ILIPOISHIA:
Kuna
wakati hofu ilinizidi na kutaka nigeuze nilikotoka lakini kitu ndani ya moyo
wangu kikaniambia nizidi kusonga mbele. Kadiri nilivyokuwa nazidi kusonga mbele
ndivyo zile sauti zilivyokuwa zinazidi kuongezeka, nikazidi kutetemeka kwa hofu
huku nikiwa sijui nini itakuwa hatma yangu.
SASA
ENDELEA...
Sauti
zilizidi kuongezeka, nikawa nasikia sauti nyingine zikiugulia maumivu makali
mno, nilitamani nione nini kilichokuwa kinaendelea lakini sikuweza kutokana na
lile giza. Ilifika mahali ikabidi niwe natembea kwa uangalifu sana kwani
nilihisi nilikuwa nikipita jirani kabisa na wale watu waliokuwa wakilia kwa
maumivu makali.
Kiasili
mimi ni mwoga sana kiasi kwamba nikiwa nyumbani kwangu, hata panya akipita
darini kwa kasi, lazima nitashtuka sana lakini nashangaa siku hiyo kadiri muda
ulivyokuwa unasonga mbele ndivyo hofu ilivyokuwa inazidi kupungua.
Haikuwa
rahisi kupita sehemu ambayo unasikia kabisa wenzako wanalia kwa kusaga meno kwa
maumivu makali kama ile. Ukiachilia mbali sauti hizo za watu, kulikuwa pia na
sauti za watoto wachanga waliokuwa wamepamba moto kulia, ungeweza kudhani
wamelazwa kwenye siafu.
Nilizidi
kutembea kusonga mbele kufuata ile sauti iliyokuwa ikiliita jina langu, zile
sauti za watu zikaanza kupungua kidogo kuonesha kwamba tayari nilishapita eneo
walilokuwepo, zikawa zinasikika za wale watoto wachanga huku pia sauti za
wanyama wakali nazo zikianza kuongezeka.
Nikiwa
naendelea kutembea, nilishtukia sauti ya kutisha ya ndege mkubwa ikija kwa kasi
pale nilipokuwepo, kufumba na kufumbua nilijikuta nikipigwa kikumbo na ndege
yule mkubwa ambaye hata sikuweza kujua ni ndege gani kutokana na jinsi
alivyokuwa mkubwa.
Kucha
zake kali zikaniparua upande wa shavu langu la kushoto na kunifanya nijihisi
maumivu makali sana. Hata hivyo, nilijikaza na kuendelea kusonga mbele. Lile
dege ambalo baada ya kunipiga kikumbo lilipotelea mbali, nililisikia likianza
kurudi tena, safari hii likipiga kelele kwa sauti kubwa kuliko mwanzo.
Sikumbuki
kama katika maisha yangu ya kawaida nimewahi kusikia mlio wa namna hiyo wa
ndege. Ilibidi niwe makini lisije kuniumiza tena, nikainua mikono na kujiziba
upande wa usoni, likaja kwa kasi na kunipita, nikasikia upepo ukinipuliza kisha
likatokomea kule ile sauti iliyokuwa ikiniita ilikokuwa inatokea.
Nilipojigeuza
pale lilipokuwa limeniparua, niligundua kwamba vitu vya majimaji vilikuwa
vikinitoka. Niliamini kwamba ni damu kwa sababu binadamu anapoumia, kinachotoka
ni damu ingawa kutokana na giza lile, sikuweza kuthibitisha hilo zaidi ya
kuendelea kujiaminisha mwenyewe.
Nikiwa
nazidi kuelekea kule ile sauti ilikotokea, kwa mbali nilianza kuona kama mwanga
hafifu ukionekana mita nyingi kutoka pale nilipokuwa nimefika. Nilishusha pumzi
ndefu kwa sababu niliamini mwanga ni dalili ya uhai, nikajua lazima naweza
kupata msaada nikifika pale kwani mpaka muda huo, sikuwa naelewa nini itakuwa
hatima yangu.
Milio
ya wanyama wa kutisha ilizidi kusikika kutoka kila upande lakini sikukata
tamaa, nilizidi kusonga mbele huku giza bado likiwa nene vilevile, akili zangu
zote zikiwa ni kwenye ule mwanga niliokuwa nauona. Cha ajabu, licha ya kutembea
sana, bado ule mwanga uliendelea kuonekana ukiwa umbali uleule, jambo ambalo
lilinishangaza sana.
Nilijaribu
kuongeza urefu wa hatua lakini ilikuwa sawa na kazi bure, miungurumo ya wanyama
wakali ikawa inazidi kuongezeka huku kwa mbali nikisikia sauti kama za yule
ndege mkubwa aliyenijeruhi zikija tena lakini tofauti na awali, safari hii
ilionesha kwamba walikuwa zaidi ya mmoja kutokana na ukubwa wa sauti zao.
“Mungu
wangu, nimekwisha,” nilijikuta nikijisemea moyoni lakini jambo la ajabu tena,
wakati mimi nikiamini maneno hayo niliyasemea moyoni, yalisikika kwa sauti
kubwa utafikiri nimezungumza kwa kufumbua mdomo.
“Jamal
mbona hufiki? Fanya haraka,” ile sauti iliyoniita ilisikika tena kutokea umbali
ambao siwezi kuukadiria, nikataka nifumbue mdomo na kumuuliza yule mtu
aliyekuwa ananiita ni nani, pale ni wapi na nilipelekwa pale kufanya nini
lakini nilipofumbua mdomo, nilishangaa sauti ikiwa haitoki.
“Leo
ndiyo mwisho wa maisha yangu,” nilijisemea moyoni baada ya kuona nimeshindwa
kuwasiliana na yule mtu lakini cha ajabu tena, sauti ilisikika kwa nguvu.
Nilishangaa sana, yaani nikifumbua mdomo na kuzungumza, sauti haisikiki lakini
nikizungumza kimoyomoyo ndiyo sauti inasikika, nilibaki nimepigwa na butwaa.
Niliamua
kujaribu kitu, kuzungumza kimoyomoyo kumuuliza yule mtu yale niliyotaka
kumuuliza. Cha ajabu sasa, sauti yangu ndiyo ilisikika kwa nguvu na naamini yule
mtu aliyekuwa ananipa maelekezo alinisikia.
“Wewe
ni nani? Hapa ni wapi na kwa nini nimeletwa huku?”
“Mh!
Hutakiwi kuuliza swali lolote,” ilisikika sauti ile kwa mwangwi mkubwa kama
ilivyokuwa mwanzo.
“Mbona
natembea lakini sifiki?” nilijisemea tena moyoni lakini sauti ikasikika vizuri
kabisa.
“Geuka
ulikotoka,” ilisikika ile sauti, safari hii milio ya wale ndege wakubwa ilikuwa
imekaribia kabisa na kwa jinsi walivyokuwa wanakuja kwa kasi, nilijua lazima
watanijeruhi tena.
Nilijaribu
kugeuka kwa kutumia upande wa kulia lakini nikashangaa mwili wangu ukiwa mzito
mno, nikajaribu upande wa kushoto, nikageuka bila tatizo lolote, nikawa
natazama kule nilikotokea ambako nako kulikuwa na giza totoro kama kule
nilikokuwa naelekea, tofauti yake ni kwamba huku nilikogeukia hakukuwa na
mwanga unaoonekana kwa mbali.
“Haya
tembea kinyumenyume,” ilisikika ile sauti, kweli nilipojaribu kupiga hatua moja
tu, nilijikuta mwili ukiwa mwepesi sana, nikawa naenda bila kikwazo chochote,
huku nyuma sauti za wale ndege zikawa zinazidi kufifia. Ndani ya muda mfupi tu,
tayari nilikuwa nimefika pale ule mwanga ulipokuwa unatokea, niliisikia ile
sauti ikiniamuru kugeuka, nikafanya hivyo, macho yangu yakatua kwenye jiwe la
ukubwa wa wastani lililokuwa likiwaka bila kuteketea.
Nilishangaa
sana kuona jiwe likiwaka, tena moto mkali unaoweza hata kuchemsha maji ndani ya
muda mfupi. Hata hivyo, licha ya kwamba jiwe hilo lilikuwa likiwaka, mwanga
wake haukuweza kunisaidia kuona chochote, nikawa naangaza macho huku na kule
nikitarajia naweza kumuona yule mtu aliyekuwa ananipa maelekezo lakini haikuwa
hivyo.
Kufumba
na kufumbua, lile jiwe lilianza kutetemeka kama kuna tetemeko la ardhi kisha
likaanza kubingirika kuelekea upande wa kushoto kutoka pale lilipokuwepo.
Nilishtuka mno, nikawa natetemeka kwa hofu kubwa. Likaendelea kubingirika kwa
kasi huku ikionesha kwamba kule lilikokuwa likiendelea kulikuwa na mteremko.
Sijui
akili gani ilinituma kuanza kulifuata lile jiwe kwani hakika huo haukuwa uamuzi
sahihi. Nilipopiga tu hatua moja, nilijikuta nikianza kuserereka kuelekea kule
lile jiwe lilikokuwa linaelekea.
Nilijaribu
kufunga breki lakini ilikuwa sawa na kazi bure, niliendelea kuserereka na kila
nilipojaribu kujishikiza sehemu, sikuona chochote cha kunisapoti, ikafika
mahali na mimi nikawa nabingirika kulifuata lile jiwe huku mteremko ukizidi
kuwa mkali kadiri nilivyokuwa nasonga mbele.
Kwa
mbali nilianza kuhisi joto kali huku lile giza nene likianza kupungua na
kumezwa na mwanga mwekundu ambao hata bila kuuliza, nilijua kuwa ni wa moto
mkubwa uliokuwa unawaka. Zile sauti za watu waliokuwa wakilia kwa maumivu
makali, nilianza kuzisikia tena lakini tofauti na awali, safari hii zilikuwa
kubwa zaidi huku ikionesha kwamba zilikuwa zikitoka kwa kundi kubwa la watu.
Nilizidi
kuserereka kwa kasi kubwa kuelekea kule chini huku joto nalo likizidi
kuongezeka. Nikiwa mdogo nimewahi kusikia kwamba Jehanum kuna moto mkali
unaowaka muda wote, ambao ni maalum kwa ajili ya kuwateketeza watu wanaofanya
dhambi duniani.
Nilianza
kuhisi kwamba huenda kule nilikokuwa nikisererekea ni kwenye moto wa Jehanum na
zile sauti za watu waliokuwa wakilia kwa kusaga meno walikuwa ni watu wenye
dhambi, nikajikuta nikitetemeka kuliko kawaida.
Mpaka
muda huo nilikuwa nimeshindwa kabisa kujizuia nisiendelee kuporomokea kule
chini, kwa mbali nikaanza kuliona shimo kubwa ambalo ukubwa wake hata sijui
nifananishe na nini lakini kwa kifupi lilikuwa kubwa mno, lisilo na mwisho,
moto mkali ukiwa unawaka ndani yake. Kibaya zaidi, na mimi nilikuwa nikiendelea
kuporomoka kuelekea ndani ya shimo hilo, nikajua huo ndiyo mwisho wangu.
Je,
nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment