ILIPOISHIA:
“Mzimu?
Mzimu gani wakati sasa hivi ni mchana?”
“Nilikuwa
nimelala nikatokewa na mzimu wa marehemu Jamal!”
“Mh!
Au unaanza kuchanganyikiwa mwenzetu? Jamal gani unayemzungumzia?”
SASA
ENDELEA...
“Nimeota kabisa naongea na Jamal wakati ameshafariki.
Ninachosema ni kweli kabisa, wala siyo kwamba nimeanza kuchanganyikiwa,”
Shenaiza alizidi kusisitiza lakini hakuna aliyemuamini.
Tangu aende kuchukuliwa kwa nguvu na
walinzi wa baba yake na kurejeshwa kwenye makazi ya siri ya familia yao, Kurasini,
alikuwa ni kama amechanganyikiwa. Muda mwingi alikuwa ni mtu wa kulia na
kuijutia nafsi yake huku akimlaumu baba yake kwamba alikuwa akimuonea kwa yote
aliyokuwa akimfanyia.
Alipokuwa akizidi kusumbua, daktari
maalum wa familia hiyo, alikuwa akipewa kazi ya kumdunga dawa za usingizi
zilizomfanya alale muda mrefu. Hali hiyo ilimfanya kwa kiasi kikubwa akose hata
nafasi ya kufuatilia kilichokuwa kinaendelea kuhusu Jamal, kitu pekee
alichokuwa anakijua akilini mwake, ni kwamba kijana huyo alikuwa amefariki
dunia baada ya lile tukio ambalo yeye ndiye aliyekuwa chanzo.
“Muiteni dokta.”
“No! I dont need any more sedatives
please, im not out of my mind,” (Hapana! Sihitaji tena kuchomwa dawa za
usingizi, mimi sijachanganyikiwa) alipiga kelele Shenaiza lakini haikusaidia
kitu, muda mfupi baadaye, daktari wao aliingia akiwa na bomba la sindano na
kichupa cha dawa mkononi kilichokuwa na maandishi yaliyosomeka Diazepam, akiwa
ameongozana na wanaume wawili wenye miili mikubwa.
Shenaiza alijaribu kufurukuta lakini wapi!
Akashikiliwa kwa nguvu na wale wanaume, daktari akatoa pamba iliyokuwa imepakwa
‘spirit’, akamsafisha sehemu ya ndani ya mkono wake, mahali kwenye mishipa ya
damu na taratibu akazamisha sindano kwenye mshipa wake na kuisukumia ile dawa
ndani, muda mfupi baadaye, Shenaiza alianza kuzungumza maneno yasiyoeleweka na
kupitiwa na usingizi mzito.
Wakati yote hayo yakiendelea, nilikuwa
nikishuhudia kila kitu, bado nikiwa katika hali ileile ambayo hakuna mtu ambaye
aliniona ingawa mimi nilikuwa na uwezo wa kuona kila kitu. Kile kitendo cha
kushuhudia Shenaiza akifanyiwa ukatili ule, kilinisikitisha sana ndani ya moyo
wangu na kunifanya nianze kumtazama Shenaiza kwa sura tofauti kabisa.
Nisiseme uongo, baada ya mfululizo wa
matukio yale, mpaka lile la mwisho ambalo liliyabadilisha kabisa maisha yangu
na kunifanya nisieleweke kama mimi ni binadamu au maiti, nilikuwa nikimchukia
sana kwa kuona kwamba yeye ndiye aliyeniingiza kwenye mtego huo kwa makusudi.
Hata hivyo, kwa kile nilichokishuhudia,
nilianza kuamini kwamba huenda haikuwa dhamira ya Shenaiza kuniingiza kwenye
matatizo makubwa kiasi kile, nikajikuta nikimuonea huruma na kuwalaani wale
waliokuwa wakimfanyia kitendo kile.
Nilijikuta nikiwasonya kwa nguvu. Cha
ajabu, ilionesha kwamba walisikia nilivyowasonya kwani wote waliokuwa ndani ya
kile chumba, wakiwemo wale ndugu zake Shenaiza waliokuwa wamefanana naye sana,
yule daktari na wale walinzi, waligeuka na kuanza kutazama huku na kule.
“Nimesikia kama mtu amesonya, au masikio
yangu yamesikia vibaya,” aliuliza mmoja, kila mmoja wao akajibu kwamba na yeye
amesikia lakini wakawa hawajui ni nani aliyefanya kitendo hicho. Japokuwa
nilikuwa palepale jirani yao, kwenye moja ya kona za chumba hicho, hakuna
aliyeniona, baadaye nikawaona wakianza kutoka mmoja baada ya mwingine, kila
mmoja akionesha kuwa na hofu kubwa ndani ya moyo wake.
Nilichojifunza, katika maisha ya
kawaida, ukijiona upo katika mazingira ambayo hakuna mtu lakini ghafla ukasikia
mtu anakusonya kwa sauti lakini ukigeuka humuoni yeyote, jua kwamba eneo hilo
hauko peke yako. Kuna mtu au watu wengine wanakuona na pengine hawafurahishwi
na unachokifanya.
Ukiwa na akili, inabidi urekebishe kile
unachokifanya kwa sababu unaweza kupata matatizo ambayo hakuna anayeweza
kuyaelezea, hapa ndipo lile neno ‘katika mazingira ya kutatanisha’
linapotumika. Kwamba unafanya tukio au unapatwa na tukio ambalo katika akili ya
kawaida, hakuna anayeweza kuelewa nini hasa kilichotokea.
Basi niliendelea kusimama palepale
nikimtazama Shenaiza ambaye tayari alishapitiwa na usingizi mzito, nikawa na
shauku kubwa ya kutaka kujua mambo mengi yaliyokuwa yamejificha nyuma ya maisha
yake.
“Jamal! Jamal! Jamaaaal!” nilisikia
sauti nzito, nene ya kutetemeka ikiliita jina langu kwa nguvu, kabla hata
sijajibu chochote, nilishangaa nikichukuliwa pale na kitu kama kimbunga kikali,
sekunde chache tu baadaye, nilijikuta nikiwa tena kulekule nilikokuwa mwanzo,
giza nene likiwa limetawala kila upande lakini tofauti na awali, nilihisi kama
nimesimama juu ya kokoto.
Ile sauti iliyoniita haikusikika tena,
ila kwa mbali nikawa nasikia muungurumo kama wa treni likija kwa kasi kubwa
pale nilipokuwepo. Muungurumo ulizidi kuongezeka, nikawa nageuka huku na kule
kutazama ulikokuwa unatokea lakini sikuona chochote, nikahisi nikiendelea
kusimama palepale huenda nikagongwa na treni hilo.
Nilipopiga hatua moja mbele, nilikanyaga
kitu kama reli, nikagundua kwamba kumbe nilikuwa kwenye njia ya treni hilo
ambalo sikuelewa ni la aina gani kwa sababu ninachojua mimi, treni huwa zinakuwa
na taa na huwa haziendi kwa mwendo kasi kiasi hicho.
Ilibidi nichangamke, nikakimbia hatua
kadhaa lakini kila nilipokuwa napita, bado nilikuwa nikikanyaga reli, ghafla
nikasikia mlio mkali wa honi uliofuatiwa na mwanga mkali wa taa, ni hapo ndipo
nilipogundua kuwa treni hilo lilikuwa limenikaribia mno na lilikuwa likija
usawa wangu kabisa kiasi kwamba kama nisingefanya chochote kujiokoa, lingenigonga
na kunisagasaga.
Cha ajabu zaidi, baada ya kunipigia honi
na kunimulika, miguu yangu iliganda palepale nilipokuwa nimesimama, sikuweza
hata kutingishika, nikawa nimeganda kama sanamu huku hofu kubwa ikiwa imenijaa
moyoni, ilibidi nifumbe macho kwani nilijua huo ndiyo mwisho wa maisha yangu.
Nilisikia kelele za vyuma vikikwaruzana,
nadhani ni matairi ya treni na reli baada ya kufunga breki kali, nikasikia
nikipulizwa na upepo mkali na kudondokea mita chache mbele, nilipofumbua macho,
lile treni lilikuwa limesimama mita chache kutoka pale nilipokuwa nimeangukia,
ile taa ikiwa imezimwa lakin likiendelea kunguruma kwa nguvu.
“Panda twende,” ilisikika sauti nzito ya
mwanaume, nilipoinua macho yangu, nilimuona mzee mmoja akiwa amekaa sehemu ya
dereva, akawa ananipungia mikono akiniashiria nifanye vile alivyoniambia.
Harakaharaka niliinuka, nikalisogelea
lile treni ambalo lilikuwa na joto kali, nadhani ni kwa sababu ya kasi liliyokuwa
nayo, yule mzee akanionesha niendelee kuelekea nyuma mpaka sehemu ya kupandia,
nilifanya hivyo lakini kutokana na giza nene lililokuwepo nilishindwa hata
kuona sehemu ya kuelekea, nikashtukia nikishikwa mkono na mtu ambaye wala
sikumuona, akanisukumia kwenye ngazi, nikapanda na kuingia ndani ya treni hilo.
Kilichonipa moyo, ndani ya treni
hakukuwa na giza kama kule nje, kulikuwa na taa ndogo iliyokuwa na mwanga
hafifu uliofanya angalau nione ndani ya lile treni kulivyokuwa. Treni hiyo
ilikuwa chakavu sana, kuanzia viti vyake, sakafu na kila kitu ndani yake.
Kulikuwa na abiria kadhaa ambao wote
walikuwa wameinamisha vichwa vyao kuonesha kwamba walikuwa wamelala, niliamini
kwamba huenda watakuwa wametoka safari ya mbali sana ndiyo maana walichoka
vile.
Muda huohuo, treni iliondoka kwa kasi
kubwa, kelele za vyuma na muungurumo zikawa zinasikika kwa nguvu huku moshi
mwingi ukiingia kupitia madirishani, nilitamani kuuliza tulikuwa tunaelekea
wapi lakini hakukuwa na wa kumuuliza. Nilitamani hata kumuona yule mtu
aliyenishika na kunisaidia kupanda lakini pia sikumuona, watu wote walikuwa
kimya kabisa, nyuso zao wakiwa wameziinamisha.
Treni ilizidi kushika kasi, ikafika
kipindi nikawa nahisi kwamba haikanyagi kwenye reli bali inapaa angani kwa
jinsi ilivyokuwa ikienda kasi. Ghafla, nilipogeuka huku na kule, nilishtuka
kugundua kwamba nilikuwa nimebaki peke yangu kwenye treni hilo, sikukumbuka
kama kuna sehemu lilisimama, nikawa najiuliza wale abiria wengine wameenda
wapi?
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment