ILIPOISHIA:
“Wewe sasa hivi una mambo ya kikubwa,
hutakiwi kuwa unachanganyikana na wenzako, inabidi uanze kukaa na sisi baba
zako, vuta kiti kaa hapa,” alisema baba, akawa ametibua shoo nzima, nilitaka
kutoa visingizio lakini hakutaka kusikia chochote kutoka kwangu, ikabidi nikae
na kujiinamia, wote wakawa wananitazama.
SASA ENDELEA...
“Una matatizo gani?” baba aliniuliza
baada ya kuniona nikiwa nimekaa huku uso wangu nikiwa nimeukunja.
“Unajua hata sisi wote unaotuona hapa,
kuna kipindi tulikuwa kama wewe, sote tulikuwa vijana hapa na tulipitia yote
unayoyapitia, kwa hiyo usitake kujifanya mjanja, umenisikia?” baba alisema kwa
msisitizo.
“Na nyie mlipitia mauzauza kama yangu?
Kwa nini kila siku huniambii ukweli mimi ni nani?” kwa mara ya kwanza nilimpandishia
baba sauti mbele ya baba yake Rahma, nikaona wameacha kucheza karata, wakawa
wanatazamana kisha wote wakanigeukia.
“Sisi ni baba zako, hutakiwi kuzungumza
kwa namna hiyo, umesikia mwanangu,” alisema baba yake Rahma huku akinipigapiga
begani. Tofauti kati ya baba na baba yake Rahma, yeye alikuwa na busara na
mpole lakini baba yeye alizoea kufokafoka tu.
“Hapana mimi nimechoka, kila siku
nikimuuliza baba aniambie ukweli hataki, mauzauza yanazidi kunitokea kila siku,
mambo ya ajabu yananikumba mimi tu, mbona ndugu zangu hakuna anayepata shida
kama mimi,” nilisema kwa uchungu huku machozi yakianza kunilengalenga.
Baada ya kusema ya moyoni, niliegamia
meza na kujilaza huku machozi yakinitoka, kiukweli nilikuwa na dukuduku kubwa
sana moyoni. Hakuna kitu ambacho kilikuwa kikinikasirisha kama kitendo cha baba
kuwa ‘ananikontroo’ kama roboti bila kunieleza ukweli uliokuwa nyuma ya maisha
yangu.
“Najua kwamba mimi ni mwanaye, tena
anayenipenda kuliko watoto wengine wote lakini kwa nini nipo tofauti? Kwa nini
haniambii ukweli?” nilisema kwa kulalama, machozi yakiwa yanaendelea kunitoka.
“Kama anaweza kufikiria haya maana yake
ni kwamba ameshapevuka kiakili, nafikiri ni muda muafaka wa yeye kuujua
ukweli.”
“Hapana, bado hajakua huyu, ana mambo ya
kitoto sana, mimi ndiyo namjua,” baba alisema, kauli ambayo ilinifanya niinuke
pale mezani na kumkodolea baba macho. Yaani kumbe alikuwa anashindwa kunieleza
ukweli kwa kipindi chote hicho kwa sababu tu alikuwa anahisi kwamba mimi bado
nina akili za kitoto?
Kauli ile ilinifanya nijiulize maswali
mengi yaliyokosa majibu. Kwa nini baba alikuwa ananiona mimi kama bado mtoto
wakati tayari nilishapevuka na kuwa mwanaume kamili? Hata Rahma aliniambia
kwamba mimi ni kidume cha mbegu, achilia mbali Isri aliyekuwa akinisifia sana.
Na kama ni hivyo, mbona pale aliponiita alisema nimeshakua mkubwa kwa hiyo
natakiwa kukaa nao?
“Kwa nini unaniona bado mdogo?”
“Kwa sababu huwezi kuelewa kitu kwa
kuelezwa mara moja. Kila unachokatazwa kufanya wewe unafanya,” alisema baba na
kurudia kauli yake kwamba hawezi kuniamini kwa asilimia mia moja mpaka
nitakapomuonesha ukomavu wangu wa akili.
Kiukweli kwa kipengele hicho baba
alikuwa amenishinda kwa pointi na udhaifu wangu mkubwa nilikuwa nimeuonesha
kwenye suala zima la mapenzi. Nakumbuka tulianza kutofautiana na baba baada ya
kukutana na Isri kwenye basi, akawa ananikataza kuwa naye karibu lakini
nikampuuza.
Pia hata tulipofika kwa akina Rahma,
mara kadhaa alishagundua kwamba tulikuwa na ukaribu usiofaa na akanikataza kwa
msisitizo kwamba nisijaribu kukutana kimwili na Rahma, tena mpaka wakatumia
kigezo kwamba sisi tulikuwa ndugu lakini bado tuliangukia dhambini, tena siyo
mara moja.
Kubwa zaidi, hata hapo tulipokuwa
tukizungumza, licha ya baba kunikataza kwamba endapo nitakutana kimwili tena na
Rahma basi atakufa, kama wasingeniita na kunizuia, pengine muda huo ningekuwa
‘nikilitafunilia mbali tunda la mti uliokatazwa’ na Rahma.
