Kwa bahati nzuri, nilipofika pale mapokezi, yule dada hakuwepo, nikatoka kimyakimya mpaka nje, nikaelekea lilipo geti kubwa huku nikijitahidi kuvaa tabasamu la uongo ili walinzi wa hoteli hiyo wasishtukie chochote.
“Aroo! We kijana... Aroo wewe,” nilisikia sauti ya mlinzi wa nje ya geti la hoteli hiyo akiniita, moyo ukalipuka paah!
SASA ENDELEA...
“Unaenda wapi?”
“Naenda dukani afande.”
“Mwenzako umemuacha wapi?”
“Yupo ndani, narudi sasa hivi, naenda kununua kinga.”
“Mbona kama una wasiwasi?” alisema yule mlinzi huku akinisogelea. Licha ya kujaribu kucheza na akili zake, ni kama alishashtukia jambo kwa jinsi nilivyokuwa na hofu. Mtu kukufia chumbani, usifanye mchezo.
Hata kama ulikuwa jasiri vipi, lazima uchanganyikiwe. Hicho ndicho kilichonitokea. Hofu ilishindwa kujificha kwenye macho yangu, nikawa nakwepesha macho kwa sababu niliamini yule mlinzi kwa jinsi alivyonishupalia, angeweza kugundua kitu. Nilitamani kufanya kitu lakini sikuwa na uwezo, harufu ya jela ikaanza kunukia.
“Mkazie macho usoni,” ile sauti ya ajabu ya baba, ilisikika masikioni mwangu, nikageuka huku na kule lakini baba hakuwepo eneo hilo. Kwa kuwa mara zote ilikuwa ikinisaidia, nilifanya kama nilivyoelezwa.
Nilimkazia macho yule mlinzi, na yeye akanitazama. Ghafla nikashangaa anakuwa mpole ghafla, mwanzo alikuwa amekunja sura lakini ghafla alitabasamu. Niliendelea kumkazia macho.
‘Haya nenda, unajua siku hizi kumekuwa na matukio ya ajabu sana kwenye hizi nyumba za kulala wageni kwa hiyo lazima tuwe makini,” alisema huku akichekacheka, akageuka na kurudi getini. Sikuamini kilichotokea.
Kwa tafsiri nyepesi, baba alikuwa anaona kila kinachoendelea kwa sababu asingeweza kuniambia maneno yale tena katika muda muafaka kabisa. Hofu yangu ilikuwa ni je, anajua nilichokifanya kule gesti? Mara kwa mara alikuwa akinikanya lakini kwa ubishi wangu nikaona kama ananibania nisifaidi.
Sikuwa nalijua Jiji la Dar es Salaam wala sikuwa najua ramani ya kunifikisha nyumbani, kitu pekee nilichokumbuka, ni barabara ile tuliyojua, nikawa natembea harakaharaka huku nikitamani kama ningekuwa na uwezo ningepaa kabisa na kutoweka eneo hilo.
Nilinyoosha na barabara na nilipofika mbali, nilianza kukimbia, hofu kubwa ikiwa imetanda kwenye moyo wangu. Kwa bahati mbaya zaidi, sikuwa nakumbuka sehemu ambayo tulikatia kona na kutokezea kwenye barabara hiyo, nikajikuta nikipoteza uelekeo, nikawa nazunguka huku na kule, kijasho chembamba kikinitoka.
Sikuwa na fedha mfukoni kwamba ningezitumia kukodi bodaboda na kuwaelekeza nyumbani. Nikiwa naendelea kuumiza kichwa, hatimaye nilipata akili mpya. Pale nyumbani, kwa nje kulikuwa na kituo cha madereva wa Bajaj na nimewahi kusikia kwamba wenyewe wana umoja wao na wanajiita City Boys wakimaanisha watoto wa mjini.
Kuna Bajaj ilikuwa ikija mbele yangu, nikaipiga mkono, ikapunguza mwendo na hatimaye ikasimama. Nilimfuata dereva na ikabidi niwe mkweli kwake, nikamwambia kwamba nimepotea na ramani pekee iliyopo kichwani mwangu, ni kituo cha Bajaj cha City Boys.
Alicheka kisha akaniambia niingie kwenye Bajaj yake, nikamtahadharisha kwamba sikuwa na fedha, akaniambia atanisaidia.
“Wewe si unakaa pale kwa akina Rahma, mbona mimi nakujua,” alisema yule kijana kwa uchangamfu, nikamshukuru Mungu wangu na kuelewa kwa nini alicheka nilipomueleza kwamba nimepotea.
‘Mimi nakusaidia lakini na wewe nataka unisaidie jambo, unajua mi nampenda sana yule dada Rahma ila naogopa kumwambia ukweli maana muda wote yupo ‘sirias’, nataka unisaidie kufikisha ujumbe, mwambie Zedi dereva teksi, ukifanikisha ntakuwa nakuja kukuchukua nakutembeza viwanja mbalimbali na Bajaj, hata ukitaka pesa ntakuwa nakutoa,” aliniambia yule dereva Bajaj.
Kwa kuwa nilikuwa na shida kwa wakati huo, nilimkubalia kila alichokuwa anakisema. Hakuwa akijua kwamba mimi ndiye mmiliki wa Rahma. Kumbe sikuwa mbali sana na nyumbani, muda mfupi baadaye tukawa tumeshafika, akanishusha getini na kunisisitiza kuhusu ombi lake, nikazidi kumdanganya kwamba asiwe na wasiwasi.
Niliposhuka niliingia moja kwa moja ndani huku bado hofu kubwa ikiwa imetanda kwenye moyo wangu.
“Ulikuwa wapi?” mama aliniuliza kwa ukali mara tu nilipofika sebuleni. Nikakosa cha kujibu kwa muda, nikawa najiumauma, baadaye nikamwambia kwamba kuna rafiki yangu nilikuwa nimemsindikiza.
“Rafiki? Rafiki gani? Una rafiki hapa mjini wewe?” mama alinihoji huku akionesha kutokuwa na hata chembe ya masihara. Ilibidi ninyamaze kimya, nikataka nipitilize kwenda chumbani lakini aliniambia nataakiwa kukaa nao hapohapo sebuleni kwa sababu ninapopewa muda wa kuwa huru nashindwa kuutumia uhuru wangu vizuri.
Huo ulikuwa mtihani mkubwa sana kwangu, ikabidi nimwambie mama kwamba bado sijisikii vizuri, akaniambia nitakapotoka tena bila ruhusa yake au bila kuaga, atanisemea kwa baba aninyooshe. Nilifurahi kwa sababu aliniruhusu niende chumbani kwangu.
Nilipoingia tu, nilijifungia kwa ndani, nikakaa kwenye ukingo wa kitanda na kujiinamia, maswali mengi yakiendelea kupita ndani ya kichwa changu. Sikuwa najua nini itakuwa hatima yangu endapo ukweli utafahamika. Hata hivyo, kwa upande mwingine, nilianza kujiuliza mimi kosa langu ni nini kwa sababu, yeye ndiye aliyenifuata hadi nyumbani na ndugu yangu alikuwa shahidi.
Yeye ndiye aliyenishawishi twende kwenye nyumba ya kulala wageni na hata tulipofika, alionesha wazi kwamba alikuwa akinihitaji na kwa vile na mimi nilikuwa kwenye hali mbaya, tulijikuta tukiangua dhambini.
Nilijaribu kujiuliza kwamba labda kuna kitu kisicho cha kawaida nilimfanyia mpaka yakatokea ya kutokea lakini sikukumbuka chochote. Bado niliendelea kujiuliza maswali mengi yasiyo na majibu.
Nikiwa nimejifungia chumbani, mara nilianza kusikia kelele sebuleni, ndugu zangu wakawa wananiita nikaangalie. Ilibidi nitoke na kwenda mpaka sebuleni. Habari za dharura au Breaking News kama wengi walivyozoea kuita, zilikuwa zikioneshwa runingani moja kwa moja kutoka eneo la tukio.
Zilikuwa ni habari za samaki hatari aina ya papa kuvamia kwenye ufukwe wa bahari ya Hindi na kusababisha vifo vya watu kadhaa, wakiwemo wavuvi na wengine waliokuwa wakiogelea ufukweni huku wengine kadhaa wakijeruhiwa. Nilijikuta moyo wangu ukilipuka kuliko kawaida.
Kilichonishtua ni kwamba, mazingira ya tukio lile, yalikuwa sawa kabisa na kile kilichonitokea nilipoenda ufukweni na Rahma.
Habari zilieleza kwamba wavuvi walaikuwa kwenye boti yao wakivuta nyavu lakini ghafla, samaki huyo aliwashambulia kwa kuvunjavunja boti yao na kuanza kuwala, mmoja baada ya mwingine, hali iliyosababisah maji ya bahari yageuke rangi na kuwa mekundu.
Yaani kilekile nilichokieleza na kila mmoja kuniona kama mwendawazimu, ndicho kilichokuwa kimetokea, taarifa ya habari iliendelea kueleza kwamba polisi na vikosi vya uokoaji, wamefika eneo la tukio na wanahangaika kupambana na samaki huyo mkubwa.
Baada ya habari hiyo kuisha, watu wote pale sebuleni walinigeukia na kunitazama kwa mshangao uliochanganyikana na hofu. Tukiwa bado tunatazamana, mara baba aliingia getini akiwa ameongozana na baba yake Rahma na askari watatu waliokuwa na silaha. Nikajua mwisho wangu umefika, nilishindwa cha kufanya, nikabaki nimesimama palepale, nikitetemeka kuliko kawaida.
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatatu kwenye Gazeti la Championi Jumatatu.
No comments:
Post a Comment