ILIPOISHIA:
SIKUELEWA kwa nini wananiambia vile, ghafla
niligeuka kutazama upande wangu wa kushoto, lori kubwa la mafuta, lilikuwa
limeshanisogelea huku likiwa kwenye mwendo wa kasi kubwa, taa zote za mbele
zikiwa zimewashwa.
“Mungu wangu!” nilisema kwani nilijua hakuna
kinachoweza kuniokoa kutoka kwenye mdomo wa mauti, ilikuwa ni lazima
linisagesage palepale kama chapati.
SASA ENDELEA...
KUFUMBA na kufumbua, hata sielewi baba
alitokea wapi, akanipitia kwa kasi ya radi na kunivutia kule nilikotokea,
nikaangukia pembeni ya barabara, lile lori likapita kwa kasi kubwa huku
likipiga honi kwa nguvu. Kila mmoja aliamini limenipitia maana niliwaona watu
wakishika vichwa, huku mama akianza kuangua kilio kwa sauti kubwa.
Mimi mwenyewe sikuelewa nini kimetokea,
niligeuka huku na kule, baba hakuwepo tena, nikawa najitazama mwili wangu
nikiwa kama siamini. Sikuwa na jeraha lolote, nikasimama, watu wote wakapigwa
na butwaa, mama akaacha kulia na kujishika mdomo.
Nilijikung’uta mwili, nikatazama huku na kule,
nilipoona hakuna gari, harakaharaka nilivuka na kwenda mpaka pale mama na ndugu
zangu walipokuwa wamesimama, wakiwa ni kama hawaamini walichokuwa wanakiona.
“Togo!” aliita mama huku akinishika mkono,
macho yakiwa yamemtoka pima. Nilimuitikia, akaniuliza kama nipo salama,
nikamjibu nipo salama, akanikumbatia kwa nguvu huku akimshukuru Mungu wake.
Watu wote walikuwa wameacha kila walichokuwa
wanakifanya, wakawa wananitazama mimi. Nadhani lile tukio la kukosakoswa na
gari liliwashangaza sana. Hata mimi mwenyewe nilikuwa bado sijui baba aliwezaje
kuniokoa.
“Kwani ulifuata nini kule ng’ambo ya
barabara,” aliniuliza kaka yangu, nikamtazama usoni nikijiuliza maswali mengi
yaliyokosa majibu.
“Halafu mbona ulikuwa unaongea peke yako?”
alihoji kaka yangu mwingine, nikazidi kushangaa. Ni hapo ndipo nilipogundua
kuwa kumbe hakuna mtu mwingine yeyote aliyemuona baba zaidi yangu, kwa tafsiri
nyepesi ni kwamba baba hakuwa akionekana kwa macho ya kawaida.
Nilitamani kusema kitu lakini nilikumbuka
kauli ya baba aliyekuwa akinisisitiza mara kwa mara kwamba lazima niwe na uwezo
wa kukaa na vitu kifuani, siyo kuzungumza hovyo.
Waliniuliza maswali mengi lakini sikujibu
lolote, nikawa namtazama yule daktari aliyekuwa akiendelea kumpa huduma ya
kwanza yule dereva ambaye alikuwa amelazwa chini na kumgeuzia juu ili kuzuia
damu isiendelee kumtoka puani.
Kwa hali niliyokuwa naihisi, niliona ni bora
nipande kwenye basi na kwenda kukaa kwenye siti yangu kusubiri dereva apate
nguvu tuendelee na safari. Hakuna kitu ambacho huwa sikipendi kama kukaa mahali
kila mtu anakutazama wewe.
Basi watu waliendelea kunitazama mpaka
namalizia kupanda ngazi za basi, kwa kuwa hakukuwa na mtu ndani ya basi,
nilienda kukaa kwenye siti iliyokuwa nyuma ya dereva kama baba alivyonielekeza.
Kwa bahati nzuri, siti hiyo ilikuwa kwa juu na ya dereva ilikuwa kwa chini,
jambo ambalo lingenirahisishia kazi ya kumnyunyizia ule unga mweusi niliopewa
na baba endapo kutatokea tena tatizo lolote.
Ilibidi niutoe kwa ajili ya kufanya majaribio,
nikachukua kidogo nakujaribu kuunyunyiza kwenye kiti cha dereva, nikaona kumbe
ni suala ambalo linawezekana kabisa, nikakaa vizuri kwenye siti yangu.
Sijui nini kilitokea kwani sekunde chache
baadaye, niliona watu wote wakianza kuingia kwenye basi, nikasimama na kutazama
pale dereva alipokuwa akipewa huduma ya kwanza, nikashangaa kuona tayari
alikuwa amesimama na sasa alikuwa akijimwagia maji kichwani na kunawa uso.
Kila kitu kilitokea kwa kasi kubwa sana kiasi
cha kunifanya nibaki na maswali mengi yasiyo na majibu. Nilichohisi ni kwamba
huenda kile kitendo changu cha kuumwagia ule unga pale kwenye siti ya dereva
ndicho kilichompa nguvu haraka dereva huyo.
