ILIPOISHIA:
“Mungu
wangu, akina nani tena hao usiku wote huu?” nilijiuliza huku nikirudi nyuma na
kujibanza pale uchochoroni, nikawaona wale wanaume wakiendelea kugonga mlango
kwa nguvu. Ugongaji wao ulionesha dhahiri kwamba hawakuwa wamekuja kwa heri,
nikawa natetemeka nikiwa sijui nitafanya nini.
SASA
ENDELEA…
Mlango uliendelea kugongwa kwa nguvu, nikiwa
nimejibanza palepale, nikitetemeka mno kwa hofu kwani nilishaona hatari
iliyokuwa mbele yangu. Niliwaona wale watu wakijadiliana na muda mfupi baadaye,
mmoja kati yao aliondoka eneo hilo. Muda mfupi baadaye, alirudi akiwa amemkwida
mtu ambaye nilipomtazama, nilimtambua haraka kuwa ni yule dereva teksi
aliyetuleta.
Japokuwa sikuwa nasikia walichokuwa wakikizungumza
lakini ilionesha wazi kwamba walikuwa wakimshinikiza awahakikishie kama pale
ndipo tulipoingia.
Nikamuona akijitetea na kusisitiza kuwa ni penyewe,
kufumba na kufumbua nilimuona mmoja kati ya wale watu akimpiga ngumi yule
dereva iliyosababisha apepesuke na kutaka kuanguka, mwenzake akamdaka na
kumsimamisha vizuri, wakawa wanaendelea kumhoji huku yule mwingine akiendelea
kugonga mlango kwa nguvu.
Kwa ilivyoonesha, baada ya mimi na Shenaiza kuondoka
hospitalini, watu wale walikuwa wakitufuatilia na ndipo walipofanikiwa kumpata
dereva aliyetuleta pale nyumbani kwangu na kumteka. Nilijiuliza wale ni akina
na nani na kwa nini walikuwa wakitufuatilia?
Niliendelea kujiuliza maswali mengi yaliyokosa
majibu, nilimlaumu pia Shenaiza kwa kutonieleza ukweli wa kilichokuwa
kinaendelea kwani mpaka muda huo, nilikuwa nimenaswa kwenye mtego ambao sikuwa
naujua. Sikuwa najua Shenaiza ni nani? Ilikuwaje mpaka akajeruhiwa kiasi kile
na aliyemjeruhi ni nani na wale watu walikuwa na uhusiano gani naye! Nilikosa
majibu.
Kingine kilichonitisha, kama yule dereva tu ambaye
hakuwa na hatia yoyote alikuwa akipigwa kiasi kile, hali ingekuwaje endapo
wangenikamata na mimi? Kwa kuwa nilikuwa nimefunga mlango kwa kufuli, tena geti
lilikuwa la chuma, niliamini hawawezi kumpata Shenaiza, kwa lugha nyepesi,
Shenaiza alikuwa salama mle ndani, tatizo lilikuwa ni kwangu mimi.
Nilichoamua kukifanya kabla hawajanishtukia, ilikuwa
ni kuondoka haraka eneo hilo na kwenda kutafuta hifadhi sehemu nyingine salama.
Harakaharaka niliondoka, mkononi nikiwa na mzigo wangu wa chipsi na kutembea
mpaka mtaa wa pili.
Nilitokezea kwenye kituo cha Bajaj na bodaboda
ambapo nilimuita dereva mmoja wa bodaboda ambaye mara kwa mara huwa ananibeba.
“Vipi bro mbona usiku? Siyo kawaida yako!”
“Aah! Chukulia poa, nataka unipeleke Kijitonyama,”
nilisema huku nikipanda kwenye bodaboda, nikawa nageuka huku na kule
kuhakikisha kama hakuna mtu anayenifuatilia. Kwa jinsi nilivyokuwa natetemeka,
ungeweza kudhani nimetoka kumwagiwa maji ya baridi.
Tuliondoka eneo hilo huku nikiendelea kujiuliza
maswali yaliyokosa majibu. Sikujua hatma ya Shenaiza pale nyumbani kwangu.
Niliamua kwenda Kijitonyama kwa rafiki yangu na mfanyakazi mwenzangu, Justice
ili akanipe hifadhi lakini pia anipe ushauri wa nini cha kufanya.
Dakika kadhaa baadaye, tayari nilikuwa nimeshafika
Kijitonyama, nikamlipa yule dereva wa bodaboda na kushuka, nikakaza mwendo
kuelekea kwenye uchochoro wa kuelekea kwenye nyumba aliyokuwa anaishi Justice.
Kwa kuwa nilijua kwa muda ule watakuwa wameshafunga
geti, nilienda kumgongea dirishani.
“Justice! Justice!”
“Mh! Nani tena usiku wote huu?”
“Ni mimi Jamal!”
“Jamal?” alihoji Justice kwa mshtuko, nikamuona
akifungua pazia, akiwa ni kama haamini kwamba nimemfuata usiku huo.
Alipohakikisha ni mimi, harakaharaka alienda kufungua mlango lakini nilipotaka
kuingia ndani, alinizuia:
“Nipo na shemeji yako, vipi kwema utokako?”
“Dah!” nilijibu kwa kifupi, kauli yake kwamba
alikuwa na mwanamke usiku huo ilinimaliza kabisa nguvu. Niweke wazi kwamba
miongoni mwa matatizo ya rafiki yangu Justice, ilikuwa ni kupenda kubadilisha
wanawake kama nguo. Mara kwa mara alikuwa na tabia ya kulala na wanawake
tofautitofauti, jambo ambalo binafsi sikulifurahia.
Kibaya zaidi ni kwamba alikuwa akiishi kwenye chumba
kimoja tu kwa hiyo akishakuwa na mgeni ndani, inakuwa vigumu kuingia, ikabidi
nimwambie atoke ili tuzungumzie nje kwa sababu nilikuwa na matatizo makubwa.
Alirudi ndani kwani kwa muda huo alikuwa amejifunga
taulo tu, alipotoka tena, alikuwa ameshavaa nguo.
“Samahani bwana sikujua kama utakuja, nisamehe kwa
sababu tunazungumzia nje, si unajua tena,” alisema Justice huku akifunga
vifungo vya shati lake, sikupoteza muda ikabidi nimueleza kwa kifupi
kilichotokea.
“Mungu wangu, sasa itakuwaje?” alisema akionesha
kupatwa na mshtuko mkubwa mno.
“Hata sielewi, ndiyo maana nimekuja kwako kupata
ushauri.”
“Umeshaenda kuripoti polisi?”
“Sijaenda kwa sababu hata huyo msichana mwenyewe
namna alivyofika nyumbani kwangu, ni kwamba nimefanya kumtorosha tu hospitalini,”
nilimwambia lakini akasisitiza kwamba ni lazima twende tukatoe taarifa polisi
ili chochote kitakachotokea, polisi wawe wanajua.
Kwa upande fulani nilikubaliana na alichoniambia,
hatukuwa na muda wa kupoteza, alirudi ndani kumuaga msichana wake na alipotoka,
tulielekea moja kwa moja kituo cha polisi. Kwa kuwa pale alipokuwa anaishi
hapakuwa mbali na Kituo cha Polisi cha Kijitonyama au maarufu kama Mabatini,
dakika kadhaa baadaye tulikuwa tumefika.
Tukaandikisha maelezo pale kaunta lakini kwa bahati
mbaya zaidi, askari aliyekuwa zamu alisema askari wote wametoka kwenda kwenye
doria kwa hiyo kama nahitaji msaada wa polisi, nisubiri mpaka warudi kutoka kwenye
doria. Kutokana na hali ilivyokuwa, sikuwa na ujanja zaidi ya kubaki kusubiri
hao askari warudi.
Kwa kuwa Justice alikuwa na mgeni wake, nilimruhusu
aondoke kurudi kwake na kumshukuru kwa msaada aliokuwa amenipa. Akaondoka na
kuniacha nimekaa kwenye benchi pale kituoni. Tayari saa ya kwenye simu yangu ilikuwa
ikionesha kwamba ni saa sita za usiku.
Kutokana na pilikapilika nyingi, nilijikuta nimekaa
muda mrefu bila kushika simu, nilipoishika nilikuta meseji kadhaa kutoka kwa
rafiki zangu, moja ikiwa ni kutoka kwa Raya, msichana tuliyekuwa tukifanya naye
kazi ambaye alitokea kunizoea sana.
Alikuwa ametuma ujumbe wa kunitakia usiku mwema kama
ilivyo kawaida yake, nilishusha pumzi ndefu na kuendelea kutafakari hatma ya
maisha yangu. Baada ya kukaa muda mrefu pale kituoni huku kukiwa hakuna dalili
yoyote ya askari kuja, ilibidi niage na kuondoka kwa sababu kesho yake
nilitakiwa kuwahi kazini kwani kuna kazi muhimu sana niliyokuwa natakiwa
kuikamilisha.
Nikiwa naondoka, simu yangu ilianza kuita mfululizo,
haikuwa kawaida mimi kupigiwa simu usiku huo, nikaitoa na kutazama namba ya mpigaji.
Alikuwa ni Raya, nikashtuka kuona simu yake usiku huo, harakaharaka nikapokea.
“Vipi Jamal, umeshalala?”
“Hapana, bado sijalala Raya.”
“Mbona nakutumia meseji hupokei? Mpaka nimepatwa na
wasiwasi.”
“Mh! Samahani kwa kuchelewa kujibu lakini usijali,
niko poa na usiku mwema pia.”
“Haya ahsante, nilitaka nisikie tu sauti yako ndiyo
nilale. Halafu mbona kama unatembea, unaenda wapi usiku wote huu?”
“Aah! Kuna mahali nimetoka ndiyo narudi nyumbani.”
“Jamal! Umetoka wapi usiku wote huu?” Raya alinibana
kwa maswali. Jambo ambalo naomba niliweke wazi kuhusu Raya, japokuwa mimi
nilikuwa namchukulia kama rafiki wa kawaida tu, alikuwa na hisia fulani juu
yangu ambazo siwezi kuzielezea kwa urahisi.
Kwanza alikuwa anapenda sana kuwa karibu na mimi
japokuwa mwenyewe nilikuwa nikimkwepa sana. Tukiwa kazini, alikuwa anapenda
muda wa lanchi tutoke na kwenda kula pamoja na ikitokea nimeenda peke yangu,
basi atanuna na kukosa raha siku nzima. Pia alikuwa anapenda hata wakati wa
kutoka, tuongozane mpaka kituoni, ahakikishe nimepanda daladala kurudi kwangu
ndiyo na yeye aende kwao kwani alikuwa akiishi Mwenge ya Mlalakua.
“Nipo Kijitonyama hapa jirani na Kituo cha Polisi
cha Mabatini.”
“Please nakuomba tuonane usiku huuhuu, baba na mama
wamesafiri tangu juzi, niko mwenyewe tu, nahisi haupo sawa na nahitaji
kukusaidia, niambie nikukute wapi, nakuja na bodaboda sasa hivi,” alisema Raya,
nikashusha pumzi ndefu.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
Nifollow kwenye mitandao ya kijamii kwa:
Facebook: Hash Power
Instagram: Hashpower7113
Twitter: Hash- Power.
No comments:
Post a Comment