ILIPOISHIA:
Nilipomtazama
usoni, macho yake yalikuwa mekundu na yamevimba kuonesha kwamba alikuwa amelia
kwa muda mrefu, hata ule uchangamfu wake haukuwepo tena. Macho yake yakatua
kwenye fulana niliyokuwa nimevaa, akanikazia macho.
SASA
ENDELEA...
“Umebadilisha
nguo saa ngapi? Na hiyo fulana umeipata wapi mbona inanukia pafyumu ya kike?”
alinihoji Raya uso akiwa ameukunja, nikashusha pumzi ndefu na kumtazama usoni,
huku nikiuvaa ujasiri wa kiume.
“Yaani
hiyo ndiyo salamu? Ama kweli mapenzi yamepungua, kwa hiyo hata nikifa huwezi
kujali tena?” ilibidi nimgeuzie kibao Raya. Moyoni nilikuwa najua kwamba
nakosea lakini ilikuwa ni lazima nifanye hivyo ili kutuliza hali ya mambo.
“Wewe
ndiyo wa kunitamkia mimi maneno hayo? Nikupende vipi Jamal, kwa nini unautesa
moyo wangu?” alisema Raya na kuanza kuangua kilio. Kauli yangu ni kama ilikuwa
imeenda kutonesha donda ndani ya nafsi yake.
Nilijisikia
vibaya lakini ikabidi niendelee ‘kumkazia’, nikamwambia wakati anaondoka kwa
kususa, nilikuwa nikimfuata lakini kwa bahati mbaya nikaanguka na kusababisha
jeraha langu lifumuke na kuanza kumwaga damu.
“Huoni
kwamba nimefungwa plasta na bandeji upya? Kama huamini muulize yule nesi,
amenisaidia sana, huenda sasa hivi ungekuja na kukuta stori nyingine,”
nilimwambia Raya, kauli ambayo ilionesha kumshtua mno.
“Mungu
wangu, kwani ilikuwaje?” alisema Raya huku akikaa pembeni ya kitanda changu,
akawa anajifuta machozi huku akionesha kushtushwa mno na nilichomweleza,
nikamwambia shati langu lilikuwa halitamaniki kwa damu na kwamba hiyo fulana
nilikuwa nimesaidiwa tu na msamaria mwema.
Maskini
Raya! Alianza kujihisi kuwa na hatia kubwa ndani ya moyo wake, ule moto
aliokuja nao ukazimika, akaanza kunipa pole na kuniomba msamaha kama ameniudhi!
Yaani japokuwa mimi ndiyo nilikuwa na makosa, yeye ndiyo alikuwa akiniomba
msamaha!
Nilimkubalia
na kumuomba apunguze wivu kwa sababu nampenda yeye peke yake na ukaribu wangu
na Shenaiza ulikuwa ni kwa sababu maalum tu. Hakutaka tena kuendelea
kulizungumzia suala hilo, akili yake yote akaielekeza kwangu kuhakikisha nakula
vizuri chakula alichokuwa ameniandalia.
Nilikifurahia
chakula alichokuwa ameniandalia, nikala vizuri na kumfanya na yeye afurahi,
nikamshukuru kisha akatoa vyombo na kuvirudisha kwenye kikapu chake, akasafisha
kila kitu pale kitandani kwangu kisha akakaa tena pembeni yangu, mkono wake
mmoja ukiwa kwenye mwili wangu, mara kwa mara akawa ananibusu kwa mahaba mazito.
“Niambie
kama kweli unanipenda Jamal!”
“Nakupenda
sana Raya na kwangu wewe si tu mpenzi, bali mke mtarajiwa, namshukuru Mungu kwa
kukuleta karibu yangu,” nilimwambia, nikamuona akitabasamu.
Maneno
yangu matamu yalienda kumaliza kila kitu, nikaendelea kumpamba, akawa anacheka
kwa furaha utafikiri siyo yule aliyeingia macho yakiwa yamemvimba na kuwa
mekundu kwa kulia. Nikawa nimefanikiwa kabisa kumsahaulisha mabaya yote.
Mpaka
muda wa kuondoka unafika, Raya alikuwa na furaha kubwa ndani ya moyo wake,
akaniaga kwa kunimwagia mvua ya mabusu na kuniambia kwamba anatamani angelala
na mimi wodini lakini kwa kuwa sheria haziruhusu, tutaonana asubuhi ya siku
inayofuatia, akaondoka zake.
“Huyo
ndiyo Raya?”
“Ndiyo!
Vipi kwani mbona umeniuliza hivyo?”
“Aah,
nilitaka tu kumjua vizuri,” nesi Shamila aliongea huku akionesha kabisa kuwa na
kinyongo ndani ya moyo wake. Kumbe muda wote wakati nikizungumza na Raya,
alikuwa kwenye ofisi ya manesi akitusikiliza kila kitu kwa mbali, akajikausha
kama hayupo mpaka Raya alipoondoka.
“Kumbe
hanizidi kwa uzuri, tena isitoshe mimi tayari nina kazi, naishi kwangu na
kuendesha maisha yangu bila tatizo lolote. Mwanaume atakayenioa atafaidi sana,”
Shamila alijipigia debe, nikawa nimeshamuelewa kwa nini anasema vile, nikakosa
hata cha kumjibu.
“Si
naongea na wewe mbona hunijibu?”
“Sasa
nitakujibu nini Shamila? Ndiyo maana nimebaki kimya,” nilimwambia kwa upole.
