavu la kushoto,” aliniambia, nikafanya hivyo, maumivu yakazidi ikuongezeka, nikawa nahisi kama ngozi ya sura inajaa kama puto.
“Nifuate,” alisema, akafungua mlango na kuelekea bafuni, nikamfuata ambapo alinielekeza namna ya kusimama kisha akafungulia maji na kuanza kunimwagia kichwa kizima huku akinisugua na kunipaka ungaunga mwingine uliokuwa na ladha kama magadi.
Alinisafisha kwa muda mrefu kisha akatoa kipande cha kitambaa na kunifuta, akaniambia nisifumbue macho mpaka atakaponiambia. Alinishika mkono na kunirudisha chumbani, akanilaza kitandani na kuniambia nifumbue macho.
“Inabidi ulale hivyo kwa dakika saba, zikiisha amka halafu ujitazame tena kwenye kioo,” aliniambia baba, akakusanya vitu vyake na kuondoka. Nikawa nasubiri hizo dakika saba ziishe maana aliniambia atakuja mwenyewe kuniambia. Baba alikuwa na mambo mengi sana yenye utata, hasa huo ujuzi wake wa mitishamba na dawa za kiganga.
Nililala pale kitandani lakini kwa mbali nilianza kujihisi hali fulani hivi isiyo ya kawaida. Sikutaka kuitilia maanani kwani bado uso wangu ulikuwa ukiwaka moto kwa maumivu. Dakika saba baadaye, kweli baba alirudi na kuniamsha, nikasogea na kujitazama kwenye kioo. Huwezi kuamini, uso wangu ulikuwa umerudi kwenye hali yake ya kawaida ingawa jicho moja bado lilibaki limevilia damu na zile alama za vidole mashavuni zenyewe hazikufutika.
Alitoka na kuniacha mwenyewe, angalau moyo wangu ukawa na amani. Nilisimama kwa muda pale mbele ya kioo nikiendelea kujitazama. Ile hali sasa ilizidi kunisumbua na kunifanya nijisikie vibaya. Yaani kwa jinsi nilivyokuwa najisikia, ilikuwa ni kama nimeshikwa na kiu kali lakini tofauti na kiu ya kawaida, ilikuwa ni kiu ya kukutana kimwili na mwanamke.
Nilibaki nikijishangaa mwenyewe kwani kadiri muda ulivyokuwa ukisonga mbele ndivyo nilivyokuwa nikizidi kuteseka. Wakati nikiendelea kuugulia ndani kwa ndani, nilishangaa kwa nini rahma mpaka muda huo hakuwa amekuja kuniuliza nimeamkaje na hata sauti yake sikuisikia. Japokuwa baba alikuwa amenikanya sana, kwa jinsi hali ilivyokuwa, niliamini yeye ndiye anayeweza kuwa msaada kwangu kwa sababu tunapendana.
Nilitoka na kusogea kwenye mlango wa chumbani kwake lakini kabla sijashika kitasa, nilisikia sauti ya mdogo wake wa kiume akiniambia kwamba hakuwepo, alikuwa ameondoka na mama yake asubuhi na mapema kufuatilia mambo ya chuo. Ni kweli jana yake alikuwa amenidokeza kuhusu suala hilo lakini sijui kwa nini sikukumbuka. Nilijikuta nikiishiwa nguvu kwani sikujua nini kitafuatia.
Nilirudi chumbani kwangu huku hali ikizidi kuwa mbaya, sijui ni machale gani yalimcheza baba, mara akafungua mlango na kunikuta nikiwa kwenye hali ambayo haielezeki.
“Ule mzizi niliokupa na kukwambia uutafune lakini usimeze, ulifanya kama nilivyokwambia?” baba aliniuliza. Kiukweli baada ya kutema mate kwenye mkono wa kushoto na kulia, mengine yaliyobakia, pamoja na mabaki ya mzizi wenyewe, nilivimeza vyote. Nilipomwambia hivyo baba, alishtuka kuliko kawaida. Sikujua kwa nini ameshtuka kiasi hicho, akatoka haraka.
Nikiwa bado naendelea kuugulia, nilisikia ndugu yangu mmoja akiniita kutokea dirishani, nikafunua pazia na kuchungulia nje. Sikuyaamini macho yangu baada ya kumuona akiwa na yule msichana tuliyesafiri naye, harakaharaka nikafungua dirisha huku tabasamu pana likiwa limechanua kwenye uso wangu.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...