ILIPOISHIA:
“Nakuapia kama
ningekutana na wewe kabla ya Raya, huenda wewe ndiyo ungekuwa mpenzi wangu na
si ajabu ningeshakuwa nimekuoa, naogopa kukueleza ukweli wa moyo wangu kwa
sababu mtu mwenyewe unakuwa mkali kwangu,” nilizidi kumseti kwa maneno matamu,
akashindwa kujizuia na kuniinamia pale kitandani, akanibusu kwa hisia za hali
ya juu na kunikumbatia bila kujali kwamba anaweza kunitonesha tena jeraha langu
la kifuani.
SASA ENDELEA...
“Hata
mimi nakupenda sana Jamal lakini nilikuwa nashindwa namna ya kukufikishia
ujumbe, ahsante kwa kuzielewa hisia zangu,” alisema Shamila huku akiwa
amenikumbatia, akaendelea kunibusu sehemu mbalimbali za mwili wangu.
Niliona
jinsi kitendo changu cha kuingiza masuala ya mapenzi kilivyomfurahisha,
tukaendelea kupiga stori mbalimbali huku mara kwa mara akinikumbatia na
kunibusu, na mimi nikawa nazidi kumsifia kwani miongoni mwa ‘maradhi’ ya
wanawake, ni kupenda kusifiwa! Dalili za kutimia kwa nilichokuwa nakitaka
zikaanza kuonekana waziwazi.
Hatukuwa
nesi na mgonjwa kama ilivyokuwa awali, sasa tukawa zaidi ya hapo, nikamuona
Shamila akizidi kuninyenyekea, kunipa huduma bora zaidi na muda mwingi akiwa
pembeni ya kitanda changu.
Sikujihisi
tena kama niko hospitali, ungeweza kusema nipo tu nyumbani. Japokuwa siku hiyo
Shamila alikuwa na ‘shift’ ya kutoka saa kumi na mbili jioni, hakutaka
kuondoka, akaniambia kwamba ataenda kuongea na kiongozi wao ambadilishie zamu,
alale tena kazini mpaka kesho yake ndiyo arudi nyumbani.
“Nimechoka
kukaa hospitali mpenzi wangu, naona kama kuna mambo ya muhimu yanazidi
kuchelewa, sijui utanisaidieaje?” nilimwambia Shamila, akiwa amekaa pembeni
yangu, muda wote mikono yake ikiwa mwilini mwangu.
“Kwani
unataka kwenda kufanya nini Jamal, mi nakuonea huruma bado hujapona vizuri.
Kuna kazi ya muhimu inatakiwa nikaifanye.”
“Kwa
nini usiniagize mimi nikakufanyie?”
“Hapana,
ni lazima niifanye mimi mwenyewe labda kama utanisindikiza tu.”
“Lakini
bado hujapona.”
“Kwani
haiwezekani nikatoka asubuhi halafu baadaye nikarudi?”
“Sasa
madaktari wakipita ‘raundi’ na kukukosa wodini itakuwaje? Si unajua wewe bado
unatakiwa kuwa chini ya uangalizi maalum na ndiyo maana umeletwa huku kwenye
wodi ya peke yako mpenzi?” alisema Shamila.
Kimsingi
hakukuwa na uwezekano wowote wa mimi kutoka kirahisi hospitalini lakini nikaona
niendelee kumbembeleza Shamila. Kwa kuwa sasa nilikuwa mpenzi wake na
nilishaanza kumpa ahadi kemkemu kuhusu maisha yetu ya kimapenzi yatakavyokuwa,
nilifanikiwa kumteka akili.
“Basi
kesho inabidi mimi asubuhi nisiondoke mapema, nitasubiri mpaka madaktari
wakishapita raundi wodini tu, tutaondoka wote mpaka nje ya hospitali.
Nitawaambia walinzi umeandikiwa vipimo ambavyo hapa hospitalini havipo,”
alisema Shamila, nikaachia tabasamu pana.