Sikutaka kumuudhi kwa sababu naye alikuwa na umuhimu mkubwa kwenye maisha
yangu, katika kipindi hicho nilichokuwa hospitalini hapo chini ya uangalizi
wake.
Tuliendelea
kupiga stori za hapa na pale, mara kwa mara akimtoa kasoro Raya na kujisifia, nikawa
namuunga mkono kwa sababu kama nilivyosema sikutaka kumuudhi na kubwa zaidi,
nilikuwa nataka kumtumia kufahamu mambo mengi zaidi kuhusu baba yake Shenaiza.
“Hivi
ukiniangalia unahisi nitaruhusiwa lini kutoka?”
“Mh!
Yaani wewe unafikiria kutoka? Unajiona umeshapona siyo? Unajua wewe unashangaza
sana!”
“Nashangaza
kivipi?”
“Hivi
unajua tangu ulipoletwa hapa hospitalini na kulazwa kwenye chumba cha wagonjwa
mahututi, ulikaa siku ngapi bila kurudiwa na fahamu zako?” Shamila aliniuliza.
“Sasa
kwani kuna uhusiano gani kati ya nilichokuuliza na hayo unayoyasema?”
“Nakuona
una mambo mengi sana. Ndiyo kwanza umerudiwa na fahamu zako lakini hutulii,
mara uinuke kitandani, mara umkimbilie huyo Raya wako, mara uende wodini kwa
Shenaiza na sasa hivi unaulizia siku ya kutoka,” alisema Shamila, nikaona ni
kama alikuwa amenipania.
Nilijua
nini kilichokuwa kikimsumbua ndani ya moyo wake. Ni kweli sikuwa na muda mrefu
tangu nirejewe na fahamu lakini kwa kuwa mwili wangu ulikuwa na nguvu, sikuona
sababu ya kuendelea kupoteza muda, hasa ukizingatia kwamba kuna kazi kubwa
ilikuwa inanisubiri.
“Hata
madaktari wenyewe nikiwaeleza hizo hekaheka ulizonazo, watashauri uwe unachomwa
sindano za usingizi muda wote ili uendelee kupumzika, sijawahi kuona mgonjwa msumbufu
kama wewe,” Shamila alizidi kunishukia.
Nisingeweza
kuendelea kusubiri wodini hapo eti mpaka niruhusiwe na madaktari, kitu pekee
nilichoona ni kikwazo kwangu kufanya kazi niliyotumwa, niliona ni lile jeraha
la kifuani tu ambalo nilikuwa nimelitonesha.
Hayo
mambo ya kupoteza fahamu hayakuniingia akilini kwa sababu kwanza siyo kweli
kwamba nilipoteza fahamu na kulala tu kitandani nikiwa sielewi kinachoendelea
bali kilichokuwa kimetokea ilikuwa ni kama tu kuhama kutoka ulimwengu mmoja
mpaka mwingine.
Jambo
ambalo kwa mtu mwenye akili alipaswa kujiuliza, hivi inawezekana vipi mtu
aliyekuwa amepoteza fahamu, awe na pilikapilika nyingi muda mfupi baada ya
kurejewa fahamu hizo kama mimi?
Yaani
mtu umetolewa leo kwenye mashine ya kukusaidia kupumua ukiwa mahututi halafu
saa chache baadaye unaweza kusimama na kutembea mwenyewe kutoka wodi moja hadi
nyingine? Kulikuwa na siri kubwa iliyojificha ndani ya moyo wangu.
Kwa
jinsi Shamila alivyoanza kunibadilikia kwa sababu ya wivu wake wa kimapenzi,
niliona njia nyepesi ya mimi kupata kile nilichokuwa nakitaka, ni kumuingiza
kwenye mtego wa mapenzi, kwamba nijifanye nampenda sana yeye kuliko Raya,
nimuaminishe kwamba atakuwa mpenzi wangu ili nimtumie vizuri kupata kile nilichokuwa
nakitaka.
Ilikuwa
ni lazima kesho yake niende kule nilikoelekezwa na Shenaiza kukutana na mdogo wake
anipe hiyo bahasha yenye maelezo yote kuhusu kilichokuwa kinafanywa na baba
yake lakini hilo lingewezekana tu kama ningekula njama na Shamila, ikabidi
nianze kucheza na akili yake.
“Lakini
Shamila, kwa nini unaongea na mimi kwa ukali kiasi hicho? Au nimekosea
kukuonesha hisia zangu kwamba nakupenda?” nilimwambia, nikamuona akishtuka
kuliko kawaida, akanitazama kwa macho yake mazuri.
“Kwani
umewahi kuwa na hisia za kunipenda Jamal?” alinihoji, safari hii kwa sauti ya
chini na ya upole, akawa ananisogelea pale kitandani huku akinitazama kwa macho
yaliyobeba hisia nzito.
“Nakuapia
kama ningekutana na wewe kabla ya Raya, huenda wewe ndiyo ungekuwa mpenzi wangu
na si ajabu ningeshakuwa nimekuoa, naogopa kukueleza ukweli wa moyo wangu kwa
sababu mtu mwenyewe unakuwa mkali kwangu,” nilizidi kumseti kwa maneno matamu,
akashindwa kujizuia na kuniinamia pale kitandani, akanibusu kwa hisia za hali
ya juu na kunikumbatia bila kujali kwamba anaweza kunitonesha tena jeraha langu
la kifuani.
Je,
nini kitafuatia? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Championi Ijumaa.
No comments:
Post a Comment