Wednesday, August 2, 2017

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 7


ILIPOISHIA:
“Mungu wangu, akina nani tena hao usiku wote huu?” nilijiuliza huku nikirudi nyuma na kujibanza pale uchochoroni, nikawaona wale wanaume wakiendelea kugonga mlango kwa nguvu. Ugongaji wao ulionesha dhahiri kwamba hawakuwa wamekuja kwa heri, nikawa natetemeka nikiwa sijui nitafanya nini.
SASA ENDELEA…
Mlango uliendelea kugongwa kwa nguvu, nikiwa nimejibanza palepale, nikitetemeka mno kwa hofu kwani nilishaona hatari iliyokuwa mbele yangu. Niliwaona wale watu wakijadiliana na muda mfupi baadaye, mmoja kati yao aliondoka eneo hilo. Muda mfupi baadaye, alirudi akiwa amemkwida mtu ambaye nilipomtazama, nilimtambua haraka kuwa ni yule dereva teksi aliyetuleta.
Japokuwa sikuwa nasikia walichokuwa wakikizungumza lakini ilionesha wazi kwamba walikuwa wakimshinikiza awahakikishie kama pale ndipo tulipoingia.

Nikamuona akijitetea na kusisitiza kuwa ni penyewe, kufumba na kufumbua nilimuona mmoja kati ya wale watu akimpiga ngumi yule dereva iliyosababisha apepesuke na kutaka kuanguka, mwenzake akamdaka na kumsimamisha vizuri, wakawa wanaendelea kumhoji huku yule mwingine akiendelea kugonga mlango kwa nguvu.
Kwa ilivyoonesha, baada ya mimi na Shenaiza kuondoka hospitalini, watu wale walikuwa wakitufuatilia na ndipo walipofanikiwa kumpata dereva aliyetuleta pale nyumbani kwangu na kumteka. Nilijiuliza wale ni akina na nani na kwa nini walikuwa wakitufuatilia?
Niliendelea kujiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu, nilimlaumu pia Shenaiza kwa kutonieleza ukweli wa kilichokuwa kinaendelea kwani mpaka muda huo, nilikuwa nimenaswa kwenye mtego ambao sikuwa naujua. Sikuwa najua Shenaiza ni nani? Ilikuwaje mpaka akajeruhiwa kiasi kile na aliyemjeruhi ni nani na wale watu walikuwa na uhusiano gani naye! Nilikosa majibu.
Kingine kilichonitisha, kama yule dereva tu ambaye hakuwa na hatia yoyote alikuwa akipigwa kiasi kile, hali ingekuwaje endapo wangenikamata na mimi? Kwa kuwa nilikuwa nimefunga mlango kwa kufuli, tena geti lilikuwa la chuma, niliamini hawawezi kumpata Shenaiza, kwa lugha nyepesi, Shenaiza alikuwa salama mle ndani, tatizo lilikuwa ni kwangu mimi.
Nilichoamua kukifanya kabla hawajanishtukia, ilikuwa ni kuondoka haraka eneo hilo na kwenda kutafuta hifadhi sehemu nyingine salama. Harakaharaka niliondoka, mkononi nikiwa na mzigo wangu wa chipsi na kutembea mpaka mtaa wa pili.
Nilitokezea kwenye kituo cha Bajaj na bodaboda ambapo nilimuita dereva mmoja wa bodaboda ambaye mara kwa mara huwa ananibeba.
“Vipi bro mbona usiku? Siyo kawaida yako!”
“Aah! Chukulia poa, nataka unipeleke Kijitonyama,” nilisema huku nikipanda kwenye bodaboda, nikawa nageuka huku na kule kuhakikisha kama hakuna mtu anayenifuatilia. Kwa jinsi nilivyokuwa natetemeka, ungeweza kudhani nimetoka kumwagiwa maji ya baridi.
Tuliondoka eneo hilo huku nikiendelea kujiuliza maswali yaliyokosa majibu. Sikujua hatma ya Shenaiza pale nyumbani kwangu. Niliamua kwenda Kijitonyama kwa rafiki yangu na mfanyakazi mwenzangu, Justice ili akanipe hifadhi lakini pia anipe ushauri wa nini cha kufanya.
Dakika kadhaa baadaye, tayari nilikuwa nimeshafika Kijitonyama, nikamlipa yule dereva wa bodaboda na kushuka, nikakaza mwendo kuelekea kwenye uchochoro wa kuelekea kwenye nyumba aliyokuwa anaishi Justice.
Kwa kuwa nilijua kwa muda ule watakuwa wameshafunga geti, nilienda kumgongea dirishani.
“Justice! Justice!”
“Mh! Nani tena usiku wote huu?”
“Ni mimi Jamal!”
“Jamal?” alihoji Justice kwa mshtuko, nikamuona akifungua pazia, akiwa ni kama haamini kwamba nimemfuata usiku huo. Alipohakikisha ni mimi, harakaharaka alienda kufungua mlango lakini nilipotaka kuingia ndani, alinizuia:
“Nipo na shemeji yako, vipi kwema utokako?”
“Dah!” nilijibu kwa kifupi, kauli yake kwamba alikuwa na mwanamke usiku huo ilinimaliza kabisa nguvu. Niweke wazi kwamba miongoni mwa matatizo ya rafiki yangu Justice, ilikuwa ni kupenda kubadilisha wanawake kama nguo. Mara kwa mara alikuwa na tabia ya kulala na wanawake tofautitofauti, jambo ambalo binafsi sikulifurahia.
Kibaya zaidi ni kwamba alikuwa akiishi kwenye chumba kimoja tu kwa hiyo akishakuwa na mgeni ndani, inakuwa vigumu kuingia, ikabidi nimwambie atoke ili tuzungumzie nje kwa sababu nilikuwa na matatizo makubwa.
Alirudi ndani kwani kwa muda huo alikuwa amejifunga taulo tu, alipotoka tena, alikuwa ameshavaa nguo.
“Samahani bwana sikujua kama utakuja, nisamehe kwa sababu tunazungumzia nje, si unajua tena,” alisema Justice huku akifunga vifungo vya shati lake, sikupoteza muda ikabidi nimueleza kwa kifupi kilichotokea.
“Mungu wangu, sasa itakuwaje?” alisema akionesha kupatwa na mshtuko mkubwa mno.
“Hata sielewi, ndiyo maana nimekuja kwako kupata ushauri.”
“Umeshaenda kuripoti polisi?”
“Sijaenda kwa sababu hata huyo msichana mwenyewe namna alivyofika nyumbani kwangu, ni kwamba nimefanya kumtorosha tu hospitalini,” nilimwambia lakini akasisitiza kwamba ni lazima twende tukatoe taarifa polisi ili chochote kitakachotokea, polisi wawe wanajua.
Kwa upande fulani nilikubaliana na alichoniambia, hatukuwa na muda wa kupoteza, alirudi ndani kumuaga msichana wake na alipotoka, tulielekea moja kwa moja kituo cha polisi. Kwa kuwa pale alipokuwa anaishi hapakuwa mbali na Kituo cha Polisi cha Kijitonyama au maarufu kama Mabatini, dakika kadhaa baadaye tulikuwa tumefika.
Tukaandikisha maelezo pale kaunta lakini kwa bahati mbaya zaidi, askari aliyekuwa zamu alisema askari wote wametoka kwenda kwenye doria kwa hiyo kama nahitaji msaada wa polisi, nisubiri mpaka warudi kutoka kwenye doria. Kutokana na hali ilivyokuwa, sikuwa na ujanja zaidi ya kubaki kusubiri hao askari warudi.
Kwa kuwa Justice alikuwa na mgeni wake, nilimruhusu aondoke kurudi kwake na kumshukuru kwa msaada aliokuwa amenipa. Akaondoka na kuniacha nimekaa kwenye benchi pale kituoni. Tayari saa ya kwenye simu yangu ilikuwa ikionesha kwamba ni saa sita za usiku.
Kutokana na pilikapilika nyingi, nilijikuta nimekaa muda mrefu bila kushika simu, nilipoishika nilikuta meseji kadhaa kutoka kwa rafiki zangu, moja ikiwa ni kutoka kwa Raya, msichana tuliyekuwa tukifanya naye kazi ambaye alitokea kunizoea sana.
Alikuwa ametuma ujumbe wa kunitakia usiku mwema kama ilivyo kawaida yake, nilishusha pumzi ndefu na kuendelea kutafakari hatma ya maisha yangu. Baada ya kukaa muda mrefu pale kituoni huku kukiwa hakuna dalili yoyote ya askari kuja, ilibidi niage na kuondoka kwa sababu kesho yake nilitakiwa kuwahi kazini kwani kuna kazi muhimu sana niliyokuwa natakiwa kuikamilisha.
Nikiwa naondoka, simu yangu ilianza kuita mfululizo, haikuwa kawaida mimi kupigiwa simu usiku huo, nikaitoa na kutazama namba ya mpigaji. Alikuwa ni Raya, nikashtuka kuona simu yake usiku huo, harakaharaka nikapokea.
“Vipi Jamal, umeshalala?”
“Hapana, bado sijalala Raya.”
“Mbona nakutumia meseji hupokei? Mpaka nimepatwa na wasiwasi.”
“Mh! Samahani kwa kuchelewa kujibu lakini usijali, niko poa na usiku mwema pia.”
“Haya ahsante, nilitaka nisikie tu sauti yako ndiyo nilale. Halafu mbona kama unatembea, unaenda wapi usiku wote huu?”
“Aah! Kuna mahali nimetoka ndiyo narudi nyumbani.”
“Jamal! Umetoka wapi usiku wote huu?” Raya alinibana kwa maswali. Jambo ambalo naomba niliweke wazi kuhusu Raya, japokuwa mimi nilikuwa namchukulia kama rafiki wa kawaida tu, alikuwa na hisia fulani juu yangu ambazo siwezi kuzielezea kwa urahisi.
Kwanza alikuwa anapenda sana kuwa karibu na mimi japokuwa mwenyewe nilikuwa nikimkwepa sana. Tukiwa kazini, alikuwa anapenda muda wa lanchi tutoke na kwenda kula pamoja na ikitokea nimeenda peke yangu, basi atanuna na kukosa raha siku nzima. Pia alikuwa anapenda hata wakati wa kutoka, tuongozane mpaka kituoni, ahakikishe nimepanda daladala kurudi kwangu ndiyo na yeye aende kwao kwani alikuwa akiishi Mwenge ya Mlalakua.
“Nipo Kijitonyama hapa jirani na Kituo cha Polisi cha Mabatini.”
“Please nakuomba tuonane usiku huuhuu, baba na mama wamesafiri tangu juzi, niko mwenyewe tu, nahisi haupo sawa na nahitaji kukusaidia, niambie nikukute wapi, nakuja na bodaboda sasa hivi,” alisema Raya, nikashusha pumzi ndefu.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
Nifollow kwenye mitandao ya kijamii kwa:
Facebook: Hash Power
Instagram: Hashpower7113
Twitter: Hash- Power.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...