Ilipoishia…
“Mungu wangu,” nilisema huku nikifikicha macho na
kutazama vizuri, kuna muda nilikuwa nahisi kwamba huenda nipo ndotoni lakini
haikuwa hivyo, sikuelewa pale kwangu nini kilisababisha watu wajae kiasi kile.
Songa nayo…
Niliendelea kujiuliza maswali mengi bila kupata
majibu. Wasiwasi wangu zaidi ulikuwa ni kuhusu Shenaiza, nilijiuliza au wale
watu niliowaona usiku uliyopita
walivamia na kubomoa geti langu hata kuingia ndani kwenda kumfanyia
unyama ndio ikawa sababu ya watu wale kujaa, lakini bado hata swali hilo
sikuweza kulipatia majibu ya moja kwa moja.
Huku moyo ukidunda niligeuza shingo yangu na kumtazama Raya,
uso wake ni kama ulikuwa unaniuliza nini kinaendelea nyumbani kwangu! Bila
kuzungumza jambo lolote niliyatoa macho yangu kwa Raya nikayarudisha kule
ulipokuwa umati wa watu waliyokuwa kwenye hamaki kubwa huku minong’ono ikiwa
imetawala.
Nilizidi kuwatazama hatimaye ukafika wakati uzalendo
ukanishinda nikaanza kusikia msukumo kutoka ndani ya mwili wangu ukinitaka
kwenda kushuhudia nini kilikuwa kimetokea nyumbani kwangu ili kama lipo la
kukabiliana nalo nifanye hivyo.
Huo ndiyo uamuzi nilioufikia baada ya kuwaza na kuwazua, kwa
ujasiri mkubwa huku miguu yangu ikitetemeka kwa woga nilianza kupiga hatua
kwenda mbele, Raya naye alianza kunifuata nyuma bila kuzungumza jambo lolote
lile mpaka tulipoufikia kabisa ule umati wa watu.
“Mungu wangu!” Nilijikuta nikitamka kwa hamaki kiasi kwamba
watu wengi wakageuza macho yao na kuanza kunitazama.
Wala sikuwa na muda wa kujali juu ya nini walikifikiria juu
yangu, macho yangu niliyatoa pima nikishangaa kilichokuwa kimetokea nyumbani
kwangu, geti langu la chuma lilikuwa limebomolewa na kutupwa pembeni jambo
lililonifanya nizidi kuingiwa na woga juu ya usalama wa Shenaiza.
Ilikuwa ngumu kuamini kila kilichokuwa kinatokea kama
kilinitokea nikiwa kwenye ulimwengu wa kawaida, muda mwingi nilikuwa nikifikiri
huenda nilikuwa naota na kuna muda ningeweza kushituka, lakini hilo lilikuwa ni
jambo lisilowezekana maana kila kilichokuwa kinatokea kilikuwa katika ulimwengu
wa kawaida kabisa.
Huku kila mtu akionekana kunishangaa nilizipiga hatua zisizo
za taratibu sana kuelekea ndani ya nyumba yangu, lakini baada ya kuvuka tu eneo
la mlango na kupiga hatua chache nilianza kuona michirizi ya damu ikitokea
ndani sebuleni.
Mapigo ya moyo yalizidi kudunda kwa kasi zaidi maana tayari
kutokana na hali halisi nilifahamu Shenaiza yalikuwa yamekwisha mkuta
yakumkuta. Nilizidi kupiga hatua za kasi kuifuata ile michirizi ya damu, wakati
huo Raya naye alikuwa nyuma yangu lakini pia baadhi ya watu waliokuwa wamefika
pale kulishuhudia tukio hilo nao walikuwa wakinifuata mpaka tukaingia ndani
kabisa.
Aisee, ilikuwa ni vigumu kuamini nilichokuwa ninakiona mbele
yangu. Mwili wa Shenaiza ulikuwa katikati ya dimbwi la damu iliyokauka huku
akiwa kimya kabisa! Kwa ujasiri ambao sikuelewa ulitokea wapi nilianza kusogea
ili kumgusa na kufahamu kama alikuwa amekufa au la, lakini nilipoendelea
kumsogelea watu waliokuwa nyuma yangu walinikataza kufanya hivyo.
“Kaka sikia, usithubutu kumgusa huyo mtu, jambo la kufanya
tutoe taarifa polisi,” ilisikika sauati ya mtu moja ikizungumza. Niligeuka na
kumtazama.
“Kweli kabisa, yanapotokea mauaji kama hukuwepo eneo la
tukio hata kama mtu anakuhusu hutakiwi kumgusa.” Mtu mwingine aliongeza.
Nilibaki nimesimama huku nikihisi miguu yangu ikiishiwa
nguvu bila kufahamu nifanye nini, Raya naye alinisogelea na kunitaka niwe imara
juu ya kile kilichotokea. Akanisihi kuwasikiliza watu hao nini walikuwa
wanasema na zaidi kujikaza kwa sababu mimi ni mwanaume na nilikuwa na kila
sababu ya kuwa imara.
