Thursday, August 10, 2017

The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 17


ILIPOISHIA:
“UNASEMA?” Mama yake Rahma aliuliza kwa mshtuko, huku  akiacha kila kitu alichokuwa akifanya. Haraka akakimbilia chumbani kwa mwanaye huku akionyesha wasawasi mkubwa moyoni mwake, mama naye akamfuata, na mimi uzalendo ukanishinda, nikainuka na kuwafuata.
 SONGA MBELE...
TULIPOINGIA chumbani, mama yake Rahma akaanza kumuamsha kwa kumwita lakini hakuitika wala kutikisika, akasema; “mwanangu umepatwa na nini?” Hata hivyo, Rahma hakuitika wala kufumbua macho, jambo hilo lilitushtua sana, mama naye alipojaribu kumwita hali ikawa vilevile, Rahma alitulia kimya.
Sikukubaliana na hali hiyo, nilijongea kitandani alipolala Rahma, nikamshika begani na kuanza kumtikisa huku nikimwita, kama ilivyokuwa kwa mama yake na mama, kipenzi changu Rahma hakuitika. Kilichofuatia ni kila mmoja wetu kuanza kulia kwani tulijua alikuwa ametutoka, kufuatia vilio vyetu baba yake Rahma alisikia akaja mbio kujua kilitokea nini, akina mama wakiwa wanalia walishindwa kumweleza chochote zaidi ya kulia.
“Eti Togo, kimetokea nini?” akaniuliza. Nilimfahamisha kilichotokea, akiwa amepata mshtuko, mzee huyo alimshika Rahma kifuani akagundua mapigo yake ya moyo yalikuwa yakidunda kwa mbali, akawauliza akina mama alipatwa na nini. Mama ya Rahma akamweleza kila kitu, mzee huyo aliwaambia wanyamaze kwani Rahma alikuwa hajafa, mzee huyo aliniambia niende haraka kwa jirani aliyekuwa na usafiri ili amkimbize Rahma hospitali.
Nikiwa nimechanganyikiwa na tukio hilo, nilikwenda kwa jirani huyo ambaye alikuja na gari lake tukampakiza Rahma na kumkimbiza hospitali, alipofikishwa huko alifanyiwa uchunguzi na kuibainika alikunywa dawa mchanganyiko ili ajiue. Madaktari walimuwekea dripu ya maji kisha antpoison kuondoa sumu hiyo, wakati akipewa matibabu hayo alikuwa hajitambui, madaktari walituambia tusiwe na wasiwasi kwani baada ya muda mfupi hali yake ingetengemaa.


