ILIPOISHIA:
Muda huo kwa makadirio ilikuwa ni kama
saa nane za usiku maana kuna sehemu nilipita nikasikia redio kwa mbali
ikitangaza kwamba ni saa nane kasoro za usiku.
“Mbona umeshtuka Togo!” alisema huku
akinisogelea. Siwezi kuficha, mshtuko nilioupata nusura nidondoke na kuzimia.
SASA ENDELEA...
Alikuwa ni yule msichana ambaye mchana
wa siku iliyopita alinifia gesti tukiwa kwenye mechi ya kirafiki na
kunisababishia matatizo makubwa mpaka nikapelekwa mahabusu nikikabiliwa na kesi
kubwa ya mauaji.
Nilitaka kukimbia nikahisi mwili wangu
ukiishiwa nguvu, nilitaka kupiga kelele lakini sauti ikawa haitoki, nikabaki
nimesimama palepale nikitetemeka kama mbwa mbele ya chatu, akawa ananishangaa
usoni kama anayejiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu.
“Wewe si ulikufa wewe?” nilisema huku
safari hii miguu yangu ikiwa imeanza kupata nguvu, nikawa narudi nyuma
nikiangalia upenyo wa kukimbia. Ni kama alishagundua ninachotaka kukifanya,
akacheka na kunisihi nisikimbie bali kuna jambo la muhimu anataka kuniambia.
Maneno yake yaliingilia sikio moja na
kutokea la pili, akili yangu ilinifanya niamini kwamba hakuwa yeye bali mzimu
wake, akawa anazidi kunisogelea mwilini.
“Najua unafikiri labda mimi ni mzimu,
siyo, nipo hai wala sijafa na leo nitakutajia mpaka jina langu,” aliniambia
huku akizidi kunisogelea. Mazungumzo yake hayakuonesha kama alikuwa mzimu au
alikuwa na nia mbaya na mimi lakini bado niliendelea kurudi nyuma, naye akawa
anazidi kunifuata.
“Jina langu naitwa Isrina au wengi huwa
wanapenda kuniita Isri. Nakuomba unipe japo dakika chache nikueleze
kilichotokea leo na historia fupi ya maisha yangu, pia nataka nikueleze kitu
ambacho hukijui kuhusu wewe ambacho kitakusaidia sana,” alisema kwa sauti ya
upole.
Sijui nini kilitokea lakini nilijikuta
nikishawishiwa na maneno yake matamu, nikasimama, akazidi kunisogelea mwilini
na kunikumbatia kimahaba. Kitendo hicho kilisababisha hofu yote niliyokuwanayo
iyeyuke ghafla kwa sababu nimewahi kusikia kwamba tofauti ya mtu na mzimu, ni
kwamba mzimu unakuwa na mwili ambao japo unauona, hauwezi kuushika ukashikika.
Nimewahi kusikia kuwa miili ya mizimu
inakuwa kwenye mfumo wa hewa, kwamba unamuona mtu lakini ukitaka kumkumbatia
anakuwa kama hewa, hashikiki. Ili kuwa na uhakika, na mimi nilimshika kiuno
chake, kweli kikashikika vizuri kabisa, tukawa tunatazamana usoni.
Tukiwa bado tunaendelea kutazamana,
alinibusu kwenye shavu langu la kushoto, nikajikuta mwili mzima ukisisimka na
ndani ya sekunde chache tu, ile hali iliyokuwa inanisumbua sana, ya kuwa na kiu
kubwa ya kucheza mchezo wa kikubwa ilinianza tena.
Ni kama Isri alielewa nilichokuwa
nakihitaji, alichokifanya ilikuwa ni kuendelea kunitoa hofu huku akiendelea
kunichokoza hapa na pale, hali ikazidi kuwa tete kwa upande wangu.
Usiku huo kulikua kimya kabisa, hakukuwa
na mtu yeyote aliyekuwa akuipita barabarani, kelele pekee zilizokuwa zinasikika
zilikuwa ni za mbwa waliokuwa wakibweka mitaani. Ilibidi tusogee pembeni ya
barabara, hakukuwa na muda wa kupoteza, kila mmoja alijiweka kwenye mkao wa
kula na kazi ilianza palepale.
Kwa jinsi nilivyokuwa na ‘kiu’,
nilimsambaratisha vilivyo Isri mpaka ikabidi aweke mpira kwapani. Hata hivyo,
angalau kidogo nilianza kujisikia vizuri, akili yangu sasa ikahamia kwenye
kutaka kuujua ukweli kwa sababu nilishahakikisha kwamba Isri hakuwa amekufa.
“Haya niambie kilichotokea.”
“Kwanza nashukuru,” alisema huku
akinikumbatia na kunibusu huku tabasamu pana likiwa limechanua kwenye uso wake.
