Saturday, August 26, 2017

The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 31


ILIPOISHIA:
Nikiwa bado naendelea kumtazama kwa jicho baya, mara nilishtuka kusikia vishindo viwili vikubwa juu ya bati, kama vile nilivyokuwa navisikia usiku uliopita, moyo wangu ukapatwa na mshtuko mkubwa mno. Mara nilisikia vishindo vingine vitatu mfululizo, nikawa nimepigwa na butwaa huku macho yangu yote yakiwa juu.
SASA ENDELEA...
Kwa jinsi vishindo hivyo vilivyokuwa vikisikika, ilikuwa ni kama kuna watu wanaruka kutoka angani na kudondokea juu ya bati kwani vilikuwa vizito mno. Safari hii nilitaka kuwa makini kushuhudia je, kile ninachokisikia mimi, kila mtu anasikia hivyohivyo maana nilishahisi kuna kitu hakipo sawa kwangu lakini baba hataki kuniambia ukweli.
Baada ya vishindo vile vya kama watu au vitu kutua juu ya bati, mara vilianza kusikika vishindo vya mtu akitembea juu ya bati.
Unajua haya matukio kama hujawahi kutokewa nayo, huwezi kuelewa ile hofu unayokuwa nayo lakini kiukweli, ni bora tu uwe unasikia lakini yasikutokee. Hakuna hofu inayotesa kama hofu ya matukio kama haya yanapokutokea, hasa usiku kama huo.
Nilijikuta nywele zikisisimka vibaya mno, mapigo ya moyo yakawa yananienda kwa kasi maana sikujua safari hii wanakuja kwa mtindo gani. Vishindo viliendelea kusikika kisha kikasikika kishindo kingine ambacho kwa makadirio yangu ya haraka, kilikuwa ni kwenye sakafu ya mle mahabusu.

Nilishindwa kuelewa, inawezekanaje usikie mtu anatembea juu ya bati, tena kwa nje halafu muda mfupi baadaye umsikie akirukia na kudondokea kwa ndani, tena jirani kabisa na pale ulipo! Inatisha sana.
“Humu ndani kuna wanga eeh! Mbona nywele zinanisisimka? Sasa ole wake mtu aniguse,” mmoja kati ya wale mahabusu tuliokuwa nao mle ndani, aliyekuwa amekaa kwenye kona nyingine, alisikika akiongea kilevilevi, akawa anaporomosha matusi mazitomazito.
Kitendo kile kilinifanya niamini kwamba hatimaye sasa sikuwa peke yangu ambaye nilikuwa nikishuhudia mchezo uliokuwa ukiendelea. Niliamini hivyo kwa sababu kwenye kona aliyokuwa amekaa yule mahabusu ambaye alikuwa akiendelea kutukana, ndiko ambapo makadirio yangu yalinionesha kwamba yule mtu aliyekuwa akitembea juu ya bati alidondokea palepale.
Matusi aliyokuwa akitukana, yalisababisha mahabusu wengine ambao bado hawakuwa wamelala, waanze kucheka kwa nguvu na kumtania kwamba amelewa lakini kelele zote zilizimika ghafla bila mtu yeyote kutoa amri, ikatokea tu kwamba watu wote wapo kimya.
Katika ukimya huo, ulisikika msonyo mkali ambao japokuwa wale mahabusu wengine waliamini kwamba umetolewa na yule mahabusu aliyekuwa akitoa matusi mazito kwa wale aliowaita wanga, mimi nililitazama tukio hilo katika sura nyingine tofauti.
Haikuwa mara ya kwanza kusikia msonyo wa namna hiyo ingawa safari hii ulionekana kutoka kwa mtu tofauti ambaye sijawahi kuisikia sauti yake. Unajua kuna watu wamezaliwa wakiwa na uwezo fulani wa kipekee, sijui niuiteje lakini kwa kifupi mtu anakuwa na uwezo wa kufikiri na kuyaona mambo kwa utofauti na wengine.
Yaani kuna baadhi ya watu, nyie wengine wote mnaweza kuamini kwa mfano ajali iliyotokea barabarani imesababishwa na uzembe wa dereva kukimbia kwa mwendo kasi akiwa hajafunga mkanda, lakini mtu mwingine hapohapo akalitazama tukio na kutoa jibu tofauti kabisa ambalo pengine halikutegemewa.
Baba amewahi kunifundisha kwamba japokuwa watu wa namna hii huwa wanachekwa au kuzomewa na kuonekana wanaishi kwenye ulimwengu wa ndoto, lakini wao ndiyo huwa sahihi kwa sababu wanautazama ulimwengu kwa jicho tofauti na watu wengine wote.
Ndicho kilichotokea mle mahabusu, wakati watu wote wakilichukulia tukio la yule mahabusu kudai kule ndani kuna wachawi kisha akaanza kuporomosha matusi, wengi walimuona kama mlevi tu lakini mimi nilimtazama kwa jicho tofauti.
Hata uliposikika ule msonyo na watu kuanza kumtuhumu kwamba anawavurugia usingizi wao, mimi nilikuwa nikiamini kwamba hakuutoa yeye na alichokuwa akikisema kwamba mle ndani kulikuwa na wanga, ulikuwa ni ukweli mtupu.
“Sikilizeni, sikilizeni,” alisema yule mahabusu, kwa msaada wa mwanga hafifu uliokuwa ukipenya kutokea nje, nilimuona akiinua kichwa chake juu kutazama darini, lakini kelele za mahabusu wengine zikamfanya ashindwe kusikia alichokuwa akitaka kukisikia.
“Au naye ana nguvu kama mimi?” nilijiuliza kwa sababu wakati akiwataka watu wote watulie ili wasikie, ni kweli juu ya bati kuna mtu alikuwa akitembea kwa vishindo kabisa kisha naye akasikika akidondokea ndani ya ile mahabusu.
Baada ya hapo, vilianza kusikika vishindo vya watu wakirukia mle mahabusu mfululizo, nikawa natetemeka nikiwa sijui nini kitatokea maana kama unavyojua, milango ya mahabusu huwa muda wote imefungwa na haiwezekani ikafunguliwa kwa muda ule. Nilichokuwa nakiomba, ni wachawi hao wasije wakawa wamekuja kwa shari kama ilivyotokea kwangu na safari hii, nilijifunza kuufyata mkia, sikutaka kuzungumza chochote zaidi ya kuzidi kukodoa macho yangu gizani kama nitaona kitu chochote.
Nilishangaa mfuko wa suruali yangu ukianza kutetemeka kama ndani kulikuwa na kitu ‘kinacho-vaibreti’, sikukumbuka kama niliweka kitu chochote mfukoni na hata kama ni simu, wala sikuwa nikimiliki baada ya baba kunipokonya ile niliyopewa na yule dada ambaye ndiye aliyesababisha muda huo nikawa nyuma ya nondo.
Kwa hofu kubwa niliingiza mkono mfukoni huku nikiwa bado nimekodoa macho, nikagundua kwamba kulikuwa na kitu kwenye mfuko wangu ambacho sikuwa najua ni kitu gani.
Mbaya zaidi, sikujua ni nani aliyekiweka kwenye mfuko wa nguo yangu kwa sababu wakati naingizwa na wale askari, waliniambia pale kaunta nitoe kitu chochote nilichokuwa nacho mfukoni na wala sikuhitaji kujisachi kwa sababu nilikuwa najua sina chochote.
Cha ajabu, nilipokigusa kitu hicho tu, kiliacha kutetemeka lakini yote tisa, kumi ni kwamba nilianza kuona vitu vya ajabu mno. Japokuwa mle ndani kulikuwa na giza, niliweza kuwaona watu wote vizuri, mpaka sura zao utafikiri ilikuwa mchana, ila tofauti yake ni kwamba hakukuwa na mwanga wenye uangavu kama wa mchana bali ulifanana kwa mbali na nuru ya mbalamwezi.
Kwa wale tuliokulia vijijini nadhani wanaelewa vizuri usiku wa mbalamwezi unavyokuwa, yaani unaweza kusema ni mchana kabisa kwani vitu vyote vinaonekana japo siyo vizuri kama vile nilivyokuwa naona mimi.
Nilianza kuwatazama mahabusu wenzangu mmoja baada ya mwingine maana kama unavyojua, niliingizwa giza likiwa limeshaingia na kwa sababu mle ndani hakukuwa na taa, watu pekee niliowaona vizuri ni wale waliokuwa jirani na mimi.
Cha ajabu, wakati nikiendelea kuwatazama mahabusu hao ambao wengi walishaanza kusinzia kutokana na uchovu, niligundua kwamba kulikuwa na watu wengine wasio wa kawaida mle ndani, nao wakiwa wamejichanganya na mahabusu lakini tofauti yao ilikuwa moja.
Karibu wote walikuwa na macho mekundu sana na walikuwa wakinitazama kama wanaosubiri kuona nitafanya nini lakini kubwa, wote walikuwa watupu kabisa. Nilipopiga jicho harakaharaka na kujaribu kuwahesabu, walikuwa kama saba hivi, tena wengine wawili walikuwa ni wanawake na kama unavyojua mahabusu huwa hawachanganywi wanawake na wanaume.
Wote waliacha kila walichokuwa wanakifanya, wakawa wananitazama kwa macho makali. Sikuelewa nini hasa kimetokea, wakati nikiendelea kuwatazama vizuri kwa mara ya pili, kuna jambo moja lilinishtua mno mpaka nikajikuta nimetoa mkono mfukoni, giza likarudi kama lilivyokuwa mwanzo.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...