Sikuwa mbishi na kama walivyoshauri wale watu ndivyo
ilivyofanyika, wao wenyewe waliamua
kusaidia kutoa taarifa polisi na baada ya robo saa gari la polisi lilifika
nyumbani kwangu pale, bila kupoteza muda askari waliovalia mipira mikononi
waliingia mle ndani tulimokuwa, wakauliza nani mwenyeji, nikajitambulisha,
wakanitaka kutoa maelezo mafupi juu ya kilichotokea.
Ukweli ni kwamba sikufahamu niseme nini. Kuhusu Shenaiza
sikuwa nikimfahamu kabisa tofauti na kuwasiliana naye ndani ya siku chache
kwenye simu, jambo lililonifanya hata kubabaika kwenye maelezo, wale askari
wakaniambia nilitakiwa kuambatana nao polisi kwa ajili ya kutoa maelezo.
Hata hivyo jambo ambalo lilinishangaza mno baada ya wale
askari kumgeuza Shenaiza waligundua kuwa hakuwa amekufa kama ambavyo sisi
tulikuwa tukifikia. Moyo wake ulisikika ukidunda kwa mbali sana jambo ambalo
kwa upande fulani nilinifanya kufurahi moyoni.
Walimbeba msichana huyo ambaye alikuwa amelowana chapachapa
kwa damu, wakampeleka mpaka kwenye gari walilokuja nalo mahali pale, wakanitaka
nami kupanda na kuambatana nao, Raya alipotaka naye kupanda ndani ya gari hilo
walimkataza, ikabidi mimi nimwambia achukue usafiri mwingine na kulifuata gari
lile la polisi ili aweze kufahamu ninapelekwa kwenye kitua gani jambo ambalo
alitii.
Safari haikuwa ndefu sana na wala haikuchukua muda mrefu
tayari tulikuwa tumekwishafika katika Kituo cha Polisi Osyterbay, bila kupoteza
muda baada ya kuchukua kibali cha matibabu (PF3), gari lile la polisi liliondoka
mahali pale na kuelekea hosipitali ambayo sikuifahamu kwa wakati huo, mimi
ikabidi nibaki kwa ajili ya mahojiano.
Ukweli ni kwamba katika wakati wote huo nilikuwa kwenye hali
mbaya sana. Nafsi yangu ilikuwa inajutia mno juu ya kumkubalia Shenaiza mawazo
yake ya kumtorosha hospitali na kwenda naye nyumbani kwangu. Huo niliuona
uamuzi wa kipuuzi usiyokuwa na mfano wake maana bila kufanya kwangu hivyo
huenda nisingeingia kwenye matatizo hayo yote.
Hata hivyo sikuwa na namna zaidi ya kukubaliana na hali halisi
iliyokuwa inaendelea, askari polisi wale waliniingiza katika chumba cha
mahojiano na kuanza kunihoji juu ya kilichotokea mpaka Shenaiza akafikia katika
hali kama ile aliyokuwa nayo, sikupenda kuficha juu ya ukweli niliokuwa
ninaufahamu, zaidi niliwaeleza kuwa hata usiku uliyopita nilitoa taarifa katika
Kituo cha Polisi Kijitonyama maarufu kwa jina la Mabatini lakini sikuweza
kupata msaada maana askari wote walikuwa kwenye doria.
Polisi wale walionyesha kushangazwa na jambo hilo, Mabatini
kilikuwa kituo kikubwa ambacho ilikuwa si rahisi askari kukauka kabisa,
kulionekana kuna uzembe fulani ulikuwa umefanyika, lakini hata hivyo maelezo
yangu juu ya tukio na juu ya kumfahamu Shenaiza yalionekana kutowaridhisha wale
askari polisi jambo lililofanya waniweke nyuma ya nondo.
Wakati hayo yote yanaendelea Raya alikuwa kituoni hapo na
aliweza kupata taarifa za kila kitu kilichotokea, alijaribu kuwashawishi askari
ili aweze kutoa dhamana lakini hawakumuelewa, walimwambia ilikuwa ni lazima
nikae mahabusu pale wakati upelelezi wa tukio hilo ukiendelea.
Raya hakuwa na namna aliamua kuondoka kituoni kwenda
kuwataarifu jamaa zangu wengine juu ya kilichokuwa kimetokea. Mimi nikiwa
mahabusu hakuna kilichoendelea ndani ya akili yangu zaidi ya majuto, nilifahamu
kabisa niliingia katika msala ambao sikuwa kabisa na hatia nao.
Saa zilikatika nikiwa bado nyuma ya nondo ambapo baadaye
kama baada ya kupita saa tatu hivi au nne nilishangaa askari polisi akija
kuniita, ambapo akanipeleka tena kwenye chumba cha mahojiano. Wakati huo
nilikutana na sura mpya ambapo baada ya salamu askari huyo mwenye sura ya mkazo
alianza kunihoji maswali.
Baada ya kumjibu jambo lililonishitua zaidi ni pale
aliponiambia kuwa ilibainika Shenazia alikuwa ni mgonjwa aliyelazwa katika
Hospitali ya Amana siku iliyopita na kutoroshwa, hoja ya msingi ilikuwa mimi
nilimtoa wapi na utetezi wangu ni upi juu ya kuhusika kwenye tukio lililompata!
Je, nini kitaendelea? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment