Monday, August 28, 2017

The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 32


ILIPOISHIA:
Wote waliacha kila walichokuwa wanakifanya, wakawa wananitazama kwa macho makali. Sikuelewa nini hasa kimetokea, wakati nikiendelea kuwatazama vizuri kwa mara ya pili, kuna jambo moja lilinishtua mno mpaka nikajikuta nimetoa mkono mfukoni, giza likarudi kama lilivyokuwa mwanzo.
SASA ENDELEA...
Japokuwa kulikuwa na giza, niliweza kuonamacho ya wale watu yaking’ara kama wanyama wakali wa porini, nikawa najilaumu kwa kile nilichokifanya. Hata sijui nini kilitokea kwani kuanzia mwanzo nilikuwa nimejiapiza kwamba siku hiyo sitaleta ujuaji wowote mbele ya watu hao lakini cha ajabu, ndani ya muda mfupi tu, tayari nilishakuwa nimewekwa mtu kati.
Sikujua safari hii wataniadhibu vipi lakini niliamua kupiga moyo konde, liwalo na liwe. Bado nilikuwa najiuliza maswali mengi kuhusu kile kilichokuwa kwenye mfuko wangu, sikujua ni nini na kilikuwa na uhusiano gani na ule mwanga uliotokeza ghafla mle ndani ya mahabusu.
Sijui nilipata wapi ujasiri lakini nilijikuta nikiingiza tena mkono taratibu mfukoni, nilipokigusa tu kile kitu mle mfukoni, ule mwanga ulirudi tena vilevile, wale watu ambao safari hii walikuwa wamejikusanya na kutengeneza kama nusu duara hivi, waliinua wote shingo zao na kunigeukia tena, nikakishika kile kitu kwa nguvu huku na mimi nikiwa nawatazama.
Katika hali ambayo sikuitegemea, nilishangaa wa kwanza akisimama na kukimbilia kwenye ile kona alipokuwa amekaa yule mahabusu ambaye awali alikuwa akipiga kelele. Safari hii alikuwa amelala, tena kwa kuinamisha kichwa mbele, katikati ya miguu yake.
Nikamuona yule mtu wa kwanza, mikono yake akiwa amejiziba sehemu nyeti, akisogea mpaka kwenye kona, alipoikaribia, aligeuka na kuanza kutembea kinyumenyume, akamkanyaga yule mahabusu kisha nikashangaa akipotelea kwenye ukuta.

Ni hapo ndipo nilipoamini yale maneno niliyowahi kuyasikia kwamba wachawi wanao uwezo wa kuingia na kutoka ndani ya nyumba hata  kama milango imefungwa. Nilishindwa kuelewa ni nini hasa kilichofanya iwezekane kwa yule mtu kupotelea kwenye ukuta.
Nikiwa bado nimepigwa na butwaa, nilimuona mwingine naye akiinuka, akaanza kutembea kuelekea kwenye ile kona, wengine nao wakasimama, wakawa wanatembea huku wote wakiwa wananitazama kwa macho mabaya. Ni kama nilikuwa nimewavurugia mipango yao, nikazidi kukishikilia kile kitu mfukoni.
“Hiyo ndiyo nafasi yako ya kutoka mahabusu, hakikisha unamshika mmoja kati yao na kumvua usinga aliovaa shingoni kisha na wewe utatoka kama hao wengine walivyotoka,” nilisikia sauti masikioni mwangu ambayo niliitambua vizuri kwamba ni ya baba.
Bado sikuwa nimeelewa ni mbinu gani anayoitumia baba kuwasiliana na mimi kwa sauti ambayo hakuna mtu mwingine yeyote anayeisikia. Hata hivyo, sikutaka sana kuhoji, nilichokifanyailikuwa ni kufuata maelekezo.
Cha ajabu, wale watu walipoona nawafuata, walianza kukimbia lakini kwa sababu ya nafasi ndogo iliyokuwepo, walishindwa kutoka wote kwa mkupuo, nikafanikiwa kumkamata mmoja ambapo moja kwa moja nilipeleka mkono shingoni ambapo alikuwa amevaa kitu kama kamba nyembamba lakini iliyosokotwa kwa nywele, ikakatika na kubaki mkononi mwangu.
Kitendo hicho kilisababisha alie kwa sauti kubwa lakini cha ajabu sasa, sauti yake ilitoka kama zile sauti zinazotolewa na mapaka yanayolia usiku, akadondoka chini na kuendelea kulia kwa sauti kubwa kama paka.
Cha ajabu, wakati nikiwa nimeshageuka na kuupa mgongo ukuta, tayari kwa kufanya kile baba alichoniambia nikifanye, yule mtu aliinua uso wake huku akionesha ishara kwamba nimsamehe. Kilichonishtua ni kwamba sura yake ilikuwa ikifanana na mimi kwa kila kitu wakati awali hakuwa vile.
Nikiwa bado naendelea kumshangaa, nilisikia sauti ya baba ikinisisitiza kutoka haraka. Sikuwa nimewahi kushiriki uchawi mkubwa kiasi hicho, nikawa natetemeka nikiwa siamini kama kweli naweza kupita ukutani. Nilipiga hatua kurudi nyuma mpaka nilipoufikia ukuta.
Cha ajabu, nilipouegamia ulilainika kama pazia, nikapiga hatua nyingine na kujikuta nusu ya mwili wangu tayari ipo nje, nikapiga hatua nyingine, nikawa nimetoka nje kabisa. Nilibaki nimesimama kwenye maua yaliyopandwa pembezoni mwa ile mahabusu nikiwa bado siamini.
Niligeuka na kutazama huku na kule, hakukuwa na mtu yeyote eneo hilo, harakaharaka nikatembea na kupotelea kwenye kota za askari wa kituo kile, nikawa nazidi kutembea nikiwa sielewi naelekea wapi. Nilizimaliza kota hizo, kwa mbali nikawa nawasikia mbwa wakibweka, nikaongeza mwendo na muda mfupi baadaye, nilitokeza kwenye barabara ya lami.
Siwezi kuficha jinsi nilivyofurahi kutoka mle mahabusu. Hapohapo nikajikuta eti na mimi nikitamani kuwa mchawi ili nipate nafasi ya kufaidi mambo mengi kwenye hii dunia ambayo binadamu wa kawaida hawawezi.
Hebu vuta picha, hata kama ni wewe, yaani ndugu yako yupo gerezani anateseka halafu leo ukiambiwa kuna ujuzi ukifundishwa ndugu yako anaweza kutoka kiulaini, tena bila kutumia nguvu wala fedha, huwezi kutamani kweli?
Labda kamauna imani kali ya dini ndiyo unaweza kuukwepa mtego huo lakini kwangu mimi, siwezi kuficha kwamba nilifurahi sana na kutamani kuwa mchawi, tena niliyebobea. Nilijiapiza kwamba nitakapopata nafasi ya kuzungumza na baba, nitamueleza nia yangu bila kujali atanichukuliaje.
Niliendelea kutembea kufuata ile barabara ya lami huku muda mwingi tabasamu likiwa limechanua kwenye uso wangu. Tafsiri ya kile kilichotokea n kwamba asubuhi polisi wangeingia na kufanya ukaguzi mle mahabusu wangekuwa na imani kwamba bado nipo, labda watashtuka kwa nini sijavaa nguo kwa sababu yule mchawi hakuwa amevaa nguo.
Nilielewa kwa nini baba aliniambia nisitoe maelezo yoyote kwa sababu kama yule mtu niliyebadilishana naye na kumuacha mle ndani mahabusu atahojiwa, maelezo atakayoyatoa yatakuwa hayaungi chochote na tukio lililotokea kwa hiyo uwezekano wa baadaye kuja kuachiwa kwa sababu ya kukosekana ushahidi ulikuwa mkubwa.
Sikujua atasota kwa muda gani mle mahabusu, tena kesi yenyewe ikiwa ni ya mauaji lakini niliona kama anastahili maana ni uchawi wa aina gani watu wanaenda kuufanyia sehemu hatari kama mahabusu? Niliendelea kutembea huku mara kwa mara nikicheka mwenyewe maana nilijiona bonge la mjanja kuukwepa msala ule.
Nikiwa naendelea kutembea nikiwa sijui naelekea wapi kwa sababu kama nilivyoeleza, sikuwa naijua mitaa ya Jiji la Dar es Salaam, nilisikia vishindo vya mtu akija huku akikimbia akitokea nyuma yangu. Baba amewahi kuniambia kwamba ukiwa unatembea usiku, ni mwiko kugeuka nyuma.
Alizidi kunikaribia, nikawa najiuliza kama atakuwa ni mtu mbaya itakuwaje? Niliendelea kujikaza kisabuni, vishindo vikazidi kunikaribia na alipofika usawa wangu, nikasikia akipunguza mwendo. Kilichonifanya niamini kwamba hawezi kuwa mtu mbaya, ni jinsi manukato aliyokuwa amejipulizia mwilini yalivyokuwa yakinukia vizuri.
“Mambo,” sauti ya kike ilisikika, safari hii ikiwa usawa wangu kabisa, ikabidi nisimame, nikageuza shingo yangu upande wa kulia alipokuwepo mtu huyo aliyenisalimu. Muda huo kwa makadirio ilikuwa ni kama saa nane za usiku maana kuna sehemu nilipita nikasikia redio kwa mbali ikitangaza kwamba ni saa nane kasoro za usiku.
“Mbona umeshtuka Togo!” alisema huku akinisogelea. Siwezi kuficha, mshtuko nilioupata nusura nidondoke na kuzimia.
Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Championi Ijumaa.


No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...