“Kati yenu ni nani wazazi wa huyu binti?” Daktari aitwaye Jason aliwauliza akina mama na akina baba! “Mimi mama yake na huyu hapa ndiye baba yake,” mama ya Rahma alimjibu daktari huyo huku akimuonyeshea mumewe. “Oke, naomba twendeni ofisini kwangu tukazungumze kuhusiana na tatizo la binti yenu,” daktari huyo aliwaambia.
“Hakuna shida daktari,” baba ya Rahma alimwambia. “Kwanza nawapeni pole kwa jambo lilitokea kwani najua ni kwa kiasi gani mmepata mshtuko,” daktari aliwaambia. “Tunashukuru dokta, pia tunashukuru kwa jinsi ulivyompokea na kumhudumia kwa wakati,” mama yake Rahma alimwambia daktari. Alipoambiwa, daktari aliwaambia wasijali kwani huo ndiyo wajibu wao kwa wagonjwa kisha akawauliza kilitokea nini nyumbani kilichosababisha Rahma kutaka kujiua!
“Kwa kweli hata sisi tumeshangazwa sana na uamuzi wake, ameamka akiwa mukheri wa afya, tumeshinda naye vizuri hadi mchana mama yake alipomtuma ndugu yake akamuamshe kwa ajili ya kula ndipo akarudi mbio na kumweleza alimwita hakuitika na alipojaribu kumtikisa alitulia tu!” baba ya Rahma alimweleza daktari.
“Oh poleni sana, lakini lazima kutakuwa na sababu kwani katika hali ya kawaida siyo rahisi kwa mtu kuchukua uamuzi wa kutaka kujiua bila ya kukwazwa na jambo f’lani, je, yupo katika uhusiano wa kimapenzi na mtu yeyote?” Daktari aliwauliza. “Hatuelewi maana hatujawahi kumuona na mwanaume yeyote,” mama Rahma alimwambia.
Alipotoa kauli hiyo, daktari Jason aliwauliza tena kama binti yao alikuwa na ugomvi na mtu yeyote hasa marafiki zake, wazazi wake wakamwambia hakuwa na ugomvi. “Labda aliomba mnunulie kitu f’lani mkamkatalia kwa ukali?”
Daktari huyo alizidi kuwabana kwa maswali ili tu kujua sababu ya Rahma kutaka kujiua. “Kwa upande wangu hajaniomba chochote labda mwenzangu,” mama yake alimjibu daktari. “Eh! Baba au alikuomba fedha ukamnyima,” daktari akamwuliza. “Hapana daktari, tena juzi tu nimempatia fedha za kutosha kwa ajili ya matumizi yake,” mzee huyo alimwambia.
Baada ya maswali hayo na majibu, daktari aliwaambia lazima kuna jambo ambalo wazazi hawalifahamu lililosababisha Rahma kutaka kujiua, akawashauri wawe wanachunguza nyendo za watoto wao hasa mabinti kwa sababu wana mambo mengi sana.
***
Wakati kule ofisini kwa daktari Jason akiendelea kuzungumza na wazazi wa Rahma, nje baba yake Togo na mama yake ambao hawakuwa na furaha walikuwa wakizungumza kuhusu tukio hilo. “Hivi mama Togo, kitendo cha kuwauliza hawa watoto kama wanafahamiana tangu zamani na kwamba ukaribu wao unatutia shaka inaweza kuwa sababu ya Rahma kutaka kujiua?” baba Togo alimwuliza mkewe.
“Sidhani, nahisi kutakuwa na jambo lingine tu mume wangu,” mama huyo alimwambia mumewe. Alipoambiwa hivyo, mumewe alimweleza mkewe kwamba huenda tayari walishaanza kufanya utundu na sababu ya kutaka kujiua ni baada ya kuwaambia walikuwa ndugu!
“Ila unachosema naona umenifungua kichwani, huenda ikawa hivyo ili kuficha aibu ya kutembea na kaka yake, lakini tusiwaze sana kuhusu hilo tutajua tu ukweli!” mama Togo alimwambia mumewe.
Hata hivyo, baba Togo alimwambia mkewe kwamba ngoja wamsubiri Togo aliyekuwa amekwenda kununua maji ya kunywa arejee ili wambane kwani walihisi alikuwa anajua sababu za mwenzake kutaka kujiua. “Nakuunga mkono, atakuwa anajua japo anajifanya hajui chochote,” mama Togo alimwambia mumewe. “Mh! Huyu mtoto ana hatari sana, hata kama wameshafanya utundu na kaka yake uamuzi aliochukua siyo mzuri hata kidogo,” baba Togo alimwambia mkewe kwa huzuni.
 “Ila mke wangu kama kweli hawa watoto watakuwa wamefanya utundu itakuwa dhambi kubwa ambayo italeta balaa na tutakuwa tumesababisha sisi kushindwa kuwaambia mapema kwamba walikuwa ndugu,” baba Togo alimwambia mkewe.

“Sijui itakuwaje sasa mume wangu, lazima balaa litokee tuombe tu Mungu Togo atuhakikishie kwamba hawafanyi mapenzi na ndugu yake,” mama Togo alimwambia mumewe. Wakati wakizungumza hayo, mara wakawaona baba na mama Rahma wanakwenda walipokuwa wakitokea ofisini kwa daktari, wakaacha mazungumzo yao. Je, kilifuatia nini? Usikose mwendelezo wa hadithi hii  katika Gazeti la Championi Ijumaa.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...