ILIPOISHIA:
“Tuondoke!” nilisema huku nikiinuka pale nilipokuwa
nimekaa kwani tayari kengele ya hatari ililia ndani ya kichwa changu, Raya naye
akainuka, tukaanza kuelekea kwenye lango la kutokea nje ya hospitali hiyo
lakini cha ajabu zaidi, tukiwa getini tunataka kutoka, nililiona lile gari nalo
likija kule tulipokuwepo.
SASA ENDELEA…
“Bodaboda! Bodaboda!” niliita kwa sauti huku
tukitembea kwa haraka kuelekea nje ya hospitali, lile gari nalo likizidi kuja
kwa kasi kule tulipokuwepo. Ilibidi nimshike mkono Raya kwani kwa jinsi
alivyokuwa ‘mayai’ ningeweza kumuacha pale na kumsababishia matatizo.
Kwa bahati nzuri, dereva mmoja wa bodaboda alituona
na harakaharaka akawasha pikipiki yake na kutufuata, mwenyewe akijiona
amewazidi wenzake ujanja kwa kuwahi abiria.
“Tupeleke Kijitonyama,” nilisema huku nikimsaidia Raya
kupanda, na mimi nikapanda lakini dereva wa bodaboda hakutaka kuondoka mpaka
tukubaliane kwanza.
“Twende bwana nitakupa kiwango chochote unachotaka.”
“Lakini siku hizi haturuhusiwi kupakiza mishikaki
nitakamatwa.”
“Twendeee,” nilisema kwa sauti ya juu, yule dereva
akaondoa pikipiki, kabla hajafika popote wote tulishtukia bodaboda
ikikoswakoswa kugongwa kwa nyuma na lile gari lililokuwa linatufuata kwa kasi.
Dereva wa bodaboda alitaka kusimama pembeni kulipisha gari hilo lakini
nilimsisitiza kuongeza mwendo na kuhakikisha analipoteza kabisa lile gari.
Akiwa haelewi kinachoendelea, hofu kubwa ikiwa
imemkumba moyoni, yule dereva bodaboda alikata kona ya ghafla na kuingia kwenye
uchochoro mita chache mbele, hali iliyosababisha lile gari ambalo lilikuwa
likijiandaa kutugonga kwa nyuma lipitilize kwa kasi, likaenda kusimama mita
chache mbele.
Raya alikuwa akipiga kelele kwa nguvu huku akilitaja
jina la Mungu wake, hakuelewa kilichotokea kiasi cha kujikuta katikati ya mtego
wa kifo kama ule, nikawa nambembeleza na kumtaka atulie.
Lile gari lilirudi kinyumenyume na kujaribu kupita
kwenye ule uchochoro kuifuata ile bodaboda lakini sehemu ilikuwa ndogo, likashindwa.
Nikawa namsisitiza dereva kuzidi kuongeza kasi, tukatokeza mtaa wa pili na
kuingia kwenye barabara ya lami, safari ikazidi kupamba moto.
“Usipite barabara kubwa, wanaweza kuwa
wanatufuatilia, ingia kushoto hapo mbele,” nilimwambia, wazo ambalo dereva huyo
alilifuata, tukawa tunazidi kukata mitaa tukitumia njia za uchochoroni.
“Nataka twende nyumbani kwetu Jamal,” alisema Raya
huku akiwa bado na hofu kubwa moyoni.
“Ok sawa,” nilimjibu kwa kifupi kwa sababu kiukweli sikuwa
nataka kupata muda wa kukaa peke yangu na Raya kama ilivyotokea usiku uliopita
lakini kwa jinsi hali ilivyokuwa sikuwa na ujanja.
Dakika kadhaa baadaye, tayari tulikuwa tumefika
Kijitonyama lakini kwa kukwepa kuonekana tumeelekea wapi, tuliamua kushuka
kwenye bodaboda, tukakubaliana bei na dereva huyo ambaye licha ya kulipwa fedha
zake, alionesha kuwa na shauku kubwa ya kutaka kujua kilichokuwa kinaendelea.
Hata hivyo, sikuwa tayari kumueleza chochote,
akaondoka kwa shingo upande huku akigeukageuka nyuma, kuna wakati alihisi
huenda alikuwa ametubeba majambazi lakini alikosa ushahidi wa hilo.
Yule dereva bodaboda alipoondoka tu, mimi na Raya tulipanda
kwenye Bajaj ambayo ilitupeleka mpaka nyumbani kwa akina Raya, tukawa na
uhakika mkubwa kwamba hata kama wale watu wataamua kutufuatilia, haitakuwa
rahisi kutupata.
“Naomba ukaoge kwanza wakati mimi nafanya utaratibu
wa chakula,” alisema Raya baada ya kuhakikisha milango yote ya nyumba hiyo
imefungwa kwa ndani, kuanzia geti kubwa la nje mpaka milango ya ndani.
Kwa kuwa wazazi wa Raya hawakuwa wamerejea safarini
kama mwenyewe alivyonieleza, kwa mara nyingine tulijikuta tukiwa peke yetu
ndani ya nyumba.
Wakati nikiendelea kujiuliza kuhusu mfululizo wa
matukio yaliyokuwa yakiendelea kuniandama kiasi cha kunifanya nikose uhakika
juu ya maisha yangu, Raya alikuwa akifikiria jambo jingine tofauti kabisa.
Niliingia kwenye chumba cha wageni ambacho ndicho nilicholala
usiku uliopita na kubadilisha nguo, nikajifunga taulo na kuelekea bafuni,
mawazo mengi yakiendelea kukisumbua kichwa changu.
Bado nilishindwa kupata majibu kuhusu Shenaiza,
sikuwa nikielewa kama Shenaiza alikuwa ni mtu wa namna gani, akina nani
walikuwa wakiyawinda maisha yake na alikuwa na uhusiano gani nao. Kila swali nililojiuliza
halikuwa na majibu.
“Shenaiza Petras Loris,” nililikumbuka jina kamili
la msichana huyo alilolitaja wakati akihojiwa na yule mpelelezi.
“Kabila langu ni Aethikes… mimi siyo Mtanzania,
natokea Greece (Ugiriki), asili yetu ni Attica, baba yangu amezaliwa na kukulia
kwenye Jiji la Athens lakini mama yangu ni mpare wa Mtae, Lushoto mkoani Tanga,”
maneno ya Shenaiza wakati akijieleza yalikuwa yakijirudiarudia ndani ya kichwa change
kama mkanda wa video.
“Lazima niujue ukweli! Lazima!” nilisema wakati nikifungulia
bomba la maji ya mvua, maji ya baridi yakawa yananimwagikia na kuufanya mwili
wangu uliokuwa umechoka sana upate nguvu mpya.
Japokuwa msichana huyo hakuwa tayari kunieleza
ukweli zaidi ya kuishia kuniambia nisubiri ataniambia, niliamua kuutafuta
ukweli kwa njia nyingine ingawa bado sikuwa naijua ni njia gani na nitafanyaje
kumfahamu Shenaiza.
Nilikaa muda mrefu bafuni, nikiwa naendelea
kujimwagia maji huku akili yangu ikienda mbio kuliko kawaida. Nilikuja kushtuka
baada ya kusikia Raya akiniita na kuugonga mlango wa bafuni.
“Mbona hutoki bafuni mpenzi wangu,” alihoji Raya kwa
sauti ya kubembeleza, harakaharaka nikafunga bomba na kuchukua taulo, nikajifuta
na kufungua mlango, macho yangu yakagongana na Raya ambaye naye alikuwa
amejifunga khanga moja tu.
“Na mimi nataka kuoga, nisubiri tuondoke wote,”
alisema msichana huyo huku akinitazama kwa macho yaliyojaa ujumbe mzito,
taratibu akanirudisha bafuni, nilishindwa kumzuia, naye akaingia na kufunga
mlango kwa ndani.
“Nataka leo na mimi nideke, naomba uniogeshe,”
alisema Raya na kunifanya nijikute kwenye wakati mgumu kwa mara nyingine, nikiwa
bado sijui nijibu nini, msichana huyo alifungua khanga na kuitundika nyuma ya
mlango, akabaki kama alivyoletwa duniani, vifuu viwili vikiwa vimechomoza
kwenye kifua chake na kunifanya nisisimke mwili mzima.
Akalishika taulo nililokuwa nimejifunga na kulivuta
kisha akalitundika pale alipoweka khanga yake, tukabaki saresare maua! Akanisogelea
jirani kabisa kiasi cha kila mmoja kuanza kuzisikia pumzi za mwenzake, tukawa tunatazamana
machoni huku ‘Jamal’ wangu naye akianza kufura kwa hasira.
***
Baada ya kumaliza kumhoji Shenaiza, yule askari
mpelelezi, alitoka hadi nje alikowaacha wenzake, akawavuta pembeni na kuanza
kuwaeleza alichoelezwa na msichana huyo, kila mmoja akawa ametulia
akimsikiliza. Maelezo aliyoendelea kuyatoa, yalimshangaza kila mmoja, wakawa
wanatazamana wakiwa ni kama hawaamini walichokuwa wakiendelea kukisikia kutoka
kwa mwenzao.
“Kwani amesema asili yake ni wapi?”
“Ni Athens, Greece! Na kubwa zaidi, amesema jina
lake kamili ni Shenaiza Petras Loris.”
“Unataka kusema kwamba ni mtoto wa Petras Loris huyu
tunayemjua?”
“Sijamuuliza lakini kwa maelezo yake, upo uwezekano
mkubwa akawa ni mwanaye au wana undugu fulani.”
“Aisee! Mbona hii inaonekana kuwa ngoma nzito?”
“Ni ngoma nzito kwelikweli, halafu kuna huyu kijana
ameingizwa kwenye mtego bila mwenyewe kujua chochote, mpaka namuonea huruma.”
Je,
nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment