Thursday, August 17, 2017

The Graves of The Innocent (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 23


ILIPOISHIA:
“Tupeleke Coco Beach, kule wanakouza mihogo,” alisema Rahma, safari ikaanza lakini mita chache mbele, nilishtuka baada ya kusikia mtu akiliita jina langu kwa nguvu, tena sauti yenyewe ilikuwa ya kike, ilibidi Rahma amwambie dereva asimame, tukageuka nyuma kutazama ni nani aliyekuwa ananiita kwa sababu mimi nilikuwa mgeni na hakuna mtu yeyote aliyekuwa akilifahamu jina langu zaidi ya wale tuliokuwa tukiishi pamoja.
SASA ENDELEA...
Mimi ndiyo nilikuwa wa kwanza kushuka kwenye Bajaj, Rahma naye akafuatia, nikawa na shauku kubwa ya kumjua aliyeniita kwa bashasha kiasi kile.
“Togo, ni wewe! Ooh siamini macho yangu, sikujua kama nitakupata!” alikuwa ni yule msichana ambaye tulikaa naye siti moja kwenye basi wakati tukisafiri kutoka Mbeya kuja Dar es Salaam. Alikuwa amevaa sketi fupi na nyepesi ambayo ilimfanya maungo yake yajichore vizuri.
Juu alikuwa amevaa blauzi ndogo ambayo iliacha sehemu kubwa ya kifua chake wazi, akawa anatembea kwa maringo akinifuata huku tabasamu pana likiwa limechanua kwenye uso wake. Kiukweli na mimi nilishindwa kujizuia kutabasamu, hasa nilipokumbuka wakati mzuri tuliokuwa nao kwenye basi mpaka tulipoachana Ubungo.
“Jamani mbona ile simu niliyokupa hupatikani hewani? Nimehangaika sana kwa kweli,” alisema akiwa tayari ameshanifikia, kufumba na kufumbua nikashtukia amenikumbatia kimahaba na kunibusu mdomoni.
“Dada mambo!” alimsalimia Rahma ambaye alikuwa amesimama pembeni yake, akiwa ni kama haamini kile alichokuwa anakiona. Ilibidi nianze kuvungavunga pale maana kila kitu kilikuwa kikitokea kwa kasi kubwa mno.

“Umepajuaje hapa?”
“Ilibidi nimtafute dereva teksi aliyewabeba wakati mnatoka pale Ubungo, kwa bahati nzuri akawa anakumbuka sehemu alipowaleta, ndiyo amenileta, yule pale kwenye gari,” alisema huku akigeuka nyuma na kuonesha upande teksi alityokuja nayo ilipokuwa imepaki.
“Mnaenda wapi kwani?”
“Tunaenda bichi,” nilimjibu harakaharaka huku nikigeuka na kumtazama Rahma usoni ambaye bado alionesha kutoelewa kinachoendelea.
“Kwa nini tusipande kwenye ile teksi, mi nimeshalipa.”
“Hapana, ahsante,” Rahma alidakia na kunishika mkono, naona uzalendo ulishafika kikomo, akatangulia kuingia kwenye Bajaj na kunivuta mkono na mimi niingie.
‘Kwani mnaenda bichi gani?” aliuliza huku akionesha bado kuwa na shauku kubwa ya kuzungumza na mimi.
Sikuwa nakujua Coco lakini kwa sababu nilimsikia Rahma akimueleza dereva wa Bajaj kuwa atupeleke wanakouza mihogo, na mimi nilijikuta nikijibu hivyohivyo.
“Coco wanakouza mihogo,” baada ya kumjibu hivyo, nilimuona haraka akigeuka na kurudi kwenye teksi aliyokuja nayo. Watu kadhaa waliokuwa eneo lile, waliacha kila walichokuwa wanakifanya na kugbaki wakishangaa muvi iliyokuwa inaendelea.
“Togo, yule ni nani?”
“Mh! Jina lake simjui lakini tulikaa naye siti moja kwenye basi wakati tunakuja.”
“Muongo! Yaani mtu uliyekaa naye siti moja tu ndiyo akuzoee kiasi hiki? Angalia amekupaka lipstiki yake mdomoni,” alisema Rahma huku akionesha kuanza kulengwalengwa na machozi.
“Kweli tena, hata ukimuuliza atakwambia hivyohivyo, hata hatujuani vizuri,” nilisema huku nikijifuta mdomoni, kweli kulikuwa na mabaki ya lipstiki aliyoniachia aliponibusu mdomoni.
“Yeye amenizoea tu lakini hakuna chochote kati yetu.”
‘Mbona nimemsikia akisema alikupa simu? Yaani inawezekanaje mtu akupe simu tu? Halafu umeona alivyovaa, kwa nje tu anaonekana changudoa, ka hiyo kumbe wewe unatembea na machangudoa? Si nakuuliza?” Rahma alizidi kunibana kwa maswali mengi. Sikuwahi kumsikia Rahma anavyozungumza akikasirika lakini siku hiyo alikasirika kwelikweli, akawa anaendelea kufoka na muda mfupi baadaye alianza kulia.
Ilibidi nianze kazi ya kumbembeleza, nikamkumbatia kifuani kwangu na kumbusu sehemu mbalimbali za mwili wake, kidogo nikamuona akianza kutulia, na yeye akanikumbatia kwa nguvu kifuani huku Bajaj ikizidi kukata mitaa.
“Halafu umemuelekeza mpaka sehemu tunapoenda, hujui anaweza kukufuata? Dereva nimebadilisha mawazo, hebu tupeleke Msasani Beach na siyo Coco tena, nitakuongeza hela,” alisema Rahma, dereva akatingisha kichwa kuonesha kwamba amemueleza.
“Unajua mimi nakupenda, kwa nini unanifanyia makusudi lakini?”
“Nisamehe Rahma, hayakuwa makusudio yangu, nimejikuta tu mambo ya ajabu yametokea, nisamehe,” niliendelea kumbembeleza na kumbusu, cha ajabu alitulia kabisa na hakusema neno lingine lolote mpaka tulipofika Msasani Beach. Sikuwa naijua mitaa lakini kiukweli nilifurahia sana mandhari ya Jiji la Dar es Salaam.
Alimlipa dereva kisha tukashuka, tukawa tunatembea kuelekea baharini huku nikiwa na shauku kubwa ya kuiona bahari maana nilikua nikisikia tu. Nilitaka pia nikaonje maji yake nihakikishe kama kweli yana chumvi kama ambavyo watu huwa wanasema.
Tulipita sehemu ambapo kuna viti vya kupumzikia, tukawaona watu mbalimbali wakiwa wanapunga upepo, wengine wakila na kunywa. Tulipitiliza mpaka baharini kama nilivyomuomba Rahma na kitu cha kwanza nilichokifanya, ilikuwa ni kunawa usoni na kichwani kwa kutumia maji ya baharini.
Niliwahi kusikia pia kwamba maji ya baharini huondoa mikosi, nikanawa kwa maji mengi na hapo ndipo nilipogundua kuwa ni kweli maji hayo yalikuwa na chumvi, tena nyingi kiasi kwamba huwezi hata kuyanywa. Kiukweli nilifurahi sana kuiona bahari na kuyagusa maji ya bahari, nikawa najisikia kama nimetua kwenye ulimwengu mwingine tofauti.
Rahma muda wote alikuwa akicheka kwa furaha, hasa kwa jinsi nilivyokuwa ‘najitoa ufahamu’ na bahari. Nilifurahi kumuona akicheka mpaka kukaukia, akiwa amekaa kwenye mchanga, jirani na pale nilipokuwa.
Baada ya kucheza sana kwenye maji, nilirudi pale alipokuwa amekaa Rahma, nikakaa pembeni yake na kumuegamia, akanibusu kwenye paji la uso na kuniambia kuwa nimemfurahisha sana. Tuliendelea kupiga stori za hapa na pale lakini mra kwa mara Rahma alikuwa akipenda zaidi tuzungumze mambo ya kikubwa.
Alikuwa anataka kusikia nina mal;engo gani naye siku za usoni, alitaka kujua napenda kuwa na familia ya watoto wangapi au nitakuwa baba wa aina gani kwa wanangu. Aliniuliza pia kama nina mpango wa kujiendelea kwenye fani yoyote ili mwisho na mimi nije kuwa na uwezo wa kutunza familia.
Kwangu mazungumzo hayo si tu kwamba yalikuwa mageni kwangu, lakini pia mambo mengi sikuwahi kuyawaza. Nadhani hili ndiyo tatizo linalowakumba watu wengi wanaopishana umri wa wenzi wao, hasa kama mwanamke akiwa mkubwa. Kwangu Rahma alikuwa mkubwa, kama nilivyowahi kusema siku za nyuma, alikuwa akilingana na dada yetu mkubwa, Sabina.
Hata mazungumzo yake, alikuwa ni mdada anayejiheshimu, mwenye busara na anayewaza mbali, alionesha kweli kwamba ameanza kukomaa kiakili. Hali ilikuwa tofauti kwangu kwa sababu hata mwanamke mwenyewe, yeye ndiye aliyekuwa wa kwanza kwangu, kwa maana sikuwahi kuwa na mpenzi wala kushiriki sanaa za kikubwa kabla ya kukutana naye.
Sikuwa nikiwaza chochote kuhusu familia, au mke au maisha ya ndoa, nadhani ni kwa sababu ya umri. Hata hivyo, kwa sababu Mungu alinipa uwezo wa kumsoma mtu haraka, sikutaka kumkasirisha mawazo Rahma, kwa hiyo ikabidi na mimi nianze kuzungumza kama mtu mzima flani hivi, tukawa tunaenda sawa.
“Mh, hebu naomba simu yangu mara moja, sijaigusa tangu tumefika,” alisema rahma, nikamsogezea pochi yake ndogo ambapo alifungua na kutoa simu.
“Mh! Baba amepiga sana, sijui alikuwa anasemaje,” alisema Rahma huku akiendelea kubonyezabonyeza simu yake, mara akanigeukia na kunitazama usoni.
“Kulikuwa na ujumbe wako hapa lakini tumechelewa sana, hata sijui itakuwaje,” alisema, hali iliyonifanya na mimi nishtuke kwa sababu ya jinsi yeye mwenyewe alivyoonekana kushtuka.
“Kuna nini kwani?” nilimuuliza, akaniambia baba alikuwa amempigia simu kwa lengo la kutaka kuzungumza na mimi na kubwa alilokuwa anataka kuniambia ni kwamba wamesahau kuniambia kwamba nikienda ufukweni nisiguse kabisa maji ya bahari. Nilishangazwa sana na maelezo hayo, nikajiuliza maswali mengi yasiyo na majibu.
Tayari nilishayagusa na siyo kuyagusa tu bali niliyachezea vya kutosha na kama Rahma asingenizuia au kama siyo woga wa bahari, nilitaka hata niogelee. Tukiwa bado tunashauriana cha kufanya, mara simu ya Rahma ilianza tena kuita, harakaharaka akaipokea.
“Samahani simu ilikuwa kwenye mkoba baba,” nilimsikia Rahma akijitetea, bila shaka aliulizwa kwa nini hakupokea simu.
“Eeeh niko naye,” alijibu tena, nikajua lazima ameulizwa kama yupo na mimi, nikamuona akinipa simu, akaniambia baba anataka kuzungumza na mimi.
“Haloo Togo.”
“Haloo baba.”
“Hebu ongea na mzee,” alisema baba yake Rahma akimaanisha nizungumze na baba, akampa simu. Alimpa simu baba na swali lake la kwanza lilikuwa ni kama nimeshayagusa maji ya bahari. Ilibidi nimjibu kwamba nimeshayagusa kwani sikuwa najua chochote.
“Mungu wangu, kuna mtu anaenda kufa,” alisema baba kisha akakata simu, nikashtushwa mno na kauli yake hiyo. Sikuelewa nini kimetokea au kosa langu lilikuwa ni nini.
“Mbona watu wanachezea maji, wengine wanaogelea bila tatizo, mimi kosa langu nini,” nilijikuta nikijisemea, Rahma akanishika na kunituliza pale chini kwani nilishaanza kuchanganyikiwa kutokana na kile alichokisema baba.
“Amesemaje kwani?” aliniuliza Rahma, nikashusha pumzi ndefu na kumtazama usoni, sikutaka kumwambia ukweli wa nilichoambiwa na baba, nikamdanganya kwamba baba amenifokea sana kwa sababu nimegusa maji hayo. Aliupokea uongo wangu, akanikumbatia na kunipa pole, nikatulia kifuani kwake.
Ghafla tulishtushwa na kishindo kikubwa ambacho hata sikuelewa kimetokea wapi.
Je, nini kimetokea? Ni kishindo cha nini? Usikose next issue.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...