ILIPOISHIA:
Alikuwa ni msichana mzuri sana, upande
wa nyuma alikuwa amejazia huku kiuno chake kikiwa kimegawanyika, kama nyigu
ambao kule kijijini tulikuwa tukiwaogopa kutokana na sumu yao wanapokung’ata.
Suruali ya jeans aliyovaa, ililifanya
umbo lake lijichonge vizuri, ghafla akageuka, akanibamba nikiwa namtazama kwa
nyuma, nikazidi kujisikia aibu.
SASA ENDELEA...
“Mbona unaniangalia hivyo?”
“Mimi?” Nilijifanya kuvunga,
akanisogelea na kunipiga kakibao kepesi begani huku tabasamu pana likiwa
limechanua kwenye kwenye uso wake. Na mimi nikawa nacheka huku aibu zikiwa
zimenijaa.”
“Dar es Salaam unaishi sehemu gani?”
aliniuliza swali ambalo lilikuwa gumu sana kulijibu kwani ukweli ni kwamba sikuwa
naijua Dar wala sikuwahi kufika kabla. Nikawa nababaika mwenyewe, akajiongeza
na kuniuliza:
“Kwani hii ndiyo mara yako ya kwanza
kufika Dar?”
“Ndiyo,” nilijibu harakaharaka kwa
sababu alikuwa amenipunguzia sana kazi ya kumjibu. Akaniambia kwamba yeye
anaishi na wazazi wake Kijitonyama. Akaniambia kwamba alikuwa amemaliza chuo
akisomea uhasibu na alikuwa anatoka Mbeya kuwasalimu bibi na babu yake wa
upande wa mama.
“Wanaishi Mbeya sehemu gani?”
nilimuuliza, akaniambia wanaishi Katumba, njia panda ya kwenda Mwakaleli.
Maeneo hayo sikuwa nimewahi kufika zaidi ya kusikia tu kwa watu, nikawa natingisha kichwa kumkubalia.
Akaendelea kunieleza kwamba mama yake alikuwa Mnyakyusa lakini baba yake
alikuwa ni mtu kutoka Mkoa wa Pwani ingawa hakunieleza ni kabila gani.
Hatimaye dakika kumi ziliisha, dereva
akaanza kupiga honi akitupa ishara kwamba muda wa kuingia kwenye basi umefika.
Kwa hizo dakika chache nilizokaa na msichana huyo, niligundua kwamba alikuwa
mcheshi, mchangamfu na asiye na maringo kama walivyo wasichana wengi warembo
kama yeye.
“Lakini hujaniambia unaitwa nani.”
“Unataka kujua jina langu?”
“Ndiyo.”
“Sitaki,” alisema huku akinipiga tena
begani, akaanza kukimbia kuelekea kwenye basi. Sikuelewa kitendo hicho kilikuwa
na maana gani, wakati anakimbia nilishuhudua kitu kingine ambacho kiliusisimua
sana moyo wangu, mpaka nikawa najiuliza zile hisia nilizokuwa nazisikia kwa
wakati huo zilikuwa na maana gani?
Kwa kifupi nilijisikia raha sana
kufahamiana na msichana huyo. Niliendelea kumtazama akikimbia mpaka alipofika
kwenye ngazi za kupanga kwenye basi, akageuka na kunitazama kisha akapanda
ngazi. Na mimi nilitembea harakaharaka huku nikiendelea kuchekacheka mwenyewe,
mkononi nikiwa na kopo la soda ambayo nilikua nimeinywa nusu.
Nilipopanda na kuingia ndani ya gari,
ndugu zangu wote walishangaa kuniona nikiwa na soda ya kopo, tena nikinywa kwa
mrija.
Niliwaona wote walivyomeza mate, wakawa
wanaulizana nimeipata wapi soda hiyo? Sikuwajali kwa sababu bado nilikuwa na
hasira nao, nikakaa kwenye siti yangu, nikageuka na kumtazama yule msichana
ambaye mpaka muda huo hakuwa amenitajia jina lake, nikashtuka tena kugundua
kwamba kumbe alikuwa ametulia akinitazama kila nilichokuwa nakifanya.
Macho yangu na yake yalipogongana,
aliachia tabasamu hafifu halafu eti na yeye akakwepesha macho yake kwa aibu,
yaani mwanzo mimi ndiyo nilikuwa nakwepesha macho yangu lakini ghafla na yeye
alianza kukwepesha macho yake kwa aibu. Dereva aliondoa gari na safari
ikaendelea.
Safari hii umakini ulikuwa ukinipungua
sana kichwani mwangu kwani mara kwa mara tulikuwa tukitazamana na yule msichana
na kuishia kuchekacheka tu. Nashukuru hakuna jambo lolote baya lililotokea
mpaka tulipoanza kuingia mjini.
Tulipofika Kibaha, gari lilisimama na
yule abiria aliyekuwa amekaa pembeni yangu, alisimama na kushuka, harakaharaka
nikamuona yule msichana akikusanya kila kitu chake na kuja kukaa pembeni yangu.
Aliponisogelea tu, nilianza tena kusikia harufu ya manukato aliyojipulizia,
ambayo kiukweli yalinivutia sana.
Akakaa pembeni yangu na kuniegamia kimtindo
kabla ya kujiweka vizuri kwenye siti yake.
“Yule niliyekaa naye hata stori hana,
muda wote analala tu bora nikae na wewe,” alisema huku akinipigapiga begani,
nikawa natabasamu tu kwani kiukweli hata mimi nilikuwa napenda kukaa naye siti
moja.
“Ulisema unataka kujua jina langu?”
alianzisha mazungumzo, niikamjibu kwa kutingisha kichwa, akaniambia ananipa
mtihani nitafute mwenyewe jina lake. Kiufupi ni kwamba, kwa muda mfupi tu
niliokaa naye, alionesha kupenda sana urafiki wetu uendelee, jambo ambalo hata
mimi nilikuwa nalipenda ingawa mara kwa mara nilikuwa najishtukia.
Hata nilipokuwa nacheka, sikuwa napenda
ayaone meno yangu kwani ya kwake yalikuwa meupe sana na masafi lakini kwangu
mimi, hata sikuwa nakumbuka mara ya mwisho kupiga mswaki ni lini, si unajua
tena maisha ya kijijini.
“Una simu?” aliniuliza swali ambalo
lilinifanya nijisikie tena aibu. Sikuwa na simu, sikuwahi kumiliki wala sikuwa
najua namna ya kuitumia, nikawa natingisha kichwa kukataa, akaniambia alikuwa
na simu mbili lakini hiyo nyingine hakuwa akiitumia kwa sababu ilikuwa ya
kizamani.
“Basi nipe mimi,” nilisema kwa utani
kwani nilijua ni jambo ambalo haliwezekani, akacheka na kufungua kibegi chake
kidogo, akatoa simu ndogo aina ya Nokia ya tochi na kunipa.
“Chukua utakuwa unatumia,” alisema.
Nikapigwa na butwaa nikiwa ni kama siamini. Kuna wakati nilihisi kwamba pengine
alikuwa akinitania lakini mwenyewe alisisitiza kwamba ni kweli amenipa. Muda huo, tayari gari lilikuwa
limeshawasili Ubungo, sikuwa napajua zaidi ya kusikia tu watu wakisema hapo
ndiyo ubungo.
Tayari giza lilishaanza kuingia, taa
nyingi zilizokuwa zinawaka kila upande zikanifanya nijihisi kama nilikuwa
kwenye ndoto.
Waliosema mjini kuzuri hawakukosea, Dar
ilikuwa na tofauti kubwa sana na kule kijijini nilikozaliwa na kukulia, kila
kitu kilikuwa kigeni kwangu. Wakati nikiendelea kushangaashangaa, nilisikia
mama akiniambia kwamba natakiwa kuwa makini kuchukua mizigo iliyokuwa imewekwa
kwenye buti.
Harakaharaka nikateremka na abiria
wengine, hata sikukumbuka nilipotezana saa ngapi na yule dada, ushamba wa mjini
ulinipa mchecheto mkubwa ndani ya moyo wangu, nikaenda mpaka kwenye buti nikiwa
na wale ndugu zangu wengine ambao nao walikuwa wakishangaashangaa, tukafanikiwa
kushusha mizigo yetu yote na kuiweka pembeni.
“Twendeni nilisikia sauti ya baba
akizungumza, kugeuka pembeni, sote tulipigwa na butwaa kumuona baba akiwa anafungua
milango ya teksi. Hakuna aliyejua baba alifika saa ngapi Dar es Salaam kwa sababu
kama aliweza mpaka kuzungumza na dereva wa teksi na kukaa pale wakitusubiri,
maana yake ni kwamba aliwahi sana kufika.
“Unajua wewe huna akili kabisa,” baba
alianza kunifokea baada ya kumaliza kupakiza mizigo kwenye teksi, nikawa
nashangaa kwa nini baba ananiambia maneno hayo.
“Yule uliyekuwa umekaa naye kwenye basi
ni nani?”
“Ni rafiki yangu.”
‘Unamjua wewe? Na hicho alichokupa una
uhakika gani kama ni simu? Ujinga wako utaiponza familianzima,” alisema maneno
ambayo yalinishangaza sana.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment