ILIPOISHIA:
Sikutaka kumuamsha Rahma, nilimtoa
kifuani kwangu taratibu kisha nikashusha miguu chini, nikawa nimekaa huku
nikitazama huku na kule. Sikuweza kuona chochote kutokana na giza lililokuwa
limetanda usiku huo. Mara nikasikia kishindo kizito kama cha kitu
kilichodondoka kutoka darini mpaka sakafuni, mapigo ya moyo yakaanza kunienda
mbio kuliko kawaida.
SASA ENDELEA...
Nilikaza macho kwenye giza kujaribu
kuangalia ni kitu gani hicho kilichodondoka, kwa mbali nikaanza kuona kama mtu
amepiga magoti kwenye kona ya chumba hicho, taratibu akaanza kuinuka, nikazidi
kumkazia macho na kadiri muda ulivyokuwa ukizonga ndivyo nilivyozidi kuiona vizuri
taswira yake.
Nilimtambua kwamba ni mwanamke kutokana
na maumbile yake ingawa alionesha kuwa ni mzee kwani niliweza kuiona ngozi yake
ilivyokuwa imekunjamana, nikamkazia macho usoni nikitaka niione sura yake. Hata
hivyo eneo la usoni lilikuwa na giza sana, nikamuona akiinua mikono juu kama
anayetoa ishara fulani, akageuka na kuanza kujisugua makalio yake ukutani.
Mara nilisikia kishindo kingine, hofu
ikazidi kutanda ndani ya moyo wangu, kijasho chembamba kikawa kinanitoka huku
nikiwa nimekodoa macho kwa nguvu zote.
Nilitamani niamke nikawashe taa lakini ujasiri
huo sikuwa nao, nilitamani niingie chini ya kitanda lakini mwili wote haukuwa
na nguvu, nilitamani kupiga kelele kuwaamsha nyumba nzima lakini sikuwa na
uwezo huo, nikawa natetemeka kuliko kawaida.
Nilipotazama kwa makini pale chini,
nilimuona mtu mwingine kama yule wa kwanza naye akiinuka taratibu lakini
tofauti yake, huyu alikuwa mwanaume kutokana na jinsi mwili wake ulivyokuwa na
alionesha pia kuwa mzee zaidi maana mpaka mgongo wake ulikuwa umepinda.
Alipoinuka, naye alisogea ukutani na
kuanza ‘kusonta’ ukutani kwa kutumia makalio yake kisha akasogea mbele na
kushikama mikono na yule mwanamke wa kwanza, wakaiinua juu na kutoa ishara
ambayo sikuielewa, mara nikasikia vishindo mfululizo.
Vilisikika vishindo kama sita hivi,
ikimaanisha kwamba watu wengine sita walikuwa wameingia, uzalendo ukanishinda.
Sijui nilipata wapi ujasiri, nikasimama wima kisha nikapaza sauti, ‘tokeni hapa
washenzi nyie, hata mimi baba yangu ni mchawi vilevile’.
Kauli yangu ni kama iliwashtua watu wale
wa ajabu ambao hata sielewi niwaelezeeje, wote wakashtuka na kunitazama,
nikazidi kushtuka baada ya kuona wote macho yao yalikuwa yakiwaka kama mnyama
mkali gizani.
Kwa wale ambao wameishi maeneo ya
maporini watakuwa wananielewa kwamba mida ya usiku, wanyama kama simba, chui,
mbwa mwitu au hata mbwa wa kawaida na paka, wakiwa kwenye giza totoro kisha
wakakukodolea macho yao, huwa yanatoa mwanga fulani wa kutisha.
Kwa jinsi walivyonitazama, hofu
ilinizidi maradufu lakini nikaona hakuna kingine cha kufanya zaidi ya kuendelea
‘kugangamala’. Sikuwa najua kama wakinigeukia nitafanya nini, sikuwa najua
mbinu zozote za kupambana nao na eti nilijikuta nikijilaumu kwa nini baba
hakunifundisha au hakunipa mbinu yoyote ya kukabiliana na wachawi.
Yule mwanamke aliyekuwa wa kwanza kuingia
mle ndani, nilimuona akinisogelea huku akionesha kutokuwa na hata chembe ya
woga. Nilihisi haja ndogo ikitaka kunitoka lakini nilijikaza kiume na kusema
liwalo na liwe, akanisogelea jirani kabisa huku akiendelea kunitazama kwa macho
yake makali, cha ajabu, licha ya kunisogelea, sikuweza kabisa kuitambua sura
yake.
Nimewahi kusikia kwamba wachawi wana
kawaida ya kula nyama za watu, nikahisi na mimi usiku huo nakwenda kuliwa huku
nikijiona. Niliujutia uamuzi wangu wa kusimama na kuwafokea watu hao, nikiwa
bado natetemeka, nilisikia kofi moja zito likitua kwenye shavu langu la
kushoto, maumivui niliyoyasikia yalikuwa hayaelezeki, nikapiga kelele kwa nguvu
nikimuita baba.
Sikumbuki kama nimewahi kutoa sauti kubwa
kama hiyo maishani mwangu, mara mlango ukaanza kugongwa kwa nguvu nje,
nikasikia kibao kingine kikitua kwenye shavu la upande wa pili, likafuatiwa na
misonyo mingi kisha wale watu wakayeyuka wote na kupotea kama moshi upoteavyo
angani.
“Togo! Nini kimetokea?” alisema baba
baada ya kuwa amefanikiwa kufungua mlango na kuwasha taa. Jambo la aibu ni
kwamba baada ya ule mchezo wa kikubwa niliocheza na Rahma, hakuna aliyekumbuka
tena kuvaa nguo zake kwa hiyo nilikuwa kama nilivyozaliwa, baba akanitazama kwa
mshangao.
Najua alishangazwa na mambo mengi kwa
wakati mmoja, kwanza kwa nini nilikuwa chumbani kwa Rahma mpaka usiku huo
wakati makubaliano yalikuwa ni kwamba kila mmoja atalala kwake, kwa maana
kwamba baada ya c hakula ilitakiwa mimi nitoke na kwenda kwenye chumba
nilichopangiwa lakini sikufanya hivyo. Yote tisa, kumi ni kwamba nilikuwa kama
nilivyozaliwa, na Rahma naye ambaye bado alikuwa kwenye usingizi mzito,
akikoroma bila kujua chochote kilichokuwa kinaendelea, hakuwa na chochote
mwilini, nikamuona baba akishusha pumzi ndefu na kunipa ishara kwamba nivae
kwanza nguo, akatoka na kuurudisha mlango.
Kumbe sekeseke hilo lilisababisha
nitokwe na haja ndogo bila kujua, ikabidi nichukue tambara la kufanyia usafi na
kufuta harakaharaka huku nikigeuka kumtazama Rahma asije kuwa ameamka na kuona
nilichokifanya. Nilipomaliza kufuta, harakaharaka nilivaa nguo zangu huku
nikitetemeka kuliko kawaida.
Baba alikuwa pale mlangoni akinisubiri,
nilipomaliza aliingia na kunionesha ishara kwamba nisizungumze kwa sauti ya juu,
akaniuliza nini kilichotokea.
“Wachawi baba, wachawi wengi wamekuja,
angalia walivyonifanya,” nilisema huku nikimuonesha mashavu yangu ambayo
nilikuwa nahisi kama yanawaka moto. Awali niliona baba hataki kuamini kama
ambavyo imekuwa kawaida yake mara kwa mara ninapotokewa na mambo kama hayo
lakini nashukuru safari hii kulikuwa na ushahidi wa moja kwa moja.
“Mungu wangu, umefanya nini?”
“Wamenipiga,” nilisema huku nikianza
kutokwa na machozi.
“Hebu niambie ukweli, umefanya tena
mapenzi na Rahma?”
“Ndiyo.”
“Lakini si tumeshawakataza nyie na
kuwasisitiza kwamba msirudie ujinga wenu?” baba alizungumza kwa hasira lakini
kwa sauti ya chini. Sikujua kwa nini alikuwa akizungumza kwa sauti ya chini,
akanishika mkono na kufungua mlango, akatazama huku na kule na alipojiridhisha,
alinipeleka mpaka kwenye chumba ambacho ndicho nilichotakiwa kulala.
“Hutakiwi kumwambia yeyote kuhusu hiki
kilichotokea, umenielewa?” baba aliniambia, nikatingisha kichwa lakini
nilijiuliza, kama yeye ameweza kusikia zile kelele nilizopiga, si ina maana
nyumba nzima wamesikia? Na kama wamesikia, kwa nini wengine wote hawakuamka
isipokuwa yeye tu?
“Lakini kwa nini haya yanatokea?” utajua
tu lakini unachoniudhi ni kwamba ukiambiwa jambo fulani usilifanye, wewe ndiyo
unalifanya. Hukuwa na mambo ya wanawake kabisa lakini tangu tumefika hapa ndiyo
umekuwa mchezo wako... utasababisha vifo vya wasio na hatia kwa nini unakuwa
mgumu kuelewa?” baba alisema, safari hii siyo kwa ukali bali kwa hisia za ndano
kabisa, kauli yake ikanishtua mno.
Yaani mimi ndiyo nisababishe vifo vya
wasio na hatia? Kivipi? Halafu kulikuwa na uhusiano gani wa mimi kulala na
Rahma na hayo yaliyokuwa yanatokea? Katika yote, jambo ambalo nilijiapiza, ni
kwamba kamwe sitamuacha Rahma maana alikuwa amenionesha dunia ya tofauti mno.
Baba alitoa kichupa kilichokuwa na unga
mweusi lakini kabla hajafanya chochote, aliniambia nikajitazame kwenye kioo
kilichokuwa humo chumbani.
“Mungu wangu,” nilisema kwa mshtuko usio
wa kawaida.
Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa
kwenye Gazeti la Championi Ijumaa.
No comments:
Post a Comment