ILIPOISHIA:
NIKIWA
bado hata sijui nini cha kufanya, nilishtukia nikifungwa mikono na miguu,
nikajaribu kukurupuka lakini sikuweza kufanya chochote, ikabidi nitulie na
kuanza kumtazama ni nani aliyenifanyia kitendo hicho na alikuwa na lengo gani
kwangu maana niliona kifo changu kikiwa kimewadia. Na hata kama ningeuawa, kila
mtu angeamini aliyekufa ni mbwa mkubwa.
SASA
ENDELEA...
“MIMI
sipendi mtu mkaidi, siku nyingine nitakuacha uwe mbwa koko, unafikiri unaweza
kunikimbia mimi?” alikuwa ni Isri, akiwa anahema huku jasho likimvuja kwa
wingi. Nilitaka nimuombe msamaha lakini sauti haikutoka, nikawa naendelea
kutokwa na machozi kwa wingi.
Aliniinamia
pale chini, akanionyesha ishara nifumbue mdomo, nikafanya hivyo, akaingiza mkono
mfukoni na kutoa kichupa kilichokuwa na maji, akayamimina yote mdomoni mwangu.
Yalikuwa machungu sana lakini nilivumilia, akanionyesha ishara kwamba niyameze.
Nilifanya
hivyo, nikahisi kama mwili wangu wote unawaka moto kwa maumivu lakini kufumba
na kufumbua, nilijikuta nikibadilika na kurudi kwenye hali yangu ya kawaida.
Alinifungua ile kamba ya shingoni kisha mikononi na miguuni, akaniambia
nisimame lakini nilishindwa kufanya hivyo kwani sikuwa na nguo hata moja
mwilini, akafungua kimfuko alichobeba mgongoni na kunirushia nguo zangu.
Yaani
kama kuna mtu anabisha uchawi haupo kwenye hii dunia, basi anajidanganya sana,
kuna uchawi na wachawi na wengine wana uwezo mkubwa kuliko unavyoweza kufikiri.
Sijui hata hizo nguo nilizivua saa ngapi na yeye alizipata wapi, sikutaka
kuhoji, harakaharaka nilizivaa huku nikitazama huku na kule kama hakuna mtu
yeyote anayetuona.
Bado
mwili wangu ulikuwa na harufu ya mbwa-mbwa na mikono ilikuwa imechubuka nadhani
ni kwa sababu ya kukimbia kama mbwa.
“Kwa
nini unanifanyia hivi Isri? Kosa langu ni nini?”
“Sasa
kwani mimi nimekufanyaje? Badala unishukuru unaanza kunilaumu tena.”
“Nikushukuru!
Nikushukuru kwa lipi,” nilisema kwa hasira huku nikimsogelea Isri mwilini,
mwili wangu ukitetemeka kwa jazba.
“Unataka
kufanya nini Togo!”
“Nataka
unieleze, kwa nini umenifanyia hivi? Unanijua au unanisikia?” niliwaka kwa
jazba. Miongoni mwa vitu ambavyo nilikuwa najivunia na hata wenzangu kule
kijijini walikuwa wakiniogopa, ni ubavu niliokuwa nao. Hakukuwahi kutokea
ugomvi wowote wa kupigana halafu nikashindwa ingawa ilikuwa si rahisi kunikuta
nikipigana mpaka mtu anichokoze sana.
“Mimi
ni nani kwako?” Isri aliniuliza swali ambalo kidogo lilizifanya jazba zangu
zitulie. Aliniuliza swali hilo kwa mara nyingine, halafu akaniuliza kama naamini
yeye anaweza kunifanyia jambo baya kwa makusudi kwa jinsi alivyokuwa ananipenda
mpaka kufikia hatua ya kunipa mwili wake wa thamani. Akaniuliza kama nimesahau
mapenzi makubwa aliyonionyesha tangu siku ya kwanza ananiona, nikajikuta
nikishusha pumzi ndefu na kujiinamia, mwili ukianza kupunguza kutetemeka.
“Twende
huku,” alisema huku akinishika mkono, nilitaka kujichomoa lakini moyo ukasita, nikawa
mpole kama kondoo anayepelekwa machinjioni, nikamfuata mpaka chini ya mwembe
mkubwa uliokuwa jirani na pale tulipokuwa. Akaniambia nimpe mkono wangu wa
kushoto, akaugeuza na kuutazama kwa muda kwenye upande wa nyuma wenye kucha.
“Unauona
huu mshipa wa damu,” aliniambia huku akinionyeshea mshipa mkubwa wa damu
uliokuwa unaonekana. Akaniambia kwamba nikifika nyumbani, kabla sijaingia
ndani, natakiwa kuchukua kitu chenye ncha kali, iwe sindano au wembe na
kujitoboa kwenye huo mshipa ili damu itoke.
“Damu
ikiwa inatoka, hakikisha unaipakaza kwenye kingo mbili za mlango kisha ndiyo
uingie ndani na usitoke mpaka giza liingie,” aliniambia huku akinipa pole kwa
yote yaliyotokea, sikumjibu kitu kwani bado sikuwa najua nini itakuwa hatma
yangu.
Baada
ya hapo, aliniambia nifumbe macho, nikatii alichokisema, akaniambia nisifumbue
mpaka atakaponiambia. Ghafla nikaanza kuhisi kama kimbunga kikali kinavuma pale
chini ya mwembe tulipokuwa, sikuelewa tena kilichoendelea mpaka niliposikia
sauti za watu ninaowafahamu wakilitaja jina langu, akiwemo Isri mwenyewe.
Ikawa
ni kama nimetoka kwenye usingizi mzito ambao hata sielewi ulitokea wapi,
nilipofumbua macho, nilishtuka mno kujikuta nipo nje ya nyumba ya akina Rahma
huku mama na ndugu zangu wakiwa wamenizunguka lakin Isri hakuwepo. Yaani kuna
mambo mengine yanatokea hata ukiulizwa yametokeaje, huwezi kuelezea.
“Vipi?
Mbona umelala nje?” mama aliniuliza huku akiniinua. Sikutaka kuwa na maelezo
marefu maana kila mtu angeniona mwendawazimu kama ningesimulia kila kitu
kilichotokea. Kwa bahati nzuri, baba alitoka na kuja hadi pale nilipokuwa,
nikiwa bado nimekaa chini kwenye maua.
Akanitazama
usoni kwa makini kisha akawaambia ndugu zangu pamoja na mama wakaendelee na usafi
kwa sababu ndiyo kwanza walikuwa wametoka kuamka na walikuwa wakifanya usafi wa
mazingira na nyumba.
Waliondoka
kwa shingo upande, mara kwa mara wakawa wanageuka na kunitazama, wakiwa na
maswali mengi yasiyo na majibu. Walichokuwa wanakijua wao ni kwamba nilikuwa
nimekamatwa na polisi na kwa jinsi taratibu za kisheria zilivyo, isingekuwa
rahisi mimi kutoka bila kuja kuwekewa dhamana na hakukuwa na mtu mwingine wa
kufanya hivyo zaidi ya baba na baba yake Rahma.
“Hebu
simama,” alisema baba huku akinipa mkono, na mimi nikampa mkono wa kushoto.
Wakati akinivuta kuniinua, nilimuona akiukazia macho mshipa wangu wa mkononi,
uleule ambao Isri aliniambia nikifika nyumbani, kabla sijaingia ndani niutoboe
kisha damu nizipake kwenye kingo za mlango.
“Umefanya
nini? Hebu tuone?” alisema baba huku akizidi kuuvutia ule mkono wangu kwake,
akautazama ule mshipa kwa sekunde kadhaa kisha nikamuona akiingiza mkono wake
mmoja mfukoni, akatoa pochi yake na kuipekuakwa mkono mmoja, huku ule mwingine
akiwa bado amenishikilia.
Nikamuona
akitoa sindano ya kushonea nguo iliyokuwa na uzi mweusi, nikiwa bado najiuliza
anataka kufanya nini, nilishtukia akinitoboa, nikaruka kwa maumivu, damu nyingi
ikawa inaruka kwa kasi. Harakaharaka, akiwa bado amenishikilia, nilimuona baba
akitoa kichupa kidogo mfukoni, cha ajabu eti akawa anakinga damu ambayo licha
ya kutobolewa sehemu ndogo, ilikuwa ikiendelea kuruka kwa nguvu.
Sikuelewa
kulikuwa na uhusiano gani kati ya ule mshipa wangu, damu iliyokuwa inanitoka na
kile alichokisema Isri. Kile kichupa kidogo kilikaribia kujaa lakini cha ajabu,
damu yenyewe ilikuwa nyeusi tii. Ilipopungua kutoka, baba aliniachia,
akakifunga kile kikopo na bila kunisemesha kitu aliingia ndani haraka na
kuniacha palepale nje.
Ndugu
zangu waliokuwa wakiendelea kunitazama kwa macho ya kuibia, walibaki
kunishangaa tu. Kwa kuwa baba hakuniambia chochote, na tayari Isri alikuwa
amenipa maelezo fulani, nilijifuta ile damu iliyokuwa ikiendelea kunivuja,
safari hii ikiwa imepungua, harakaharaka nikasogea mlangoni na kuipaka kwenye
kingo za mlango, nikawa nageuka huku na kule kuhakikisha hakuna anayeona
ninachokifanya.
Nilipofanya
kitendo hicho tu, nilisikia kama masikio yamezibuka hivi, nikawa nasikia sauti za
ajabuajabu kama miluzi hivi ambayo awali sikuwa naisikia, nikajikuta
nikilazimika kuziba masikio kwa mikono, nikaingia ndani.
Cha
ajabu, nilipoingia ndani tu, ile miluzi ilikoma kusikika, nikarudi kwenye hali
yangu ya kawaida ingawa bado damu ilikuwa ikinitoka kidogo.
“Togoooo!”
Rahma ambaye ndiyo kwanza alikuwa akitoka chumbani kwake baada ya kuamka,
alisema huku akinikimbilia pale koridoni nilipokuwepo, akaja na kunikumbatia
kwa nguvu huku akipiga kelele, akasema eti haamini kama ameniona.
“Mbona
unatoka damu?”
“Nimeumia,”
nilimjibu kwa mkato, akanipa pole sana na kunishika mkono, akawa ananipeleka
kule chumbani kwake. Mwili wangu ulikuwa mchafu na nilikuwa nanuka lakini
mwenyewe hakujali. Furaha aliyokuwa nayo, iliweza kabisa kuumaliza uchovu wa
asubuhi aliokuwa nao, uso wake ukachangamka mno, akawa anatembea kwa madaha
huku akijinyonganyonga.
Kabla
ya kupatwa na yale matatizo siku iliyopita, hatukuwa tumeonana na Rahma kwa
sababu asubuhi aliwahi sana kuamka na kuondoka na mama yake kufuatilia mambo ya
chuo, hatukupata muda wa kuwa pamoja.
“Togoo!”
nilisikia baba akiniita kwa sauti ya juu akiwa amesimama kwenye mlango wa
chumba anacholala na mama.
“Naam
baba,” niliitikia huku nikijaribu kumtoa Rahma maana alikuwa amenishika
kimahaba, baba akaja mbiombio na kunishika mkono, akamwambia Rahma kuna kazi
hatujamaliza kwa hiyo anisubiri, alinishika mkono na kuanza kunivuta kuelekea
nje lakini tulipofika kwenye kingo za mlango tu, jambo la ajabu lilitokea.
Je,
nini kitafuatia? Usikose Jumatatu kwenye Gazeti la Championi Jumatatu.
No comments:
Post a Comment