ILIPOISHIA:
Nakumbuka neno la mwisho nililofanikiwa
kulisema, ingawa ilikuwa ni kwa taabu kubwa kutokana na midomo yangu kuwa
mizito, ilikuwa ni: Mungu nisaidie! Nikafumba macho na giza totoro likatawala
kila sehemu, sikuelewa tena kilichoendelea baada ya hapo!
SASA ENDELEA...
Katika
hali ambayo sikuitegemea na ambayo mpaka leo huwa siwezi kuifafanua, muda mfupi
baadaye nilijikuta nikizinduka lakini nikiwa kwenye hali ya tofauti kabisa.
Nilizinduka nikiwa palepale nilipokuwa nimelala awali lakini katika hali ya
ajabu, nilikuwa mwepesi sana.
Nikajikuta
nikianza kupaa taratibu kuelekea juu. Nikiwa juu kidogo, niligeuka na kutazama
pale nilipokuwa nimeangukia, nikashangaa kuona bado mwili wangu ulikuwa umelala
palepale, damu nyingi zikiendelea kutoka kwenye jeraha la kifuani, tena safari
hii zikitoka kwa mabongemabonge.
“Mungu
wangu! Hiki ni kitu gani tena?” nilijikuta nikisema kwa sauti ya chini,
ungeweza kudhani nilikuwa kwenye ndoto lakini haikuwa hivyo. Nilijiuliza kama
mwili wangu bado ulikuwa pale chini, mimi niliyekuwa napaa nilikuwa ni nani?
Sikupata majibu.
Niliendelea
kupaa kuelekea juu mpaka nikafikia umbali wa mita kadhaa, ulioniwezesha kuona
vizuri kila kitu kilichokuwa kinaendelea eneo la tukio. Niliwaona watu wakizidi
kumiminika kwa wingi eneo la tukio, wengine wakishika vichwa vyao baada ya
kuuona mwili wangu ukiwa kwenye hali ile.
Hali
hiyo ya ajabu iliendelea kunitokea, nakumbuka niliendelea kushuhudia kila kitu
kilichoendelea, jinsi mwili wangu ulivyochukuliwa kutoka eneo la tukio na
kukimbizwa mpaka hospitali ambako nako niliona madaktari walivyokuwa wakichakarika
kuokoa maisha yangu.
Niendelee
kusisitiza kwamba wakati haya yote yakitokea, katika ulimwengu wa kawaida
sikuwa na fahamu hata kidogo, nilikuwa nimefumba macho na kulala pale kitandani
kama maiti, nikiwa nimeunganishwa na mashine ya kunisaidia kupumua lakini
katika ulimwengu mwingine ambao hata sijui niuiteje, nilikuwa nimesimama kwenye
pembe moja ya ile wodi, nikishuhudia kila kilichokuwa kinaendelea.
Kazi
ya kuokoa maisha yangu iliendelea, madaktari na manesi wakawa wanapishana huku
na kule, huyu kabeba dawa, huyu kabeba chupa ya damu, huyu mikasi na sindano,
ilimradi kila mmoja alikuwa bize.
Nilijisikia
ahueni kubwa ndani ya moyo wangu kuona watu ambao pengine hata hawakuwa wakinijua,
wakipigana kuokoa maisha yangu. Niliendelea kuwatazama wanavyohangaika, kuna
wakati machozi ya uchungu yalikuwa yakinitoka kwa sababu ya kilichotokea,
nikawa naendelea kujiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu.
Narudia
tena, mpaka leo huwa napata sana ugumu kuelezea hasa kile kilichotokea ni nini,
yaani mimi niliyekuwa nashuhudia hayo yote nilikuwa nani na ule mwili ambao
watu wote walikuwa wakiamini kwamba ni mimi, ulikuwa kitu gani?
Jambo
pekee ninaloweza kusema, ni kwamba kila jambo linatokea maishani linatokea kwa
sababu maalum na kuna mambo mengi sana yanayoendelea kutokea hapa duniani
ambayo mimi na wewe hatuyajui. Huenda mimi nilitokewa na haya ili leo nije
kutoa ushuhuda kwa watu ambao huwa ni wagumu kuamini kwamba kuna maisha mengine
zaidi ya haya tunayoyajua.
Maisha
haya ya kawaida ya binadamu tulio wengi, yamejawa na mambo mengi sana ambayo
kwa akili za kawaida huwezi kuyaelewa na nilichojifunza ni kwamba mambo mengi
humu duniani, hayapo kama ambavyo tumezoea kufikiria yapo. Kwamba hakuna jambo
ambalo linatokea kwa bahati mbaya! Hata hizi ajali ambazo wengi huwa tunaona kwamba
zimetokea kwa bahati mbaya, huwa hazitokei tu!
Waingereza
wana msemo mmoja maarufu kwamba ‘everything is predestined’ wakimaanisha kila
kinachotokea maishani tayari kilishapangwa! Nasisitiza hakuna kitu kinachotokea
kwa bahati mbaya.
Yawezekana
hata wewe usinielewe kwa sasa lakini napenda kukuhakikishia kwamba mambo mengi
sana ambayo tunayajua na kuyaamini, hayapo vile ambavyo kwa miaka mingi
tumekuwa tukiyaamini. Nikisema dunia nzima imejaa vitu vingi ambavyo havipo
kama tulivyozoea kuviona, huenda ukawa hunielewi kwa urahisi lakini mimi
nasimulia mambo ambayo yamenitokea mwenyewe.
Ukitaka
kuamini, kuanzia sasa, anza kutazama kila kitu kwa jicho la tatu! Hata lile
jambo ambalo ulikuwa unaamini kwamba unalijua au ulikuwa unaamini kwamba ni
ukweli, hebu anza kulitazama kwa namna nyingine na jiulize maswali katika kila
jambo, kuanzia kuhusu wewe mwenyewe, kwamba wewe ni nani, kwa nini upo duniani,
umetoka wapi na unaelekea wapi na mambo yote yanayokuzunguka, utaanza kuelewa
ninachokimaanisha.
Basi
nikiwa nimesimama palepale kwenye pembe moja ya ile wodi, nikishuhudia kila
kilichokuwa kinaendelea kwenye mwili wangu uliokuwa umelazwa pale kitandani
ukiwa hauna fahamu hata kidogo, nilishtuka baada ya kuhisi upepo mkali ukianza
kuvuma mle ndani ya wodi.
Sikuelewa
ule upepo umetokea wapi kwa sababu milango na madirisha yote yalikuwa
yamefungwa, baadhi ya vifaa vilivyokuwa mezani, vilianza kudodondoka, vikiwemo
vichupa vya dawa na vifaa vingine vya kidaktari, manesi wakawa na kazi ya
kuviokota na kuviweka sawa.
Ghafla
nilihisi kama nashikwa na mtu mwenye nguvu sana, nikanyanyuliwa kutoka pale
nilipokuwepo, kufumba na kufumbua, nikajikuta nipo kwenye mazingira mengine
tofauti kabisa, mahali ambapo hata sijui nipaelezeeje. Kulikuwa na giza totoro
kila upande, kiasi kwamba hata ukisogeza kidole jirani kabisa na jicho lako,
usingeweza kuona kitu chochote.
Yule
mtu ambaye alikuwa amenishika na kunitoa kule wodini, ambaye nasema ni mtu kwa
sababu mikono yake ilikuwa ya kibinadamu kwa sababu na mimi nilimshika nikitaka
kumjua ni nani lakini nikashindwa hata kumuona kwa sababu ya giza, aliniachia,
nikajikuta nimesimama sehemu ambayo sikujua mbele ni wapi wala nyuma ni wapi,
giza lilikuwa nene kikwelikweli.
“Jamal!”
nilisikia sauti nzito, iliyokuwa ikisikika kama mwangwi, ikiliita jina langu.
Umewahi kuingia kwenye sehemu ambayo ina uwazi mkubwa halafu ukatamka neno
lolote na kusikia likijirudiarudia? Basi hivyo ndivyo ilivyokuwa kwangu, ile sauti
nzito ilijirudiarudia mara kadhaa.
“Mungu
wangu, hiki ni nini tena?” nilijisemea moyoni kwa hofu kubwa lakini tofauti na
nilivyotegemea, wakati mimi nikiamini kwamba najisemea moyoni, niliisikia sauti
yangu ikisikika utafikiri niliyatamka maneno yale mdomoni wakati ukweli ni
kwamba niliyasemea moyoni.
Nikajikuta
nikitetemeka kuliko kawaida, hofu kubwa ikiwa imeukumba moyo wangu ambao sasa
ulikuwa ukidunda kwa nguvu kiasi cha mapigo yake kusikika vizuri kabisa hata
kwa mtu aliyekuwa pembeni yangu.
“Jamal!”
ile sauti ilisikika tena lakini tofauti na mwanzo, safari hii ilisikika
ikionesha aliyeitoa alikuwa amesogea mbali kabisa na mimi, nikawa natamani
kuitikia lakini nilishindwa kutokana na hofu kubwa iliyokuwa imenizingira.
“Jamal!”
ile sauti ilisikika tena kwa mara ya tatu, safari hii ikionesha kwamba
aliyekuwa akiniita alikuwa mbali zaidi. Katika hali ambayo siwezi kuielezea,
nilijikuta nikianza kutembea kuelekea kule sauti ile ilikokuwa inazamia. Kwa
mbali nikaanza kusikia sauti kama za watu wanaougulia maumivu makali, sauti za
watoto wachanga waliokuwa wakilia na sauti za kutisha za wanyama ambazo
nyingine hata sijawahi kuzisikia tangu nizaliwe.
Kuna
wakati hofu ilinizidi na kutaka nigeuze nilikotoka lakini kitu ndani ya moyo
wangu kikaniambia nizidi kusonga mbele. Kadiri nilivyokuwa nazidi kusonga mbele
ndivyo zile sauti zilivyokuwa zinazidi kuongezeka, nikazidi kutetemeka kwa hofu
huku nikiwa sijui nini itakuwa hatma yangu.
Je, nini kitafuatia?
Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment