ILIPOISHIA:
Dereva alizidi kuyumba huku gari likiongeza
kasi, hali iliyofanya abiria waanze kupiga kelele kwa nguvu, wengi wakilitaja
jina la Mungu.
Gari
lilizidi kuongeza kasi, likawa linashuka kwenye mteremko huo kwa kasi kubwa
huku likiendelea kuyumba huku na kule, kelele ndani ya basi zikazidi
kuongezeka.
SASA
ENDELEA...
Katika hali ambayo hata sielewi
ilikuwaje, nilijikuta nikipata nguvu na kusimama, nikawa natazama nje kwa
kupitia kioo cha dereva. Cha ajabu na cha kushtua, nilimuona baba akiwa
anapigana na mtu ambaye sikumtambua ni nani, pembeni ya barabara.
Kwa macho yangu, nikamshuhudia baba
akimpiga yule mtu kwa nguvu, akamdondosha chini na kuanza kumbamiza kwenye
lami, damu nyingi zikatapakaa eneo lote.
Kufumba na kufumbua, nilishtukia baba
akiwa ameshika usukani wa lile basi tulilokuwa tukisafiria, sikuwahi kumuona
baba hata siku moja akiendesha gari lakini eti siku hiyo ndiyo alikuwa ameshika
usukani. Sikukumbuka ameingiaje ndani ya basi, tena likiwa katika mwendo mkali
kiasi kile.
Kila kitu kilifanyika kwa kasi kama ya
radi, akamtoa dereva na kumsukumia pembeni, akaanza kubadilisha gia huku akiwa
ameung’ang’ania usukani, katika hali ambayo hakuna aliyeitegemea, gari liliacha
kuyumbayumba ingawa halikupunguza mwendo, likawa linazidi kukimbia kwa kasi
kubwa, likishuka kwenye mteremko mkali maarufu kama Mlima Nyoka.
Abiria wote walitulia, hata wale
waliokuwa wakipiga kelele, walikaa kimya, wakawa wanaendelea kumuomba Mungu
ndani ya mioyo yao, hakuna aliyeona mabadiliko yaliyofanyika upande wa dereva
zaidi ya mimi nadhani na watu wachache waliokuwa wamekaa mbele.
Nilimshuhudia baba akiendelea kupangua
gia kwa kasi, gari likaanza kupunguza mwendo na mita chache mbele, alifunga
breki, gari likaserereka na hatimaye likasimama kandokando ya barabara, watu
wote waliokuwa ndani ya basi walianza kushangilia na kumpongeza dereva huku
wakikimbilia kwenye mlango wa kutokea nje.
Harakaharaka na mimi nilielekea kule
mbele lakini lengo langu kubwa ilikuwa ni kwenda kumuuliza baba nini
kilichotokea maana sikuwa naelewa chochote.
Cha ajabu, nilipofika pale kwenye siti
ya dereva, nilimuona yule dereva ambaye ndiye aliyetoka na sisi Mbeya mjini
akiwa ameegamiza kichwa kwenye usukani, akiwa ni kama amepitiwa na usingizi.
Nilibaki nashangaa kwa sababu kitendo
cha kuinuka kutoka pale kwenye siti niliyokuwa nimekaa mpaka pale kwa dereva,
sikuwa nimetumia hata dakika moja kamili, zilikuwa ni sekunde tu lakini eti
baba hakuwepo tena na aliyekuwa amekaa pale kwenye usukani alikuwa ni dereva.
Niligeuka huku na kule kutazama kama
nitamuona baba lakini sikumuona, abiria walikuwa wakiendelea kugombea kutoka na
muda mfupi baadaye, wote walikuwa wameshateremka, kila mmoja akawa anamshukuru
Mungu wake. Yaani kama ingetokea ajali, kwa jinsi mteremko ulivyokuwa mkali,
sidhani kama kuna mtu angetoka salama ndani ya basi lile.
Ilibidi nimguse begani yule dereva
ambaye bado alikuwa amelala na kuegamia usukani ili nimuulize nini
kilichotokea. Cha ajabu, nilipomgusa, alishtuka sana, akawa ni kama
aliyezinduka kutoka kwenye usingizi mzito, akawa anageuka huku na kule.
Hakukuwa na mtu mwingine yeyote ndani ya gari, isipokuwa mimi na yeye tu.
“Nini kimetokea? Hatujapata ajali? Mungu
wangu,” alisema yule dereva huku akianza kujikagua mwili wake. Nilishangazwa
sana na hali ile, yaani kumbe na yeye hakuwa anaelewa kilichotokea kwa hiyo kama
zisingefanyika jitihada zile, ni kweli tungepata ajali mbaya sana.
“Kwani wewe unakumbuka nini?”
nilimuuliza.
“Wakati tunauanza huu mteremko wa Mlima
Nyoka, nilianza kuhisi kizunguzungu, nikajaribu kupunguza mwendo ili nisimame
lakini cha ajabu, badala ya kukanyaga breki nilikanyaga mafuta, gari likaongeza
mwendo na kizunguzungu kikazidi, sikumbuki tena kilichotokea,” alisema yule
dereva huku akiendelea kugeuka huku na kule.
“Tushuke,” nilimwambia, harakaharaka
akafungua mlango na kushuka, na mimi nikashuka. Wale abiria waliokuwa chini,
walimzunguka dereva na kuanza kumpongeza kwa kazi kubwa aliyoifanya. Ilibidi
awe anaitikia tu lakini kiukweli hakuwa anajua nini kimefanyika na imekuwaje
mpaka basi limesimama.
Akiwa anaendelea kupongezwa, tabasamu la
uongo likiwa limechanua kwenye uso wake, alishtuka baada ya kuanza kuona damu
zikimtoka puani, abiria wote nao wakashtuka. Mara ya kwanza alipojifuta,
zilikuwa ni damu kidogo lakini mara ya pili, zilikuwa nyingi, tena zikiwa na
weusi fulani hivi, kila mmoja akapatwa na hofu kubwa ndani ya moyo wake.
Kwa bahati nzuri, miongoni mwa wale
abiria alikuwepo daktari ambaye ilibidi amshike mkono na kumsogeza pembeni, akawataka
abiria wengine wasogee pembeni ili apate hewa, akamlaza chini na kuanza kumpa
huduma ya kwanza.
Nikiwa bado sielewi nini cha kufanya,
nilimuona baba akiwa ng’ambo ya pili ya barabara, akanionesha ishara kwamba
nimfuate. Nikaangalia kushoto na kulia, nilipoona hakuna gari, nilivuka
barabara na kusogea kule baba alipokuwa amesimama.
“Huku nyuma, mama na ndugu zangu wengine
walishangaa kwa nini navuka barabara, mama akaanza kuniita. Nilishangaa kwa
nini ananiita mimi tu wakati pembeni yangu alikuwepo baba, nikakosa majibu.
“Vipi, umeona kilichotokea?” baba
aliniuliza huku akinitazama usoni, nikawa namtazama huku nikiwa na maswali
mengi yasiyo na majibu.
“Baba wewe si tulikuacha stendi?
Umefikaje hapa? Halafu uliingiaje kwenye gari na kuzuia ajali isitokee? Yule
uliyekuwa unapigana na...” nilijikuta maswali mfululizo yakinitoka.
Alichokifanya baba, ilikuwa ni kuniziba mdomo kwa kutumia kiganja cha mkono
wake, ambao bado ulikuwa na damudamu.
“Nimeshakwambia, ukiwa mwanaume maana
yake unatakiwa kuwa na kifua, siyo kila unachokiona unatakiwa kukisema,
umenielewa?” alinihoji baba huku akinitazama, nikatingisha kichwa.
Akaniambia kwamba safari yetu ilikuwa
imeandamwa na mabalaa makubwa na mtu pekee ambaye angeweza kushirikiana naye
kuhakikisha tunafika salama, ni mimi. Akaingiza mkono mfukoni na kutoa
kikaratasi ambacho kilifungwa unga fulani mweusi, akaumimina kidogo mkononi na
kuniambia natakiwa kwenda kumpulizia yule dereva usoni.
Akaniambia baada ya hapo, mambo yote
yangekuwa sawa na akaniambia natakiwa kukaa siti ya nyuma ya dereva, nikiona
jambo lolote haliendi sawa, nivue viatu kisha nivivae upya kwa kuvigeuza, yaani
cha kushoto nivae kulia na cha kulia kushoto kisha nishike sehemu zangu za
siri.
“Umenielewa?”
“Ndiyo baba.”
“Mimi natangulia kusafisha njia,”
alisema kisha akaniambia nivuke barabara, nikafanya hivyo. Kwa bahati mbaya,
wakati navuka barabara, safari hii sikutazama kushoto wala kulia, nikavuka tu
kama ng’ombe. Nikiwa nimefika katikati ya barabara, nilisikia mama akipiga
kelele kwa nguvu pamoja na watu wengine, wote wakinionesha ishara kwamba
nikimbie.
Sikuelewa kwa nini wananiambia vile,
ghafla niligeuka kutazama upande wangu wa kushoto, lori kubwa la mafuta,
lilikuwa limeshanisogelea huku likiwa kwenye mwendo wa kasi kubwa, taa zote za
mbele zikiwa zimewashwa.
“Mungu wangu!” nilisema kwani nilijua
hakuna kinachoweza kuniokoa kutoka kwenye mdomo wa mauti, ilikuwa ni lazima
linisagesage palepale kama chapati.
Je,
nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment