ILIPOISHIA:
Nikiwa bado nashangaa, mwili ukiwa
unatetemeka kwa hofu, nilishtukia wale watu wakikimbilia pale kwenye moto na
kujipanga foleni, yule babu akasogea kwenye zile nyama, akawa anagawa, kila
mmoja anapita na kupewa kipande chake kisha anatafuta sehemu ya kwenda kukaa na
kuanza kula. Nilihisi kama nipo ndotoni lakini haikuwa hivyo.
“Hongera, umekuwa sasa,” alisema baba
huku akinikumbatia, akanishika mkono na kunipeleka kwenye foleni, akaniingiza
kwenye foleni.
SASA ENDELEA...
“Hapana baba, siwezi! Siwezi...”
nilisema huku nikitaka kutoka kwenye foleni lakini baba alinishika mkono kwa
nguvu. Nilikuwa natafuta upenyo ili nijitie vidole mdomoni kujitapisha ile
nyama lakini ni kama baba alinishtukia.
Hakunipa upenyo hata kidogo, nikawa
naendelea kutetemeka kwa hofu kubwa, nikiwa sielewi hatima ya yote yale itakuwa
nini. Tofauti na mimi, watu wengine wote waliokuwepo eneo lile, akiwemo baba,
baba yake Rahma na wale watu wengine wote, walikuwa na furaha kubwa ndani ya
mioyo yao.
Kingine kilichonishangaza na kuniacha na
maswali mengi, kila mtu aliyekuwa akifika pale mbele kwa yule babu aliyekuwa
akigawa nyama, akikabidhiwa yake alikuwa akifurahi sana na kwenda kukaa pembeni
na kuanza kuila bila wasiwasi wowote.
Nimewahi kusikia sana kuhusu stori za
watu wanaokula nyama za watu lakini siku zote nilikuwa naona kama ni mambo ya
kutunga, iweje mtu amle mwenzake? Ni hapo ndipo nilipoelewa kwamba kumbe siyo
stori za kusadikika tu bali ni mambo ambayo yapo na yanafanyika kwa wingi.
Nilijiuliza sana, wale waliokuwa
wakiliwa nyama ni akina nani? Walifanya makosa gani mpaka waliwe? Walikuwa
wanaishi wapi na nyama zao zilifikishwaje pale? Je, walikuwa wanaume au
wanawake, wakubwa au wadogo? Sikuwa na majibu.
Foleni ikawa ikazidi kusogea mbele,
mwili wangu ulikuwa na maumivu sehemu mbalimbali, hasa yale maeneo ambayo yule
babu alikuwa amenichanja lakini huwezi amini, kwa jinsi nilivyokuwa na hofu,
wala sikuwa nasikia chochote.
Foleni iliendelea kusogea mbele, hofu
ikazidi kunijaa lakini sikuwa na cha kufanya. Mara nilipata wazo, kwamba
nikifika na kupewa nyama yangu, nijifanye naenda pembeni kuila lakini nikifika
pembeni niitupe na tukirudi nyumbani, nitoroke na kurudi Chunya maana sikuwa
tayari kwa kile kilichokuwa mbele yangu.
Ni kweli mara kadhaa nilijikuta
nikitamani kuzijua mbinu mbalimbali za kichawi, kama kuweza kujilinda kwenye
nyakati za hatari au kumuadhibu anayekuudhi lakini sikuwa tayari kuona nakuwa
sehemu ya jamii hiyo iliyokuwa na mambo ya kutisha kiasi hicho.
Hatimaye zamu yangu iliwadia, yule mzee
mgawaji, huku akijitafuna na damudamu zikiwa zimelowanisha mdomo wake,
alinitazama usoni huku tabasamu pana likiwa limechanua kwenye uso wake.
Kuna kipande alikuwa amekishika mkononi
lakini alipoona ni mimi, nilimuona akikirudisha pale chini palipokuwa na nyama
nyingine nyingi, zikiwa zimewekwa juu ya majani ya migomba, akachaguachagua na
muda mfupi baadaye, aliibuka na mnofu mkubwa wenye damudamu, akanipa huku
akiinamisha kichwa kama ishara ya heshima.
Huku nikitetemeka nilipokea, macho yangu
yakiwa hayatulii, nilikuwa nikilichunguza kwa umakini lile rundo la nyama pale
chini ambalo sasa lilikuwa limepungua sana. Nilichokiona awali ndicho
nilichokiona tena, kulikuwa na miguu iliyokatwa, viganja vya mikono na viungo
vingine vya mwili.
Nikiri kwamba moyo wangu haujawahi
kupatwa na hofu kama niliyoipata siku hiyo na kilichonitisha zaidi, ni pale
nilipogundua kwamba katika rundo lile, kulikuwa na miguu na mikono ya watoto
wadogo kabisa. Maskini... hawakuwa na hatia yoyote!
Baba naye alipewa kipande chake,
akanishika mkono huku akiniongelesha kwa sauti ya chini. Aliniambia kwamba nina
bahati sana kupewa heshima kubwa kama hiyo na mzee huyo ambaye baba aliniambia
huwa wanamuita Mkuu kwa sababu ndiye kiongozi wao wa kanda. Akaniambia kwamba kitendo
cha yeye kuinamisha kichwa chake tu, ilikuwa ni ishara kwamba amenikubali mno.