Waliosema
mapenzi yana nguvu hawakukosea. Shamila alikuwa tayari kuhatarisha kazi yake
kwa sababu ya kutetea penzi! Basi tulifikia muafaka, ukaribu wa mimi na Shamila
ukazidi kuongezeka utafikiri tulifahamiana miaka mingi iliyopita.
Hata
yale masihara aliyokuwa ananiletea awali, nikaona yamepungua sana, muda mwingi
akawa anapenda tuzungumzie kuhusu penzi letu. Unajua wanaume wengi huwa
wanafanya makosa sana kushindwa kufahamu namna ya kuishi na mwanamke ambaye
anaonesha hisia za kukupenda.
Tofauti
na wanaume ambao akimpenda mtu huweza kumwambia moja kwa moja kwa ujasiri,
wanawake huwa hawana ujasiri huo labda wachache. Kama mwanamke anakupenda, kuna
baadhi ya dalili atakuwa anakuonesha akiamini ukiziona, utajiongeza mwenyewe
kichwani.
Ukishaziona
dalili hizo, hata kama huna malengo ya kuanzisha naye uhusiano wa kimapenzi,
kuna namna ya kumuonesha kwamba umemuelewa hata kabla hajatamka chochote na
kwamba unaziheshimu hisia zake.
Ikitokea
anakuonesha dalili fulani lakini wewe unaendelea kujifanya kipofu, kihulka
wanawake ni wepesi sana wa kujisikia vibaya, atahisi umemdharau, ataamini
hajakuvutia ndiyo maana umeshindwa kuelewa hisia zake na mwisho utashangaa
anaanza kujitenga mbali na wewe na kukujengea chuki.
Kwangu
mimi niliamua kupiga ndege wawili kwa mpigo kwa Shamila, japokuwa kiukweli
hakuwepo kwenye mawazo yangu kwa sababu tayari nilishaamua kumkabidhi moyo
wangu Raya, niliamua kumuonesha kwamba nampenda sana kwa sababu mbili; kwanza
sikutaka ajisikie vibaya kwamba ananionesha ishara kwamba ananipenda lakini
nampuuza lakini kubwa, nilitaka anisaidie kwenye ile kazi kubwa iliyokuwa
inanisubiri.
Malengo
yangu yalianza kutimia haraka kuliko hata nilivyotegemea kwa sababu tayari
jambo moja muhimu lilikuwa likienda kutimia; kwenda kuonana na Firyaal, mdogo
wake Shenaiza ambaye angenipa bahasha yenye taarifa kuhusu baba yao na biashara
hatari alizokuwa anazifanya.
Usiku
huo Shamila wala hakwenda kukaa kwenye chumba cha manesi kama utaratibu ulivyo,
muda wote alikuwa na mimi wodini na hata muda wa kulala ulipofika, alisogeza
kitanda tupu kilichokuwa pembeni karibu kabisa na kitanda changu, akajilaza juu
yake huku tukiendelea kupiga stori za hapa na pale mpaka nilipopitiwa na
usingizi.
Kesho
yake asubuhi, Shamila aliwahi kuamka na kuniamsha na mimi, akanisaidia
kubadilisha shuka pale kwenye kitanda changu, akaniandalia mswaki na taulo na
kuniambia inatakiwa nikaoge ili nipate nguvu. Akanisisitiza kwamba nihakikishe
maji hayagusi kwenye jeraha langu.
Nilijikaza
na kuamka, nikaenda bafuni ambako nilioga kwa mara ya kwanza tangu nirudiwe na
fahamu zangu, nikajisikia mwili ukipata nguvu kubwa, nikarudi wodini ambako
nilikuta Shamila akiandaa kahawa, niliporudi kitandani tukakaa pamoja na kuanza
kunywa, sote tukachangamka.
Baadaye
madaktari walipita kwa ajili ya kutazama maendeleo yangu, wakafurahishwa sana
na jinsi nilivyokuwa nikipona haraka, wakawa wanampongeza Shamila kwamba
amefanya kazi yake ipasavyo ndiyo maana nilikuwa napona haraka, wote
tukafurahi.
“Bila
shaka sasa unaweza kutusimulia kuzimu kulivyo maana naamini ulifika na kukutana
na mtoa roho ila akaamua kukusamehe tu,” alisema yule daktari kijana aliyezoea
kunitania, wote tukacheka.
Nikaandikiwa
dawa nyingine za kukausha jeraha langu kisha wakaondoka na kuendelea kuwatembelea
wagonjwa waliokuwa wamelazwa kwenye wodi nyingine, Shamila akanitazama, macho
yetu yakagongana, nikamuona akishusha pumzi ndefu na kunisogelea huku
akitabasamu.
“Sasa
itabidi uwe makini sana, mtu yeyote akituuliza tunaelekea wapi utamjibu kwamba
nakufanyisha mazoezi, sawa?” Shamila aliniambia kwa sauti ya mamlaka,
nikatingisha kichwa kuonesha kukubaliana naye.
Tukajiandaa
kisha akachukua mkoba wake, tukatoka taratibu huku tukiendelea kupiga stori za
hapa na pale. Kwa kuwa Shamila alikuwa akifahamika hospitalini hapo, hatukupata
usumbufu wowote, tukatoka mpaka nje kabisa ya geti bila kuulizwa chochote na
mtu yeyote.
Tukaenda
mpaka kwenye maegesho ya teksi, madereva wakatudaka juujuu na kuanza
kutukaribisha, tukaingia kwenye teksi moja kisha Shamila akanigeukia.
“Tunaanzia
nyumbani kwangu, sawa?”
“Hapana,
naomba kwanza twende Kurasini halafu ndiyo tutaenda kwako, niko chini ya miguu
yako nakuomba,” nilimwambia, akanitazama kwa macho yake mazuri na kutingisha
kichwa kuonesha kukubaliana na nilichokisema.
“Naomba
tupeleke kwenye Mtaa wa Mama Zayumba, Kurasini,” Shamila alimwambia dereva
huyo. Alishakuwa anaujua mpaka mtaa kwa sababu aliniuliza na nikamuelekeza kama
na mimi nilivyokuwa nimeelekezwa na Shenaiza, safari ikaanza.
Safari
iliendelea na hatimaye tukawasili kwenye mtaa huo ambao ndiyo ilikuwa mara
yangu ya kwanza kufika, tukafuata ramani aliyonipa Shenaiza na hatimaye
tukatokezea kwenye jengo la kisasa la ghorofa tatu, likiwa na geti kubwa
lililozungushiwa nyaya zinazopitisha umeme upande wa juu huku kukiwa na mlinzi
mwenye silaha.
Tukasogea
na teksi mpaka jirani kabisa na lile geti, yule mlinzi akamuonesha dereva
ishara ya kusimama kisha akatusogelea na kutusabahi,mimi nidyo nikawa
mzungumzaji mkuu.
“Nikajitambulisha
kwamba ni rafiki yake Shenaiza na kuna kitu alikuwa amenituma kuja kukichukua
kwa mdogo wake, Firyaal. Kwa jinsi nilivyompa maelezo, wala hakututilia
mashaka, hasa alipomuona pia Shamila akiwa amevaa nguo zake za kazini, akajua
tumetoka kuonana na Shenaiza hospitalini.
Nikamuona
akiingia kwenye chumba cha walinzi na kushika mkonga wa simu, akawa anazungumza
na upande wa pili kisha akarudi pale tulipokuwa tumepaki gari na kutuambia
tusubiri hapohapo. Tulikaa kwa zaidi ya dakika tatu, tukaona mlango mdogo
uliokuwa pembeni ya geti ukifunguliwa, wote tukakazia macho kutaka kuangalia ni
nani aliyekuwa anatoka.
Je,
nini kitafuatia? Usikose Jumatatu kwenye Championi Jumatatu.
No comments:
Post a Comment