Kama kigezo hicho pekee ndicho kilikuwa
kinaonesha kwamba mtu amekuwa mkubwa, basi ni kweli nilikuwa nimefeli mtihani
uliokuwa mbele yangu, nikawa mdogo kama ‘piriton’.
“Eti ni kweli anachokisema baba yako?”
aliniuliza baba yake Rahma, nikakosa cha kujibu.
“Unajua kwa jinsi sisi baba zako
tulivyo, na pengine wewe ukija kupata nafasi hiyo, hakuna kitu ambacho
kinaheshimika kwenye jamii yetu kama utii. Ukiambiwa jambo ni lazima ufanye
vilevile ulivyoambiwa na si vinginevyo, kosa dogo tu linaweza kusababisha
matatizo makubwa mno ndiyo maana baba yako anakuwa mkali,” alisema baba yake
Rahma.
Kauli hiyo ilinifanya nijiulize maswali
mengine mengi zaidi. Aliposema ‘jamii yetu’, baba yake Rahma alikuwa
akimaanisha nini? Nilianza kupata picha kwamba huenda naye alikuwa anafahamu
kila kitu kinachoendelea na kama alikuwa jamii moja na baba, basi moja kwa moja
na yeye alikuwa akishughulika na mambo kama yale ya baba.
Tangu tumefika, baba yake Rahma hakuwahi
kutoka kwamba labda anaenda kazini au kwenye biashara zake, muda wote alikuwa
nyumbani tu lakini alikuwa na maisha ya hali ya juu sana. Nikiwa bado naendelea
kujiuliza maswali mengi, baba yake Rahma alinisogelea.
“Baba yako anasema hakuamini kwa sababu
bado una akili za kitoto lakini mimi nikikutazama nakiona kitu kikubwa sana
ndani yako, tucheze dili?” aliniuliza kwa sauti ya chini huku akinikonyeza kwa
jicho moja. Sikujua ni dili gani ila kwa sababu nilikuwa nataka kujua ukweli wa
maisha yangu, nilitingisha kichwa kuonesha kumkubalia.
“Inatakiwa mimi na wewe tukazungumze
lakini hatuwezi kuzungumzia humu ndani, inabidi tutoke nje! Lakini hapohapo,
baba yako ameniambia kwamba kuna ‘madhambi’ mengine umeyafanya kiasi kwamba
wewe na yeye hamuwezi kutoka mpaka giza liingie, ni kweli au si kweli?”
“Ni kweli.”
“Sasa mtihani wa kwanza, unatakiwa
ukazivunje hizo nguvu zako za giza ulizozitega pale mlangoni.”
“Mimi sina nguvu zozote za giza wala sijatega
chochote...” nilimkatisha lakini alinitazama usoni na kunikumbusha kwamba utii
ni jambo muhimu sana, nikaufyata mkia.
“Unauona ule mlango, inatakiwa utembee
kinyumenyume mpaka pale, ukiukaribia, unaugeukia lakini unatakiwa kufumba
macho, kisha unakojoa mkojo wa kutosha kulowanisha eneo lote la mlango,”
alisema baba yake Rahma, macho yakanitoka kama mjusi aliyebanwa na mlango.
“Hakuna kitu kinachoweza kuvunja na
kumaliza kabisa nguvu za giza kama mkojo, haya fanya kama nilivyokwambia,”
alisema baba yake Rahma. Ama kweli huo ulikuwa mtego mkali sana kwangu, yaani
nikakojoe mlangoni, tena mahali ambapo watu wote waliokuwa sebuleni wangeweza
kuniona?
Sikujua ndugu zangu watakichukuliaje
kitendo hicho, wala sikujua Rahma na wadogo zake nao watanichukuliaje ila kwa
sababu nilikuwa na shauku ya kuujua ukweli, nilipiga moyo konde.
Wakati nikijiandaa kwenda, nilimsikia
Rahma akiimba huku akitoka koridoni na kwenda kule sebuleni, nadhani
alishachoka kusubiri na kuamua kunifuata, mtihani ukazidi kuwa mgumu. Ningemjibu
nini Rahma endapo angeniuliza kwa nini nakojoa mlangoni wakati choo kipo, tena
siyo kwamba nimelewa au naumwa, nina akili zangu timamu kabisa!
Baba na baba yake Rahma walikuwa
wametulia wananitazama huku nikimuona baba uso wake ukionesha ishara kama
anayesema ‘hawezi huyu, akili zake bado za kitoto’. Niliamua kujilipua,
nikasema liwalo na liwe, nilisogea usawa wa mlango, nikageuka na kuupa mgongo,
nikaanza kutembea kinyumenyume kuuelekea kisha nikafumba macho, nilipoukaribia,
niligeuka, macho nikiwa nimeyafumba.
Nilifungua zipu kisha nikaanza kufanya
kama vile nilivyoelekezwa. Nikiwa naendelea na kitendo kile cha aibu na cha
aina yake, nilisikia watu wote waliokuwa sebuleni wakishtuka, nadhani waliniona
nilichokuwa nakifanya, sikuwajali, nikaendelea kuumwaga, mara kilisikika
kishindo kikubwa ambacho kilinifanya nishindwe kuendelea kufumba macho,
nikayafumbua.
“Mungu wangu!” nilisema kwa sauti ya
juu.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment