Monday, August 28, 2017

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 24


ILIPOISHIA:
Treni ilizidi kushika kasi, ikafika kipindi nikawa nahisi kwamba haikanyagi kwenye reli bali inapaa angani kwa jinsi ilivyokuwa ikienda kasi. Ghafla, nilipogeuka huku na kule, nilishtuka kugundua kwamba nilikuwa nimebaki peke yangu kwenye treni hilo, sikukumbuka kama kuna sehemu lilisimama, nikawa najiuliza wale abiria wengine wameenda wapi?
SASA ENDELEA...
Kuna wakati nilihisi pengine huenda nilikuwa kwenye ndoto lakini bado sikuwa na uwezo wa kuthibitisha kwamba ile ilikuwa ni ndoto, maisha halisi au kitu gani, kila kitu kilikuwa gizani. Treni lilizidi kushika kasi, moshi mwingi ukiwa unazidi kuingia ndani na kufanya hata ule mwanga hafifu niliokuwa nauona awali nao umezwe na moshi huo mweusi.
Ghafla, nilihisi kama naguswa na mtu pembeni yangu, nikajikuta nikiruka kwa hofu kubwa, nilipogeuka na kumtazama aliyenigusa, alionesha ni mwanamke kwa jinsi alivyokuwa amevaa lakini uso wake alikuwa ameuinamisha chini.
“Jamal! Jamal, ni wewe?” alisema yule mtu kwa sauti ya chini lakini ambayo ilisikika vizuri licha ya kelele ya vyuma vya treni lile, muungurumo mkubwa na upepo uliokuwa unavuma.
Badala ya kuitikia, niligeuka na kumtazama kwa hofu kubwa mno, yeye wala hakugeuka kunitazama zaidi ya kuendelea kujiinamia vilevile, akisubiri majibu kutoka kwangu. Licha ya zile kelele na yeye mwenyewe kuzungumza kwa sauti ya chini, bado niliweza kuitambua vyema sauti hiyo, haikuwa ngeni kabisa masikioni mwangu.
“Mbona hunijibu!” aliuliza tena lakini tofauti na mwanzo, sauti yake ilisikika kwa nguvu ikiambatana na mwangwi ambao uliyaumiza masikio yangu.

“Wewe ni nani?” nilimuuliza lakini nikashangaa sauti haitoki, nikakumbuka sheria za huko ambapo haraka nilifumba mdomo na kuzungumzia moyoni, sauti kubwa ikasikika lakini badala ya kunijibu, nikamuona akiinua uso wake taratibu na kunigeukia.
“Mungu wangu!” nilijisemea kwa hofu kubwa. Kwa msaada wa mwanga hafifu uliokuwepo ndani ya treni hiyo, niliweza kumtambua kwamba yule mtu alikuwa ni Shenaiza lakini tofauti na yule ninayemfahamu, maeneo yake ya kwenye macho yalionesha kutokuwa na macho ya kawaida kama binadamu wengine, yalikuwa meusi tii ambayo hata sijui niyafananishe na nini.
“Ni mimi Shenaiza, au umenisahau? Nataka kukufuata huko uliko, nimechoka maisha ya duniani, nichukue Jamal!” alisema na kuanza kugugumia kwa kilio kilichoonesha kwamba yupo kwenye maumivu makali mno.
Nilishindwa kuelewa kilichokuwa kinaendelea, muda mfupi uliopita nilikuwa nikizungumza naye katika kile mwenyewe alichoeleza kwamba yupo ndotoni na ameniona mimi kama mzimu, lakini muda huo tulikuwa tukizungumza kwa kawaida, akiniambia kwamba anahitaji nimchukue!
Kwanza nilishangaa, nimchukue kumpeleka wapi? Na hapo tulipokuwepo ni wapi? Na yeye alitokea wapi kwa sababu wakati mimi napanda kwenye treni hilo la ajabu, hakuwepo, aliingiaje? Nilijiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu.
“Mbona unanishangaa hivyo Jamal?” aliniuliza huku mkono wake mmoja akinishika shingoni, nikashangazwa na jambo jingine kwamba mwili wake ulikuwa wa baridi kuliko kawaida. Nilitamani kupiga kelele kwa hofu niliyokuwa nayo, nilihisi kama nimekutana na kiumbe wa ajabu mwenye sura ya kibinadamu na sasa alikuwa anataka kuyakatisha maisha yangu.
“Usiniogope Jamal! Hata mimi mwanzo nilikuwa nakuogopa lakini hushangai sikuogopi tena?”
“Kwani hapa ni wapi Shenaiza na wewe umefikaje huku?”
“Mh! Hata mimi sielewi hapa ni wapi lakini nafikiri tunaelekea sehemu nzuuuri ambayo ndiyo itakuwa makazi yetu ya milele, si unajua duniani tunapita tu?”
“Sijakuelewa, kwa hiyo hapa siyo duniani?”
“Siyo duniani Jamal, duniani si kule tulikokuwa tunaishi siku zote? Kwani unaona hapa kunafanana na kule?”
“Sasa kama siyo duniani ni wapi na wewe imekuwaje uje huku?”
“Sijui hapa ni wapi, mimi nimekuja huku kwa sababu nimechoka kuishi, yaani kila siku wananichoma dawa za usingizi, nikiamka tu wananichoma tena, leo nimeamua kujiovadozi kwa makusudi ili nife?”
“Niniii? Shenaiza, unazungumzia nini mbona sikuelewi?”
“Nimeamua kukufuata Jamal, kwa kuwa wewe ulikufa na mimi nikiwa ndiyo chanzo, nimeamua na mimi nife tu.”
“Lakini mimi sijafa Shenaiza, mimi niko hai.”
“Ungekuwa hai ndiyo ungekuwa huku? Acha kujidanganya Jamal!”
“Hapana sijafa! Mimi sijafa! Niko haiii,” nilisema kwa sauti kubwa iliyofuatiwa na kilio.
***
Hali ilikuwa ya patashika nguo kuchanika ndani ya makazi ya siri ndani ya jumba la kifahari la baba yake Shenaiza, lililokuwa Kurasini. Hakuna ambaye alielewa nini kimetokea kwa sababu kama ilivyo kawaida, Shenaiza alizinduka kutoka usingizini baada ya dawa alizokuwa amedungwa awali kuisha nguvu.
Tofauti na awamu zote, safari hii alipozinduka usingizini,  alijikokota na kuinuka kutoka kitandani kwake, akasogelea mpaka kwenye kabati lililokuwa ndani ya chumba hicho. Mfanyakazi maalum aliyepewa jukumu la kuhakikisha anapata huduma zote muhimu, alishtuka kumuona akiwa amefungua kabati, ikabidi amuwahi na kumlaza kitandani.
“Nasikia njaa sana, kaniletee chakula,” alisema Shenaiza, harakahara yule mhudumu akatoka kwenda kumletea chakula kwani tayari kilishaandaliwa kwa ajili yake. Alipotoka tu, Shenaiza alisimama na kurudi tena pale kabatini.
Muda mfupi baadaye, alichukua kichupa kidogo pamoja na bomba la sindano, harakaharaka akarudi pale kitandani kwake na kujilaza, akavificha vile vitu chini ya mto. Mhudumu alipoingia akiwa na sinia lililokuwa limejaa vyakula vya kila aina, Shenaiza alitulia kimya kama hajui kinachoendelea.
Yule mhudumu alimuandalia chakula ambapo tofauti na alivyotegemea kwamba atakula kwa sababu alikuwa na njaa kama mwenyewe alivyodai, Shenaiza alishikashika tu kisha akamwambia atoe.
“Mbona sasa hujala?”
“Hamu ya kula imeniisha ghafla, weka nitakula baadaye.”
“Lakini dada, mimi nilikuwa na ushauri mmoja juu yako. Unajua baba anakupenda sana ila anase...”
“Shiii! Ishia hapohapo, we toa vyakula vyako kisha uondoke, sitaki kusikia kitu chochote kwa sasa, niache,” alisema Shenaiza kwa sauti iliyoonesha kutokuwa na masihara hata kidogo.
Yule mhudumu alikusanya vyombo vyake na kutoka nje, akawaacha walinzi wakiwa mlangoni hapo kumlinda Shenaiza kama walivyoelekezwa na baba yake.
Baada ya mhudumu huyo kutoka, harakaharaka Shenaiza alichukua kile kichupa kilichokuwa na maandishi yaliyosomeka Diazepam, akakitingisha na kuchukua bomba la sindano, akavuta dawa nyingi kiasi cha kulifanya bomba lote lijae, akachukua mtandio wake na kujifunga mkononi kwa nguvu, akatafuta mshipa mkubwa wa damu.
Akajichoma na kuanza kuisikumia ile dawa ndani ya mshipa wake wa damu. Hakuweza kuimaliza yote, aliposukuma kiasi cha nusu ya bomba kuingia mwilini mwake, usingizi mzito ulimpitia, akalala huku bomba hilo likiwa bado linaning’inia mkononi.
Yule mhudumu aliporudi kwa mara ya pili kuja kumalizia vyombo vichache vilivyosalia, alishtuka kupita kiasi baada ya kuona damu nyingi ikiwa inatoka kwenye mkono wa Shenaiza na kulowanisha shuka lake huku mwenyewe akitapatapa kama anayetaka kukata roho, mapovu yakimtoka kwa wingi mdomoni na puani.
Harakaharaka, huku akilia, aliwaita walinzi ambao nao walimuita daktari wa familia hiyo, muda mfupi baadaye wote wakawa wamejaa ndani ya chumba hicho wakijaribu kuokoa maisha ya msichana huyo lakini ilionesha kwamba tayari walikuwa wamechelewa.
Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Championi Ijumaa.
NB: Kufuatia maombi ya wasomaji wetu, sasa simulizi hii itakuwa inatoka mara mbili kwa wiki; Jumatatu kwenye Championi Jumatatu na Ijumaa kwenye Championi Ijumaa.


No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...