ILIPOISHIA:
Kitu cha mwisho nilichokumbuka, wakati
nataka kufumbua macho nilimuona yule mwanamke aliyekuwa kwenye usukani,
akikunja usukani ghafla kama aliyeona kitu cha hatari mbele na sasa anataka
kukikwepa, ndipo kikafuatia kile kishindo.
“Nenda haraka, hakikisha unamtoa mtoto
kwenye gari na kuja naye hapa, pale kwenye gari ulipomtoa utaweka hiki,”
alisema baba huku akinipa kipande cha mgomba.
SASA ENDELEA...
“Nikikamatwa je?”
“Nenda, hakuna mtu yeyote atakayekukamata
wala kukuona, usiongee chochote na mtu yeyote, hata wakikusemesha usijibu,”
alisema baba. Basi huku nikitetemeka, nilitoka na kile kipande cha mgomba,
nikatembea harakaharaka mpaka pale barabarani.
Lile gari dogo lilikuwa limepata ajali
mbaya na kupinduka, matairi yakiwa juu, likiwa limegeukia kule lilikotokea. Kwa
mtu yeyote lazima angejiuliza sana kilichosababisha ajali hiyo kwa sababu
kwanza lilikuwa ni eneo la tambarare na hakukuwa na kona wala tuta lolote.
Damu zilikuwa zimetapakaa kuanzia
barabarani mpaka kando ya barabara, pale gari hilo lilipokuwa limepinduka.
Ilibidi nifanye kile nilichoambiwa kabla watu hawajaanza kujaa. Niliinama
kwenye upande aliokuwa amekaa yule mtoto, nikakitingisha kioo ambacho
kilishapasuka kwa sehemu kubwa, kikamwagika chote kwenye lami.
Nikaingiza mikono na kumvuta mtoto huyo
aliyekuwa amebanwa pale kwenye siti, kwa kuwa nilikuwa na nguvu za kutosha,
nilifanikiwa kumtoa, nikamlaza barabarani kisha nikachukua kile kipande cha
mgomba na kukirudishia palepale nilipomtoa yule mtoto, kama baba
alivyonielekeza.
Nilipomaliza, nilisimama, mapigo ya moyo
wangu yakizidi kunienda mbio kuliko kawaida, nikageuka kutazama pale nilipokuwa
nimemlaza yule mtoto. Cha ajabu, niliwaona watu wengine kama wanne hivi, nao
wakiwa wanamtazama yule mtoto kama wanaoshauriana kama wamchukue au la.
Nilipowatazama vizuri watu hao, hasa
maeneo ya usoni, niligundua kwamba hawakuwa binadamu wa kawaida, nikaona
wanataka kunizidi ujanja. Kwa hasira nilipiga kishindo kwa nguvu kwenye lami,
wote wakashtuka huku wakinitazama kwa woga, wakaanza kurudi kinyumenyume.
Ishara ya kupiga kishindo chini,
alinifundisha baba tukiwa bado kule Chunya lakini aliponiambia kipindi hicho,
alisema kwamba eti waganga ndiyo huitumia kuwashtua wachawi ambao mara nyingi
wanapofanya mambo yao, huwa wanaamini hakuna anayewaona kwa hiyo ukipiga mguu
wa kushoto chini, huwafanya waelewe kwamba kumbe umewaona.
Walipokuwa wanarudi nyuma, na mimi
nilipata nafasi ya kumnyanyua yule mtoto aliyekuwa akitapatapa kama anayeelekea
kukata roho, damu nyingi zikimtoka mdomoni na puani. Cha ajabu, licha ya kwamba
sehemu aliyokuwa amekaa ilikuwa imebondeka vibaya, hakuwa na jeraha lolote
zaidi ya kuvuja damu kwa wingi.
Hata sijui ujasiri niliupata wapi,
nilimbeba begani, kiumri alikuwa na kati ya miaka sita au saba, mtoto wa kike
mzuri, akiwa amevalia sare za shule kuonesha kwamba alikuwa ametoka shuleni.
“Pole kwa ajali, tunaomba tukusaidie
kumbeba,” alisema mmoja kati ya wale watu, kwa sauti iliyokuwa ikisikika kama
mwangwi, nikamkata jicho la ukali bila kumjibu chochote kisha nikazamia kule
vichakani, nikawa nakimbia kuelekea pale nilipowaacha baba na baba yake Rahma.
“Safi sana,” alisema baba na kuungwa
mkono na baba yake Rahma, wakawa wananipigia makofi kunipongeza.
“Mlaze hapo kwenye hayo majani ya mgomba
kisha rudi tena eneo la tukio katoe ile mizizi yote ya mtunguja uliyoifunga, si
unakumbuka mahali ulipoifunga? Ukiiacha magari mengine yataendelea kupata ajali
hovyo,” alisema baba huku akinipa kisu, harakaharaka nikarudi mpaka eneo la
tukio ambapo nilikuta watu wameongezeka lakini nilipowatazama vizuri,
niligundua kwamba wote walikuwa ni wa jamii moja.
Walichokuwa wanakifanya kilinishangaza
sana, wengine walikuwa wakilamba damu pale kwenye lami bila hofu hata kidogo
huku wengine wakiwa bize kutaka kumtoa yule mwanamke aliyekuwa akiendesha gari
hilo ambaye ilionesha amejeruhiwa vibaya.
Nilipofika, nilifanya kama nilivyofanya
awali, nikapiga mguu chini kwa nguvu, wote wakatawanyika kisha nikaanza kukata
zile dawa nilizokuwa nimezifunga pande zote mbili za barabara. Nilivuka
barabara, nikakata ya kwanza, nikarudi pale katikati, nikaiokota ile nyingine
ambayo ilikuwa imelowa damu kwani pale ndipo gari lilipopatia ajali kabla ya
kubinuka na kwenda kugota kando ya barabara.
Niliokota ile nyingine iliyokuwa upande
ule ilipotokea ajali, nikaenda kumalizia na ile ya mwisho iliyokuwa upande ule
waliokuwepo baba na baba yake Rahma, cha ajabu, nilipomalizia kukata ile ya
mwisho tu, wale watu waiokuwa wamejaa eneo lile, walianza kutokomea mmoja baada
ya mwingine, wengine nikawa nawasikia wakiachia misonyo mikali. Sikuwajali kwa
sababu hata mimi nilitaka kuwahi kuondoka eneo hilo kwani ningeweza kukamatwa
ikawa balaa.
Bado hakukuwa na gari wala chombo
chochote cha usafiri kilichopita eneo hilo, nikatokomea vichakani na kurudi
pale nilipokuwa nimewaacha akina baba, mwili wangu ukiwa umelowa damu.
Waliendelea kunipongeza, baba akaniambia natakiwa kumalizia kazi yangu.
“Kivipi baba?” nilimuuliza huku nikihema
kwani niliamini kazi nzito nimeshaimaliza.
“Inabidi tuelekee kilingeni ukamkabidhi
Mkuu alichokuagiza, tukifika itabidi umtenganishe kichwa na kiwiliwili kwa
kutumia hicho kisu nilichokupa, hakikisha hizo dawa unazitunza vizuri,” alisema
baba na kunifanya nishtuke kupita kawaida.
“Nimchinje?” nilihoji macho yakiwa yamenitoka
pima.
“Sasa kazi kubwa umeshaifanya unaogopa
nini?” alisema baba huku akiinuka, baba Rahma naye akainuka na wote tukasogea
mpaka pale yule mtoto alipokuwa amelazwa juu ya majani ya migomba, akionesha
kuwa kwenye hatua za mwisho kabisa za uhai.
Baba alinipa ishara kwamba tuiname pale
yule mtoto alipokuwa amelala, mkono mmoja akamshika yule mtoto, mwingine akampa
baba yake Rahma ambaye naye mmoja alimshika yule mtoto na mwingine akanipa
mimi, na mimi nikafanya hivyohivyo.
“Usifumbue macho mpaka tutakapokwambia,
dawa zako zote si unazo maana ndiyo tunaondoka hivyo,” alisema baba,
nikatingisha kichwa kama ishara ya kukubali, akahesabu mpaka tatu, sote
tukafumba macho.
Baba na baba yake Rahma walianza kuongea
maneno fulani nisiyoyaelewa kwa kurudiarudia, wakawa ni kama wanaimba mapambio
ya kutisha, mara upepo mkali ukaanza kuvuma kwa nguvu, sikuelewa tena
kilichoendelea mpaka niliposikia nikitingishwa begani.
“Tumeshafika, mbona unazubaa,” alisema
baba, kufumbua macho, nikashtuka nipo eneo lingine tofauti kabisa, nikageuka
huku na kule, kumbukumbu zangu zikanijia kwamba hapo ndiyo pale ambapo usiku
uliopita tulikuwa tumekusanyika. Nilitazama huku na kule, hata sura za watu
karibu wote zilikuwa zilezile, nikamuona mkuu amekaa katikati kabisa, huku
akiwa anajitafuna mapengo kama wanavyofanya watu waliozeeka sana.
Japokuwa huko kote tulikotoka nilikuwa
nimevaa nguo zangu, nilishangaa kujikuta eti nimevaa kaniki kama ilivyokuwa
jana yake, kila kitu kilikuwa ni zaidi ya maajabu.
“Mpeleke mpaka pale kwenye kile kichanja
ulichokuwa umelazwa jana kisha sikiliza maelekezo kutoka kwa Mkuu,” baba
aliniambia kwa sauti ya chini, yeye na baba Rahma wakaenda kukaa kule pembeni walikokuwa
wamekaa wale watu wengine na kutengeneza duara.
Nilimbeba yule mtoto ambaye kadiri muda
ulivyokuwa ukizidi kuyoyoma ndivyo mapigo yake ya moyo yalivyokuwa yakizidi
kufifia huku akianza kulegea, nadhani ni kwa sababu ya kupoteza damu nyingi.
Watu wote walikua kimya kabisa, nikambeba mpaka pale nilipokuwa nimelazwa jana
yake, kwenye kitanda kilichotengenezwa kwa miti.
Mkuu alisimama na kusogea pale kwenye
kile kitanda, akanionesha kwa ishara kwamba nimgeuzie kichwa upande wa
Magharibi, nikafanya hivyo kisha akasogea na kumgusa kifuani, nadhani alitaka
kuhakikisha kama bado hajakata roho.
Nilimuona akitingisha kichwa kisha
akainua mikono juu, watu wote wakapiga makofi kwa wingi, sikuelewa lakini
nadhani ilikuwa ni kama sehemu ya kunipongeza. Watu wote walipotulia, bila
kusema chochote, alinionesha ishara kwamba niendelee, nikakumbuka maneno ya
baba kwamba akinipa ishara, maana yake anataka nimchinje mtoto huyo.
Tangu nizaliwe, sikuwahi kuchinja hata
kuku tu, achilia mbali ndege tuliokuwa tukiwawinda kule kijijini kwetu lakini
sasa eti nilikuwa natakiwa nimchinje binadamu, mtoto asiye na hatia yoyote ili
nifaulu mtihani na kuwa mwanachama kamili, nilijikuta nikitetemeka kuliko
kawaida.
Nilikichomoa kisu pale kiunoni
nilipokiweka, mikono ikawa inatetemeka kuliko kawaida, nikawa namtazama mtoto
yule usoni, nilijikuta nikiingiwa na huruma isiyo ya kawaida.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
Lini inaendelea au nawezaje kuipata yote bro
ReplyDelete