Kwa kuwa siti hiyo haikuwa yangu, mwenye siti
yake alipokuja na kutaka kukaa, nilimuomba akakae kwenye siti yangu, kwa bahati
nzuri hata yeye kumbe alikuwa akiogopa kukaa mbele hasa kutokana na ile hali ya
kunusurika ajali iliyotokea, nikamuonyesha siti yangu ambapo alienda kukaa.
Muda mfupi baadaye dereva aliingia ndani ya
basi huku akijifuta maji aliyonawa kwa kutumia kitambaa kidogo, akakaa kwenye
siti yake na kufunga mkanda lakini kabla hajawasha gari aligeuka nyuma, macho
yangu na yake yakagongana.
“Sura yako kama siyo ngeni,” alisema huku
akinitazama kama anayejaribu kukumbuka jambo fulani. Kiukweli mimi sikuwa
namjua wala sikumbuki kama niliwahi kuonana naye sehemu yoyote, nikatingisha
kichwa kumkatalia, akawa bado anaendelea kung’ang’aniza kwamba kuna sehemu
tumewahi kuonana. Ilibidi nimkubalie tu huku tabasamu la uongo likiwa
limechanua kwenye uso wangu.
“Jamani naomba kila mmoja asali kwa imani yake
kabla hatujaendelea na safari,” alisema dereva, kweli kila mtu akaanza kusali
kwa imani yake. Ilichukua kama dakika mbili hivi, kumbe mle ndani kulikuwa na
walokole ambao nao walianza kunena kwa lugha.
Baadaye dereva aliwasha gari, akapiga ‘resi’
nyingi kisha akaliondoa gari kwa mwendo wa taratibu, akaliingiza barabarani na
kuendelea kuliendesha kwa mwendo wa taratibu, watu wote ndani ya basi walikuwa
kimya kabisa.
Tuliendelea kushuka kwenye mteremko wa Mlima
Nyoka mpaka tulipofika chini kabisa, akabadili gia na tukaanza kuupandisha
mlima mkali uliopo eneo hilo. Kwa wakazi wa Mbeya au watu waliowahi kufika
huko, watakuwa wananielewa vizuri ninapouzungumzia Mlima Nyoka.
Safari iliendelea na hatimaye tukaumaliza
mlima huo, nikaona kila mtu ndani ya basi ameanza kurudi kwenya hali yake ya
kawaida, stori za hapa na pale zikaanza, wengi wakimshukuru Mungu wao kwani
pengine muda huo tungekuwa tukizungumza mengine.
Dereva naye alizidi kutulia kwenye usukani,
akaongeza mwendo na sasa tukawa tunaenda kwenye mwendo ambao mabasi ya mikoani
hutumia. Safari iliendelea vizuri huku wengi wakianza kusahau kilichotokea. Kwa
upande wangu muda wote nilikuwa makini kabisa kuhakikisha natekeleza kile
nilichoambiwa na baba.
Kwa bahati nzuri, hakukuwa na kikwazo kingine
chochote kilichotokea, majira ya kama saa nane mchana tukawa tayari tumewasili
Ilula, Iringa mahali ambapo abiria hupata mapumziko mafupi ya chakula cha
mchana.
Dereva alitutangazia kwamba tuna dakika kumi
ya kwenda ‘kuchimba dawa’ pamoja na kununua vyakula, abiria wote wakaanza
kushuka. Mama na ndugu zangu nao walishuka, na mimi nikaungana nao.
Jambo la kwanza tulienda kuchimba dawa,
tuliporudi mama akawa anatuuliza kila mmoja anataka kula chakula gani.
Tuliagiza vyakula, kila mmoja anachokitaka, mama akatunulia na soda kisha
tukarudi ndani ya basi.
Muda mfupi baadaye, abiria wote walirudi ndani
ya basi lakini kabla hatujaondoka, dereva alituambia kwamba tunaelekea kwenye
Mlima Kitonga ambao ni mbaya kuliko Mlima Nyoka, akatuambia kwamba kila mmoja
asali tena kwa mara nyingine kwa sababu hajui kama tutavuka salama. Sikuwahi
kufika Kitonga lakini stori nilizokuwa nikizisikia, ni kwamba lilikuwa eneo la
hatari sana ambalo mara kwa mara ajali mbaya zilikuwa zikitokea na kusababisha
vifo vya watu wengi kila kukicha.
Nilijikuta nikitetemeka sana lakini nikajipa
moyo kwamba kila kitu kitakuwa sawa. Tuliendelea na safari na muda mfupi
baadaye, tulifika eneo ambalo bila hata kuuliza, nililitambua kwamba ndiyo
Kitonga, kutokana na jinsi lilivyokuwa.
“Kuna tukio baya linataka kutokea, kuwa
makini,” nilisikia sauti ya baba ikiniongelesha sikioni mwangu, nikageuka huku
na kule, baba hakuwepo, nikajua kwa vyovyote lazima alikuwa ameona jambo ndiyo
maana akanipa tahadhari, nikajiweka vizuri kitini, nikawa natazama huku na
kule.
Je, nini kitaendelea? Usikose next issue!
No comments:
Post a Comment