HASH POWER 7113
NI matumaini yangu kwamba msomaji wangu uko poa. Ni wiki nyngine tunapokutana kwenye busati letu ambapo tunajuzana na kujadiliana mambo mbalimbali kuhusu uhusiano wa kimapenzi.
NI matumaini yangu kwamba msomaji wangu uko poa. Ni wiki nyngine tunapokutana kwenye busati letu ambapo tunajuzana na kujadiliana mambo mbalimbali kuhusu uhusiano wa kimapenzi.
Nakushukuru wewe unayetuma ujumbe mfupi ukitoa
maoni, kuchangia au kutaka ushauri kuhusu mambo mbalimbali, hata kama
hujajibiwa elewa kwamba ujumbe wako umefika na utafanyiwa kazi.
Mada ya leo ni maalum kwa watu ambao tayari mpo
kwenye uhusiano wa kimapenzi, iwe ni wapenzi wa muda mrefu, wachumba au
wanandoa.
DALILI
ZA PENZI LILILOKUFA
Umewahi kuhisi kwamba penzi lako limefikia mwisho
japo bado upo na mpenzi wako, mchumba au mumeo/mkeo? Yaani upoupo tu, zile
hisia tamu za mapenzi
ulizokuwa nazo wakati mnayaanza mapenzi yenu hazipo tena,
hufurahii kuwa naye, hamzungumzi mkaelewana badala yake kila siku ni ugomvi na
migogoro isiyoisha!
Kila unachokisema au atakachokisema hata kama ni
kizuri vipi kinakuwa sawa na petroli kwenye moto, kinazidi kuchochea uhasama na
chuki kati yenu. Kila mnapoanza kuzungumza, hata kama ni jambo zuri lazima
muishie kutukanana, kufokeana au kupigana.
Unaishi naye nyumba moja lakini kila mmoja analala
kwenye chumba chake, hata mkilala pamoja kila mmoja anageukia upande wake,
hujisikii chochote juu yake, hata akiugusa mwili wako unaona kero na hutaki
hata kumtazama usoni. Hujisikii hamu tena ya kuwa naye faragha, kila
unachokifikiria kuhusu yeye kinakupandisha hasira na kukuudhi!
Unatamani uhusiano wenu ufikie mwisho hata sasa
hivi ingawa hujui uanzie wapi… unatamani mwenza wako afe kwa ajali au apate
mabalaa makubwa yatakayowatenganisha.
Ukiona hayo yote niliyoyataja na mengine mengi
yanakutokea, huo ni uthibitisho kwamba unaishi kwenye mapenzi yaliyokufa,
Wazungu wanasema Dead Love. Kwa wale ambao wameishi kwenye uhusiano wa
kimapenzi kwa muda mrefu watakuwa wananielewa vizuri zaidi, kama upo kwenye
penzi jipya, huwezi kuelewa vizuri.
KUACHANA
NDIYO SULUHU?
Wengi wanapofikia hatua hii ya kuishi kwenye
mapenzi yaliyokufa, huwa wanakosea sana kuamini kwamba njia pekee ni kuachana.
Hata kama ni wanandoa na walishafanya mambo mengi pamoja ikiwa ni pamoja na
kuzaa, wataishia kupeana talaka! Inasikitisha sana.
Hata hivyo, hiyo siyo dawa kwani ni kuyakimbia
matatizo! Utaachana na wangapi? Wataalamu wa mahusiano na mapenzi wanasema kila
penzi lililokomaa, lazima lipitie kwanza kwenye hatua ya kufa, ukweli ambao ni
wachache huweza kuukubali. Wahenga wanasema dhahabu ili ing’ae lazima ipitie
kwanza kwenye moto.
NINI
CHA KUFANYA?
1. Hatua ya kwanza, jiwekee nadhiri kutoka ndani
ya moyo wako kwamba upo tayari kulifufua penzi lako lililokufa. Yawezekana wewe
umeamua hivyo lakini mwenzako hayupo tayari, hilo lisikukatishe tamaa. Jiambie
moyoni kwamba utafanya kila kinachowezekana kurudisha furaha, amani, hisia za
mapenzi, msisimko na upendo kama ilivyokuwa wakati mnaanzisha uhusiano wenu.
2. Jipe muda wa kutafakari nini kilisababisha
mwanzo mkawa na furaha na kupendana sana. Jaribu kukumbuka mambo uliyokuwa
ukimfanyia mwanzo mpaka akakupenda na kuwafanya muishi kwa amani na upendo.
Anzia hapohapo, anza kufanya yale yaliyomfanya
akupende mwanzo, kuwa mpole kwake, acha kumuonesha kisirani, dharau, jeuri au
kujibizana naye. Badili hisia zako za ndani, badala ya kufikiria mabaya yake,
fikiria yale mazuri aliyowahi kukufanyia.
3. Kubali kuwajibika. Japokuwa wengi huwa
wanashindwa kwenye kipengele hiki, jibebeshe mzigo wa lawama wewe mwenyewe hata
kama si kweli kwamba wewe ndiyo mwenye makosa. Jiambie mwenyewe kwamba wewe
ndiyo umesababisha mfikie hapo mlipofika kwa sababu kama alikukosea, ungeweza kumsamehe
kuanzia siku ya kwanza na wala msingefikia hatua hiyo.
Ukishakubali kuwajibika, utakuwa kwenye hatua
nzuri ya kuzidi kumkaribia, hata ile chuki uliyokuwa nayo, utashangaa inayeyuka
kama barafu iyeyukavyo juani na mapenzi yanaanza kuchanua upya moyoni mwako.
4. Muoneshe kwamba unajisikia vibaya kwa aina ya
maisha mnayoishi na hata kama hajakuomba msamaha, jiambie ndani ya moyo wako
kwamba umemsamehe bure na upo tayari kufungua ukurasa mwingine mpya.
Lilazimishe tabasamu kwenye uso wake, badala ya kuwa
mnapishana ndani kama wanyama, anza kuwa unamtazama usoni kwa upole, hata kama
yeye hatakuangalia lakini ataanza kuhisi kitu cha tofauti ambacho kitaanza
kumbadilisha naye taratibu.
5. Msaidie kazi ndogondogo za nyumbani. Kama wewe
ni mwanamke na kwa kipindi chote cha ugomvi hukuwa ukimfulia nguo, kusafisha
chumba anacholala au kumuandalia chakula kizuri, jilazimishe kuyafanya hayo
hata kama moyo wako unakataa. Yafanye akiwa hayupo.
Kama ni mwanaume, jitoe fahamu kwa kumsaidia kazi
za nyumbani hata zile ambazo hukuwahi kuzifanya. Msaidie kuosha vyombo,
kusafisha nyumba, kuwaogesha watoto (kama mlishazaa), kumfulia nguo zake au
kuwaandalia watoto chakula.
Hata kama utakuwa hujamwambia neno lolote,
atayaona mabadiliko na taratibu utaanza kuzigusa hisia zake kwa mara nyingine.
Muda mwingi atakuwa anajiuliza kwa nini unayafanya yote hayo kwa ajili yake na
mwisho atajipa jibu kwamba kumbe bado unampenda na unamhitaji.
6. Rejesha mawasiliano. Mnapokuwa kwenye penzi
lililokufa, si ajabu hata salamu mkawa hampeani wala hamzungumzi vizuri tena.
Baada ya kuwa umeshayafanya yote niliyokueleza hapo awali, anza kumsemesha.
Msalimu kila asubuhi unapoamka na kila unaporudi kutoka kazini au mpigie simu
na kumtumia sms nzuri. Hata kama atakuwa hakujibu kwa uchangamfu, usichoke,
endelea na taratibu utaanza kuona naye anakusemesha na kukujibu vizuri.
Katika mawasiliano hayo mapya, jitahidi kutokuwa
mzungumzaji sana bali msikilizaji. Lazima atakuwa na dukuduku la mambo mengi
uliyomfanyia kipindi ambacho hamuelewani au yaliyosababisha mkafikia hatua
hiyo, kuwa msikilizaji na muoneshe kwamba unamuelewa kwa kila anachokwambia.
Epuka kubishana naye hata kama unaona anachokwambia siyo sawa.
Uzuri wa mbinu hizi, ukizifanyia kazi, matokeo
yake yanaonekana kwa macho.
7. Rejesha mapenzi kwake. Yawezekana ikawa vigumu
kwako kuanza kumpenda tena baada ya kuishi kwenye migogoro kwa kipindi kirefu
lakini kama kweli unataka kufufua penzi, anza kumuonesha kwamba unampenda.
Kama unapata wakati mgumu kurudisha mapenzi,
jaribu kujenga taswira kichwani mwako kwamba umekutana na mpenzi mpya na ndiyo
mnaanzisha uhusiano wa mapenzi. Kuna usemi wa Kizungu usemao: Love conquers all
(Mapenzi yanashinda nguvu vitu vyote). Ukimuonesha mapenzi, migogoro, chuki na
uhasama vitayeyuka vyenyewe taratibu kwa sababu penzi la kweli lina nguvu sana.
8. Muoneshe uaminifu wa asilimia 100. Kama awali
ulikuwa na tabia ya kuchelewa kurudi nyumbani bila sababu za msingi, badilisha
ratiba zako. Kama ulikuwa unaweka password kwenye simu yako, itoe na mruhusu
kushika simu yako kwa uhuru. Usiende kupokelea simu nje au pembeni, kuwa muwazi
kwake kadiri uwezavyo.
Kama ulikuwa na ‘michepuko’, achana nayo kabisa na
elekeza nguvu zote kwa mpenzi wako. Taratibu utaona anaanza kukuamini tena na
endeleza uaminifu kadiri uwezavyo. Utaugusa moyo wake na penzi lake kwako
litaanza kuchanua upya.
9. Mkumbushe maisha yenu wakati wa furaha. Mnaweza
kutazama picha zenu za harusi mkiwa pamoja au mlizopiga kipindi cha mwanzo cha
uhusiano wenu. Utazirudisha kumbukumbu zake nyuma na atakumbuka matukio ya
furaha zaidi kuliko maudhi.
Unaweza pia kumfanyia mambo mliyokuwa mkiyafanya
pamoja kipindi mlipokuwa na furaha kama kutazama movie nzuri pamoja, kusikiliza
muziki anaoupenda au kumtoa ‘out’ kwenye mazingira mliyokuwa mkienda kipindi
mapenzi yenu yalipokuwa motomoto.
10. Mfanyie mambo mazuri. Jitahidi kadiri ya uwezo
wako kufanya mambo yatakayokuwa yanamfurahisha. Mnunulie zawadi, hata kama ni
ndogo zitaufurahisha moyo wake. Mwambie maneno mazuri ambayo pengine ulishaacha
kumwambia kwa kipindi kirefu.
Msifie kama yeye ni mrembo au hendisamu, mueleze
kuwa hujawahi kupenda kama unavyompenda yeye na mchombeze kwa maneno mazuri
kila mara unapokuwa karibu naye. Rudisha upendo kwa ndugu zake, marafiki zake
na watu wake wa karibu.
Jitahidi kutafuta muda wa kutosha wa kukaa naye
kila siku, hata kama ubize wa kazi unakuelemea, tenga muda kwa ajili ya kuwa
naye, kula naye chakula cha jioni, kutoka ‘out’ pamoja na kwenda kwenye
matembezi mkiwa pamoja huku muda mwingi ukijitahidi kuwa na tabasamu usoni
mwako.
Uzuri wa mbinu hizi, ukizifanyia kazi kwa
ukamilifu, matokeo yake yanaonekana haraka kuliko unavyotegemea. Kama huamini,
anza leo na zingatia mbinu zote kisha utaona matokeo mwenyewe. Utakuwa
umefanikiwa kurejesha furaha kwenye penzi lenu na atakupenda zaidi kuliko hata
ilivyokuwa mwanzo. Cha msingi ni kujizuia kurudia maudhi mara kwa mara.
Mwisho.
Ahsante
ReplyDeleteSafi sn imenigUSA hiI ntazingatia nifufue la kwangu lililokufa
ReplyDeleteAsante
ReplyDeleteAsante
ReplyDeleteasante san nitaanza ss
ReplyDeleteNimekuelewa sana, tatizo Mimi yuko mbali tunaishia kwenye cmu cwezi kumfata
ReplyDeletesomo nzur, nimejifunza mengi yatakayoendeleza furaha kwenye maisha ya mahusiano.
ReplyDeleteNimejifunza kitu nitafufua penz langu lililokufa🙏🙏
ReplyDeleteDah paka nmelia..wengine hapa ndo kila cku ya mungu ugomvi..moyo unakataa kabisa kupenda tena..ila umenisaidia..ntaweka nia na nijaribu..asante sana
ReplyDeleteMimi langu ndio linaelekea kufa nataka nijitahidi in Shaa Allah kwa uwezo wa Allah ntafanikiwa nilikuwa kwenye sintofaham nifanyeje ila nimepata suluhisho ubarikiwe ndugu!
ReplyDeleteAsante sana, nakomaa na namba 6 hadi kieleweke
ReplyDeleteMimi mpaka anataka kuondoka akaanze upya maisha yake yaani mwanaume amechoka mpaka sielewi naanzaje
ReplyDeleteAsantee
ReplyDeleteKosa lilikuwa langu kwasasa nimerudi kwake,na nikaona wote tulikuwa bado tunapendana lakini kabadilika sana.Ila nitajitahidi kufanya kila njia awe sawa kama zamani.
ReplyDelete