“Usijali, ahsante na wewe,” nilisema,
akazidi kucheka. Alivuta pumzi ndefu na kunitazama usoni, Japokuwa ilikuwa ni
usiku, kwa msada wa mbalamwezi niliweza kumtazama vizuri jinsi alivyokuwa
ananiangalia kwa macho yaliyojaa ujumbe.
Alishusha tena pumzi ndefu kisha
akanikumbatia na kujilaza kifuani kwangu, akaniambia kama sitajali, tutafute
sehemu na kukaa kwa sababu alikuwa amechoka sana. Nilimkubalia, tukasogea
kwenye nyumba ambayo ilikuwa ikijengwa lakini bado haijakamilika, tukakaa
kwenye msingi na kuanza kuzungumza.
Aliniambia kwamba aligundua kwamba nina
kitu fulani cha kipekee siku ya kwanza tulipokutana ndani ya basi, wakati
tukisafiri kutokea Mbeya kuja Dar es Salaam. Aliniambia kwamba yeye amezaliwa
katika ukoo wa kichifu kwani babu yake mzaa baba, alikuwa ni kiongozi wa mila
wa Wanyakyusa waliokuwa wakiishi kandokando la Mlima Rungwe na alikuwa
akiheshimika sana. Aliniambia kwamba hata babu yake huyo alipofariki,
alimrithisha mikoba yake baba yake ambaye licha ya kuwa msomi, akiwa ni daktari
kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, pia alikuwa akiendelea na shughuli za
kimila na ndiyo maana yeye alikuwa na uwezo wa tofauti na watu wengine kwani
ndani kwao yeye ndiye aliyekuwa wa kwanza kuzaliwa.
Maelezo hayo bado hayakuwa yamenisaidia
kuelewa chochote, niliona kama ananizungusha tu lakini sikutaka kumkatisha,
nikatulia na kuendelea kumsikiliza.
Aliniambia kwamba kwa kuwa yeye ndiye
mtoto wa kwanza kwenye familia yao, na kawaida zile kazi za kimila huwa
zinarithishwa kwa mtoto wa kwanza, baba yake alikuwa amefanya kitu kimoja
kibaya sana kwenye maisha yake ndiyo maana siku aliponiona mimi alifurahi sana.
“Unamaanisha nini?”
“Mimi ni kaburi la wasio na hatia Togo,
nimeamua kukueleza ukweli kwa sababu wewe ndiye mwanaume pekee ambaye umeweza
kuuvuka mtego wa kifo,” aliniambia, nikawa simuelewi kabisa. Sikuelewa
anamaanisha nini anaposema yeye ni kaburi la wasio na hatia na anamaanisha nini
anaposema mimi nimeweza kuuvuka mtego wa kifo?
Nikiwa bado na shauku kubwa ya kutaka
kumsikiliza alichomaanisha, nilipoinua uso wangu na kutazama upande wa
barabarani, nilishtuka sana kuona kulikuwa na watu wengi wamekusanyika, wote
wakiwa wanatutazama.
“Mungu wangu,” nilisema kwa mshtuko
kwani ilionesha kuna jambo halikuwa sawa kwetu na ndiyo maana walikuwa
wakitutazama. Tofauti na mimi, yeye alipowatazama wala hakushtuka, akaniambia
ni haki yao kushangaa kwa sababu hatukuwa tukionekana wa kawaida.
“Unamaanisha nini?”
“Umewahi kusikia stori za majini?”
aliniuliza, nikamgeukia na kumtazama usoni kisha nikawatazama tena wale watu,
walikuwa wakizidi kuongezeka kwa wingi, safari hii baadhi yao wakawa wanatupiga
picha kwa kutumia simu zao. Niliweza kuligundua hilo kwa sababu ya mwanga wa
flash uliokuwa ukitumulika.
Nilimtaka tuondoke lakini akasema wala
nisiwe na wasiwasi, hawawezi kutufanya jambo lolote na hawana uwezo huo.
Alipoona situlii, aliniambia nimpe mkono wangu wa kushoto, nikafanya hivyo,
akashika kidole changu cha mwisho kisha akaniambia na mimi nifanye hivyohivyo,
nikamshika.
“Nahesabu mpaka tatu, nikifika tatu
fumba macho na usifumbue mpaka nitakapokwambia,” alisema, nikatii kile
alichoniambia. Alipofikisha tatu, nilifumba macho, nikashtukia ghafla tumehama
pale tulipokuwa na kwenda upande wa pili, kule barabarani ambako watu wengi
walikuwa wamesimama wakishangaa, tukajichanganya na wale watu.
“Hebu angalia wanachokishangaa,” alisema
huku akinitaka nitazame pale tulipokuwa tumekaa awali. Macho yalinitoka nikiwa
ni kama siamini.
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatatu kwenye
Gazeti la Championi Jumatatu.
No comments:
Post a Comment