Hatukwenda mbali, tulikaa chini huku
baba akinielekeza namna ya kukaa. Haukuwa ukaaji wa kawaida, mguu wa kushoto
ulikuwa ukitangulia chini, kisha unakuja wa kulia halafu unakaa juu ya vifundo
vya miguu yote miwili huku ukiwa umeikunja na kutengeneza alama ya V mbili.
Nilijaribu lakini miguu ikawa inaniuma
sana, nilipowatazama watu wengine, wote walikuwa wamekaa kwa mtindo huo na wala
hakukuwa na aliyekuwa akibabaika kama mimi, walikuwa wakiendelea kupiga stori
za hapa na pale huku wakifurahia ‘kitoweo’, baba akaniambia atanifundisha
taratibu.
Lile wazo langu la kwenda kuitupa ile
nyama liliyeyuka kutokana na baba alivyonibana, ambapo muda mfupi baadaye, baba
yake Rahma naye alikuja na kuungana na sisi pamoja na wanaume wengine watatu
ambao sikuwa nawafahamu.
Kwa muda wote huo nilikuwa nikizugazuga
tu kwani kiukweli sikuwa tayari kuila ile nyama ambayo ilikuwa ikichuruzika
damu, mara kwa mara nilikuwa nikiitazama kwa woga, nikitamani hata niirushe
mbali na kupiga kelele kwa hofu lakini haikuwezekana.
“Kula, muda unaenda,” baba aliniambia
kwa kunihimiza, wale watu wengine ambao sikuwa nawafahamu, wakawa wanamuuliza
baba mimi ni nani.
“Ni mwanangu, hamuoni tunavyofanana,”
aliwajibu na wote wakawa wanampongeza kwa hatua ya kunisajili rasmi, wakawa
wananipongeza na mimi wakiniambia kwamba sitajuta kujiunga na jamii yao. Kwa
kuwa wote sasa walikuwa wakinitazama huku wakiendelea kunisifia, ilibidi
nijikaze kiume maana baba alikuwa akinitazama kwa jicho kama la kunidharau hivi
au kuonesha kwamba zile sifa nilizokuwa napewa sistahili.
“Umekua sasa si ndiyo?” baba yake Rahma
aliniambia huku akinipigapiga begani na mkono wake uliokuwa na damu, mdomoni
akiendelea kujitafuna. Nadhani aliongea hivyo kama kunikumbusha kile
tulichokuwa tukitofautiana mara kwa mara na baba, akidai kwamba mimi bado nina
akili za kitoto.
“Ndiyo,” nilimjibu kwa msisitizo,
nikafumba macho na kupeleka ule mnofu mdomoni, nikaziba pua ili nisisikie hata
harufu nikaanza kutafuna huku nikijikaza kisawasawa, sikuwa nataka kuonekana
bado nina akili za kitoto kwa hiyo nilijikuta nikifanya kitu nisichopenda
kukifanya ilimradi tu nimdhihirishie baba na baba yake Rahma kwamba sikuwa
mtoto tena.
Mara kadhaa nilikuwa nikitaka kutapika
lakini mwisho, hatimaye nilifanikiwa kuitia yote tumboni mwangu na kuufanya
mwili wangu usisimke sana.
“Tafuna hii,” alisema baba yake Rahma
huku akinipa vitu kama mizizi fulani hivi, nikavitafuna haraka na kuvimeza. Cha
ajabu, mpaka muda huo, kumbe mimi ndiye niliyekuwa wa mwisho kumaliza ‘shea’
yangu, watu wote walikuwa wameshamaliza na sasa walikuwa wakipiga stori za hapa
na pale.
“Vipi una swali lolote kwa kijana?” baba
yake Rahma alimwambia baba kwa kejeli, nilishaelewa kwa nini amesema vile.
Kwamba kwa sababu baba alikuwa ananiona kama nina akili za kitoto, je alikuwa
na swali lingine lolote baada ya mimi kuonesha kile nilichokionesha pale mbele
yao?
“Umenitoa aibu mwanangu, zawadi
nitakayokupa hautakuja kuisahau maishani mwako,” aliniambia baba akionesha kuwa
na furaha kubwa.
Mara sauti ya kama pembe la ng’ombe
lililopulizwa kwa nguvu ilisikika, watu wote wakainuka walipokuwa wamekaa na
kuanza kujipanga kwa mtindo wa duara kama ilivyokuwa mwanzo.
“Sasa hivi unaenda kukabidhiwa rasmi
nguvu za giza ili uwe kama sisi, naomba ujasiri uliouonesha kwenye kula
uuoneshe hapa pia, nenda pale ulipokuwa umekaa mwanzo,” baba aliniambia huku
akinipigapiga begani kwa upole.
Kwa akili yangu nilijua kwamba tayari
kazi imekwisha, kumbe kulikuwa na kazi nyingine, nikaanza kutetemeka tena huku
nikigeuka huku na kule kuwatazama wale watu ambao wote walikuwa na nyuso za
furaha. Nilipogeuka upande wa kushoto, nilimuona mtu aliyenifanya nishtuke mno,
nilifikicha macho nikiwa ni kama siamini.
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatatu
kwenye Gazeti la Championi Jumatatu.
No comments:
Post a Comment